Careem

Emcee Careem alianza kuskika angazangu mwaka jana alipoachia ngoma yake ya kwanza na iliyomtambulisha kwa mashabiki wengi, Nane Kumi Na Sita. Jamaa huyu ambae anatokea kule mitaa ya Kisauni, Mombasa nchini Kenya mwishoni mwa mwaka jana alirudi studio tena nakuachia EP yake ya kwanza Talent Ipo.

Leo tumepata fursa ya kuongea nae ili tuweze kumfahamu yeye, sanaa yake na hali ya Utamaduni wa Hip Hop kule Mombasa.

Careem tueleze kidogo kuhusu historia yako, ulizaliwa wapi, ulisomea wapi, shule ya msingi, upili na baada ya hapo uliendelea hadi wapi ki masomo? Utoto wako ulikuaje?

Nilizaliwa Mombasa ya Kisauni mwaka 1988. Nilisoma shule ya msingi ambayo ilikua inaitwa Burhaniya Primary School (iliyopo Nyali Bridge) kwa sasa inaitwa Bloomberg, ipo karibu na M.M Shah Primary School. Nilipofika darasa la tano nikabadili shule ya msingi nikaenda soma shule inaitwa Fat-hul Adhim iliyoko Bakarani huko ndo nilimaliza masomo yangu ya msingi KCPE.

Shule ya upili nilisoma Sheikh Khalifa Bin Zayed, KCSE graduate 2007. Baada ya hapo nikasoma Chuo Kikuu Masinde Muliro University 2010-2015 Bachelor in Social Science- field of disaster management (humanitarian assistance).

Utotoni mwangu nilikua kijana mtulivu. Nilikulia mazingira ya familia mzuri ya kiarabu. Mamangu ni Mganda. Nilikua nikipenda kuskiza muziki tokea utotoni. Nakumbuka shule ya msingi Burhaniya nikijiunga kwenye miondoko kuimba kwaya siku za Students Talent Day. Nakumbuka nikipenda somo la music and arts shuleni na hil lilichangia kunitia hamu ya muziki.

Kiujumla utotoni nilikua nikusoma sana na nilikua kijana mwerevu shuleni nakumbuka shule upili nilikua mwanafunzi bora kwenye somo la kingereza kule Kisauni kwenye mtihani wa KCPE 2003.

Hip Hop nilikutana nayo nilipokua shule ya msingi mara yangu ya kwanza kusikia muziki wa Hip Hop ni kwa matatu za abiria na hapo basi nilipenda hiyo miondoko yake. Enzi hizo ngoma zilizochezwa sana zilikua ni za kina Tupac, Biggie Snoop Dogg, Dr.Dre, Ice Cube, Eminem nk. Nikataka jua zaidi kuhusu hizi nyimbo na njia niliyotumia ilikua kupitia marafiki shule ya msingi. Hivyo ndo Hip Hop iliniingia damuni.

Mbona ukaamua kujiita Careem kama jina lako la kisanii? Jina linamaanisha nini na lilikujaje?

Niliamua tu kutumia jina langu la kisanii liwe tu jina langu hivyo tu "Careem" sikutaka kujipatia jina tofauti kama wasanii wengine.

Jina Careem linamaanisha mtu mkarimu. Niliitoa tu kwa jina langu Abdul Karim (mtumwa wa mkarimu) Careem kiisalmu/kiarabu nikatika majina ya Mungu Al Karim (aliye mkarimu).

Tueleze kuhusu historia yako ya muziki, ulianzaje kupenda muziki wa rap na ulikuzaje kipaji hadi ukaanza kuandika na kuchana mistari yako mwenyewe?

Muziki nilianza nikiwa shule ya msingi nikijiunga kwenye siku za Talent Show kwenye kwaya nikiwa Burhaniya Primary School. Nilikua nikipenda soma vitabu vya mashairi ambavyo nilikua na nunuliwa na mama yangu.

Na msukumo pia nilipata zaidi baada ya kusikia ngoma za Hip Hop kwenye hizi hizi matatu za abiria ambazo zilikua zikipiga muziki wa Hip Hop, hapo ndipo nilipenda  hizo ala zake na mashairi yake. Nikataka kuijua zaidi nikaijua kupitia marafiki shuleni na runinga pia ilichangia pakubwa.

Baada ya hapo nilipojiunga shule upili nikaanza jifunza kuandika mashairi mwenyewe ya Hip Hop, nilikua nikifanya tu kwa siri nikichora mashairi nikijifungia chumbani na ku rap nikiwasoma wasanii tofauti jinsi wanavyo andika na kurap kama vile kina Eminem ,Talib Kweli, Common, Black Thought, Vigeti, Nikki Mbishi, Fid Q hizi ni enzi za 2003 hadi 2010.

Zangu zilikua nikuandika kwa vitabu na kurap kwa room yangu home tu.

Nilipo jiunga chuo kikuu 2010-2015 ndo nikapata ule msingi mzuri wa kujitambulisha. Chuo kikuu ni mahali nilikutana na vijana ambao walikua ni wasanii, ma rapper nikawa na jiunga kwenye cypher za Hip Hop kama zoezi, rap battles, hii lilinijenga  sana nikaipenda hii sanaa na kujihisi niko huru sana sababu shule ya msingi na upili sikuwahi pata wala kuona vijana ambao ni wasanii na waliokua tu wanapenda mziki tu.

Niliendelea na masomo hadi ku hetimu nikaeka nia siku moja nitakuja kujiunga na sanaa na Hip Hop.

Ulipokua unaanza ni wasanii gani Mombasa, Kenya Africa Mashariki na mamtoni waliokupa hamasa ya kuchana?

Wasanii walinipa hamasa ni kutoka Mombasa, Cannibal, Afrika Mashariki, Fiq Q na Nikki Mbishi ilahali

Mamton, Eminem, Common, Talib Kweli, Chamillionaire, Big L, Wretch 32.

Vipi hali ya Hip Hop Mombasa kwa sasa? Je utamaduni unakubalika na wasanii wanaachia kazi? Enzi hizo ili msanii wa Mombasa aweze kuonekana alikua analazimika kufunga virago vyake na kuhamia Nairobi. Hali ipoje kwa sasa?

Hali ya Hip Hop Mombasa kwa maoni yangu ni kua ipo na uchangamfu na inakua kwa kasi. Utamaduni umekubalika, wasanii wanajitahidi kuachia kazi, ni kitu ninacho kishuhudia kwa wingi.

Kwa moani yangu siku hizi si lazima ufunge virago kwenda kanairo😀... kuwepo kwa mtandao unasaidia wasanii wengi kuonekana Mombasa kwa kupitia mitandao ya kijamii na pia YouTube. Mimi ni mfano mzuri nimejulikana na wasikilizaji kupitia mtandao hadi wasanii wa underground Nairobi wananijua kupitia mitandao ya kijamii na YouTube. Muziki wangu wa kwanza hit single Nane Kumi Na Sita ilifika hadi Nairobi Hot 96 ikachezwa na DJ Jessy kwa kipindi cha wiki mbili. Icon Radio, Bahari FM wanacheza muziki wangu na wamenijua tu mtandaoni. Ukitoa muziki mzuri utaskika tu mtandaoni kupitia platform za muziki bila wasiwasi na muziki wako hautakua na pingamizi.

Changamoto zipo kwenye kila aina ya kazi, zako ni zipi na unakabiliana nazo kivipi?

Nimekua nikitumia mitandao kutangaza biashara zangu changamoto mwanzo ulikua mgumu kwa sababu sikua na mtaji mzuri wakununua vifaa husika na pia vifaa kwa Tanzania vilikua adimu ila niilitumia uwezo wangu na vifa nilivyo kua navyo kuhakikisha kazi zinakua vizuri. Kidogo kidogo nilianza kupata wateja mitandaoni ingawa wengi hawakuniamini kwa sababu mitandao imekua na matapeli wengi so nilihakikisha na weka na video nikiwa nachor. Kuna watu walianza kuniamini na kuvutiwa na kazi na hawakujali umbali wa mkoa au nchi. Kila mteja nilihakikasha kazi yake ameifurahia. Kuptia mmoja mmoja mteja nilipata connection za marafiki zake.

Careem umebobea kutokana na mistari yako ya kijanja na kama unavyosemaga, "Hapa Bars Tu!” Nini kinacho kuhamasisha kuandika mistari yako?

Mistari ya kijanja 😀 mimi zaidi ya mjanja ni mwerevu haswa! Hapa Bars Tu, nilianza itumia nilipoamua kuingia kwenye ulingo wa Hip Hop, nilikaa chini kasema kitu gani kitanihamasisha nisianguke kimistari kiwe kinanikumbusha kua nafaa kua consistent ju kuna wasanii huanza vyema baaden ku flop. Ndo nikaamua kuja na hiyo slogan ya Hapa Bars Tu ambayo niliitoa kwa marehemu Magufuli ambae alikua anasema “Hapa Kazi Tu!” nikaiibadili ikawa "Hapa Bars Tu". Huo msemo hunipatia changamoto ya kuhakikisha hiyo mistari ninayo andika iwe ya hali ya juu na nisianguke kimistari huko mbeleni.

Kinacho ni hamasisha ni mazingira ninayo ishi, maisha ninayopitia na visa ninavyo viona na kusikia ndani ya mazingira yanayo nizunguka

Tueleze kuhusu kazi zako, mpaka sasa una miradi mingapi na inapatikana wapi?

Kwa sasa nina mixtape moja, Hapa Bars Tu Vol 1 na EP moja Talent Ipo yenye nyimbo tano.

Miradi hii ipo kwa platform zote YouTube, spotify apple music boomplay etc. Pia unaeza nunua mziki wangu kupitia careemmusic.hustlesasa.shop

Binafsi mimi nilianza kukuskia kwenye wimbo wako Nane Kumi Na Sita. Je wimbo huu kwako binafsi unaweze sema ndio ulikutambulisha kwa mashabiki wengine pia? Nane Kumi Na Sita ulikua na maana gani hapa?

Kweli kabisa Nane Kumi Na Sita ndio kitambulisho changu kwa sasa. Mashabiki zangu wengi walinijua kupitia huo wimbo. Je uta amini nikikwambia ndo wimbo wangu wa kwanza kutunga nilipoingia studio? Kwa hivyo mimi ni msanii aliye unda ngoma ya kwanza baada kuingia studio mara ya kwanza na ikawa hit!

Nane Kumi Na Sita ni ngoma niliyounda kuonesha ugwiji wangu wa kutunga mizani za Hip Hop (bars). Kujinaki, kiufupi kuonesha wasanii wa Hip Hop kua niko vizuri hadi kuzarau ma rapper ambao hawana mistari. Wasipochunga nachukua nafasi yao. Ujumbe upo tu kwa chorus ukiskiza.

Nane Kumi Na Sita ina maanisha (8 or 16 bars) yani nikiangusha 8 or 16 bars mistari lazma unipe heshima!

Ni watayarishi gani umefanikiwa kufanya nao kazi hadi sasa?

Nmefanya kazi na producer PMG na Musa Kiama na kijana mmoja alieko Nairobi, kijana yuko handakini anaitwa Kamaar, yeye ameniundia instrumental kibao, mtaziskia nikiendelea na muziki wangu.

Mtayarishaji amabae nimefanya nae kazi ni Musiq Jared amabae aliniona mtanadaoni Facebook na nina matumaini kutokea kwenye kazi zake za muziki anazozitayarisha sasa na mbeleni kwenye safari ya muziki.

Kati ya wasanii niliofanya kazi ni Monsta Monk, emcee amabae nakumbuka nikimfuatilia sana miaka ya 2015 na nilipenda miondoko yake sana na kufanya nae kazi ilikua ndoto. Natumia kufanya kazi na wasanii wengine wakubwa zaidi Kenya na Afrika Mashariki.

Careem na Mtayarishaji PMG (R.I.P)

Muziki unalipa kaka, au dawa yake ni kazi ndio uweze kufanikisha kwenye hii rap game?

Kulingana na msemo wa waliotutangulia, muziki unalipa. Kupitia kuuza muziki (nakala – ngumu na nyepesi) na kupiga shoo kwenye matamasha, ridhaa (endorsements) na ushirikiano. Kwangu mimi kwa sasa naona dalili za muziki kunilipa sababu naona wasikilizaji wakinunua muziki wangu kupitia tovuti ya Hustlesasa ila kwaasasa bado haujanilipa na kuniwezesha kujikimu kimaisha kutokana na! Kwa mda huu itabidi niweke juhudi zaidi ili nionekane zaidi ndo muziki uweze nilipa.

Umuhimu wa mitandao ya kijamii na streaming apps kwa sanaa yako unaizungumziaje? Je imekusaidia au unauzu sura tu?

Mitandao ya kijamii imenisaidia kuonekana, hapo siwezi kudanganya. Streaming apps ambayo imenitoa sana na kunifanya nionekane ni YouTube. Nane Kumi Na Sita ilisambaa vizuri pale YouTube hadi kufanikisha ngoma nilizotoa baadae kwenye EP pia kusambaa kwa kiasi kizuri.

Natumai muziki wangu pia utaonekana kwenye streaming apps tofauti bora, ni mikakati ya marketing tu.

Changamoto kubwa zinazo wasibu vijana wa Kisauni na Mombasa ki ujumla ni ukosefu wa ajira na utumiaji wa mihadarati. Wewe kama kijana na msanii unafanyaje kukabiliana na changamoto hizi na una ushauri gani kwa vijana wenzako?

Ajira na uraibu ndo changamoto kubwa Kisauni na Mombasa kiujumla. Suluhisho la ajira nikujitafutia ajira, jipe shuguli ikiwa huna ajira jitahidi uwe hata makanga/konda/mpiga debe wa matatu/daladala, kuna kazi ndogo ndogo nyingi za kufanya ambazo unaweza vumbua na ukapata mkate na maziwa wa kila siku na ukajilisha na kusaidia nyumbani.

Uraibu: nasaha yangu kwa vijana ni tujiepushe na janga hili tuangalie wale wanaoathirika na mihadarati, hali zao walivyo maisha yalivyowaharibikia. Tujiepushe na marafiki wasiokua na mwelekeo na vikao vya mihadarati.

Mwaka huu umeachia miradi gani na tutarajie nini kingine kutoka kwako pia?

Mwaka huu 2023 nimebahatika kufanya colabo kiasi jambo amabalo limenipa motisha kwani inaonesha wasanii wanaheshimu talanta yangu.

Mradi amabao nitaachia mwaka huu kabla ya Desemba kuisha ni mixtape yangu ya pili Hapa Bars Tu Vol 2. Mradi huu utakua na freestyle kumi ambazo nitakua nachana mistari tu. Pia napanga kuachia ngoma mpya kwenye EP yangu ya pili.

"Mombasa twaja kali…" enzi hizo ndio walikua wanasemaga. Ma emcee na watayarishaji gani kutoka Mombasa tunaotakiwa kuwafuatilia kwa ukaribu kwani wanakuja kwa kasi ni akina nani?

Kweli sana msemo wa legendary Pharaoh umenikumbusha mbali. Rapper mkali Mombasa anaetarajiwa kufwatiliwa ni Katishanboy. Huyu kijana ni kati ya ma emcee wakali na wenye kipaji kikubwa hata ilibidi nipige kazi nae kazi ili kujipima uzito wangu ila ma emcee wako wengi wazuri wanajitahidi.

Tukimalizia gumzo letu, una ushauri gani kwa ma emcee chipukizi?

Ushauri wangu kwa ma emcee chipukizi ni kua mbunifu kwenye mistari yako na usiige msanii yoyote ki miondoko au hata kimistari. Kua wewe na acha kuingiza umagharibi mwingi ongea mambo yanayo tendeka ndani ya mazingira yako.

 Ungependa kuwagotea akina nani?

Ningependa kuwagotea marafiki zangu walionipa motisha tokea siku ya kwanza kama kina Saddam Wangara, Mwakina, Moses Omondi, Teddy, Jay Kalu, watu wangu wa maskani niliyo kulia Bakarani Kanu.

Unapatika wapi kwenye mitandao ya kijamii?

Facebook: careemke
Instagram: careem__ke
Twitter: @careemke

Neno la mwisho?

Tarajieni muziki mizuri kutoka kwangu madamu nipo hai. Hip Hop iko safe na Careem, Coast kiujumla.

Shukran sana kaka Careem kwa mda wako!

Shukran kaka, Micshariki (Africa).