Afande Sele

Toka mwaka 2002 mpaka sasa 2024 ni miaka 22 imepita toka album ya "Mkuki Moyoni" toka kwa Afande Sele izame sokoni.  Mwaka 2004 hii album kwa uzito wa nyimbo zake ilitosha kabisa kumtangaza mfalme wa rhymes ni Afande Sele.

“Mkuki Moyoni” ni miongoni mwa album bora kwa muziki wa kizazi kipya wa Hip Hop kwa Tanzania wa mda wote. Ubora wa hii album unabebwa na ubora wa tungo na washiriki ambao walipewa nafasi ya kutia mashairi kwenye nyimbo.

Wimbo wa "Mayowe" alioshirikishwa Jay Mo ndio wimbo wa kwanza kutoka kwenye hii album na ndio wimbo ambao ulimtambulisha kama msanii huru, yote baada ya kuwa karibu sana na Sugu kwa mda mrefu kidogo.

Kumbukumbu zinaonesha hata wimbo wake wa kwanza "Afande Anasema" ulitoka akiwa kwa Sugu na ukawekwa katika album ya Sugu.

Fununu zilisema mwanzoni kabisa album ilitakiwa kupewa jina la "Mtazamo" lakini mtu mzima Afande Sele akaona bora jina na kuipa jina la "Mkuki Moyoni" wimbo ambao ulibeba historia nzima ya maisha yake.

Uzinduzi wa hii album ulikuwa mkubwa sana yaani raia walijaa sana, yote kutokana na ukubwa wa Afande Sele. Pamoja na kujaza mashabiki inasemekana pia watu walimtapeli mfalme mpaka ikasababisha kutokuelewana na baadhi ya wasanii ambao walialikwa kwenye uzinduzi.

“Mkuki Moyoni” album ilitoka chini ya P Funk “Majani” pale Bongo Records. Ukisikiliza hii album utagundua Afande toka mda mrefu anapenda ushirikiano na wasanii wenzake japo wasanii wenzake wanaogopa kumshirikisha kwa hofu ya kufunikwa kimashairi.

Album ilikuwa na nyimba 10.

  1. Mkuki moyoni ft Daz Baba
  2. Kama Nitapata Ukimwi ft. K Basil
  3. Mayowe ft. Jay Moe
  4. Mayowe Part 2 ft. Papii Kocha
  5. Mtu Na Pesa ft. Bwana Sam
  6. Nikiwa Mbali ft. MC Koba
  7. Habari Kamili ft. AY na Black Rhyno
  8. Mimi Na Wewe Basi ft. Mr Nice
  9. Mtazamo ft. Solo Thang na Professor Jay
  10. Mpenzi Njoo ft Bwana Sam

Cover ya hii album ilisadifu kile kilichomo kwenye album hii. Tutagusia nyimbo chache kuona ilikuaje kuaje.

‘Mkuki Moyoni’ ndio wimbo uliobeba albamu na ndio jina la albamu. Huu wimbo unaelezea kisa ambacho kilimtokea Afande Sele miaka ya nyuma. Mwaka 2017 Afande sele alipost picha yake ya kwanza akiwa na mama yake mzazi. Mwaka 2022 Afande Sele ameondokewa na mama yake mzazi.

Wimbo unaanza kwa kiitikio toka kwa Daz Baba akisema

Mateso unayonipa mwilini/
Ni vigumu we kuyatambua usoni/
Umeshanichoma mkuki moyoni/
Siwezi tena kuishi duniani na wewe/
Nioneshe huruma yako we mama (we mama)/
Nionyeshe huruma yako we mama (we mama)/
Nionyeshe huruma yako we mama (we mama)/
Kabla mimi sijafa kiama/

Ukisoma chorus unapata picha kubwa toka kwa Afande Sele kuwa kuna mda ambao alitaka apate upendo toka kwa mama yake mzazi pamoja na yote akamuomba mama ake amuoneshe japo huruma kidogo aweze kuishi kwenye hii dunia lakini mama alikaza.

Baada ya chorus kupita ndipo ubeti wa kwanza unaanza toka kwa Afande Sele.

Aah! Kabla kifo cha baba nilipata nilichotaka/
Na toka alipoanguka sioni hata pa kushika/
Dingi alivyonipenda nashindwa hata kueleza/
Ndugu zangu walinuna walisema ananidekeza/
Ndo maana alipokufa wakapanga kuniangamiza/
Visa vingi wanafanya ila mimi namuachia Mungu/
Mkombozi uliye juu, na muumba nchi na mbingu/
Kama kweli unayaona matendo ya walimwengu/
Naamini utasimama na utalinda maisha yangu/
Maana siko salama na kisa ni urithi wangu/
Ndugu wameniandama waipoteze roho yangu/
Nami sina pa kwenda, na sina mtetezi wangu/
Mama alishakimbia na akaniacha peke yangu/
Nateseka kivyangu, mchana jua ni langu/
Usiku mvua ni yangu/
Oh! /

Ukisoma ubeti huu inaonesha labda mama alimkimbia Afande Sele baada ya kuona kuna uzinguaji kwenye mali za mumewe na mengine mengi akaona bora akimbie huku akimuacha mtoto wake sehemu ambayo sio nzuri kuishi japo marehemu baba yake aliacha vitu vingi.

Sasa, baada ya kifo cha baba/
Mama aliniacha pekee, kasonga mbele kivyake/
Miaka mingi ikapita sikupata salamu zake/
Kwenye vyombo vya habari nikatuma ujumbe wake/
Tena kuna gazeti nilitoa hadi picha zake/
Waungwana walioziona walisema yupo Kigoma/
Na zaidi wakanieleza kuhusu maisha yuko njema/
Nikaenda kumtazama/
Nipate kuhakikisha kama alipo ni salama/
Mnajua uchungu wa mama, eh? /
Hasa mkipotezana kwa muda usiojulikana/
Kwa bahati njema nikampata/
Bahati mbaya ikafata, najuta yalionikuta/
Ni vigumu kuamini lakini ukweli nitakufa
Mama alinikataa, kwanza sikumuelewa nikabaki namshangaa/
Kisha nikamuuliza, vipi mama una kichaa?/
Mwenyewe umenizaa, hivi sasa unanikataa!/
Jibu alilorudisha sikuamini kwa masaa/
Alisema sikujui na geti akafunga pah!
Shoga zake jirani wakanieleza kwa ufasaha/
Kumbe kaolewa tena na amesema hajazaa/
Hivyo angenikubali mumewe angemkataa/
Mwili ulikosa nguvu nikabaki nimeduwaa/

Huo ubeti wa pili ukisoma unaona wazi mama alipokimbia huku nyuma alimpa kazi kubwa mtoto wake kumtafuta kila kona. Alitumia kila njia mpaka akaja kufahamu mama ake alipo na akamfuata cha ajabu mama nae akamtosa hapo ndipo ukirudi kwenye chorus ndio unapata picha kwa nini alitaka japo apate huruma ya mama kidogo.

Kweli nilishangaa/
Mama ‘angu alionizaa kuniacha kwenye mataa/
Takribani nusu saa sikuongea kama bubu/
Watu walinizunguka, nikainama chini kwa aibu/
Ntaishi vipi ugenini, akilini sikuwa na jibu/
Kule sikuwa na ndugu, nkaishi maisha ya tabu/
Sometimes ilinibidi nilale nje kama bawabu/
Mbu, baridi kali, kwa kweli nilipata tabu/
Maisha kwa kiumbe mimi yalionekana kama adhabu
Na kama unavyoelewa wenye pesa wengi waarabu/
Wapo wenye ustaarabu, ila wengine hawana adabu/
Nilipoomba msaada walitaka kwanza taarabu/
“Washenzi, hamna adabu”/
Ndivyo mimi nilivyo wajibu
Dhiki ukiendekeza haki ya Mungu watakuharibu/
Hilo nililelewa nikaliweka kumbukumbu/
Nilipokosa chakula ilibidi nilale njaa/
Nikikosa pa kulala nazuga kwenye mitaa/
Maisha kifo mkononi, kifupi mi niliishi kama mtoto wa mtaani/
Ndo maana naona mbali, naona mbali/
Kwa darubini kali!/

Ubeti wa tatu ulimaliza kila kitu kuhusu safari yake ya kumsaka mama ake.

‘Kama Nitapata Ukimwi’ huu wimbo ulizungumzia kuhusu gonjwa hatari la ukimwi. Kama akipata ni jinsi gani ataweza kujilinda na kulinda wenzake?

Kwenye “Mayowe” (Part 1 na Part 2) Afande Sele alitaka watu wasipige sana kelele kwa wale ambao kusikia na kuelewa kwao ni ngumu yani bora kuwaacha yawakute ndio wataelewa.

“Watu Na Fedha” ulizungumzia jinsi nguvu ya pesa ilivyo huku nguvu ya utu ikipotezwa vibaya mno na nguvu ya pesa.

“Nikiwa Mbali” huu wimbo ulizungumzia mkoa wa Morogoro mpaka utunzaji wa mazingira katika mkoa wa Morogoro.

“Habari Kamili” ulizungumzia mambo mbalimbali ya kwenye jamii yetu jinsi yalivyo.

“Mimi Na Wewe” ni wimbo wa mapenzi umezungumzia uvumilivu na upendo mpaka kuachana.

“Mpenzi Njoo” huu nao ulizungumzia kuhusu mapenzi na upendo wa dhati kabisa.

“Mtazamo” huu wimbo nitakupa mashairi yake na utajua ulikua mtazamo wa nini…

[Solo Thang]

Yeah…/
Yeah…/
Hakuna S bila O/
L bila O/
Mwingine aitwe’ Thang bila Solo/
Shupavu’ awajibike kama Apollo/
Jay, Afande! /
Ni ukuta wapi uchochoro? /
Hakuna S bila O/
L bila O/
Mwingine aitwa Thang bila Solo/
Shupavu awajibike kama Apollo/
Jay, Afande! /
Ni ukuta wapi uchochoro? /
Yo naghani ni mtazamo wa fani/
Ile dhana ni uhuni wameleta hawa katuni/
Kuna ku-rap na kubwata/
Ma-reppa na ma-rapper/
Katuni, tungo tata/
Wapi ulipo we jaku? /
Unakuwa mtumwa ili upewe promo kuuza/
Au kama ni binti’ ukalale kwa prodyuza/
Ma-Promoter wanauma tu hawajui na kupuliza/
Na siku wakipuliza jua kidonda kishaoza/
Natamani kuwa huru mnyonyaji asinidhuru/
Wanaitwa “ma-emcee” hawajui mitindo huru/
Huu mtazamo wangu naona vingi vioja/
Yaani watangazaji sasa ndo ma meneja/
Vidato sita nlivyopitia/
Ndivyo vinavyonisaidia/
Mbunifu ukiizingatia/
Hata wakinibania/
Ni kipaji tu/
Ni mtazamo tu/
Msikasirike washkaji/
Haya mawazo tu/
Ulamaa…/

Ukianza na ubeti wa Solo anakuonesha wazi kwenye huo wimbo hakuna mnyonge wa mashairi "Jay, Afande ni ukuta wapi uchochoro" kwa kupima kwako hapo tu unaona kabisa hakuna mnyonge wa mashairi kwenye huu wimbo.

Ni mtazamo zamo emcee usiogope kivuli/
Bora ukemee mabaya na usifie mazuri/
Ni mtazamo zamo emcee usikwepe umande/
Okoa sanaa ya Bongo ili uchumi upande/
Ni mtazamo zamo emcee usiogope kivuli/
Bora ukemee mabaya na usifie mazuri/
Ni mtazamo zamo emcee usikwepe umande/
Okoa sanaa ya Bongo ili uchumi upande/
Kwi kwi, Ulamaa, Professor Jay, Afande/

Chorus ndio imepita hapo ubeti wa pili unafuata

[Professor Jay]

Ni mtazamo rap inakuwa ni mikingamo/
Sasa watoto wadogo wanajiita watu wa makamo/
Wanakwenda hatua mbili, wanarudi kumi na kujipongeza/
Bila kuzingatia hatua nane walizopoteza/
Hao ni mafukara wa akili zao na uwezo wao/
Wasiotambua nini na nini ni hatma zao/
Magwiji vichwa chini utadhani wanatunga sheria/
Lakini sheria msumeno isije ikawarudia/
Yes, ma-underground wanafanya rap inang’ara/
Lazima muwe vinara imara kwenye msafara/
Rap na mazingaombwe abadani haviendani/
Msitegemee tawilee iwaokoe katika fani/
Ni vyema ukafikiri kabla ya kufanya maamuzi/
Tazama mbele usije ukanywa chai kwa mluzi/
Naamini askari shupavu lazima upitie depo/
Vinginevyo ndugu yangu utakuwa unapaka rangi upepo/
Kama unapata moja kwa nini usipate na mia/
Hiyo inawezekana kwa wote mlio na nia/
Sioni sababu za msingi kuomba kwenye mitaa/
Kama una kipaji iweje ufe na njaa/

Ubeti wa tatu

[Afande Sele]

Asante Professor Jay
Majani na Ulamaa mmegusa n’napopataka/
Nami kwenye mtazamo nina jambo nataka kuweka/
Maana kila kukicha emcees wanaongezeka/
Nasema very nice, yes rap kama dhehebu
Emcees kama wafuasi/
Wingi wa wasanii unaonesha ni dini safi/
Yaani imekubalika, waumini tuko wengi
Lakini bado nna shaka/
Sijapata uhakika, wote tumesadiki/
Ama wengine ni fake mmetumwa kama mamluki/
Maanake hamna maana/
Mna-rap mradi rap, mistari imekosa vina/
Yenye vina haina maana/
Na kila mnapokaa mnapenda kusengenyana/
Mnapenda kutetana na mnapenda kulumbana/
Mimi naogopa sana,
Kwa jinsi navyoelewa mwishoni mtatukanana/
Ama inawezekana mwishoni mkaja chinjana/
Na wote tunao-rap tuonekane hatuna maana/
Wapi ilipo Taarab/
Ilikuja kwa kishindo, hata wagumu walishausudu/
Kwa ajili ya malumbano mwishoni ikafa kibudu/
Shabiki piga simu, changia mawazo yako/
Nani tutamlaumu, kama rap ita-cease kwa kuendekeza upuuzi/
Nani tumchune ngozi, producer aliyerekodi/
Ama labda DJ anayepiga kwenye kipindi/
Wengi wanapenda rap, ajabu rap haiwapendi/
Waungwana wanaiacha, wapumbavu hawaambiliki/
Hivi kwani lazima tuwe wote wanamuziki/
Mi nadhani ingetosha wengine mbaki ushabiki/
Huu ni wangu mtazamo masela msijenge chuki/
Hata na Majani, yoh/

Kwa kupimia tu huu wimbo ungetoka miaka hii unaona ni nani angeweza kufiti hapo kimashairi?

Baada ya hii album na ushindi wa rhymes mtu mzima akatoka na album yake ya pili ‘Darubini Kali’…