Msanii: D14
Kanda Mseto: The Kulture Mixtape
Tarehe iliyotoka: 17.01.2021
Nyimbo: 10
Wapiga midundo na ma producer: Dr. Luis, Man Fure, Ringle Beats
Studio: North Block Records, Lost Poets Production, GM Records
Hip hop ni aina ya muziki unaoelezea aina ya usanii na utamaduni uliotokana na jamii ya Wamarekani Weusi na Walatino tokea miaka sabini mjini New York City, hasa katika kitongoji cha Bronx kule America.
Utamaduni huu umeenea duniani kote na kupendwa na watu wa mataifa mbali mbali bila kuzingatia rangi ya ngozi au jinsia. Utamaduni wa hip hop una nguzo tano tofauti moja wapo ikiwa ni uchanaji/uchenguaji.
Kupitia nguzo hii ya uchenguaji kule Arusha Tanzania D14 akapata fursa ya kutuonesha upendo wake juu ya utamaduni wa hip hop kwa kutuletea kanda mseto iitwayo “Kulture Mixtape” au kwa tafsiri ya Kiswahili (isiyo rasmi) ni, “Kanda Mseto ya Utamaduni”.
Deonatus Eliud Veneti ambaye ni mzaliwa wa Arusha alizaliwa tarehe 14 mwezi wa 4.
Jina lake lilipatikana kwa kuchukua herufi D toka kwa jina lake la kwanza Deonatus ilhali 14 ni tarehe aliowasili rasmi humu duniani hivyo kuanza kujiita D14.
Baada ya kuanza mziki mwaka 2008 kimchezo mchezo aliendelea kukuza kipaji hadi mwaka 2014 alipoamua kuingia rasmi kwenye fani ya hip hop.
Mwaka huu D14 aliachia rasmi mradi wake wa kwanza ambao ni kanda mseto ambayo ilikua na nia ya kuonesha jinsi kijana huyu alivyo na upendo na utamaduni wa Hip Hop.
Kanda mseto hii kando na kuonesha tu utamaduni wa hip hop ki ujumla pia inaonesha vile utamaduni huu umepenyeza hadi Oldadai Arusha ambayo ni mitaa anayowakilisha D14.
Na umakini, upendo na heshima ya D14 kwa utamaduni wa Hip Hop unaskika vizuri kwenye wimbo uitwao “Toka Zama” (Rap Ni...) akiwashirikisha D2, Sam na Luis. D14 anatupa mafunzo kidogo kuhusu historia ya hip hop wakati akisema,
“Kabla hujaanza rap jipange/
Usitambe, mguu sawa kiafande/
Bila Dj Kool Herc na Bambataa/
Sijui mngekuwa nani, fundi mwashi au muuza mkaa/
Toka kipindi tuna shine na logo/
Kabla hawa ma emcee dress code kuwa modo/
Kabla ya nyodo/
Hawajui rap ni global/
Rap si shobo/
Kabla ya Hasheem kuwa Dogo/”
Wimbo huu unaonesha vile D14 anathamini utamaduni wa hip hop kwani anatukumbusha enzi za akina Dj Kool Herc na Bambataa. Hapa anawapa fursa wana hip hop kwenda kuchimba vitabu vya historia ili kujifunza utamaduni wa hip hop na kujua chimbuko kabla ya “rap kua global”.
“Wrong Turn” ndio singo ya kwanza toka kwenye mradi huu. Ni singo yenye spidi kali iliyo mshirikisha emcee Toxic Man na mdundo kuundwa na Dr. Luis toka North Block. Dr. Luis anaonesha ubunifu wake pale anapooanisha picha iliyochorwa na ma emcee hawa na beat kama movie yenye jina la wimbo huu iitwayo Wrong Turn. Mashine za kukata mbao, kelele za wanaokatwa na milango inayojifunga inasikika unapoanza wimbo huu kuashiria picha la hatari ndio linaanza. Wrong Turn ni picha la kutisha na track hii pia ni ya kutisha wakisema ma emcee hawa wawili, “Cheki binadamu wanavyochinjwa kama kuku/Halafu damu yake inavyonyweka kama supu/”. Jitahidi kona utakayopiga isikupeleke walipo ma emcee hawa maana watakumaliza ki mistari.
“Afrika” iliyoundwa na Ringle Beats ni ombi la ma emcee D14 na D2 ambapo wanaenzi bara letu. D14 akitufungulia akisema,
“Tanzania, Kenya, Burundi mpaka Ethiopia/
Algeria na Somalia, Sudan huku Nigeria/
Afrika tusiachane, tuungane kila area/
Tutokomeze ujinga na magonjwa kama malaria/
Tunakuomba utusaidie eh Mola/
Utulinde, utuepushe na magonjwa kama Ebola/”
Nae D2 haachwi nyuma akisema,
“Na flow kwa mistari halisia/
Mweusi rangi yangu, Afrika asilia/
Tanzania nchi yangu kwa uchungu naililia/
Kwa uongozi huu, eeh Mola saidia/
Wanaharakati bora wengi tumewafukia/
Na sijui ni lini malengo tutafikia/”
Sauti za baba wa taifa la Afrika Kusini, Tanzania na Zimbabwe mahayati Nelson Mandela, Mwalimu Julius Nyerere na Robert Mugabe zinabariki mdundo huu.
Ma emcee kadhaa wanamtia moyo D14 kama vile AZ, Cannibus, Ice Cube, Colly Poison, Chindo Man, Vigeti na Mnazi. Kwenye singo iitwayo “What They Want” inayonikumbushia singo iyendayo kwa jina hili pia ya DMX, emcee D14 anapata fusra ya kujipima nguvu ki mistari na moja wa ma emcee wakongwe wa hip hop toka mamtoni, AZ.
“Shika Moja” ni singo moja mzuka ukiiskia tu utaskia mkono wa Dr. Luis kwenye wimbo huu aliyo washirikisha ma emcee Frema MC & Gborn pamoja na Joe Mic toka kundi la RPGs. Singo hii imenikumbusha ule wimbo wa “Chagua Moja” wa Fid Q au nyimbo ya Jay Moe iitwayo “Mvua na Jua”. Mistari yenye ucheshi inaskika,
“Tumia kipaji/Au wacha miguu wazi/”
Au pia wakisema,
“Chagua moja kati ya sembe au donna/
Mara unataka Jeje mara kesho Capadonna/”
Wimbo huu umejaa madini kibao ya kukufanya utafakari kuhusu maamuzi yako ya kila siku. Chagua moja kwani mtaka vyote hukosa vyote.
Nyimbo nyingine zilizosimama ni kama “Majukumu” akiwa na Ollachuga pamoja na emcee/producer De La P aliyekipiga kinanda murua huku kiitiko kikisema,
“Huku mitaa life bado gumu/
Watu wanakufaa njaa, nani wakumlaumu? /
Wengine wanajiua, si vyema kujihukumu/
Wee zidi kuomba dua, pambana na majukumu/”
Pia “Tunainuka” akiwa na Tejo Clan ni track nzuri sana inayoonesha vile ma emcee hawa wa A-Town wana habari ya mambo yanayoendelea duniani wakisema,
“Kaa mbali na sisi kabisa/
Tukiamshaga vagi BBC itaskika/
Ni mauji ya kimbali si KE, Garissa/”
“No Matter” ni track inayotufungia mradi na mistari ya kijanja ya D14 inaonekana pale anaposema,
“Na still tuna hustle hizi jasho hazipo silent/
Watu wengi wanasifika kwa promo na si talent/” au pale anaposema,
“Ujumbe unapotea kwa kasi, hakuna cha maana/
Zinazopewa promo, “Nikikupea, Utawezana? / “
Hili ni dongo linaloelekezwa si tu kwa Femi One toka Kenya bali kwa ma promoter na ma DJ na redio zinazopatia promo nyimbo mbovu ma emcee wenye mistari ya kitoto kama anavyosema Toxic Man pia,
“Ingia chocho jizame kwenye kidocho/
Fungua macho nikupe mapochopocho/
Wakiandika vesi wanaandika makorokocho/
Tena vina vyepesi na mashairi mdosho/”
Mixtape hii inaonesha vile D14 kaamua kuchukulia kazi yake ya kwanza kubwa kwa uzito unao takikana. Kila wimbo una lengo na mistari pamoja na mdundo linafanikisha nia ya D14. Ma emcee wote na ma producer pia walikua juu ki uandishi na kwa upande wa kuunda midundo. Kanda Mseto hii kwa kweli ni Kulture yaani Utamaduni wa Hip Hop, na utamaduni huu pia unapatikana Arachuga. Kama Tatizo Ni Dollar basi ukiwekeza kwenye mradi huu utapata thamani ya pesa zako.
Tunatarajia album ya D14 sasa tutamuona akisimama mwenyewe kwa asilimia kubwa bila ya kukaribisha ma emcee wengine wengi kama alivyofanya kwenye nyimbo zote za kanda mseto hii. Hii inakua changamoto kwa mtu ambae hajawai kumskia D14 kufahamu sauti yake na kuitofautisha na sauti za ma emcee wengine.