Bankslave kazini

Unapozungumzia utamaduni wa graffiti nchini Kenya huwezi kumaliza gumzo bila ya kumtaja mchoraji BankSlave. Bank Slave ambaye ni mzaliwa wa Nairobi ameweza kufahamika na wengi kupitia kazi zake hata kabla watu hao hawajamfahamu aliyehusika na kazi zile ni nani. Michoro yake inapatikana sio tu Nairobi bali hata Arusha pamoja na nchi za ulaya.

Na mimi ni mmoja wa watu hawa ila kwa kuwa nina nafasi ya kipekee ya kutaka kuihabarisha jamii yangu kuhusu sanaa na wana sanaa niliweza kutafuta mda na kuwasiliana na BankSlave ili kuweza kumfahamu na kufahamu sanaa yake na mchango wake kwenye sanaa ya graffiti pale Kenya.

Karibu sana Micshariki Africa kaka Bank Slave. Historia yako ni ipi? Jina lako rasmi na unajishughulisha na nini kimaisha?

Asante sana Micshariki Africa kwa mwaliko wenu.

Mimi nilianza kuchora kitambo nilipokua miaka kumi na mamangu alinisaidia sana kukuza kipaji changu cha kuchora kwani alikuwa anajivunia kuwa kijana wake anajua kuchora na alikuwa anawaomba watu wanipe kazi za uchoraji niwafanyie. Kitendo hichi kilifanya nifahamu kuwa nina uwezo wa kuchora nikiwa na umri mdogo.

Jina langu ni Kevin Esendi na mimi najishughulisha na sanaa ya uchoraji.

Niambie kidogo kuhusu BankSlave umetokea wapi, ulikulia wapi, utoto wako ulikuaje na umesomea wapi umefikia wapi hadi sasa?

Bank Slave ama Kevin alizaliwa Kibera hapa jijini Nairobi ambapo Kibera ni moja ya makazi duni makubwa yaliyopo mashariki ya kati ya Africa. Nilisomea shule za karibu na hapo kama vile Olympic Primary School. Hapo shule ya msingi ya Olympic kulikua na mashindano ya uchoraji yaliyo dhaminiwa na kampuni moja inayotengeneza rangi za viatu na mie niliweza kushiriki na kuibuka mshindi wa tatu. Sikufa moyo ila niliendelea kusomea sanaa yangu na kuzidi kujinoa.

Unafanya sanaa ya aina gani?

Mimi nafanya kila aina ya sanaa; nafanya sanaa ya uchoraji kwa kutumia brashi, pia natumia spray paints/rangi ya kupuliza, pia nachora kwa matatu/hiace/daladala, kwa restaurants/migahawa. Pia nina uwezo wa kuchonga vinyago, ninaweza kufanya uchongaji wa mawe na kutengeneza kwa mfano sanamu, naweza kutumia udongo na kuunda kinyago. Katika sanaa mimi nafanya kila aina ya sanaa.

BankSlave, ni nini Story ya nyuma kuhusu hili jina? Lilitoka wapi na lina maana gani?

BankSlave; sisi sote ni ma bank slave kwa maana kuwa mahali tupo huu mfumo wa ubepari unatulazimisha tuwe tunategemea mahali flani ili kujimudu kimaisha na hapo ndipo tunajipata kila wakati kwani hatuna uwezo.

Pia mimi kwenye utafutaji wangu wa riziki nikajibatiza jina hili hadi wa leo.

Kwenye bio yako Instagram inasema Tabibu/Mjengaji/Mchora picha za watu mtaani/Na Graffiti…Tueleze kidogo kuhusu haya.

Mimi nina uwezo wa kumfanya mtu atulize hisia zake kwani rangi ninazotumia kwenye uchoraji wangu zina uzito flani ambao unachangia yeye kutulia kama alikuwa na shida kibao anapopata fursa ya kuangalia michoro yangu ukutani na inamtuliza roho, inamfurahisha na kumburudisha. Kwa hiyo hali ya kufurahi mwili unajiskia vizuri na kama alikua na msongo wa mawazo anaanza kupona na yale mawazo kuanza kupotea kwa sababu ya kuangalia mchoro wangu. Kutokana na hili ndio maana najiita Tabibu.

Kwa upande wa ujengaji au kwa kimombo builder mimi ni yule kijana anayejenga na wale wanao jenga, kama wewe unajiongoza na kujituma mimi ni rafiki yako kwani kwa kushirikiana tunaweza kwenda mbele kwenye safari. Kwa hiyo Mjengaji kwangu linamaanisha mimi najihusisha na mtu anayejisaidia, mtu anaye jituma. Sitawahi jihusisha na mtu anayekaa pale kijiweni anangojea nimpatie shilingi ishirini ilhali yeye kakaa hapo siku nzima bila kujituma kwa chochote, umenipata eh? Haya.

Kwa upande wa sanaa ya graffiti nimeipenda kwa sababu naweza kuichora kwenye ukuta, nje na kokote pale duniani. Sanaa hii ambayo inatumia rangi ya kupuliza au spray paint kwa lugha ya kimombo inafanyika kwa mda mfupi tofauti na ile ya kutumia paint brush/brashi ya kupaka kwenye canvas kwa sababu ile rangi ya kupuliza huenea sehemu kubwa kuliko kama unatumia rangi ya brashi.

Kazi yako inatoa maoni gani juu ya maswala ya sasa ya kijamii au kisiasa?

Kazi yangu kawaida lazima niongelee vitu ambavyo vinaendelea maishani mwetu; kinachotudhulumu au kinacho tusaidia. Kwa mfano ninapochora picha za watu ambao wamepiga hatua na tuzwa shahada flani kama vile Wangari Maathai kwa kazi ambayo amefanya kwa ile shughuli yake ya kusaidia kutunza mazingira kwa kuzuia ukataji wa miti na kwa kuhimiza upandaji wa miti hapa nchini. Pia mchoro wa rais wa awali wa America Barrack Obama ambaye ni mkenya huonesha kujivunia kwetu kwa yeye kuwa mkenya na mwafrica na kuonesha vijana kuwa wao wanaweza kuhitimu pale ambapo hawangeweza kudhania wata hitimu kwani wengine hawangeweza kuwa na matumaini ya kuhitimu bila ya kumuona Barrack Obama.

Pia kuna yale maswala ya kisiasa ambayo huwa nagusia hapa na pale kama vile umuhimu wa kudumisha amani  wakati wa uchaguzi. Pia huwa nagusia maswala yanayogusa jamii kama vile maradhi na kadhalika.

Je ni nani alikuvutia pakubwa kwa mambo ya uchoraji na kukupa hamasa ya kuwa mchoraji? Pia ni nini hukupa hamasa na motisha ya kuchora?

Kuna watu wengi ambao nilikua nawafuatilia kabla ya kuanza kuchora kama vile wachoraji toka America, kutoka Ujerumani kama vile Task Crew(America), Stick Up Kids(Ujerumani), Tassle(The Macleen Crew) ni watu ambao wamechora sana miaka ya nyuma na wenye rangi zinazochora vizuri na zinasaidia kutoa kazi zao vizuri zaidi. Hawa wamenipa hamasa ya kuwa mchoraji na pia kuweza kubaki nilipo kwani nikichora watu wanavutiwa na kazi zangu na naendelea kufanya kazi hii kwani inanisaidia kulipa bills.

Motisha ya kuchora pia ni kufanya kazi ambayo inaweza kukumbukwa kila wakati kwa mfano nikimchora mtu ambaye alikua anaenziwa na wengi na hatutaki kumsahau basi huwa najitwika jukumu la kumchora kwenye ukuta na watu wanapata fursa ya kumuona na kumkumbuka mwendazake kwa mazuri yake alipokua hapa duniani.

Je ni changamoto gani unazozipata unapotaka kuchora mural au graffiti mtaani?

Changamoto zipo, kwa mfano kutopata rangi ambazo zinaweza kufanya kazi vizuri. Pia rangi zenyewe zinapatikana ughaibuni na ni ghali kuzileta ila tuna matumaini kuwa mambo yatakuwa mazuri baadaye.

Changamoto nyingine ni kupata ukuta wa kuchorea au wakati ninapochora watu wanakuwa wengi ila ni changamoto ambazo tunaishi nazo kama street artist.

Pia hizi ndio changamoto zinazotujenga sisi kwani ukishaimaliza na ukirudi siku nyingine kuitazama unafurahi wewe mwenyewe kwa sababu ya kazi yako nzuri uliyoifanya.

Tueleze kidogo kuhusu kazi yako, ni nini unahitajika kuwa nacho ili uweze kufanya hii kazi vizuri?

Unachohitajika kuwa nacho ni kwa mfano picha ya kuangalia ili kuweza kuunda mchoro wako na picha yenyewe lazma iwe ya hali juu, pia unahitajika kuwa na rangi zenye viwango, pamoja na brashi pamoja na spray paints nzuri na salama.

Unapotaka kuchora mural ya graffiti ni bora upate ukuta mkubwa kwani kazi yako itatoka vizuri sana kwani rangi zitaenea vizuri sana na kuwezesha kazi yako kuwa bomba sana na kazi itakuwa rahisi na kuchukua mda mchache sana.

Umekuzaje kipaji hiki hadi kimekupa ajira?

Nimeweza kukuza kipaji hichi kwa kuweka nidhamu au kwa kimombo discipline kwani bila hii sio rahisi kwani lazma ujitume na moyo mmoja, ukiwa na mteja lazima uskizane nae vizuri na hata kama umekosea usisahau mteja mara zote huwa yupo sahihi kama wahenga walivyosema.

Mimi binanfsi sijawahi kukosana na mteja wangu na nashkuru kwa hili na yote ni kwa ajili ya nidhamu kwa kazi hii ukishachorea mtu mmoja ndio anakuwa afisa masoko wako kwani ndio atakutangazia jina. Kwa hiyo ukaribu wako na mteja ni muhimu sana.

Je unatafutaje fursa za kazi?

Fursa za kazi zinakuja kwangu zenyewe kwa sababu ya kazi ninayoifanya kwani nikishamfanyia mtu mmoja yeye huniunganisha kwa mtu mwingine mwenye hitaji la kufanyiwa kazi. Mimi sijawahi kukimbiza kazi kwani kazi huja kwangu zenyewe na nashkuru sana kwa hili.

Kazi zako hupatikana kwa bei gani na je inakulipa?

Kazi yangu mimi hutegemea complexity au ugumu wa kazi ninayoifanya. Hivyo kazi huwa nalipisha kulingana na ugumu huwa mara mbili kuliko kama ingekua kazi rahisi.

Kwa mfano unapochora uso kuna changomoto ya kuuchora vile unavyotakiwa uwe tofauti na michoro ya design za African print ama designs za leso (kanga kwa watanzania) ni rahisi kuliko kumchora mtu mahali. Hii hufanya bei ya kazi kuwa tofauti ila mimi hulipisha Kes 10,000.00 kwa mita mraba au kwa dollar ni $ 100.00 kwa mita mraba.

Kazi hii inanilipa, nashkuru.

Graffiti ni moja ya nguzo tano za Hip Hop? Je we pia ni mtunza misingi wa Hip Hop?

Yeah, yeah, mimi ni mtunza msingi wa Hip Hop. Grafitti ndio nguzo ya kwanza ya Hip Hop kwani kuna watu pia waliona nimechora na wakaenda palipo na mchoro wangu na kuanza ku freestyle, pamoja na Dj kufika na ku spin, pamoja na watu wengine kufika pale na ku breakdance na mwishoni kuna watu wakafika pale na ku emcee, kwa sababu mimi nilikuja pale nikawa inspire, kwani walikuta nilicho chora kwenye ukuta ni fire! (Hahaha, msela hapa akajaribu kughani kiasi!)

Ulishawahi kufanya kazi na ma emcee wa hip hop nje na ndani ya Kenya, Mashariki Africa na Africa kiujumla?

Ndio nishawahi kufanya kazi na emcee Kaa La Moto, Kaligraph Jones na wengine wengi toka Kenya sanasana. Pia nimewachorea backdrops wanamziki toka Uganda na Tanzania huwa nimecheza sana na rafiki yangu Farid Kubanda (Fid Q).

Kule Africa Magharibi kama vile Senegal nimeshafanya kazi za graffiti ambazo walizitumia kama background kwa kazi zao.

Fid Q - Bankslave - Kaa La Moto

Umeshafanya kazi na wana Hip Hop, na kwa miradi ipi?

Ndio nishafanya kazi na wana Hip Hop kwenye tukio la WAPI (Words And Pictures) hapa Nairobi ambayo tulikuwa tunashirikiana na wasanii wengine wa Hip Hop pamoja na watu wa mitindo huru (freestyles), b-boys na wengine wengi. Baada ya tukio huwa tunaendeleza harakati nje na tukio na kuendeleza shughuli za Hip Hop.

Je watu wanakuchukuliaje unapofanya hii sanaa yako ya graffiti?

Watu hufurahia sana mimi nikichora graffiti, wananipongeza, wameweza kuniweka pale nipo, wana ni support na mimi binafsi nafurahia kufanya sanaa hii.

Kazi ya Mwalimu Nyerere uliichorea wapi? Ilikujaje kumchora baba wa Taifa la Tanzania?

Nilifurahia sana kumchora rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pale Arusha Tanzania kwenye MCDC center kwani alistahili kuchorwa pale na bado nikifanikiwa kwenda Dar Es Salaam nitamchora pale yeye na ma rais wengine wa Tanzania, Inshallah.

Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Tofauti yako na hawa graffiti artists wengine nini? Ni nini mtu akiona kazi yako atajua moja kwa moja huyu ni BankSlave?

Kazi yangu mimi hupenda kuitofautisha na wale wachoraji kwa njia ya technique ninayo tumia kuchora pale kutokana uvutio ambao nimejaribu kuweka ndani na jinsi ninavyomalizia kazi yenyewe ambayo mimi huwekelea sana details kwa kazi yenyewe.

Tueleze kidogo kuhusu chata(logo) lako la NRB FLY? Zinapatikana wapi na kwa shilingi ngapi?     

Nairobi Fly au kama inavyo andikwa ki chata NRB FLY ni label yangu ambayo natengeneza nguo ndani, ma sticker na kadhalika. Ni element yangu moja ya fashion ya kuvalisha watu wa Nairobi na kote dunia na imetokana na maisha ya kitaa ya Nairobi ambayo ni mimi kama graffiti artist najaribu kuiskuma izidi kujulikana kote duniani.

Niko na ukurasa wa Instagram kwa ajili ya chata hili NRB FLY ambayo mtu yoyoye anaweza kuingia pale na kununua chochote anachotaka kama stickers, hoodies na t-shirts ila baadae nitaongeza bidhaa zingine kama vikombe, vikombe vya plastiki na vingine vingi ambavyo mtu anaweza kuvitumia kwa maisha yake ya kila siku hata kwenye migahawa na sehemu za kulia bata.

NRB FLY

Shughuli hii hukuchukua mda gani kukamilisha?

Inategemea. Tunarudi pale kwenye urahisi au ugumu wa kazi ninayoifanya. Kama ni kitu kina ugumu flani inachukua mda mrefu lakini kama ni rahisi inanichukua mda mchache. Kwa hiyo inategemea inaweza kunichukua masaa matatu au dakika 5 au siku nne au hata wiki 4 inategemea na kazi ninayoifanya.

Siku yako huanzaje?

Siku yangu huanza hivi; nikiamka hua napasha kidogo kwa kupiga zoezi la kujinyoosha (stretches), napiga swala na popote ninapoenda kuchora kabla ya kazi huwa lazima nipige zoezi kidogo. Pia nina ukuta ambapo ninaweza kuchora, inategemea siku inaanzaje kwani kama ni siku baada ya kujivinjari basi siku lazma itaanza tofauti.

Wewe unapenda nini sana kuhusu kuwa mchoraji na je ni kitu uliwahi waza utakuja fanya?

Kuchora ni kitu ambacho nimependa kutoka utotoni na nilipokua mdogo nilikuwa najisemesha kuwa nikiwa miaka flani nitakuwa naweza kuchora vitu flani. Mimi mwenyewe nilikuwa najua kuwa hii sanaa naipatia mda na kuwa kitu ambacho siwezi kuchora sahizi baada ya mda flani nitakuwa na uwezo wa kuichora.

Mimi mwenyewe nilikuwa najipatia motisha ya kuendelea kuchora na mawazo yalikuwa pale toka awali ya kuwa mchoraji nifikapo miaka flani, yeah napenda sana kuchora.

Je kuna kazi uliyoifanya ambayo unajivunia zaidi? Waweza nitumia picha ya mchoro/ wenyewe kama upo?

Kazi zote ambazo nimefanya nazipenda kwa sababu kila moja ina story yake. Kila kazi niliyoifanya ina utofauti wake ambapo siwezi sema kazi hii ilikua na uzito zaidi ya nyingine kwa sababu kile ambacho nachora kinatoka kwenye hisia zangu na nikikiweka pale nje kinaonekana na kila mtu na nisingependa kuweka kazi ambayo waliopo karibu na mtaa nilipofanya hiyo kazi hawaelewi nilichokifanya.

Mimi hujaribu kuchora kitu ambacho watu wanapokiangalia wanaelewa moja kwa moja nilikua ninasema nini kupitia picha ile ili kuzuia watu kunitafuta ili kuwaeleza kuhusu kazi niliyoifanya badala ya kutafutwa kwa sababu ya mtu kutaka kukuongezea shilingi mfukoni kwa ajili ya kazi ulioifanya.

Kando na shughuli hii ya uchoraji/Graffiti una vipaji au talanta gani zingine? Pia unajihusisha na shughuli gani tofauti Na sanaa hii?

Kwa upande wa talanta naeza sema naweza kudansi. Pia naweza kucheza mchezo wa raga (Rugby) kwani mimi nilikuwa mwanaspoti sana japokuwa kuna mda pia ulienda na nikawacha na nikaweza kuendelea na shughuli zangu za graffiti.

Janga la Uviko 19 limeathiri vipi shughuli zako za uchoraji ? Na umefanyaje ili uweze kupeleka mkono kinywani?

Wakati ugonjwa huu ulifika Kenya mimi tayari nilikuwa kazini ambapo wale wateja walikuwa washanipa mikataba ya kuwachorea pamoja na mahoteli ambayo hayakuwa na watu yaliweza kusafisha maeneo yao ya kuogelea (swimming pools) ili kuniwezesha mimi kuingia pale ili nichore hivyo basi niliweza kupiga kazi japokua maisha hali ya kiuchumi kiujumla nchi ilikua imeanza kuzorota

Je unafunza watu kuwa wachoraji kama wewe? Gharama zikoje?

Ndio mimi nafunza watu kuchora ila lazima nitafute mda wa kuweza kuandaa madarsa hayo kwa sababu mimi pia hubanwa na mda kutokana na ratiba zangu. Ila kuna watu niano wafunza ilhali huna wale wanaotazama mkono wangu na vile ninavyofanya.

Pia kwenye YouTube page yangu huwa naweka tutorials ambazo watu wanaweza soma na kuona vile ninavyochora na rangi ambazo ninavyozitumia.

Nimeona we pia unapenda kutumia Kiswahili. Watu wa Nairobi mnafahamika sana kwa sheng, hapa ilikuaje?

Mimi hupenda kutumia Kiswahili kwa sababu ni lugha ambayo inaeleweka kwa nchi kadhaa hapa Africa Mashariki ambapo naweza kuwafikia watu wengi na pia naweza kutumia lugha hii ili kuweza kuwafikia waafrika wote na kuwafunza Kiswahili na kuweza kuwafanya waafrika kuwa wamoja kwani hapa tutaweza kuwa na uzito flani kinyume na matakwa ya wakoloni.

Tukiongea lugha moja tutakuwa kitu kimoja kiroho  na kuweza kuwa na nguvu za kuamua tunachokitaka na kuweza kutimiza vitu vingi ambavyo vimekuwa vikitusumbua kwa miaka kama waafrika.

Ulishawahi kushinda tuzo zozote kutokana na shughuli yako ya uchoraji?

Ndio nishawahi kushinda tuzo kama vile la Unkut Awards Africa, Unkut Hip Hop Awards (Best Graffiti Artist/Graffiti Artist Of The Year) na tuzo nyingine kibao zinazotokana na kazi ninazo zifanya kitaani.

BankSlave

Una ushauri gani kwa artist yoyote anayeanza kwenye fani hii?

Kwa anayeanza anatakiwa ajue kuwa hii si fani rahisi ya kuingia na anatakiwa ajue ya kwamba na mtu anatakiwa kujipanga ki hisia, ki mawazo na kiakili. Inatakiwa ujitahidi kujifunza ili kuweza kuwa mchoraji mzuri au hodari kadri ya uwezo wako na hili utaweza kwa kufanya mazoezi tu.

Mazoezi ndio silaha ya kukufanya uwe mchoraji hodari kwa mda. Pia inatakiwa uwe mtu wa kustahimili mambo na mwenye uvumilivu kwani shughuli hii huchukua mda kabla ya mtu kuwa stadi. Ni kama mtu akijifunza kuendesha baiskeli au anapotaka kujenga misuli, mda unahitajika ili kupata matokeo mazuri pale mbeleni.

Kuwa na nidhamu kwani ukiwa nayo utaweza kwenda mbali kwani shughuli hii haitaki mtu anaye jichocha sana (kujiamini hadi kupitiliza ilhali uwezo ni mdogo). Stay humble, fanya mambo yako na ndani yam da utakua mchoraji hodari.

Unapatikana wapi kwenye mitandao ya kijamii na tovuti?

Kule kote najulikana kama BankSlave

Instagram: Bankslave

Pia napatikana YouTube ambapo kazi zangu kibao ninaziweka hapo na kama ungependa kusomea chochote au kuniuliza swali flani nitakua pale nikiwajibu maswali yenu yote.

YouTube: Bankslave