Karne ya 200 ilipofika tamati ndio muda alioanza kuonekana mchanaji fulani wa kipekee aliye na ujuzi wa hali ya juu wa kuchana, mwenye mvuto flani na shauku yenye mvuto kama sumaku. Damu Ya Mashujaa aka The Bishop’s Son anapiga muziki wa hip hop na ni mtu makini sana inapokuja kwenye maswala ya utunzi kama walivyo waandaji wa muziki wa classical kutoka ughaibuni. Fani yake imejaa ndoto, hisia na maoni makali kuhusu jamii, uongozi, maadili na ukoloni mamboleo. Ukimskiza, anakusafirisha kwa njia ambazo usingedhani zinawezekana katika muziki wa Hip Hop. Mtunzi stadi wa hadithi na mashairi ya Waafrika mijini na vijijini.
Hivi juzi tulikaa nae ili kujadili kazi yake ya muziki na haswa nini kinachompa msukumo kupiga kazi vile anayofanya, filosofia na mwelekeo wake kimuziki na kimaisha.
Damu Ya Mashujaa, mbona ulijiita jina gumu hivi 😀, jina lilikujaje na linamaanisha nini?
Jina hili halikuwa langu la kwanza la usanii. Nilijipa jina la usanii la kwanza nikiwa shule ya upili pale nikajiita Yung Taekun. Wakati ule Lil Wayne alikuwa maarufu sana na jina hilo nilikuwa kama nimeiga kutoka kwake.
Kisha nikafanya maamuzi nikiwa shule hiyo ya upili kufanya conscious rap/ Hip Hop, nikiwa sana nimepewa msukumo na nyimbo za Kalamashaka na wenzao kutoka kundi la Ukoo Flani Mau Mau ambao pia umaarufu wao ulikuwa umefika kilele wakati huo. Nikabadili jina nikawa Mfalme Campari kutokana na majina yangu mawili ya kati. Munene humaanisha 'mfalme' kwa Kitharaka na Campari ilikuwa utohozi wa jina M'Chabari. Kwa wakati huu pia nilikuwa nimeanza uandishi wa hadithi na kutunga mashairi ya kisiasa ama revolutionary and resistance writing na nilihisi kwamba mwimbaji Mfalme Campari na malenga walikuwa watunzi wawili tofauti. Hivyo mwimbaji kawa Mfalme Campari aliye na jina la utunzi ama "pen name" ya Damu Ya Mashujaa. Kisha baadaye nilipoanza safari ya kuwa msanii wa kulipwa ama professional na nikaweka nguvu zaidi kwa muziki ndipo nikaamua kuwakutanisha hawa watunzi wawili kuwa Damu Ya Mashujaa.
Damu Ya Mashujaa linaashiria heshima kwa wote waliopigania na wanaopigania uhuru wa binadamu kwa jumla na wa waafrika kwa maalum. Wale mashujaa wa kisiasa kama Marcus Garvey, Dedan Kimathi, Kwame Nkrumah, Mwalimu Nyerere, Malcolm X, Che Guevara, Steve Biko; waandishi kama W.E.B Dubois, Walter Rodney, Ngugi wa Thiong'o, Chinua Achebe; na wengineo waliofanya juhudi mbali mbali, hata katika kuinua hadhi na elimu ya waafrika na uhifadhi wa tamaduni na mazingira kama vile Mama Wangari Maathai. Pia linaheshimu mashujaa wasanii wa uimbaji kama Bob Marley, Kalamashaka, Tupac Shakur na wengine wengi nisiowataja. Ni jina linaloashiria heshima kubwa, nia na ari ya kufuata mafunzo, maelezo na kielelezo chao ili kujikomboa kutoka kwa minyororo ya utumwa iliyotufunga hadi leo na kuwapa wengine mfano na matumaini. Mimi ni kizazi chao na ndio maana Damu Ya Mashujaa.
Tueleze kidogo historia ya maisha yako kidogo ili wasomaji wetu waweze kukufahamu vizuri; ulizaliwa wapi, mpo wangapi kwenye familia yenu na ulisomea shule gani za msingi na upili na baada ya hapa uliendelea hadi wapi?
Mimi ni mzaliwa na mpaka sasa ni mkaazi wa eneo la Tharaka katika kaunti ya Tharaka Nithi, nchini Kenya. Nilizaliwa kijiji cha Mukothima Ingawa nililelewa miji mbali mbali ya nchini Kenya kwa sababu, babangu mzazi amekuwa kasisi mishonari wa kikristo hivyo alihamishwa hamishwa katika shughuli zake za kazi.
Mimi ni mwanae wa pili. Kakangu mkubwa na pia mdogo wangu wote ni ma wakili. Pia nina dada mmoja kitinda mimba cha mamangu ambaye ni mtaalamu wa sayansi ya kompyuta.
Nilisomea shule ya msingi huko Tharaka na katika shule ya bweni upande wa Meru. Kisha upili nikaenda shule ya kitaifa inayoitwa Moi Forces Academy huko Nairobi.
Baada ya hapo nikajiunga na Chuo Kikuu Cha Kenyatta nilipohitimu na shahada ya Bachelor of Economics and Finance. Kisha nimesoma pia Masters ya Economics.
Tueleze historia yako ya muziki, uligunduaje una kipaji cha uchanaji na ulikikuzaje hadi hapa ulipofikia?
Safari yangu ya muziki ilianza utotoni. Mamangu ni mtunzi na mwimbaji wa nyimbo za dini, hivyo kipawa hiki kipo kwenye damu.
Kuna kakake babangu alipenda sana kuimba nyimbo na alinifunza kupiga gitaa na piano. niliiimba naye sana na akanifunza mengi kuhusu utunzi wa muziki. Alipenda sana Soul, RnB na Country Music. Kwa bahati mbaya huyu mjombangu aliaga dunia nikiwa umri wa miaka kumi na mmoja. Jina M'Chabari nililitoa kwake. Mimi humwona yeye kuwa ni babangu kimuziki. Katika baadhi ya nyimbo za kwanza nilitoa wimbo unaoitwa 'Karugu M.C' dedication kwake.
Kwa nini uliamua kwenda na Hip Hop na sio mahadhi mengine kwenye tasnia hii?
Kwanza kabisa, napenda aina zote za muziki. Napenda jazz, reggae, soul, funk, blues, rock and roll, rhumba, lingala...aina zote.
Hip Hop ilinivutia sana kwa sababu tatu; kwanza, mimi kama mshairi, nilipenda sana utunzi wa rhyme na technique na kutumia sauti yangu kama ala ya muziki. Ni njia ya kipekee sana ya utunzi na uimbaji na inatumia uzoefu na maarifa mengi sanasana kwenye zile mada huwa nalenga zaidi.
Pili, niliona kuwa Hip Hop ndio tasnia ambayo mtunzi ana uhuru wa kuandika maneno mengi hata takriban elfu moja ama zaidi kueleza dhana yake kwa wimbo mmoja. Hivyo niliona kwamba Hip Hop ingeweza kueleza kwa kina mawazo na maudhui niliyonuia kuangazia.
Tatu, utunzi wangu unaegemea sana kuwa militant kumaanisha kuna aggression na urgency fulani katika jumbe ninazoangazia ambazo ni Hip Hop tu inaweza kuipata vizuri. Hip Hop imekuwa kama mwavuli uliobeba aina zote za kujieleza kutoka kwa undani wa kiroho na ufahamu hadi hata kuelezea majigambo na vurugu. Ni aina ya sanaa inayo wawakilisha vyema wanaume wa kiafrika mweusi sana. Na hivyo ndivyo nilivyo.
Tueleze kuhusu mara yako ya kwanza kuingia studio, ilikuwa lini, ni wimbo gani uliunda na mapokezi ya ngoma hii yalikuwaje?
Mara ya kwanza niliingia studio mwaka wa 2009. Wakati ule Jerry Joe alikuwa na biashara fulani hapo Tom Mboya Street, Nairobi. Nikamwambia natamani kuingia studio akanipa contact ya Cedo. Wakati ule hakuwa maarufu kama sasa hivi. Alinipeleka studio fulani huko River Road. Nikarekodi wimbo nilouita Damn! ambao sikuuachia sababu nilihisi ulikuwa umewalenga waskilizaji waliopo mkondo mkuu sana. Tokea hapo nikawa nafanya tu spoken word hadi 2014. Mwaka huo wa 2014 nikafanya kazi na jamaa mwingine anaitwa Producer Cosmic. Wakati huo tuliimba na kakangu mdogo nikitumia jina la usanii la KiPot. Tukatoa nyimbo kadhaa baadhi yake kuna Heavy na Kuspit na Crown. Zenyewe ziko YouTube.
Kufikia 2018 ndio mwaka nilijituma sana kimuziki nikarekodi na kuachia EP mbili, ya kwanza inaitwa Lifted na ya pili inaitwa Lyrical Madness 1. Project hizi zilipokelewa vizuri na ndio zilinipa umaarufu handakini mwa Kenya (underground). Baadhi ya ngoma zilizovuma sana pale ni B.C na Ningekuwa na Doe ambao ulikuwa wimbo wangu wa kwanza kuchezwa kwenye radio za kitaifa.
Tupe historia kidogo kuhusu wakati uliokulia ki muziki, akina nani walikuvutia ndani na nje ya Kenya na sana hadi ukasema na mimi lazima nichane?
Nimekua nikiwa katika muziki na nikiwa karibu na watu walioupenda sana. Nikirudisha mawazo hadi utotoni Michael Jackson alinivutia sana. Nilipofika umri wa miaka kumi hivi niliskia nyimbo za Hip Hop kwenye radio zikanivutia sana. Niliowatambua sana kwa wakati huo ni akina Rakim, Tupac na Scarface. Tupac alikuwa keshafariki wakati nilipoanza kuusikiliza muziki wake kwa kina.
Hapa Kenya Kalamashaka ndio nashabikia zaidi kwenye hii fani. Nakumbuka vizuri sana Cool James na wimbo wake wa Sina Makosa. Baadaye nikiwa shule ya upili nilipenda sana nyimbo za Nas. Napenda sana kuwaskiza wasanii wanaotilia mkazo zaidi technique yao ya utunzi na uchanaji kama vile marehemu Wicky Mosh, Notorious BIG, Andre 3000 na MF DOOM.
Kutoka Tanzania nilivutiwa sana sana Ngwair, Fid Q na Mwana FA kwa kutaja wachache tu. Nikiwataja wote walionipa motisha ya kufanya hii kazi nitataja wasanii wote wa Hip Hop na Rap.
Kaka una bonge la catalogue…hebu tueleze kuhusu hii miradi yako yote; inaitwaje, ilitoka lini na kama ni EP, Mixtape au album.
Tangu nianze hii safari nilikuwa na focus ya kufanya kazi zilizo na upana. Hivyo nilinuia kufanya sana albums na EPs. Ilikuwa pia mbinu ya kujitambulisha vyema kwa wasikilizaji wa Hip Hop kwa kuwapa kazi nyingi. Nilitaka nioneshe uzoefu na pia uwezo wa kufanya Hip Hop na kuangazia mada na style mbali mbali za tasnia hiyo.
Nilitoa EP ya kwanza, Lifted, mnamo mwezi Juni 2018. Lifted ulikuwa mradi mwingine mzuka sana. Nilikuwa na kiu. Baadhi ya nyimbo ninazozipenda sana katika hii project ni B.C, Ningekuwa na Doe, Rivers na Do Dat. Baada ya hapo nilikuja na EP nyingine Agosti mwaka huo huo inayoitwa Lyrical Madness 1. Nayo pia ilikuwa na nyimbo kadhaa ambazo zilionesha ustadi wangu wa uandishi na uchanaji wa mistari kama vile Stolen, New Kings, Resurrection na Set My People Free.
Baada ya hapo tuliingia studio kuunda album yangu ya kwanza, Bishop’s Son ambayo tuliiachia mwaka wa 2019. Album hiyo ilinipa umaarufu zaidi na single yake tuliyotoa inaitwa Step ilivuma hata nikapata kufanya interview kwa radio na TV station kadhaa hapa Kenya na nikapata kutajwa kama mmoja wa wachanaji bora hapa Kenya na wasanii kadhaa wa kutajika. Nilikuwa kwenye orodha ya Homeboyz Radio Freshmen wa mwaka huo pia.
Wakati wa janga la Uviko 19 niliweza kutoa EP nyingine mwaka wa 2021 inayoitwa Eternal Poetry iliyobeba ngoma kama Say Something, King na Wonder. Majuzi tena nimetoa kazi nyingine, album yangu ya pili inaitwa Practice Run.
Album ambayo nishawahi kuipa skio la ukaribu kutoka kwako ni The Bishop’s Son...Kazi nzuri sana ile. Tueleze kuhusu hii kanda, mbona mradi unaitwa The Bishop’s Son na maudhui yake ni yapi?
Album hii ni personal sana. Kwanza kabisa babangu ni Askofu katika kanisa la Methodist. Hivyo mimi ni mwanawe, The Bishop’s Son. Pia kuna dhana imekithiri kwamba watoto wa wahubiri ni wapotovu na kwa sana huishia kwa madawa, anasa na maovu mengine. Kwa ile album nakiri kwamba mimi ni mwana wa askofu ndio, lakini pia ni mwanadamu aliye na mawazo na maisha yaliyojaa michanganyiko na panda shuka kama yeyote mwingine. Pia inalenga zaidi ndoto yangu tangu utotoni ya kufanya muziki wa Hip Hop. Mada ambazo nazizungumzia kwa kina katika zile nyimbo kumi zilizo kwenye album hiyo.
Kutokana na kuwa wewe umetoka kwenye familia ya kidini, je wazee wako wamelichukuliaje swala hili la wewe kuwa mchanaji kutokana na dhana ya watu wengi kusema huu ni muziki wa shetani/muziki wa kihuni? Je wamekuunga mko au kukupinga kwenye hii safari yako ya kuwa emcee anayeelimisha dunia?
Wazazi wangu wametokea kwenye kizazi kinachothamini sana elimu ya shule na ajira aina ya "white collar job". Hivyo, hata kando na maadili yao ya kidini walionelea kwamba mwanao kufuata njia ya sanaa haikuwa nzuri. Kusema kweli walitaka niimbe tena niimbe nyimbo za dini kama ilikuwa sharti niwe mchanaji, ila iwe kama uraibu tu na sio fani yangu.
Mvutano huu ulisalia hadi wakati ambapo nyimbo zangu zilianza kupata umaarufu hata wakaniona kwenye luninga ndipo msimamo wao ukalainika kidogo. Pia wanafahamu fika kwamba mimi siimbi uhuni bali nina nyimbo zilizo na ujumbe wa kuelimisha jamii. Nadhani wasiwasi wao mkubwa ni kwamba fani ya mwanamuziki huku kwetu mara nyingi haiwezi kumkimu mtu na familia yake kifedha.
Babangu mara kwa mara huniuliza kama bado napiga shughuli ya muziki hivyo najua anani support kimya kimya. Vile nimefanikiwa ki masomo, wasi wasi wao umepungua. Kwa sasa lakini sijawaambia nina mpangobwa kufanya kazi hii kuwa full-time katika miaka michache ijayo.
Tueleze mchakato wako wa kuandaa kazi zako huwa unaanzaje kutoka upate wazo mpaka ukamilishe ngoma.
Kwa sana mimi ni mwandishi wa mashairi na napenda sana kuandika. Napenda pia mbinu ya mitindo huru, lakini hisia zangu ni kwamba maneno ninayoyasema huwa nahitaji muda kuyafikiria na kuyapanga jinsi roho yangu inavyoelewa beat ambayo producer ameniandalia.
Huwa nahisi kana kwamba mimi ni chombo cha kuleta ujumbe kutoka ufahamu wa kiulimwengu na kiroho wakati ninapotunga nyimbo zangu. Nyimbo nyingine hunijia upesi sana hata huhisi kana kwamba napata shairi lenyewe kutoka kwa ulimwengu kama tayari limetungwa. Kazi yangu ni kuweka shairi hili kwenye mdundo tu. Mara nyingi ninapoingia booth huwa narekodi kazi zangu na one take!
Uandishi wangu unaingiliana sana na mawazo na hisia zangu; vitabu nilivyosoma na ari ya kuleta mabadiliko katika mawazo na maisha yangu na ya wanadamu wenza. Hupewa maudhui mengi na historia ya utumwa, ukoloni, ukoloni mamboleo na mchakato wa kupata uhuru katika maeneo mbali mbali duniani na sana sana Afrika. Pia hujivunia sana mafanikio yaliyoko kwenye historia yetu katika juhudi za kujitambua na kujenga jamii zetu.
Mwaka huu umeachia ngoma mbili Stay Sharp na Anthem ya Ugwange…ndio tumefunga mwaka au ndio mwanzo ukoko unaalika maua?
Stay Sharp ni single kutoka kwenye album nimetoa majuzi inaitwa Practice Run. Album hii tulirekodi tukaiweka sana bila kuitoa hivyo tumeonelea tuiuze kwa bei nafuu zaidi ya shilingi mia moja za Kenya katika platform ya Hustle Sasa. Ni album yenye ngoma nyingi nzuri lakini pia inaashiria kufunga chapta hiyo yangu ya style hiyo ya utunzi na hata filosofia ya maisha.
Anthem ya Ugwange nayo ni kifunguo cha sura inayofuata. Kwa sasa nyimbo zangu nyingi nitaimba na Sheng' kinyume na nyingi za kizungu za hapo awali. Pia ni ishara ya kukua kwa mtindo na mbinu yangu kama MC. Niko studio nashughulika na kazi mpya ambazo nina hisia nzuri sana nazo. Nafurahia sana kuzitunga na kuzirekodi. Yaani siwezi kusubiria kuziachia kwa mashabiki zangu waziskilize.
Hali ya muziki ipoje Kenya kwa sasa hivi? Je tunapenda vya kwetu na kuvipa support au cha mgeni ndio tunachokipenda zaidi?
Hahaha. Sitaki kuzungumza na machungu vile wasanii wengi Wakenya huzungumza. Ni kweli Wakenya tunapenda mitindo ya kigeni zaidi ya kikwetu. Lakini kama kazi yako ni nzuri na ya kipekee Wakenya hukukubali ndani ya roho zao na kupenda kwa dhati kazi yako. Nitakupa mfano katika fani hii yetu na Kalamashaka, Juacali, Abbas Kubaf na Nyashinski. Katika tasnia nyingine kuna Sauti Sol na wengine. Wasanii walio na uzoefu, walioshikilia style yao na wanapendwa hata zaidi sasa hivi kuliko hapo zamani za ujana wao.
Hivyo mawazo yangu ni, Wakenya hawafurahishwi sana na vya haraka upesi. Ukitaka heshima yao lazima uweke bidii maradufu na uwe na kitu cha kipekee. Huwa wanakubali sana mtu anayechapa kazi na kujituma. Mbinu mpya ya usanii.
Kando na muziki unajihusisha na shughuli gani nyingine ili uweze kujikimu au wewe ni mwanamuziki muda wote?
Kama nilivyotaja awali mimi nimefanya masomo ya uchumi hivyo kwa sasa nina kazi ninayoifanya katika nyanja hizo. Maoni yangu ni kwamba kama una uwezo na akili ya kufanya mambo kadhaa yafanye. Kwa sasa najaribu nifanye mengi katika uwanja wa masomo kabla muziki uchukue kiwango kikubwa cha muda wangu. Ingawa sijafanya maamuzi kama nitafanya shahada ya uzamivu (PhD) ya uchumi, nikipanga kuupa muziki muda wangu zaidi.
Kwa chipukizi anayekusoma mpe madini yanatokana na safari yako ya muziki…
Subira. Subira. Na bidii isiyochoka.
Kulingana na aina ya muziki unayofanya na maudhui unayoangazia, unaweza jaribu kufuata trend. Hilo si baya. Ila mafanikio yake ni ya muda tu.
Napania kufanya kazi za muziki zitakazoishi miongo kadhaa na muziki wangu. Kazi za muda mrefu kama hiyo inahitaji subira na kujitolea kwa wingi. Aminia ndoto yako kwa sababu ni wewe tu unajua jinsi ya kuieleza na maana na umuhimu wake.
Tutarajie nini kutoka kwako hivi karibuni kaka?
Kazi zinazokuja ni nyingi kuliko zile zishatoka hapo awali. Ningetaka nisizungumzie kazi hizo sana, wacha muziki wangu uongee. Tutapatana hapa tena tuzijadili. Kuna album mbili tunazifanyia kazi sasa hivi. Msururu wa kazi zitakazokuja sio za kitoto.
Neno la mwisho?
Langu la mwisho ni kutoa shukran kwa wote walioweka imani yao kwa hiki kipaji changu. Watayarishaji wangu DJ Klobo, Shen Yunng na Koome. Nashukuru familia yangu kwa support. Ndugu zangu. Nikimpa shukran za kipekee kakangu Calvin Mwenda tuliyeanza safari hii naye na ni shabiki mkubwa wa Hip Hop. Huyu siku nyingi hunikumbusha siwezi achana na hii kazi juu ina inspire wengi and it's bigger than me. Nashukuru mashabiki wote wa Hip Hop. Ni kwa ajili yao moyo unazidi kuwa na hamu kubwa ya hii kazi. Nakushukuru sana pia wewe Kefa na timu ya Micshariki kwa kunipa nafasi hii kuzungumzia kazi yangu.
Wapi unapatikana wewe pamoja na kazi zako za muziki ili mashabiki waweze kuwasiliana nawe na kuskiliza kazi zako?
Katika Instagram na X (Twitter) handle yangu ni
Instagram: @damu_yamashujaa
Twitter @damu_yamashujaa.
Pia Nina page pale Hustle Sasa ambapo unaweza kupata project zangu zote kwa bei nafuu.
Project zangu pia zinapatikana YouTube. Page inaitwa Damu Ya Mashujaa.
Nenda kwa simu yako follow, subscribe na uweke notifications na uwajulishe wenzako.