10th Wonder

10th Wonder ni producer wa mziki wa Hip Hop wa kujitegemea nchini Tanzania. Amefanikiwa kujijengea jina kama mtayarishaji midundo mbunifu anayekupatia unachohitaji. Amefanya kazi na ma emcee kibao wa Tanzania wanaokubali kazi zake wakiwemo Adam Shule Kongwe, Kevoo, Ponera,Eddy Mc, Wabeti, Gamba Mc na wengine wengi. Pia amehusika kuunda albam kadhaa za ma emcee kama DemeCRASIA na Mask OFF za Ponera, Africa Revolution ya Kevoo na DIRA ya DDC na Africa(Alkebulan) ya Watunza Misingi, Mzuka EP ya B Boy Blackfire

Kwenye orodha ya maajabu ya dunia 7 yanayofahamika 10th Wonder kwa juhudi zake na nidhamu yake kwenye mziki wa Hip Hop ameweza kuingia kwenye orodha mpya ya maajabu ya dunia kumi na yeye ndiye anafunga orodha ya washindi.

Kazi zingine za 10th Wonder:

Ghost The Living – Koboko - https://www.youtube.com/watch?v=zddXJi5AuYk
Ponera na Oddu El Shabazzy – Pogbars - https://mdundo.com/song/1353438
Wabeti – Kesho - https://youtu.be/7Uzyz0667dc?t=600
Swahilimusic – Kimewaka - https://mdundo.com/song/89652
Kevoo –Waafrika - https://audiomack.com/ksonrap/song/afrika

Leo tumepata fursa ya kuwa na mahojiano na Mr. Boombap mwenyewe ili tuweze kumfahamu vizuri pamoja na dunia yake ya mziki.

10th wonder ni Nani,kazaliwa wapi na anatokea/kupatikana wapi?

Mimi ni mzaliwa wa mkoa wa Ruvuma, wilaya ya Manispaa ya Songea mjini. Huku ndipo niliposomea.

Unaitwa nani rasmi?

Jina langu rasmi ni Japhet Willhard.

Kwa nini wajiita au waitwa 10th wonder?

10th Wonder limetokana hivi; 10 ni mwezi niliozaliwa mimi, pia toka enzi za utotoni hadi sasa mimi ni mcheza soka na namba 10 ndio namba mgongoni. Wonder nayo lilikuja hivi, kando na soka kwa upande wa mziki, nilkuwa mwepesi kushika mambo ya mziki hata kuzidi waliokuwa wamenitangulia hivyo wengi waliniona kama maajabu flani kuwa naweza shika vitu kibao kwa haraka sana. Nilianza kujiita Japhezillah kwanza kipindi nilikua natafuta jina la kujiita na baadhi ya mashabiki zangu bado wananitambua kama Zillah. Wakati nikidadisi mambo ya mziki nikampata producer wa Hip Hop kule America anayekwenda kwa jina 9th Wonder hivyo basi nikaamua nijiite 10th Wonder kuwa mie ndio ntakuwa ajabu la kumi kimziki baada ya 9th.

Wee ni muunda midundo(beatmaker) tu/beat maker au mtayarishaji(producer)?

Mimi ni producer.

Historia yako kimziki ikoje, ulianzaje kuwa mtayarishaji wa muziki?

Harakati(za mziki) nilianza 2008 kipindi niko kidato cha kwanza nilipokutana na Tenzinolojia na wote tukawa tunapenda mambo ya production. Tenzinolojia akapata program ya FL (Fruity Loops) ambayo kwa kukosa tarakilishi yetu wenyewe ilibidi tutumie ya rafiki yetu ambaye kutokana na uwezo wa familia yao walimnunulia. Kwa wepesi wa kichwa changu nilipata fursa ya kujifunza vitu haraka vikiwemo kujiundia midundo mwenyewe pamoja na kutumia sampuli toka kwa kazi za watu wengine".

Ni kipi kilichokupatia motisha ya kubaki hapo?

Kuwa na ukaribu na watu pamoja na kujuana na watu na hata kupata senti ya kujikimu kimaisha. Il kikubwa zaidi ni upendo kwa mziki wa Hip Hop na upendo wa wana Hip Hop. Nafanya for the love

Ukiangalia hawa ma producer waliopo kwenye game Tanzania na duniani ni nini kilichokufanya uamini utafanikiwa kama producer ?

Ili kufanikiwa lazima ukubali kujifunza kila siku, kila siku unapoishi lazima ujue kuwa hatuwezi kujua kila kitu. Unaweza dhania unajua kumbe hamna kitu hivyo ukubali kukosolewa na kujifunza kila siku. Kiu ya kujua pamoja na moyo wa kukubali kukoselewa ndivyo vilivyonisaidia kufanikiwa kama producer. Kila siku ya Mungu nilijiona nikizidi kujiboresha kwenye ufundi huu na niliamini ipo siku nitakuwa mtaalam.

Je unatengeneza aina gani ya miziki?

Mziki wa Hip Hop.

Ni kipi kilichokusukuma usiache fani hii?

Upendo wa Hip Hop ki ujumla pamoja na utamaduni wake. Pia mambo kibao chanya kwenye tasnia hii.

Ilichukua muda gani hadi 10th aanze kusikika kwenye kazi yake?

Imenichukua takribani miaka mitano hivi kwani baada ya kumaliza shule 2011 nilisimama kwenye hizi shughuli za mziki.

Wewe hupata vipi wateja wako?

Utandawazi umekua na umeniwezesha kupata karibu ya asilimia tisini ya wateja wangu kwa kupitia mitandao ya kijamii. Nilishapata wateja hadi kutoka Kenya kwa kupitia njia ya Instagram. Asilimia ishirini iliyobaki nimekutana nao ana kwa ana. Jah ana bless.

Ushawahi kuwaza kutoka Tanzania ili kujipatia kazi zaidi?

Hapana sijawahi kuwa na mawazo hayo ila nina matumaini ya kufanya kazi na ma emcee toka nje ya Tanzania.

Umeshafanya kazi na ma emcee gani kwa miradi gani?

Aisee nimeshafanya kazi na ma emcee kibao huku Tanzania. Kwenye miradi mingi ya hip hop ya miaka mitatu ya nyuma ukicheki vizuri utapata mie nimetajwa kama beat maker au hata producer wa miradi hiyo.

Wewe upo chini ya umiliki wa studio au una studio zako mwenyewe?

Kwa sasa sina studio ila natarajia kufanya kazi na Black Ninja wa Boom Bap Clinic (B.B.C) japokuwa pia nilikuwa na nia ya kuanzisha studio yangu ya BlackNation Records. Nimeshajiunga na BBC na hapo ndipo nitakapofanya kazi zangu.

Je unaelezeaje mtindo wako wa kufanya kazi na msanii ?

Mtindo wangu wa kufanya kazi ni maelewano ya mimi na mhusika na kuhakikisha tupo fair kwa pande zote mbili.

Ni wimbo gani au mradi gani unaoupenda sana ambao uliufanyia kazi?

Kazi zangu zote nazikubali kwani zote huwa najitosa asilimia mia wakati ninapo ziunda.

Gharama zako kwa kazi hii ni kiasi gani?

Gharama huwa siwezi kutaja (akitabasamu) kwani ni siri ila kukiwa na kazi tunachekiana kisha tunakubaliana. Ila sifanyi kazi bure kwani kazi zangu pia natumia gharama kuziunda kama vile kutumia studio, umeme, usafiri na kadhalika. Bei ninayotoa ni rafiki kwa ajili ya mteja ila lazima iwe bei yenye manufaa kwangu na kwa mteja pia.

Je ni jambo gani moja kila wimbo lazima uwe nalo ili uwe thabiti?

Ni kuskia content ya msanii ninatengeneza kwa kuuliza jina la wimbo au hata kwa kuskia mashairi kadhaa ya wimbo wenyewe ili kuhakikisha mahusiano yetu mazuri yanaleta chemistry kati yangu na yake ili kutuwezesha pamoja tuunde kitu kizuri.

Ni nani mtayarishaji bora wa muziki anayefanya kazi katika tasnia hii leo na unaye mkubali?

Wapo wengi sana huhusan handakini.

Nje ya muziki 10th hujishughulisha na nini?

Huwa najishughulisha na biashara mbali mbali.

Ni watayarishaji gani,waimbaji au wasaniii waliokupa motisha yako ya msingi?

Wapo wengi sana kama vile Tenzinologia ambaye tulianza movement wote, pia kuna Blee beat pamoja na Black Junior da capo toka pale 99 Records Songea. Black Junior kachangia pakubwa sana kuniwezesha mie niwe producer mzuri kwa kunifunza sio tu ku mix hadi ku record, shoutout kwake!. Pia Salii Teknik alizidi kuninoa nilipokutana nae. Salii anapenda ujue vitu na ni mwalimu mzuri sana alienisaidia kujua mengi. Black Ninja pia namkubali sana kwani ye ni the real definition of Hip Hop ki lifestyle.

Je ni masomo gani muhimu ambayo umejifunza juu ya kutengeneza midundo ambayo ma producer pamoja na wasanii chipukizi wanaweza kujifunza?

Mimi sikwenda shuleni kujifunza mziki nimejifunza mtaani kwa kujichanganya na watu na kuwa na upendo na mziki toka utotoni. Nikiwa mdogo nilipenda kudadisi vifaa tofauti vya mziki. Pia nimejifunza zaidi pia kupitia YouTube na kadhalika.

Una ushauri gani kwa ajili ya ma producer chipukizi?

Siku zote wakubali kujifunza na pia wasilewe sifa bali waendelee kupiga kazi. Kazi ziongee zaidi kuliko mdomo! Hii ndio silaha inayodhihirisha ubora wa watu. Pia mie mwenyewe napatikana kirahisi kwa ajili ya kubadilishana mawazo na ushauri.

Pia shukran sana kwa Micshariki Africa kwa kunipa fursa ya kunihoji kama producer wa kwanza aliyewahi kuhojiwa na jalada hili. Asante kwa heshima mliyonipa.

Ni nini cha mwisho unachoweza kutuambia ki ujumla ambacho sijakuuliza? Pia tutegemee nini toka kwa 10th wonder hivi karibuni na baadaye?

Nilishawahi fanya EP yangu kama BlackNation ilhali kuna albam natarajia kuachia mwaka huu. Album hii nilianza kuiandaa toka 2017 na ipo hatua za mwisho za kuimalizia. Pia kazi zenye ubora zitaendelea kutoka kwenye mikono ya ajabu la 10 kwa ajili ya ma emcee watakao fanya kazi nami hivyo support yenu ni muhimu.

Mpate Tenth Wonder kwenye mitandao ya kijamii:

Facebook: Tenth Wonder
Instagram: 10thwonder_