Uchambuzi Wa Album: Love Story
Emcee: Budder Manolo
Tarehe iliyotoka: 07/06/2022
Nyimbo: 16
Watayarishaji, Mixing & Mastering: Tunchy Master, Wiser On The Beatz
Studio: Tongwe Records
Nyimbo Nilizozipenda: Mwanamke (Intro), Give Me A Hook, Mapenzi Gani, Doctor Love, Futa Machozi, Usinipe Moyo, Christmas Girl, Tunapendana, Hupati Mchumba, I Love You, Bora Tuachane, I Miss You, Dear Ex, Utanikumbuka, Kwa Nini, Sitokuacha,
Emcee Budder Manolo ni mzaliwa na mwenyeji wa Dar Es Salaam anayepatikana kule Kimara. Kijana huyu alianza kuchana kipindi akiwa shule ya msingi miaka ya 2006 akiwa na miaka 11. Alikuwa akiwaskia ma emcee kama Professor Jay, Jay Mo, Afande Sele Daz Nundaz na kundi la East Coast team. Fid Q ndio rapper aliye mu inspire kuanza kuandika na kuchana nyimbo zake mwenyewe na licha ya kuanza kuandika nyimbo kwenye madaftari kutoka 2007 alibahatika kuingia studio kwa mara ya kwanza 2012.
Changamoto za kufanya viwili kwa wakati mmoja vilimshinda yaani kusoma na mziki wakati mmoja hivyo basi aliachana na muziki kwa muda wa miaka minne hadi pale alipomaliza masomo yake 2016 na kuachia nyimbo kama Everything Will Be Ok na Kabla Sijafa ambazo alirekodi Tongwe Records.
Katikati ya mwaka huu emcee Budder Manolo alikuja na album yake ya kwanza rasmi Love Story ambayo alirekodi chini ya studio za Tongwe Records chini ya usimamizi wa watayarishaji Tunchy Master na Wiser.
Album hii ambayo ina nyimbo 16 ambazo zote ni hadithi husika za mapenzi ambazo zinaungana kusimulia story ya kijana ambaye alikuwa anaingia kwenye mapenzi, misimamo yake kuhusu wanawake na pia kutongoza wanawake.
Mradi unaanza na wimbo flani mzuka sana ambao unapiga kinanda freshi sana Mwanamke (Intro) ambapo emcee huyu anaanza kumuongelea mwanamke na mapenzi akisema,
“Mwanamke hukupenda Kwa ulichonacho,
So mthamini akikupenda ila huna budi kuwa macho,
Iko wazi Kuna vitu vingi ambavyo,
Mwanamke atataka Ili uwe wake awe wako,
Wengi huamini kuwa mapenzi ni tiba mseto,
Huangalia tu chini hawakumbuki kuna kesho,
Na akizama kwenye tope, kutoka ni kazi,
Atataka umuongoze Kila kitu iko wazi,
Utampora fikra atabaki na kichwa,
Ukimtoa bikra ndo atazama kabisa,
Ni ukweli sio uongo haya mambo yanatokea,
Na ni mademu wengi wa bongo ambao wameongopewa,
Hawatambui mapenzi ni sumu kwenye amani,
Kiakili hawakui kama binadamu wa zamani,
Wengi hupenda sababu ya peer pressure,
Ila wanaume huwatenda wakijipatia pleasure,”
Na kwenye kiitikio ambapo emcee huyu anakuonesha pia kando na kuchana anaweza kuimba anakwambia
“Mwanamke ni kiumbe anaye-run dunia,
Alinizaa mimi hata na wewe pia,
Mwanamke akikupenda ni vingi atakufanyia,
Hata maumivu anayopitia ni mengi….”
Baada ya wimbo huu emcee huyu anaendelea taratibu kwenye Give Me A Hook kabla ya kushirikiana na muimbaji Mycol kwenye Mapenzi Gani. Mpaka sasa unachokiona mashairi yanavyo andikwa na kuwasilishwa vizuri.
Kwenye Doctor Love akiwa na Nelly Ne kwenye kiitikio emcee huyu anajigamba vile yeye ni daktari wa mapenzi aliyehitimu. Dr. Budder anaongelea vishawishi anavyovitumia kuvutia akina dada wakati akitaka mapenzi. Ni wimbo flani ulioandikwa ki reverse psychology kuonesha vile ma playboy wanavyofanya kuwanasa wanawake. Ila anatoa tahadhari kua sindano yake haipo kwa ajili ya machoko akisema, “Abadani sigawi vidonge sana/ hatukutani kama sex zetu zinafanana”. Wimbo mwingine ambao unaendana na maswala haya ya playa ni Usinipe Moyo akiwa na Lodd.
Muimbaji Nelly Ne anashirikishwa tena kwenye Futa Machozi ambapo unaanza kuona story telling ya Budder Manolo vile ipo top notch juu ya mdundo mzuka sana ambapo bass guitar linagonga freshi.
Christmas Girl ni wimbo ambao unaonesha kijana Budder kapata kile alichohisi ni mapenzi ya kweli kwenye sikukuu ya Christmas baada ya kuvunjwa na kuvunja moyo mara kadhaa hapo awali. Lakini kama wasemavyo waingereza Karma is a bitch mpenzi wake anamsaliti na kumuacha kijana na jeraha la moyo hadi kuzama ndani ya sonona. Wimbo freshi sana, story, ujumbe, uwasilishaji, kiitikio pamoja na mdundo.
Ngoma nyingine ambazo nilivutiwa nazo ni Tunapendana akiwa na Maria ambao unaweza ukacheza na mwenzio kwani una piga drums na piano safi sana ilhali sauti nzuri inaimba kwenye kiitikio. Pia kuna Hupati Mchumba, I Love You na Bora Tuachane akiwa na Lodd kwenye hizi ngoma mbili tena.
Mradi unazidi kutema madini ya mapenzi kwenye I Miss You akiwa na Naomisa pamoja na Dear Ex ambao umetumia sampuli nzuri toka kwa wimbo wa Aviation, You Were My Everything kabla ya mtayashaji Wiser kushika doria kwenye single ya kwanza toka mradi huu Utanikumbuka akimshirikisha Nate Dogg wa Bongo, One Six.
Kwa Nini akiwa na da’ Maria tena ni wimbo wa majuto baada ya penzi la kijana kusalalitiwa pamoja na wimbo unaotamatisha mradi huu Sitokuacha akiwa na Lodd tena.
Love Story ni mradi ambao uliandaliwa na nia ya kuongelea mapenzi mwanzo mwisho na kusema kweli Budder Manolo kupitia debut album yake amefanikisha hili. Kuanzia mada, mashairi, uwasilishaji na waimbaji waalikwa emcee huyu amesimama peke yake na kuchana bila ya emcee yoyote yule kusaidizana nae kwenye mradi huu. Budder inapokuja kwenye mada ya mapenzi ana madini kama Buddha.
Mfuatilie Budder Manolo kwenye mitandao ya kijamii kupitia;
Instagram: budder_manolo
Twitter: budamanolo