Abby MP

Abby MP ni mtu ambaye kwa sababu ya uwezo wake wa kufanya vitu vingi tofauti vyenye quality nzuri amejikuta akiwa busy sana. Abby MP ambaye kitambo alikuwa emcee, ni beat maker na producer mwenye midas touch flani kwa kila kazi inayopita mikononi mwake.

Leo tumepata fursa ya kufanya naye mahojiano producer huyu ambaye catalog ya kazi nzuri alizo zifanya ni nyingi sana.

Karibuni sana.

Karibu sana. Kwanza tufahamishe kwanza Abby MP ni nani, kazaliwa wapi na anatokea/kupatikana wapi?

Asante sana Micshariki Africa kwa mwaliko huu.

Abby MP ni producer. Ni mzaliwa na mkazi wa Dar Es Salaam ila kiasili mimi ni mtu wa Mtwara.

Unaitwa nani rasmi?

Majina yangu rasmi ni Abdillahi Yusuf Mohammed.

Kwanini wajiita au waitwa Abby MP? Jina lilikujaje na lina maanisha nini?

Abby ni kifupi cha jina langu Abdillahi na MP ni kifupi cha Multi-Purpose. Nimejiita Multi-Purpose kwa sababu ya kitu ninachokifanya kwani nina uwezo wa kufanya kitu zaidi ya kimoja kama vile kuandaa beat na pia kufanya production ki ujumla kwa hiyo nikaona jina linaloni fit ni Multi-Purpose

We ni muunda Midundo tu/beat maker au producer au hata pia MC?

Nadhani mimi niko full, kuunda beat, kufanya production nk. Kwa hiyo mimi ni producer.

Historia yako ki mziki ipoje?

Mimi nimeanza mziki kipindi kile nipo Mtwara nikiwa mdogo sana nilipoanza kuvutiwa na mziki kwa kuusikiliza na hata kuucheza mziki wenyewe. Enzi zetu zile uliingia mziki wa ki Congo; akina Mbuta Likassu, Pepe Kale, Wenge BCBG, Koffi Olomide, Awilo Longomba na ukatufanya wengi tupende ku dansi mimi nikiwa mmoja wa walioingia kwenye makundi ya ku dansi.

Baadaye ma bro wangu wa karibu miaka hiyo ya ’96, ’97, ’98 walianza kuandika mistari ya rap na makundi mengi ya rap yalikuwa yameanzia huko. Akina 2proud (Mr. 2) kipindi kile alipokuwa akiachia albam zake tukawa tunaziskia na ndipo nikaanza kuijua rap. Pia tukawa tunaskia miziki ya akina Notorious B.I.G pamoja na 2pac Shakur na mie nikawa nimevutiwa na nikajikuta  nimeanza kuandika mashairi.

Taratibu taratibu nadhani mwaka ’99 kama sijakosea, Professor Jay alikuwa anafanya mapinduzi ya mziki wa rap Tanzania, akaanza kutoka na kikundi kikubwa cha watu na mie nikazama huko na kuanza kuandika mashairi. Nimedumu huko mda mrefu sana na kuandika mashairi mpaka 2005 nilipoanza kutembelea ma studio tofauti tofauti hadi 2006 nilipoanza kuvutiwa na maswala ya production.

Kwa hiyo nikawa studio moja inaitwa Tattoo Records ilikuwa pale Mwananyamala kwani mwenye studio alikuwa karibu na mimi hadi 2008 rafiki yangu wa karibu alifungua studio yake na nikapata fursa ya kukutana na ma producer tofauti kama vile Jack P, Pallah Midundo nk. Nadhani pale ndio nilikuwa deep zaidi kujifunza kupiga midundo na kuzamia kwenye aina ya midundo ya Boombap ambayo akina Pallah na Bunduki Midundo walikuwa wanaipiga. Kuanzia hapo nadhani safari yangu ilianza rasmi kwenye utayarishaji wa midundo na ndipo nilipoacha ku rap na kuelekeza nguvu yangu kubwa kwenye production.

Ulianzaje shughuli ya u producer na ni kipi kilicho kupatia motisha kubaki hapo?

Nadhani nilishalijibu swali hili ila cha kuongezea ni kuwa pale Tattoo Records mimi nilikua ni meneja wa studio hivyo nilipata fursa kibao za kujifunza na hamasa ikawa kubwa kwa sababu nilikuwa nikifanya, nafanya vizuri hadi wale ma producer wengine wakawa wananitia moyo na kuniambia, “Abby una kitu, kwani unapiga beat vizuri, unapanga chords vizuri na pia arrangement iko vizuri. Hivyo ukiwekeza nguvu utakuwa mtayarishaji mzuri sana!” Basi na mimi nikazidi kuamini kuwa naweza na nikawa natamani kua madhubuti zaidi.

Ukiangalia hawa ma producer waliopo kwenye game ya Hip Hop East Africa na duniani ni nini kilichokufanya uamini utafanikiwa kama producer?

Wao wananipa hamasa kubwa sana kwa namna vile wanavyo fanya wao. Unajua kama unahitaji mafanikio ni lazma uwe unasikiliza wengine na kufuatilia wengine wanafanya kitu gani katika hicho unachokifanya wewe.

Kwa kuwaangalia ma producer waliopo duniani nadhani napata hamasa, hasira ya kuwa bora katika shughuli hii ya production.

Je unatengeneza aina gani ya miziki?

Mimi natengeneza aina nyingi za mziki japokuwa nimeegemea zaidi kwenye Hip Hop. Natengeneza Afro Pop, Zouk, Singeli na kadhalika ila mimi kama Abby MP passion na kitu kinachonivutia sana kufanya ni Hip Hop kwani ni mziki nilioufanya (kama emcee) na pia nauishi kwa asilimia 90 ya maisha yangu.

Ulishawahi kuwa na shaka kuwa utafanikiwa kwenye hili?

La sikuwahi kuwa na mashaka hata siku moja juu ya hiki ninacho kifanya kwani nilijua siri ya kufanikiwa ni kujifunza na kupambana kwa hali na mali ili kuweza kufanikisha ndoto zangu. Pia niliamini nitakuwa mimi na naamini nitakua zaidi ya hapa kwani malengo yangu ni kuwa zaidi ya hapa.

Ni kipi kilichokusukuma usiwache fani hii?

Ni mapenzi kwa kile ninacho kifanya na pia mda niliouwekeza huku hivyo hii ni kazi na sehemu ya maisha yangu. Pia najiskia amani zaidi kwani nafanya ninachokipenda.

Ilikuchukua mda gani hadi uanze kusikika kama producer?

Ilinichukua mda wa takriban miaka mitatu mpaka minne kuweza kua fiti, kuwa imara na watu kuweza kuniamini na haikuwa mimi kupanga kusikika bali ninachokifanya ndio kiliamua wakati gani nianze kusikika.

Bidii pamoja na uimara wa kufanya kazi zangu ndio kilichofanya watu wakaanza kuvutiwa na wengine kuniamini na kazi zikaanza kutoka na kuskika sehemu tofauti tofauti.

Bidii pamoja na uimara wa kufanya kazi zangu ndio kilichofanya watu wakaanza kuvutiwa na wengine kuniamini na kazi zikaanza kutoka na kuskika sehemu tofauti tofauti.

Ni changamoto gani zinazo endana na shughuli yako ya production

Changamoto zipo kibao ila kubwa kati ya yote ni pale ninapofanya kazi na msanii ambaye sipendi anachokifanya. Yaani unajikuta wewe ni kama producer unamfanyia kazi msanii ila kwa sababu ame pay, ameshakulipa kiasi unachokihitaji inabidi umfanyie kazi ila huvutiwi na kile anachokifanya.

Mtihani mkubwa unakuja pale unapofanya mixing; haupendi sound yake, haupendi vile alivyo fanya na ni mtu ambaye huwezi kumrekebisha na mwingine anakupinga kabisa kumtoa kwa mziki wake aliokuja nao. Hivyo inabidi ufanye hicho hicho ailichokuja nacho yeye.

Hii changamoto sipendagi kukutana nayo kabsaa!

We hupata vipi wateja wako?

Mie huwapata wateja kwa wale waliosikia kazi zangu toka kwa watu ambao nishafanya nao kazi. Pia kuna wale ambao huni DM(Instagram) na wengine ambao hunipigia simu moja kwa moja.

Ungetoa ushauri gani kwa yoyote anayependa kufuata nyayo zako?

Ushauri wangu ni kuwaambia wasivunjike moyo kwani mafanikio huja kwa anayeyahitaji, anaye jituma. Kikubwa cha kujua ni kuwa production sio kitu kigumu kama ungependa kukijua kwani wanao fanya ni watu kama wewe. Wewe una uwezo wa kujifunza, kufikiria, kupambanua mambo na kuelewa kama mtu yoyote. Chamsingi atafute wenye ufahamu ili waweze kumuelekeza na kumfunza zaidi.

Pia kuna mitihani utakutana nayo, kuna watu watakunja (mioyo yao), kuna watu watakukatisha tamaa ila cha kukushauri usife moyo au kutaa tamaa kwani wewe mwenyewe ndiyo mtu wa kwanza kabisa ambaye anaweza kukufikisha pale unapotamani kufika.

Kikubwa ni kujifunza na utazidi kuwa bora.

Ushawahi kupata kazi kutoka wasanii wa nchi za nje?

Nishafanya kazi na wasanii wa Uganda na Kenya

Ni nini maoni yako pale unaposkia mtu anasema kuwa Hip Hop ni mziki wa wahuni?

Hip Hop sio mziki wa kihuni kwa sababu ni mziki ambao unagusa maisha ya watu, unakemea juu ya uovu na kukemea uhuni wenyewe ambao wanasema upo ndani ya Hip Hop.

Kuna baadhi ya tawala ambazo hukemewa na wana Hip Hop hivyo hivyo tawala hizi hufanya kampeni dhidi ya mziki huu ili kukatisha watu tamaa wasiuskilize.

Hip Hop sio uhuni ni culture ya love iliyo na burudani ya mziki na elimu.

Labda huenda wakawa wahuni flani ndani ya Hip Hop ila Hip Hop sio uhuni.

Umeshafanya kazi na ma emcee gani na kwa miradi gani?

Nimeshafanya kazi na Nash Mc katika mixtape yake ya kwanza iitwayo Hazina, pamoja na albam yake Mzimu Wa Shaban Robert pamoja na kufanya mixing and mastering kando na ku produce albam yake Diwani Ya Maalim.  Pia nishafanya kazi na Nikki Mbishi pamoja na Zaiid kwenye mixtape yake Kanda Mbovu.

Pia nimeshafanya kazi na Mantiki Barz kwenye sophomore albam yake Shahada Ya Mtaa pamoja na albam yake ya tatu Uzito Wa Juu.

Nimehusika katika album ya Stereo, Experience. Hivi majuzi pia nimehusika kwenye albam ya Kamusi, Kaka Kuona Mengi.

Nyimbo ni kibao ambazo nimeziandaa mimi na pia wasanii ni wengi ambao nimefanya nao kazi.

We upo chini ya umiliki wa studio ya mtu au unamiliki studio yako mwenyewe?

Mimi sipo kwenye studio ambayo nimeimiliki mwenyewe kwa asilimia ila pia sio mwajiriwa. Nipo kwenye studio ambayo nime share na Troo (Funk) kwenye studio ya Digg Down Records(Sinza).  

Umeshafanya kazi na wasaniii wa mamtoni au nchi jirani?

La sijafanya kazi na wasanii wa mamtoni ila nishafanya kazi na wasanii wa nchi jirani.

Je unaelezeaje mtindo wako wa kufanya kazi na msanii ?

Mimi hupenda kumfanyia msanii kitu anachopenda. Msanii akija na wazo lake napenda nisitoke kwenye wazo lake. Mtindo wangu ni kumsikiliza zaidi yeye msanii anahitaji nini, anachowaza kukifanya na mimi nibaki kwa kile anachotaka yeye ambapo mimi nitaweka wazo langu ili kuweza kuboresha kile alichokua anataka mteja kwani ni kama mimi na yeye tunajenga nyumba moja hivyo sipendi sana afate fikra zangu bali huwa napenda sana tufuate fikra zake.

Ni wimbo gani au mradi gani unaoupenda sana ambao uliufanyia kazi?

Nina nyimbo kibao ambazo nimefanya na kuvutiiwa nazo ila zaidi navutiwa sana na mradi wa Uzito Wa Juu ya Mantiki Barz.

Kwenye albam ya Uzito Wa Juu kuna wimbo ambao unaitwa Mbali Na Nyumbani ambao kusema kweli naupenda sana. Wimbo huu unaeleza vile watu walio nje ya nchi(ughaibuni/mamtoni) wanavyoishi, tukidhania wanaishi maisha ya gharama na starehe kumbe wenyewe wapo kwenye dhiki kokote kule walipo. Ingawa mimi sio msafiri najaribu kuingia ndani ya viatu vyao na pia kulinganisha story za watu ambao wapo hapa ila awali walikuwa ughaibuni.

Unajiskiaje kuwa unaskika kila mahali sasa?

Najiskia vizuri kuwa nipo kila mahali sasa hivi kwa sababu hiyo ndio ilikuwa ndoto yangu. Nashkuru wana wananiunga mkono na ku support ninacho kifanya kama hivi wewe (Micshariki Africa) ulivyonitafuta na kuamua kufahamu machache kunihusu na naomba tuendelee kushikana mikono ili tuweze kusukuma hili gurudumu mbali zaidi ya hapa.

Gharama zako kwa kazi hii ni kiasi gani?

Gharama zinatofautiana, inategemea ni kitu ninacho kifanya ila bei ya wimbo mmoja ni laki tatu ila tuweza tukaelewana na kufanya chini ya hapo ila gharama rasmi ya ofisi ni Tshs 300,000.00 kwa wimbo.

Je ni jambo gani moja kila wimbo lazima uwe nalo ili uwe thabiti?

Ni kuwa makini sana kwenye final ya wimbo kwa kusikiliza na kufanya arrangement nzuri ili mziki wangu uweze kuskika tofauti na kubaki na sound ya kwangu mimi Abby MP ilikuzidi kuwa thabiti kwenye maskio ya mashabiki

Ni nani mtayarishaji bora wa muziki anayefanya kazi katika tasnia hii leo unayemkubali?

Wapo wengi sana wanaofanya vizuri na wananivutia, sina mmoja.

Nje ya muziki Abby MP hujishughulisha na nini?

Hamna kingine ninachokifanya nje ya mziki. Mziki ndio kazi yangu na mda mwingi huwa nautumia kwenye maswala ya mziki na huwa napatikana studio.

Ni watayarishaji gani, waimbaji au wasaniii waliokupa motisha yako ya msingi?

Ni P Funk Majani, akina Duke Tachez, wamenipa motisha sana. Katika mziki ni kama akina Professor Jay ame play part kubwa sana kufanya mimi niwe vile nilivyo kwa sababu nilishika sana mashairi yake hadi kufikia hatua hadi nilikua na ghani kama yeye.

Professor Jay amenipa sana motisha!

Unazungumziaje game ya hip hop underground/handakini toka Tanzania na Africa Mashariki?

Nadhani East Africa sahizi tuko vizuri katika game ya Hip Hop hasa underground. Watu wengine wanaoonekana kuwa bora sasa hivi zao lake ni underground.  Tanzania ukiangalia akina Nikki Mbisi, Zaiid,  P The Mc, chimbuko lake ni huko. Pia ukiangalia sasa hivi akina Mantiki Barz, Dizasta vina pia chimbuko lao ni huko.

Pia ukiangalia Kenya ma emcee kama Khaligraph Jones pia chimbuko lao ni underground.

Je ni masomo gani muhimu ambayo umejifunza juu ya kutengeneza midundo ambayo ma producer pamoja na wasanii chipukizi wanaweza kujifunza?

Mimi kwa bahati nzuri sikupita kwenye mashule ili kufanya production. Mimi nimepita kwenye mikono ya ma producer tofauti ambao wamenifunza kwa vitendo. Sasa hivi ninachokifanya kwenye dunia hii ya utandawazi ni kutumia YouTube na kujifunza kwa njia za tutorials ili niweze kuboresha kipaji changu.

Ushauri wangu ni kama una uwezo unaweza kwenda sehemu tofauti kujifunza ila kama hauna uwezo wa kulipia basi unaweza kwenda studio ukajifunza na pia kutumia tutorials ili uweze kujisomesha.

Ni nini cha mwisho unachoweza kutuambia ki ujumla ambacho sijakuuliza?

Watu wa support kazi, wanunue kazi kutoka kwa wasanii ambao wanaamini kuwa ni wazuri. Pia matabaka, migawanyiko na mipasuko inayopatikana sasa hivi kwenye underground inabidi yavunjike. Nadhani mda wa kuvunja matabaka, ukanda, ubinafsi na vitu vingine visivyo na maana.

Watu washikamane, warudishe nguvu moja katika Hip Hop, wafanye kitu kwa msimamo. Kama wenyewe tushatengwa na tukaanza kutengana basi hakuna kitu kitakachofanyika. Mwisho wa siku tutadidimiza utamaduni wa Hip Hop na tunaweza  kukosa vijana watakaokuja kuskia mziki wetu na pia tutakaowarithisha utamaduni huu.

Una miradi yako binafsi iwe ni EP, mixtape and albam ambayo ulishawahi iachia sokoni?

Yah, miradi ninayo miwili; Upande Wa Pili Wa Sarafu pamoja na Heshima ambayo ni albam ambayo mimi binafsi nilirap kwenye albam moja tu. Kwenye heshima pia niliwaalika ma producer wengine waliochangia midundo kama vile Kise P, Ringle Beats na Troo Funk. Wasanii walioshiriki kwenye mradi wa Heshima ni kama Dizasta Vina, P The Mc, Bin Simba, Dambwe La Hip Hop, Black Fire, Ghetto Ambassador, Kiraka Rado, Adam Shule Kongwe, Xperience na mwenzake Nyenza toka Morogoro, Maarifa Big Thinker, Kamusi, ma emcee kibao. Nashkuru Mungu walini support na albam ikatoka 2018 ambayo bado ipo sokoni kwa bei ya Tshs10,000.00

Tutegemee nini toka kwa Abby MP hivi karibuni na baadae?

Tegemeeni kazi bora kutoka kwangu na ninachokiahidi na kupania kukifanya ni kuhakikisha kila msanii anayekuja kufanya kazi kwangu mimi anatoka kilicho bora sana kwani kazi yake ikipitia mikononi mwangu ni kazi yangu.

Pia mbeleni tegemeeni vitu vizuri na kua nitakuja na albam nyingine. Kazi nyingi zipo jikoni.

Tupe majina unayotumia kwenye mitandao ya kijamii

Instagram: AbbyMP47
Facebook: AbbyMP

Shukran.