Album: AN.KO
Msanii: Adam Shule Kongwe
Nyimbo: 17
Tarehe Iliyotoka: 15 December 2018
Utayarishaji wa Beat na Mixing: Bin Laden, Tongwe Records
Vocal recordings: Producer Papa, Biorn Records

Ni miaka miwili sasa tangu Adam Shule Kongwe aangushe album yake ya kwanza iitwayo AN.KO. Album hii ilitoka tarehe 15.12.2018 na leo tumeamua kuichambua album hii kwani ni moja ya miradi mikali iliyowahi kuachiwa na mmoja wa ma Emcee walio handakini mwa Tanzania.

Adam Shule Kongwe alianza muziki wa hip hop kati ya mwaka 2004 na 2005 na alianza kujifunza kuandika mistari yake mwenyewe. Kwa wakati huo alikua shabiki wa miziki aina yote kiujumla na Adam aliendelea kunoa uandishi na uchanaji wake hadi 2013 alipoachia wimbo wake wa kwanza.

Adam ambaye chimbuko lake ni Singida Tanzania anawakilisha Dodoma ambapo muziki wake umezaliwa rasmi.

Baada ya kuwa handakini mda mrefu yeye pamoja na Javan (Chuna Ngozi) waliachia project yao ya pamoja walio iita Chini Kabisa (CK), 2017. Wote wakitokea kwenye kundi la hip hop la toka Dodoma, Dom Down Click (DDC). Baada ya mradi huu, 2018 Adam aka achia album yake ya kwanza AN.KO.

Adam Shule Kongwe ni jina lililotokana na yeye kupenda mziki wa rap “old school” (Shule Kongwe) au golden era. Jina lake rasmi ni Adam Hamisi Selemani Abubakar Adam na alizaliwa 21 mwezi wa Julai kule Singida. Adam pia ni msomi anayemiliki Shahada ya Mipango na Usimamizi wa Mazingira (Bachelors Degree in Environmental Planning and Management) hivyo ni mwanamziki msomi ambae anatumia chombo cha mziki kuelimisha jamii yake ndani na nje ya Tanzania.

Kwa nini album iliitwa AN.KO na jina la album lina maana gani? Baada ya kuandika wimbo uitwao ANKO mda mrefu, Adam ambaye nyimbo zake ni za kiutu uzima anayependa kushauri na kuongoza jamii alishawishiwa na Javan (Chuna Ngozi) kuwa wimbo huu ulitosheleza kua jina la album. Maana halisi ya ANKO ni Achana Na Kongwe au pia ANKO ni Uncle au kwa Kiswahili mjomba yaani Mjomba Shule kama unavyoitwa wimbo mmoja kwa album hiyo.

ANKO ki maudhui imegawanyika sehemu mbili; ANKO, mchizi ambaye ni noma ki uchanaji, kwa utunzi wa mistari yake na jinsi anavyotema nondo zake ilihali upande wa pili ANKO ni mtu huru ambae hajafungwa na minyororo ya kisiasa na pia ana mitazamo yake binafsi ki maisha. Huu upande wa pili wa ANKO Shule unaskika vizuri kwenye nyimbo kama Kupe na Hohehahe toka kwa hii album.

Mjomba Shule anapata ushawishi wa utunzi kutoka nyanja tofauti tofauti maishani mwake kama vile utamaduni wa hip hop wenyewe, changamoto za maisha yetu ya kila siku na pia Marapa wabovu humpa hasira ya kufanya utunzi mzuri anapo andika mistari yake.

Kwa sasa wasanii wanaompa motisha sana kwenye game la hip hop toka ughaibuni ni Ransom, Che Noir, Benny The Butcher, Conway The Machine, El Camino kwa nje ya Tanzania ilhali ndani ya Tanzania ni wachanaji kama Javan, Nikki Mbishi, Bokonya, Kinya Mistari, Magazijuto, Maujanja Saplayaz na wengineo.

Album ya AN.KO ni album iliyofanyiwa beat production nyimbo zote na Bin Laden. Production ni ya hali ya juu na kila beat imepikwa vizuri. Chemistry kati ya Adam na Bin Laden inaonekana kwenye kila wimbo ndani ya hii album.

Album hii inaanza na introduction toka kwa Gego Master wa “Akilimia, Asilimia” na anakuonesha kuwa Adam ni mtu aliye level tofauti na ana kuandaa kupokea kazi yake ambayo imekaa kitofauti pia. Album inaanza na wimbo wa “Hohehahe” kisha “AN.KO” hadi anapoweka nukta kwenye wimbo aliomshirikisha Javan uitwao “Fullstop.”

Kisha anaendelea kuachia “Mistari” na kutusaidia kupata “Kurasa Zilizopotea” zinazotupa kumbukumbu ya historia yetu hadi pale “Simu” inapopigwa na kupokelewa na Papah. “Hatuwazi” inaendeleza maudhui ya album hadi pale tunapomkuta “Chatu” njiani. “Daima” dawamu kwa wanaopenda rap, mashabiki wa kweli wanajua kua Adam kamwe hajawahi kuwa “Kupe” bali ni “Mjomba Shule”anayewapa elimu kwa gharama ndogo tu ya elfu kumi ili kupate nakala halisi ya album yake.

Tujue kwamba “Walimwengu” wana mambo yao ila unapopata mtu anaye kupa support kwa kitu unachokifanya unakua kama “Damme Wabee” yani Van Damme wawili kama vile Chuna anavyokutana na Kongwe. Kongwe “Vs” Wale jamaa fake, anawaacha bila usalama hadi tunasema “Asante” tukiwa na Nitho tukielekea kufanya “Outro” na Makanta.

Album Hii ni safari ya maisha ya Shule Kongwe inayogusa uhalisia wa mtu wa kawaida wa Afrika hususan Afrika Mashariki. Hivyo basi leo kwenye jarida la Hip Hop Afrika mashariki tunamuenzi Anko Shule Kongwe na mradi wake AN.KO.
Mistari kadhaa Ya kunukuu toka kwenye mradi;

Hohehahe
Toka kwenye vesi ya kwanza,

“Huu ni mwaka wa mwisho wa kupinda kijinga/
Kutia huruma na kupiga mizinga/
Nakiri, mzembe hainuki mtu mzima/
Naenda shamba maana jembe halimtupi mkulima/
Umesanda, wananitania masela wangu/
Ni Kama nadhihirisha ufeki wa Bachelor yangu/
Wanakwetu mambo ya dhihaka sitaki/
Huku huulizwi una uzoefu wa miaka mingapi/
Hapa mjini nimeshinda shida tele/
Siwezi nikashindwa kwenye vita na ngedere/
Nitakaa macho asubuhi hadi usiku/
Nipambane na wadudu waharibifu/"

Na toka kwenye vesi ya pili,

“Mpiga kura wako ni mkulima mwenye shida/
Wee unachomhubiria ni kilimo chenye tija/
Piga kimya, huo ni u smart wa kitoto/
Sidhani kama unayajua hata masharti ya mikopo/
Wee unadhani hatupendi kulima buni/
Ekari za hatari, tusifiwe ulimwenguni/
Tuna vinusu eka si wengine hali zetu/
Kwa hiyo hatuna budi tuvilime alizeti/"

AN.KO
ANKO shule ni nani? Shule yupo hivi,

“Na sio wale mabroo wa mambo mengi/
Muelewe tu, maana ukimsoma hasomeki/
Amani, yeye ni Rasta kuliko wewe/
Utata, yeye ni Mafia kuliko wewe/"

Pia,

“Kifupi, mwana ni ngumu kumchambua/
Anaweza kuwa kati yenu na ngumu kumtambua/
Mchizi flani Bonge bonge ni mref/
Ni mpole na habongi huyo ndo Kongwe himself/"

Mjomba Shule

“Kustawi kwa matawi ni tokeo la mizizi/
Ubovu au ubora pia hubebwa na msingi/
Kubali kuwa chanzo ndo mambo yote/
Tuweke sawa kule halafu ndio mambo yanyooke/
Madogo wote hadi jinsia ya ‘ke/
Njooni tuzoze muache kuwasumbua wazee/
Kama mnalegeza na mnapenda vitita/
Sasa mtafanya kazi gani, muwe ma Vera Sidika? /
Muwe na pilika/
Muweze go global, right/
Vizuri, kuwa hata ma model, fine/
Ila mmeuona huo uozo wa hao ma socialites?/"

Album hii ni ya kipekee kiutunzi na kiuandishi. Toka mwanzo hadi mwisho album imesheheni madini zaidi ya Tanzanite na Dhahabu, ukipata nakala utajitibu kuliko kikombe cha Loliondo alichokuwa akitupatia babu.Pata nakala yako.

Kupata nakala yako ya mradi huu wasiliana na Adam kupitia;

Facebook: Adam Shule Kongwe Hamisi
Instagram: Adamshulekongwe_
Twitter: Adam Shule Kongwe
WhatsApp: +255629192107