Dambwe La Hip Hop

Dambwe La Hip Hop ni kundi la emcees/wanaharakati wanaotokea Dar Es Salaam Tanzania. Ma emcee hawa ambao pia ni waandishi na wajasiriamali wamekubalika sana handakini mwa Tanzania kutokana na jumbe zao zinazoongelea uhalisia wa maisha yetu ya kila siku.

Karibuni tuweze kuwafahamu vijana hawa wanaotumia kinasa, kalamu, karatasi na midundo ya boombap kuelimisha, kurekebisha na kuburudisha jamii.

Dambwe La Hip Hop, Jamii Kwanza!

Karibu sana kaka Element. Kwanza tuanze kwa kukufahamu wewe Element. Unaitwaje rasmi, unatokea wapi na unajihusisha na nini?

Kwanza kabisa kwa majina rasmi mm naitwa John Martin Njau natokea Dar Es Salaam (Mbagala) najihusisha na ujenzi ...

Dambwe La Hip Hop, kundi lilianza lini? Kwanza jina la kundi lilikujaje, lina maana gani na mpo wangapi kwenye kundi hili, wanaitwaje majina yao ya kisanii pamoja na majina yao rasmi?

Dambwe La Hip Hop lilianza mwanzoni mwa mwaka 2014 ambapo kabla ya mwaka huo lilikuwa likifanya shughuli zake pasipo kurasimishwa.

Kuhusu jina, wakati wa mijadala mbalimbali ya kutafuta jina litakalo beba maana halisi ya muungano wetu, ndugu yetu Zebabe aliweza kutoa jina hilo na likapitishwa kwenye vikao vya Dambwe.

Dambwe ni neno la Kiswahili lenye maana ya pahali watu hukutana na kufanya jambo la aina moja iwe ni biashara, sanaa, siasa na kadhalika.

Dambwe lilianza na emcees 15 ila kutokana na majukumu, malengo na mitazamo limebaki na emcees 8 ambao ni;

- Mwinja The Son (Hassan Mwinja)
- Anosang (Anord Sanga)
- Sir General (Philipo Kigombezi)
- Element (John Njau)
- Nyenzo Kiranja (Justin Mussa Kazungu)
- M1_Dambwekazi (Omary Oxzavery)
- Maalim Ponda (Salum Ponda)
- Ndevu Emcee (Christopher Ivan)

Dambwe La Hip Hop

Malengo ya DLH ni yapi?

Malengo na mitazamo yetu kiujumla yamejikita kwenye kuikomboa jamii dhidi ya ujinga, maradhi na umasikini na sasa tupo kwenye mchakato wa kusajili NGO itakayo deal na mambo ya kijamiii.

Ni akina nani waliwa inspire hapa nyumbani na nje ya nchi inapokuja kwa utamaduni wa Hip Hop?

Ndani ni makundi kama HBC, X PLASTAZ (M.A.P Father Nelly). Nje ni makundi kama WU TANG CLAN na NWA. Kiukweli sisi huvutiwa na makundi yanayofanya mziki wa harakati kwenye kuikomboa jamii kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine...

Mpaka sasa DLH ninafahamu mna miradi minne. Miradi yenyewe inaitwaje na ilitoka lini?

Mradi wa Macho Ni Ngumu Kuona (album) ulitoka 2016
Mradi wa Usingizi Kulala Kifo EP ulitoka mwaka 2018
Mradi wa Risasi 8 Za Moto Mixtape umetoka 2022
Mradi wa Macho Ni Ngumu Kuona Kitabu kiliandikwa 2016 kikatoka 2022.

Kando na miradi hii kuna kitabu (Macho Ni Ngumu Kuona) mlikuwa mnapatia mashabiki wenu pale walipokuwa wananunua mradi wenu wa hivi karibuni Risasi Nane Za Moto. Tueleze kidogo kuhusu kitabu hiki na mbona mliamua kuwabariki mashabiki na kitabu hiki?

Kitabu cha Macho Ni Ngumu Kuona kiliandikwa 2016 ambapo chachu ilikuwa ni album iliyokwenda kwa jina hilo hilo na vilitegemewa vingetoka pamoja na album hiyo ila mambo hayakwenda kama tulivyopanga.

Kila wimbo uliopo kwenye album ni kurasa ya kitabu iliyopo kwenye kitabu cha Macho Ni Ngumu Kuona ambapo tumeelezea kwa upana zaidi juu ya maarifa na dhima ya jumbe kwenye kila wimbo uliokua kwenye album.

Hebu tuongee kuhusu mradi wenu classic Macho Ni Ngumu Kuona. Huu mradi ulikujaje na mlifanikisha vipi kuandaa mradi wa kudumu hivi?

Hip Hop ina jicho pana sana na tulitumia jicho hilo kutazama mambo yanayoendelea kwenye jamii zetu zinazotuzunguka na kuweza kuyazungumzia. Ilituchukua mwaka mzima kuweza kuandika na kuandaa production ya kila wimbo sambamba na documentary inayokwenda kwa jina hilo hilo. Ni mradi uliokuwa umegawanyika sehemu 3 ambazo ni album, kitabu, documentary. Salute sana kwa Troo Monk mkurugenzi wa Digg Down Records kwa kushirikiana kwenye kila jambo na hatua mpaka kufanikisha mradi huo.

Dambwe La Hip Hop naona mmeweka kazi kidogo sana kwenye hizi digital platform hususan Mdundo na YouTube. Mbona mmekuwa wazito wa kukumbatia hizi mbinu mpya za kusambaza muziki. Dukuduku linaletwa na nini?

Hakuna dukuduku la kutukwamisha ila zaidi ni kuendelea kujifunza njia sahihi na salama za kutengeneza fedha na kuwafikia mashabiki na walengwa kwa ujumla kupitia njia hizi za kidigitali.

DLH mmesajiliwa Digg Down Records maana naona mmepiga kazi kibao pale. Pia nimeona mna chemistry noma sana na watayarishaji waliopo pale, hapa nawazungumzia akia Troo Funk Monk, De La Funk na Abby MP. Hili unalizungumziaje?

Yes Dambwe La Hip Hop limeanza kufanya kazi na Digg Down Records toka bado Digg Down iko kwenye fikra za mkurugenzi Troo, mpaka baada ya kufikia hatua ya ufunguzi wa studio rasmi. Na wakati wote huu umetufanya kua na chemistry nzuri ya kimawazo, malengo na hata utendaji kazi kwa ujumla.

Wakati nikipiga utafiti kuhusu DLH nilikutana na ngoma flani mlipiga na Aslay ambaye enzi hizo alikuwa Mkubwa Na Wanawe. Mlikujaje mkafanya kazi na Aslay na je hamkuonekana kama mme acha misingi. Je kuna tatizo aliepo handaki kufanya kazi na msanii ambaye yupo mainstream?

Kazi na Aslay ilikuwa ni baraka toka kwa Mkubwa Fela baada ya kutembelea studio yake pale TemeKe tukiwa na diwani wa kata ya Kibonde Maji. Baada ya mizuka ya kutwa nzima producer Shriko alidundisha mdundo kisha kazi ikaandikwa na kufanyika siku hiyo hiyo. Aslay ni mkazi wa mbagala hivyo tukaiwakilisha 95 vyema.

Hakuna tatizo lolote mtu wa Hip-Hop kufanya kazi na muimbaji iwe yupo mainstream au laah. Since back in the days tumekuwa tukisikia ngoma kali za hip hop zikiwa na hook/chorus kali za waimbaji mbalimbali wa R&B.

SEKeTa (Sanaa Endelevu Kenya Tanzania), Element ulienda Kenya kuiwakilisha Tanzania kwenye kongamano hili. Nini maoni yako kuhusu shughuli ya aina hii na je wewe binafsi ulijifunza na kunufaika vipi?

Harakati za namna hii zinahitajika sana na umoja huu ukidumu basi sauti zinaweza kusikika vyema zaidi. Tuliwekewa mipaka tutawaliwe kirahisi kwa hiyo harakati za namna hii zinaweza ondosha mipaka (hata mipaka ya kifikra) na tukaweza kujitawala sisi pia.

DLH nimeona pia mna machata yenu. Je yanapatikana wapi na kwa bei gani?

Machata ya Dambwe yanapatikana dambweni na bei ni 20K hadi 25k. Kwa mahitaji ya bidhaa zetu pitia ukurasa wetu wa Instagram: @dambwelahiphop_dlh tu inbox mahitaji ya bidhaa unayohitaji kisha utapata muongozo zaidi.

Pia kama unahitaji bidhaa zetu kwa ajili ya biashara wasiliana nasi kupitia Barua Pepe: dambwekazi14@gmail.com.

Ule wimbo wenu classic Chumvi Ya Majuto, hivi ni kweli mlijaribu kwenda ikulu kumweleza kero zenu raisi au pang'ang'a tu? Nini kiliwazuia na mbona mwishowe mkaamua kuandika wimbo huu? Je ujumbe uliwafikia walengwa kupitia wimbo huu na kuna matokeo yoyote mlioyaona iwe ni hasi au chanya?

Chumvi Ya Majuto ni wimbo wenye matukio ya kweli kabisa yaliyowatokea ndugu zetu wakulima wa mashamba ya Amboni huko mkoani Tanga ambapo walidhulumiwa ardhi yao na kupewa muwekezaji aliyejenga kiwanda cha chumvi ambapo balozi wa chumvi ile alikuwa ni marehemu Majuto. Hivyo Dambwe La Hip Hop katika kutimiza malengo na dhamira yetu ya kuwa sauti ya jamii kwa kushirikiana na Jukwaa La Wajamaa Tanzania (JULAWATA) tulitembelea maeneo hayo na kupata maumivu halisi ya wananchi hao ambayo ndio yalizaa wimbo wa Chumvi Ya Majuto (chumvi iliyoleta majuto kwa wananchi/chumvi ilikuwa ikitangazwa na marehemu Majuto) ndio maana ya nyuma ya wimbo huo.

Je muziki huu umewanufaisha kwa njia yoyote ile au ni kazi ya kanisa?

Manufaa hutafsiriwa kwa nyanja tofauti na hutegemea malengo ya wanufaikaji wenyewe.

Kulingana na malengo yetu Dambwe La Hip Hop tumenufaika sana sana na aina ya upande tuliouchagua, ikiwa ni maendeleo ya jamiii, jamii yetu kuamini kuwa sisi ni kimbilio la kupigania changamoto zao na kadhalika pia manufaa mengine ni mauzo mbalimbali ya bidhaa na miradi yetu ambayo hutusaidia kuendesha shughuli mbalimbali na kusaidia watu wa mazingira magumu pasipo kuwatangaza wala kuwapiga picha.

Nini mashabiki watarajie kutoka DLH hivi karibuni?

Tupo kwenye maandalizi ya album yetu ya pili ikiambatana na miradi na ngoma nyingine kibao zinakuja. Zaidi kwenye shughuli zetu hizi za kijamiii tunaendelea na hatua za usajili wa NGO ya Dambwe La Hip Hop.

Zaidi ya yote pia tupo kwenye hatua za katikati za uandishi wa kitabu chetu cha pili kitakachokuwa kikifundisha misingi ya ujasiriamali na mauzo.

Ushauri wowote kwa chipukizi yoyote yule anayejaribu kutoka akitumia nguzo yoyote ile ya Hip Hop?

Watu husema watu hubeza ila ajifunze kusikia zaidi kuliko kusikiliza na kama kweli anahitaji basi anaweza kutimiza ndoto zake. Ndoto ni ndoto tu kama usipoamka na kuifanyia kazi.

Kipi cha mwisho ungependa kutuambia ambacho sijakuuliza?

Kumekuwa na evolution chafu ya muziki kwa sasa, hivyo sisi sote humu kama wasanii, ma emcees ma DJ, bboys, bgirls, na kadhalika, waandishi wa vitabu kuzingatia kwenye kila tunachosema, tunachoandika au kupiga tuikumbuke jamii inayoenda kusikiliza. Tunajua kuna vitu jamii inapenda kusikia na kuna vitu inapaswa kusikia hivyo tuhakikishe tunapeleka vinavyopaswa maana ndio vya muhimu zaidi.