Ba Mwenga akichora picha ya Sean Price. Picha hii ilimpa umaarufu sana kwa wana Hip Hop

Japokua Ba Mwenga amekua mchoraji kwa mda sasa kazi zake zilianza kuonekana vizuri duniania pale alipojititwika jukumu la kumchora marehemu emcee Sean Price. Sean Price alikua ni rapper, mwandishi wa nyimbo pamoja na mtayarishaji wa mziki kule Marekani

Mchoro huu ulimpatia sifa nyingi bwana Ba Mwenga na kumtambulisha kule Marekani baada ya mchoro wake kusambaa hadi studio iliyomsajili Sean Price, Duck Down Records.

Leo hii tumeamua kumtafuta Ba Mwenga ili kuweza kupiga gumzo ili kumhamu yeye na sanaa yake.

Karibuni sana!

Historia yako ni ipi? Jina na unajishughulisha na nini kimaisha?

Majina yangu kamili naitwa Hassan Ramadhani Bamchawi. Najishughulisha na uchoraji, kwa ujumla najishughulisha na uchoraji maana kuna vitu vingine nafanya ila uchoraji ndio nime base kwa kiasi kikubwa.

Niambie kidogo kuhusu Ba Mwenga, umetokea wapi, ulikulia wapi na utoto wako ulikuaje, umesomea wapi? Unaitwa nani rasmi na jina la Ba Mwenga lilikujaje?

Mimi naitwa Ramadhani Hassan Bamchawi. Nimesoma Kijitomongo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani. Hii Ba Mwenga watu walikuwa wanatumia badala ya Mchawi kwa jina jingine ni Mwanga kwa hiyo watu walikuwa wananiita mimi Ba Mwanga badala ya Ba Mmchawi.

Lakini mimi ki utundu nikaangalia kwenye makabila ya kaskazini mwa Tanzania, Tanga Tanga  huko Mwenga inatumika kama namba moja alafu kwa upande wa Ba utaskia, “Ba Mwamadi, Ba Mwenga, Ba nani..”wakimaanisha bwana nani. Kwa hiyo mimi ni bwana moja yani. Eeh ndio maana ya Ba Mwenga.

Kwa nini uliamua kuwa mchoraji?

Kuhusu uchoraji mimi nilijikuta tu automatically nachora kwa sababu baba yangu alikuwa mchoraji.

Je ni nani alikuvutia pakubwa ki uchoraji na kukupa hamasa ya uchoraji? Pia ni nini hukupa hamasa na motisha ya kuchora?

Aliyenivutia labda baba yangu kwa sababu nilikuwa naona sana baba yangu akichora kwa sababu mimi nimezaliwa nje ya ndoa. Hatukua tukiishi pamoja lakini nilimuona baba yangu akiwa anafanya eeeh.

Umekuzaje kipaji hiki hadi kufikia kukupa ajira?

Dah! Nimepita kwenye msoto mkali, mazingira magumu. Nishajipendekeza sana kwa watu kwa sababu mimi baba yangu alishawahi kupitia kwenye uraibu wa mambo flani flani. Kwa hiyo kipindi mimi nakua baba yangu yeye alikuwa anafanya hivi vitu lakini alikuwa keshakuwa mraibu wa hivi vitu.

Kwa hivyo sasa wakati huo mimi nilikua na wakati mgumu ikawa inanilazimu kufuata watu wengine ambao walikuwa watu baki ambao sio baba yangu, sio mama yangu, hatuna undugu wa nasaba yoyote. Eeeh ipo hivyo.

Kazi yako inatoa maoni gani juu ya maswala ya sasa ya kijamii au kisiasa?

Mi napenda sana kuchora kuhusiana na mazingira ya kiafrika Africa, sunset zile, mazingira ya nature, ma beach, au views za mbuga, wanyama wapo kwa mbali hivi jioni jioni, asubuhi. Mara nyingi napenda kuchora picha zile.

Kinyume na hapo labda kama sijatumwa napenda kuchora kuta kuta hizi mambo ya murals. Mara nyingi huwa napenda kuchora picha za wanaharakati eeh, napenda sana kuchora picha za watu ambao wanazungumza kweli.

Je unatafutaje fursa?

Fursa  mimi natafuta katika mitandao ya kijamii yani kwa sababu mimi nina page na kwa sasa page yangu nimeambiwa nilipie ila kipato changu kipo hovyo nashindwa kuilipia kwa hiyo post zangu mimi naona watu wa like tu. Nyingine naambiwa kabisa utaona peke yako huwezi ku boost. Uki boost itawafikia

Kwenye mitandao ya kijamii nina page, nina group nina account ya Instagram nina account ya Facebook eeeh, hii hii mitandao ya kijamii inanitafutia fursa au kinyume na hapo sehemu nyingine nikienda kufanya kazi huwa naacha mawasiliano yangu pale.

Nini kilichokusukuma kuchora picha za magwiji wa Hip Hop kama vile Sean Price na Eazy E? Je ulishawahi kuhusika kuchora picha kwa ajili ya jalada za miradi ya wana Hip Hop?

Daah, kinachonisukuma ni mizuka tu. Mimi napenda Hip Hop yaani automatically napenda Hip Hop. Napenda Hip Hop lakini napenda kuchora sana watu ambao hawajulikani wa underground. Ndio maana mimi sipendi kuchora mara Tupac sijui nani. Ujue dunia hii watu wengi wanafanya vitu wapate kujulikana na watu kuwa wao ni noma sana Lakini mimi sipo kwa ajili ya kujulikana, sipo kwa ajili ya pesa. Yaani mimi nipo kwa ajili ya kuwapa elimu ili kuweza kuwajuza watu kuhusu vitu ninavyojua mimi na watu wengine hawajui yani

Kuhusika kuchora picha kwa ajili ya majalada ya Hip Hop, hapana hii sijawahi.

Kazi zako hupatikana kwa bei gani?

Kazi zangu mimi kama sanaa yoyote ile hazina kima au kiasi maalumu kama vitu vingine kwani inategemea kitu anachotaka kufanyiwa mteja mwenyewe .

Maana mtu mwingine atataka nifanye kazi kwenye ukuta wa futi 20 alafu wewe unamtajia bei ya futi mbili heeh, kwa kitu anachotaka kukichora inabidi uangalie material gani utatumia, sehemu ina changamoto gani nitatumia mda gani kwa akili yangu. Ndio hapo bei inapokuja.

Lakini hakuna bei maalum kwamba bei ni hii, hiyo siwezi kuelezea kusema kweli.

Je mtu akitaka kujua kuchora unaweza kumfunza?

Yaani kufundisha mimi nafkiri ni taaluma binafsi, kipaji binafsi, uwezo binafsi. Siwezi mimi kumfunza mtu labda awe ananiangalia mimi ninavyofanya nae afanye kwa sababu mimi nilijua kwa hivyo tu wala sikufunzwa  kuchora. Mimi kuchora sikufunzwa kwa hiyo daah itakuwa ngumu kusema eti naanza kufundisha. Na kwa kuwa mimi sijawahi kukaa kwenye darasa lolote linalofundisha kuchora, sijui hata watu wanafunzwaje.

Kwenye hiyo nakutana na changamoto sana watu wananiambia(ga) mimi mbinafsi na kila kitu lakini daah, siwezi. Yani kama mtu ataniangalia mimi ninavyofanya basi ndio itakuwa darasa kwake.

Michoro hukuchukua mda kiasi gani ili Kuweza kukamilika?

Inategemea na huo mchoro wenyewe. Picha nyingine inachukua hadi siku kumi. Kwa sababu mimi nafanya kwa brush, umeona bana, sina air brush, sina vitu vya kusawazisha. Mimi nafanya local umeona bana.

Huwa inanichukua siku tano, siku mbili, siku tatu . Mchoro mwingine unachukua hadi siku 10.

Kando na kazi hii ya kuchora wasanii wa nje ulishawahi kumchora msanii yoyote kutoka Tanzania?

Niliwahi kumchora msanii mmoja, Godzilla,. Siku moja nilikaa na ndugu yangu nash emcee wakati Godzilla alipofariki kabla hajazikwa akaniambia bwana tum dedicate jamaa. Kwa hiyo tukachora.

Jamaa akanunua mabango nini, alivyonunua mabango akanunua na rangi na mimi ikawa mchango wangu kuchora, kipindi kile kulikua na matamasha flani ya kinasa walikua wanafanya wale jamaa. Kwa hiyo nikachora bango likaenda likawekwa kwenye jukwaa na ikawa kama siku yake hiyo Godzilla. Watu wakawa wanaongea ongea mambo yao kuhusu Godzilla eeh.

Wewe huskiliza mziki unapochora ? Huwa unapenda kuskilizia nini kama jibu la swali la kwanza ni ndio?

Yaah ndio huwa napenda kuskiliza muziki na muziki ambao mimi napenda kuskiliza mara nyingi ni Hip Hop miziki yenye midundo ya moja mbili, one two, wenyewe wanaita Boombap. Naskiliza sana muziki. Yaani muziki unaniwekea hamasa kwenye shughuli  zangu

Siku yako huanzaje?

Mimi naishi kwa kutegemea sana simu. Mtu anaponipigia simu kuhusu kazi mimi hapo hapo ndio napata riziki. Mimi siku yangu ninapoamka huwa nafanya mazoezi kisha natulia kwa sababu sina ofisi rasmi

Je kuna mchoro uliochora au uliobuni ambao unajivunia zaidi? Waweza nitumia picha ya mchoro wenyewe kama upo?

Picha kumi hizo hapo unazoziona hizo za Sean Price ndio mchoro ulionifanya nijulikane hadi kule Duck Down Records kule Marekani.

Ni nini ambacho unakipenda kuhusu uchoraji au kuwa mchoraji ?

Kitu ambacho mi napenda kwanza kwenye fani yangu ya uchoraji kikubwa kabisa ninachopenda watu wajue na waone mimi ninachofanya. Kwa sababu watu wengi tunafanya lakini tunatofautiana.

Mi napenda watu waone ninachokifanya.

Una ushauri gani kwa mchoraji anayeanza?

Kwa mchoraji anayeanza ushauri wangu mkubwa ni wawe na uvumilivu kwa sababu sanaa hapa kwetu ni ngumu, sijui nchi zingine wala sijafanya sanaa kwenye nchi nyingine ila nchi hii nishafanya sana na naona mazingira ya sanaa jinsi yalivyo haya mazingira ya sanaa ni magumu sana, eeh. Yani watu  wengi wanapenda sana kuwasifia watu au kuwatambua watu hali ya kuwa washakua kwa kiasi kikubwa. Lakini wakati unatokea chini hapo ndipo kunatokea kukatishwa tamaa, utakutana na vikwazo vingi kwa hiyo watu wavumilie.

Yaani ukiingia kwenye sanaa maswala ya pesa weka lakini usiweke mbele kwa sababu sanaa ujue imefanana sana na wale watu kwenye mashimo ya kuchimba madini eeh. Inawezekana umeingia tu kwenye sanaa ukafanikiwa, ukawaacha hata watu ambao ulikua umewakuta na inawezekana ukakaa mda mrefu pia usipita kile unachokihitaji ukawa unapata kidogo kidogo.

Kwa hiyo mimi nawashauri uvumilivu mwingi sana na heshima pia uliowakuta ili upate kujua vingine ambavyo wewe huvijui. Nafkiri ni hivyo kwa sababu hata serikali zetu haswa hapa nilipo mimi Tanzania haitambui, inapuuza, sio kwamba haitambui sanaa ya uchoraji.

Kwa sababu hata wanapo wazungumzia wasanii inawazungumzia bongo flava na bongo movie, wasanii wa kuchora hawatambuliki. Hata hizo shule zilizopo Bagamoyo, shule za sanaa hakuna somo la uchoraji. Watu wanaenda kucheza ngoma za kibisa na vitu vingine kama kuigiza, kufinyanga na kuchora chora.

Hata hao watu wanaopewa sijui certificate, masters of arts sio mtu kabobea kuhusu kuchora. Sanaa ya kuchora itayumba sana ingawa watu wanakuja hapa, hao hao watu wa serikali wakati wa kampeni wanawatumia watu kuchora vitu vyao wakiwa na shida zao. Kwa hiyo daah, nashauri wawe wavumilivu. Kwa sababu sanaa ya kuchora ni ngumu kimtindo. Afadhali kidogo sasa hivi mtandao wa kijamii umekuja kurahisisha, kwa hiyo wawe wavumilivu na wenye heshima.

Shughuli zako za uchoraji unazifanyia wapi au ofisi zako zinapatikana wapi?

Shughuli zangu mimi nafanyia mtaani, nikimaliza na post mtandaoni kama hivyo ndio watu wanaona kuwa jamaa hivi na hivi ila mimi sina address kusema eti ofisi yangu iko hapa, hapana. Shughuli zangu mimi nafanyia mtaani.

Kipi kingine ambacho ungependa kusema ambacho sijakuuliza?

Mimi kingine sina isipokua nina ushauri. Ujue hizi serikali zetu hizi zinatakiwa zitambue. Yaani ikiwezekana katika mitaala yao ya elimu watambue kwamba kuna kuchora pia kuanzia shule za msingi, chekekea katika shule za serikali, kuwepo na somo la kuchora.

Kuna watu kibao ambao wanajua kuchora. Lakini ni kama limedharaulika hili swala. Mtu yoyote ambaye anachora hapa Tanzania ukija kumchunguza kama kasoma shule basi kasoma shule hizo za shule binafsi au kasoma nje ya nchi, ndio huyo ambaye kasomea.

Lakini kinyume na hapo hawa watu wengine waliosomea shule za serikali utaskia bana mimi mjombangu mchoraji nilikua nakaa nae. Au kaka yangu rafiki yake alikua anachora. Au mimi mwenyewe tu bidii zangu eeh. Kwa hiyo serikali inatakiwa itambue kwamba kuna kitu kinaitwa kuchora, yani iwepo katika mitaala ya kufundishia. Ni hivyo tu.

Shukran sana kaka Ba Mwenga kwa mda wako. Nashukru kwa gumzo, limekua gumzo zuri na tumejifunza mengi kutoka kwako na natumai wasomaji wetu na waskilizaji wetu pia watapata neno kutoka kwako ambalo litawajenga, litawaonesha ubunifu huwa unakuzwaje na unaweza kumnufaisha mtu kivipi maishani mwake.

Asanteni hadi pale tutakapo kutana tena kwenye kipindi kingine cha Micshariki Africa, nawatakia siku njema asante.

Wasiliana na Ba Mwenga kupitia;

Facebook: Ba Mwenga
Instagram: bamwenga