Msanii: Ambecal AMC
EP: Mbali Sana
Tarehe iliyotoka: 03.02.2021
Nyimbo: 7
Wapiga midundo na ma producer: Last born, Sheem king, Eco Wa Miracle,
Studio: H.K Records, Master Records

Ambele David ni mchenguaji aliyejiandaa vyema kwa ajili ya safari za mbali sana. Wazazi wake chimbuko lao ni Kyela, Mbeya na kutokana na baba yake David kuwa mwanajeshi wa jeshi la kujenga taifa (JWTZ) jambo la kuhamishwa kikazi lilikuwa la kawaida. Barua ya uhamisho ilifika ili kumhamisha babake David mbali sana na Kylela na kumpeleka zaidi ya kilomita 1,000 hadi Mwanza.

Kule Mwanza mnamo mwaka 1996, hospitali ya Bugando, wazazi hawa walibarikiwa kupata kitinda mimba wao ambaye walimpa jina Ambele David. Akiwa bado mdogo kijana huyu aligundua karama yake ya uchoraji akiwa shule ya msingi. Ni huko pia alipofika darasa la 6 alipo vutiwa na mziki wa aina ya Hip Hop. 2012 Ambele alizidi kuzama kwenye harakati za mziki alipo ingia shule ya upili ambapo alikutana na watu mbali mbali ambao walimpa hamasa na msukumo juu ya hili swala la uchanaji hadi kuunda kundi lililoitwa Rhymes Marker 2014.

Kati ya 2010 hadi 2012 David alipokuwa ameanza mziki rasmi alifanya ngoma yake ya kwanza na katika uandishi wake alikuwa anapenda “word play” au kucheza na maneno na pia “repetition of words” au kurudia kwa maneno na hivyo katika vina vya kati na mwisho alikua anapenda kuandika maneno yanayoishia na “cal”, kwa mfano physical, chemical, logical na kadhalika. Kutoka kwa mtindo huu wake wa kipekee mashabiki wake walichukua “Ambe” toka kwa jina lake rasmi Ambele na kuliunga na “cal” na kuumpa kijana Ambele David jina lake la usanii Ambecal. Ambele hakuafiki hili jina na akaunda jina lake mwenyewe, AMC ambalo alilitoa kwenye herufi zinazopatikana kwenye jina la Ambecal yani (A)..(M)be..(C)al. Baada ya kujitambulisha kama AMC mashabiki walilifanya hili kuwa jina lake la pili la usanii na wakamuita Ambecal AMC na Ambele akajibatiza rasmi jina hili kama lake la usanii.

Ambecal AMC kama vile safari ya wazazi wake ametoka mbali sana ki uchanaji sawia na jinsi alivyo pata jina lake la usanii. Mwaka wa 2019 mwezi Febuari tarehe 2 Ambecal AMC alitoa mradi wake wa kwanza ikiwa ni kanda mseto aliyoiita RFA (RAP FROM AMBECAL). Mnamo 2 mwezi wa Febuari 2021 tena Ambecal AMC aliachia mradi wake wa pili rasmi, EP ijulikanayo kama Mbali Sana.

Kama jalada linavyoonesha vizuri maisha ya mwanadamu safari ya kutoka utotoni hadi uzeeni ni ya mbali sana. Binadamu anapitia mambo mengi toka kuzaliwa, kuishi hadi kufa. Album hii ya Ambecal imejaribu kuweka safari hii yetu sote ndani ya nyimbo saba pamoja na maisha yake mwenyewe AMC.

Mradi unaanza na wimbo uliobeba jina la EP, Mbali Sana akituambia, “Hata mimi nimetoka kule(mbali)” ili kusisitiza kua kwa chumvi aliyokula anacho cha kuwaambia mashabiki wake kwa hiyo wakae kitako kupokea madini.
The Next AMC ni mdundo murua sana anapotuuliza AMC hivi?

“Can you give up? Never give up/
And you still rap? Yes never leave rap/
Just for hip hop can you keep up? /
Yes AMC man i will always be on top...”

AMC ndio The Next big thing na anajiamini kwa kipaji alichonacho juu ya mdundo uliopikwa vizuri sana na Last Born.

Eco Wa Miracle anachukua doria kwenye mdundo wa Mwanza ambapo Ambecal anaiwakilisha mitaa yake kama aalivyoienzi Ngosha enzi hizo.

Rap soka iliyoundwa na Last Born ni singoo inayotupeleka dimbani kwenye mchuano kati ya Rap Vs Ujinga. Mechi ambayo washambuliaji magoli wa Rap wanaitandika timu ya ujinga goli 7 bila.

Masaa 12 ni singo inayoeleza vizuri jinsi mtu anaweza kufanya vitu vingi chanya ndani ya masaa kumi na mbili jua linapo chomoza hadi kutua kwa ajili ya kuboresha maisha yake.

Science & Technology(Sayansi) ni track inayosoma kama kitabu cha historia ya maisha ya mtu alivyo na anavyotumia sayansi ili kuboresha maisha yake na vile pia Sayanis inaweza kutumika vibaya.

Anasema Ambecal hivi kuhusu Sayansi,

“Toka zamani kabla binadamu hamjawa/ inasemekana mlitokea unyamani na mkawa /
Mkitembea kwa mikono na miguu kila mara/
Mkiwa watupu hamna lugha mlibonga kwa ishara/
Mi hamkunijua ila mlikua na ndoto/
Hadi kufikia kipindi ambacho mligundua moto/
Ili Jua litoweke msipate tabu usiku/
Ikawa atua hadi kujua vipi mpate mkate wa kila siku/
Miaka ikayoyoma ikapita/
Kifikra nikaitika mlivyoniona mkaniita/
Nikafanya zaidi ya kuona na kushika/
Mkajifunza mkashona mkasoma na kuandika/
Hadi kuwa wakulima wafugaji /
Mkanikuza nikawa shina la ubunifu na vipaji/
Na hapo ndipo kwangu ilipoanza historia/
Mkanipa Jina niitwe Sayansi na Teknolojia/...............”

Rock City Cypher ndio track inayomaliza mradi wetu.

Ambecal AMC ana safari ya kwenda Mbali Sana kama msanii na amepiga hatua ya pili nzuri inayompa msingi wa kusimama na kuwalikisha mji wake wa Mwanza na Taifa lake kama muandishi na mchanaji mzuri. Kongole AMC twakutakia safari njema kwani unapokwenda ni Mbali Sana.