Ufupi wa Cafu Da Truth sio kizuizi kwake bali ni baraka. Ufupi wake umemuwezesha yeye kufanya vitu chini ya maji bila kuonekana na pale watu wanapomgundua ameshafanya yake na kusepa. Uwezo huu ndio ulimuwezesha yeye kuliangalia janga la Uviko 19 nchini Kenya kwa jicho tofauti lililo muwezesha kuwa mwanahistoria marufuku aliyeorodhesha madhambi mengi waliyofanyiwa waKenya wakati wa janga la Uviko.
Cafu Da truth kama vile mchezaji wa mpira wa miguu ambapo jina lake limetokea ni beki au kwa kiingereza defender, anapenda kulinda familia pamoja na watu wake wanaomtegemea kwa kutumia kalamu yake.
Karibu sana msomaji uweze kujifunza toka kwa Cafu Da Truth.
Karibu sana kaka Cafu Da Truth kwenye jukwaa letu la Hip Hop. Kwanza tuanze kwa kukufahamu Cafu Da Truth ni nani? Majina yako rasmi? Unatokea wapi?
Shukran sana kaka kwa mwaliko wako.
Majina rasmi ni Stephen Mwangi Njuguna, Cafu Da Truth a.k.a The Tall Rap Midget na ni emcee, battle rapper, ni artivist (anaye tumia sanaa kufanya harakati), freestyler, mwandishi, mwandishi wa nyimbo na mshairi pia. Mimi natokea mitaa ya Soweto, Kibera jijini Nairobi, Kenya.
Mbona wajiita Cafu Da Truth?
Nilipewa jina Cafu mwaka 1996 na marafiki zangu ambao tulikua nao darasa moja shule flani ya msingi. Marafiki hao Rashid Obeid na Patrick Muriuki walinipa jina hilo kwa sababu nilikuwa nacheza ball (mpira wa miguu) sana kama beki wa kulia kama alivyokuwa anacheza mchezaji mpira mkongwe wa Brazil, Cafu.
Toka hapo jina liliniganda kama kupe kwa ng’ombe hadi leo. Baadaye niliamua kulimiliki kama jina langu la usanii na nikapata malengo kupitia jina hilo na nikalikuza na likawa utambulisho wangu kwani karibu kila mahali nilipoenda sikukosa mtu anayenijua. Toka shule ya upili hadi nilipokuwa chuo kikuu nilipata marafiki ambao walizidi kulisambaza jina hilo.
Maana ya undani ya jina langu hii hapa;
Cafu Da Truth👇🏾
C-onscious
A-nd
F-actual
U-ndertakings
D-at
A-re
T-riggered
R-ight
U-nder
T-he
H-orizon
Tueleze kidogo kuhusu historia yako ki mziki?
Wakati nikikua nilikuwa napenda fasihi sana. Nilikuwa pia napenda kusoma sana ila sikudhania kama nitakuwa rapper ama nitakuja kufanya mziki hadi 2003 nilipoingia shule ya upili.
Baada ya kumaliza shule ya upili nilijiunga na mtandao wa kijamii Facebook ambapo nilikuwa kwenye kundi lililojiita PCL (Punchlines and Crazy Lines) ambapo tulikuwa tunafanya battles za kuandika on the spot yaani moja kwa moja ndani ya group hilo pale Facebook.
Huu ndio ulikua mwanzo wangu kuchukulia rap serious na kutaka kurekodi. Kundi la PCL lilikuwa na wasanii wakali sana na tukakubaliana kwenye kundi letu pale Facebook kuwa lazima tu rekodi kazi pamoja na hapo ndio tukaingia studio mara ya kwanza kama kundi.
Mimi naweza sema kuwa Mc Mutant ndio alikuwa mentor/mshauri mkuu kwenye kundi hili. Kwa kukutana mara ya kanza rasmi ndipo kulituwezesha sisi kufahamiana sote na kwenye kundi alikuwemo Brax Commissioner, Illicit, Magode, Wordz, Maneno, Adesola(Nigeria), Wulfpac(Nigeria), Rhabid Dawg, Sicknature, Tolua (Australia) yaani orodha ya ma emcee ni ndefu kusema kweli.
Session ya kwanza studio ilikuwa 2012 na tulifanya ngoma kwa James ElShado 32 Recordz, Dandora na ngoma tukaiita Shida na wimbo ulikuwa na ma emcee wafuatao; Magode, Mc Farrakan, Wordz, P-Shizo, Maneno, G-blac Babu Wa Nai, MC Mutant, na Kitusewer.
Hapa ndipo safari yangu ya kurekodi mziki wa Hip Hop ilipoanzia rasmi. Tulifanikiwa kutoa albam iliyoitwa Safari Ya Kitengela kama kikundi cha PCK kati ya 2015 hadi 2016. Pia nilifanikiwa kuhusishwa kwenye miradi kadhaa ya ma emcee wengine kama vile Mahat Mabangi – The Untold Story ya Dabliu na Magode, Azania Na Wanawe ya Fikrah Teule pamoja na EP ya Okysde iitwayo Deliver The Package (DTP) No Excuses ambapo nilishirikishwa kwa wimbo unaoitwa Tuko Macho.
Albam ya Safari ya Kitengela ilikuwa produced by Adel Chigga wa Higher Linxx Records. Pia kando na rap battles ambazo zilinisaidia kukua kama rapper, niliweza kufanya kazi pia na Queen Nefertiti anayemiliki The Crown Global Management ambapo tulifanya cyphers au ukipenda vinasa kadhaa ambapo kazi kadhaa zilirekodiwa pale Batoz Music.
Kuna miradi kibao ambayo natarajia kuiachia hivi karibuni kando na miradi niliyoshirikishwa na wasanii wengine.
Umeshatoa albam ngapi hadi sasa na Mambo Kavu EP ni wangapi?
Mambo Kavu EP ndio mradi wangu wa kwanza ila albam iliyo rekodiwa chini ya usimamizi wa Mambo Makes Music label inatarajiwa kuwa sokoni hivi karibuni
EP yako Mambo Kavu ilitoka lini?
Mambo Kavu iliachiwa rasmi tarehe 7 July 2020.
Mradi huu uliundwa na ma producer gani kwenye studio zipi na pia Mixing and mastering nani alifanya?
Mradi huu uliundwa na producer Mambo Makes Music ambaye alifanya mixing na mastering kwa studio yake ya Mambo Makes Music ambapo EP nzima ili redokiwa
Maudhui ya mradi huu ni yapi?
Mradi unaitwa Mambo Kavu kwa sababu unahusisha Mambo Makes Music na mimi Cafu Da Truth. Mambo Kavu sio Mambo Cafu. Maudhui ya mradi huu yanazungukia zile changamoto za unyanyasaji kwenye jamii yetu inayotuzunguka na sanasana yale maonevu yaliyofanyika wakati wa janga la Uviko.
Niliona kuna ulazima wa kuweka rekodi ya changamoto tulizopitia wakati wa hili janga la Corona kwani mimi binafsi nilidhurika moja kwa moja na janga hili baada ya biashara na mipango yangu kimziki kuharibika sana.
Kando na changamoto kwenye mziki mimi pia nilipoteza kazi na hali yangu kiuchumi ikawa mbaya sana. Kwa hiyo Mambo Kavu kwa kimombo unaweza iita Zeitgest ya Corona inaangazia unyama wa polisi dhidi ya wananchi, ufujaji wa pesa, ufisadi wa hela zilizotengwa kukabiliana na janga hili na hela zozote za uma sana sana kipindi cha janga la Uviko 19.

Mambo Kavu EP
Mambo Makes Music, ilikuaje mkafanya naye mradi huu?
Mambo Makes Music tulijuana na yeye kupitia Zebbyblacks ambaye ni theluthi moja kundi la Unit 1678, mimi tukiwa na Cosy The Main Man.
Mambo Makes Music pia ni rafiki yangu tumejuana kwa mda sasa , na sana resonate poa sana na yeye kimziki. Kando na hilo studio yake inapatikana mitaa ninayo tokea na wakati wa Uviko 19 nilipata wazo la kuandaa mradi wangu na wakati tukiuunda tulipata mda pia wa kurekodi mradi wa kundi letu la Unit 1678.
Mradi ambao tulikuwa tumenuia kuufanya na Mambo Makes Music ilikuwa ni albam ila tukasitisha mpango wa kuunda albam na tukaamua kuunda EP kwanza kwa sababu tuliona kuna umuhimu wa kuwepo stakabadhi yenye rekodi au kumbukumbu ya mambo yaliofanyika wakati wa janga la Corona huko Kibera kwani tulitupiwa tear gas baada ya serikali kuanza curfews.
Tuliona badala ya kukaa ndani tu tukaamua kuwa wabunifu na tukaanza kutengeneza ngoma ma Mambo au Dr. Dre kama tunavyopenda kumuita Mambo kwa jina lake la utani kwani yeye ni muunda midundo mzuri sana. Yeye pia alikua na motisha sana na mradi huu tuliweza kufanya ndani ya mwezi mmoja kwani mistari yangu niliiandika na kuiriekodi ndani ya wiki moja na kumuacha Mambo afanye sehemu yake.
Mambo Makes Music kando na kuwa muunda midundo ni rapper na muimbaji mzuri sana kwa hiyo alinipa viitikio vizuri sana kwenye mradi huo kando na kuchana beti moja kwenye ngoma inayoitwa Assume ambayo inapendwa na mashabiki kibao.
Nani kama emcee aliku inspire ki mziki, nje na ndani ya Kenya?
Inspiration yangu ya mziki naeza sema kwanza kabisa ilianzia nyumbani kwani mama yangu alikuwa muimbaji wa kwaya ambayo ilienda kushiriki mashindano ya choir kule Hungary na wakawa wa kwanza na kupewa zawadi ya kwaya bora. Hivyo basi mizizi ya miziki ilianzia nyumbani. Baba yangu nae pia alikua shabiki mkubwa sana wa Bob Marley na alipenda sana kuskia wanamziki wa Kikuyu.
Kando na wazazi kaka yangu Maish aliweza kuni introduce kwa mziki wa Reggae ilhali mwingine kwa jina Sam alinipa support kubwa sana katika safari yangu ya mziki kando na kunipatia albam kibao za Hip Hop. Huyu Sam tulifanya naye kazi kwenye ile albam ya Safari Ya Kitengela. Sam ni mshairi mzuri sana ambae amekua Slam Africa.
Kwa upande wa wasanii walio ni inspire ni ma emcee wote wa kundi nililochipukia la PCL pamoja na Kitu Sewer, Ukoo Flani, Kalamashaka, K South Flava. Kimataifa kuna Nas, Masta Ace, Wu Tang Clan na wengine wengi.
Kando na mziki unajihusisha ni kipi kingine?
Kando na muziki mimi pia ni mtaalam wa Health Records Management ambaye nahusika na Patient Monitoring databases na chochote kinachohusiana na data sana sana analysis (uchambuzi na ukusanyaji wa taarifa) pamoja na kuripoti taarifa zilizokusanywa.
Pia nimesomea uuzaji pamoja na cozi ya Huduma Kwa Wateja (Customer Service and Client Engagement/Management). Si unaona vile nina bonge la CV, leta kazi kaka. Oh kando na haya yote mimi pia ni bonge la hawker/machine anayeuza vyombo vya nyumbani.
Pia mimi nina brand yangu ya Mambo Kavu ambapo nauza T shirt pamoja na hoodies.
Tueleze kidogo kuhusu art work ya mradi?
Hii ungekosa kuniuliza lazima ningejiuliza na kujijibu kwenye haya mahojiano yetu G! Hahaha. Kwanza kabisa hongera kwa Seth Skchr kwa kazi nzuri aliyoifanya kwani aliichora kama maoni yangu yalivyokuwa ila aliboresha maoni yangu zaidi ya nilivyotarajia, ni masterclass memoir. Shoutout kwake kwa kulifanisha hili kwani mchoro wenyewe ni muktasari wa EP.
Mbukinyaa kama single ilibeba albam yote alitoa mfano na kuhusisha Basi La Mapinduzi kama unavyoona kwenye mchoro wa jalada kua basi linaitwa Revolution High. Pia maandishi kwenye kuta, barakoa pamoja na vitakasa mikono (sanitizer) barabarani vinakupatia picha kuwa EP hii ina maudhui gani.
Kama ujuavyo michoro ya jalada ya albam ni kitu kikubwa sana kwenye utamaduni wa Hip Hop na Seth alilifanikisha hili mara moja!
Pia naona unajiita Tall Rap Midget, tueleze kidogo kuhusu hili
Tall Rap Midget ni a.k.a yangu nyingine inayoonesha uwezo wangu kwenye kinasa. Tall Rap Midget ndiye anakuonesha ujuzi na uwezo wangu kando na “artivism” au sanaa yangu ya uharakati. Tall Rap Midget ni msee mfupi na mistari mirefu. (Kama vile Nala Mzalendo anavyojiita Mtu Mfupi Mistari Mirefu – nyongeza ya mwandishi). Bars G!! Bars, yaani ni nondo juu ya nondo!
Tutarajie nini toka kwako hivi karibuni?
Albam yangu ya kwanza iko njiani kwani ishakamilika imebaki kuiachia tu. Pia nimefanya collabo ambazo hazijatoka kwa mradi flani wa ninja wangu Liggato ambapo nilifanya mziki aina ya Drill kwa mara ya kwanza.
Kuna nyimbo kadhaa kwenye mradi wa Shynobi na Tgun, 3rd Person Narration Mixtape na Lyrical Fridays kule Batoz Music na pia mradi ambao haujaingia soko wa Global Managemt wa Who Owns The Crown. Bado kuna miradi kibao ambayo natazamia kufanya pia.
Je mziki hususan Hip Hop unalipa?
Mziki wa Hip Hop unalipa. Inawezekana sijatengeneza pesa kibao toka kwa mziki wangu ila usisahau mimi bado ndio nina anza hivyo basi lazima nipatie kipaji changu mda ili nizidi kukua zaidi na nilipo kwa sasa kwani naelewa ninachokifanya japokua mambo ni magumu. Cha msingi ni kulenga maendeleo ya utu wangu binafsi kisha watu wakinikubali mambo mengine yatajipa yenyewe.
Watu husema Hip Hop ni mziki wa kihuni, unaliongeleaje hili?
Emcee/mwalimu KRS One alisema hivi, “Kama Hip Hop ina uwezo wa kuharibu akili (ya mtu au watu) basi pia ina uwezo wa kuinua uplift akili hizo hizo pia”.
Ulijiskiaje wakati uliposhinda the Unkut award kwa kwa sababu ya ya EP yako Mambo Kavu?
Tuzo ya Unkut ya Hip Hop ilikuwa ya kwanza kwangu. Na kuwa nilitunukiwa tuzo hii kwa ajili ya mradi wangu wa kwanza ninacho weza kusema ni kuwa iliniwachia kumbukumbu nzuri sana. Kwa wale wote walionipigia kura kwa wingi napenda kuwashukuru sana kwa upendo walionionesha.
Pia natoa shoutout kwa waandaaji wa tuzo hii kama vile Ruby, HBR na timu yote ya Unkut. Asanteni sana pia mashabiki wangu na familia yangu kwa support yenu kubwa.
Hali ya Hip Hop nchini Kenya ipoje kwa sasa? Je ma emcee toka pande zingine za Kenya wanasikika kando na wale wa Nairobi tu? Nakumbuka enzi hizo ili mwanamziki aweze kutoka ilikuwa analazimika atie kambi Nairobi.
Hip Hop ipo kiwango chake na ipo mahali inafaa kuwa kwani kwa sasa so na ni kila mtu aweke juhudi zake ili kuipeleka kwa viwango tofauti. Utofauti unakubalika na talanta huwa inaheshimika. Mimi naheshimu kila mtu anayefanya anacho kifanya kwani siku hizi upendo upo kila mahali na nimekuja kuona kuwa una uwezo wa kujifunza mengine kama utapatia wenzako maskio yako na ukawaskia pia.
Kwa upande wa majimbo au makundi ki mziki kitu ninacho weza kusema ni kuwa hali imeendelea kuwa bora kwani siku hizi kuna ma emcee kama Kaa La Moto, Fikrah(Teule), Ohms Law ambao wanaiwakilisha vyema Mombasa.
Pia kuna ma emcee kama Trabolee toka Nakuru, Muki Rai toka Kikuyu (Kiambu), Djungle pamoja na Tin Kais kutoka Thega(Thika) na wengine wengi. Watu wanaekelea kazi kutoka kokote kule walipo na kuweza kufikia kilele kwenye hii industry ya mziki kama ilivyokua hapo awali
Aminia kaka.
Ungependa kutuwacha na ushauri au neno/maneno gani ya mwisho?
Uko hapa kwa sababu unaleta kitu tofauti, endelea kufanya yako, endelea kuonesha upendo, kwani ni watu ambao wana thamani zaidi kwani wao ndio wana uwezo wa kufanya mambo yatokee. Kila kitu kinaishi kwa sababu ya watu. Kwa hivyo tunathamini kila mtu kwa jukumu analolifanya, iwe ni mtu mbaya/adui au hata shujaa, wote ni muhimu kwa maisha kuweza kuwa kama yalivyo.
Unapatikana wapi kwenye mitandao ya kijamii?
Niko available platform zote YouTube, Twitter, Spotify, Audiomack, Mookh, SoundCloud, Deezer, Facebook, IG, Bandcamp etc zote Kwa hii link;