Uchambuzi Wa Album: Uwanja Wa Fujo
Emcee: Adam Shule Kongwe
Tarehe iliyotoka: 31.05.2021
Nyimbo: 21
Watayarishaji: SlimSal, Whossain Qwitch, Patrino, Abby Bangladesh, Duke Tachez, Dj Kushmatic, Joe Mic, 10th Wonder, Sigger
Mixing & Mastering: Bin Laden
Studio: Fighters Records, Tongwe Records

Nyimbo Nilizozipenda: Bia Nane, Chini Juu, Hawa Viumbe, Jumlisha, Kinuke Tu Mwanangu Shule, Kula Ugali Wako Ukalale, Lucky Me, Punchndemic, Shida, Sio Sawa, Sitaki, Subira, Usalama Wa Taifa, Wa Ngau, Mara Mbili, Msongo

Moja ya album kali zilizowahi kudondoka mwaka 2021 ilikuwa ni album ya emcee Adam Shule Kongwe anayewakilisha Singida na Dodoma. Debut album yake akiwa peke yake ANKO ilipodondoka 2018 mashabiki waliutambua kama mradi wa kimapinduzi kule handakini na swali lilikua je mradi wake wa pili utaweze kufikia viwango alivyojiwekea emcee huyu kwenye debut album yake?

Tulipokua tunakaribia kufikia katikati ya mwaka jana emcee Adam Shule Kongwe alitubariki na mradi wake wa pili na hapo tulipata jibu kama viwango vitakua vya juu au vitayumba. Uwanja Wa Fujo ilidondoka tarehe 31 Mei 2021 na kusema kweli mradi ni Tanzanite kama madini ya Mjomba Shule kwenye ANKO.

UWF kama ilivyofanyika kwenye ANKO umesimama kwenye msingi wa mashairi mazuri, uchanaji mzuri, uchaguzi wa midundo mizuri, uwasilishaji freshi, viwango vya juu vya sauti, wageni waalikwa waliosimama kwa zamu pamoja na mixing na mastering ya viwango.

Mradi ulitambulishwa kwetu na singo mbili zilizoachiwa rasmi ambazo ni Lucky Me akiwa na Jadah MaKaNTa na akitumia mdundo mzuka sana kutoka kwa SlimSal pamoja na Nioneshe iliyotumia sampuli nzuri ya Papa Wemba, Show Me The Way ambapo mdundo umeundwa na Pallah Midundo aliebobea kwa kutumia sampuli za ngoma za Africa za kitambo.

Kando na singo hizi ngoma imeshiba maudhui, hadithi na simulizi, majigambo, onyo pamoja na elimu kibao, kutia matumaini, changamoto za maisha, kwa ajili ya msikizaji. Kwa upande wa hadithi Adam anatupatia na simulizi nzuri kwenye Bia Nane, Chini Juu, Usalama Wa Taifa, Mara Mbili.

Kwa upande wa majigambo ngoma zinazowasilisha maudhui haya ni Peligrosos ulioundwa na 10th Wonder akimshirikisha Nikki Mbishi pamoja na Punchndemic akiwa na wana DDC, Makala, Kevoo na Mkakamavu pamoja na Kinuke Tu Mwanangu Shule unaomkuta Adam akijigamba kuwa,

“Huwa napata mzuka watu wangu wakisema/
Tunangoja hizi kazi kwa hamu na kwa pressure/
Maana wakiniskia niki rhyme that pleasure/
Ni kama unga unavyogusa damu ya mteja/”

Yaani mashabiki kwa miradi ya Adam wako addicted mbaya.

Inapokuja kwa kutupatia matumaini Adam anawacha alama mioyoni mwetu kwenye ngoma kama Jumlisha akiwa na Mo Konzi kwenye kiitikio na Abby Bangladesh kwenye mdundo. Wimbo chanya sana kwani kila mmoja wao kafanikisha kuweka hisia chanya sana kwenye wimbo chanya. Kwenye mada hii pia utaskia wimbo singo ya mradi pia Nioneshe na Subira. Kwenye Subira utaona vile Adam kageuza kitendo cha subra kuwa mpenzi wake ambaye hawezi ishi bila yeye. SlimSal kauwa sana kwenye mdundo kama anavyofanyaga wanapokutana na Adam.

Changamoto za maisha amezigusia kwenye nyimbo kadhaa zikiwemo wimbo ulioundwa na Pallah Midundo tena, Shida, Sio Sawa ulioundwa na Sigger wa Paradise Apple, pamoja na ngoma iliyosimamiwa na Dj Kushmatic, Msongo.

Adam pia anachukua mda kupatia jamii onyo kuhusu mienendo yao kwa kupitia ngoma kadhaa kama vile Kula Ugali Wako Ukalale ambao umeandikwa kinabii hivi, Usalama Wa Taifa pamoja na ngoma ilioundwa kiustadi sana Hawa Viumbe. Duke Tachez na Adam wanashirikiana pia kutuonya zaidi kwenye Staki ambao ni moja ya wimbo chanya sana toka kwenye mradi huu akisema Adam;

“Sikubali wala kusapoti usoro man/
Kujichocha IG na ghost followers/
Likes zitaunda hata madawati hata mawili?/
Walau watoto sita waache kukaa chini?/
Na nikitajwa mara kumi kwa siku/
Stori itachimba msingi wajenge nyumba ya mwalimu?/”

Onyo kwa wapenda kiki na umaarufu usiokuwa na mbele wala nyuma. “Tutakufanya u trend/ (staki).

Ooh na utafutaji pia umegusiwa kwenye Wa Ngau akiwa na Dizasta Vina ambapo ma emcee hawa wananata na mdundo wa SlimSal wakituambia kuhusu utafutaji wetu wa kila siku akisema Adam,

“Mi Na Like Chapaaa Kubaff Kariobangi/
Story nyingine ni upumbavu ka sio ganji/”

Tafuteni hela.

Adam Shule Kongwe kupitia kazi hii bado kahakikisha ametupatia kazi nzuri. Ni vizuri kuona mtu anabuni kwanza kwa ajili yake na kuhifadhi vigezo vyake na kisha kutupatia alichokibuni na sisi pia tukakikubali kama anavyo jikubali.Mradi si wa kukosa huu, Uwanja Wa Fujo.

Kupata nakala yako ya mradi huu kwa shilingi alfu kumi tu za kitanzania mcheki Adam Shule Kongwe kupitia;

WhatsApp/Simu: +255629192107
Facebook: Adam Shule Kongwe Hamisi
Instagram: adamshulekongwe_
Twitter: AdamShuleKongwe