Papaa Frege

Papaa Frege ni Mbeti toka kundi la Hip Hop linalotokea Kahama Wabeti. Frege ni emcee wa Hip Hop ambae watu wanaofuatilia Hip Hop ya handaki Tanzania mameshaskia kazi kazi. Binafsi nimeanza kumfahamu baada ya kupata nakala ya EP ya Wabeti iendayo kwa jina Ukubwa ambayo ilikua mradi mzuri sana.

Tarehe 13 mwezi wa Desemba 2021 tulipata fursa ya kufanya mahojiano na emcee huyu kwenye kundi moja la wadau wa mziki lilipo WhatsApp, Muziki Na Maisha ili kuweza kumfahamu yeye na harakati zake za Hip Hop.

Karibuni sana.

Karibu sana kaka Frege. Tuanze kwa kufahamu jina lako halisi. 

Jina halisi ni Fred Fabian.

Kwanini uliamua Hip Hop na sio mziki mwingine bwana Frege? Jina Papaa Frege lilikujaje?

Kuhusu muziki ni tangu 2002 ndo nilianza kufanya.

Kipindi hicho nilikuwa mdogo kiaina kwa hiyo kibongobongo nilikuwa napagawa sana nikisikia Ndio Mzee za kina Professor Jay, akina Jay Moe, Solo Thang basi noma tupu. Ndo hapo nilipokuwa nafuata nyayo na baadaye kuendelea kusikiliza wakongwe wengine mpaka wa mamtoni..

Papaa waliniita washikaji zangu sekondari kutokana na perfomance za jukwaani na kipindi kile walimaanisha Baba Wa Rap pale skuli. Na nilichagua Hip Hop kwa sababu ni kitu ambacho ndo nakiweza na kukipenda. Mi siwezi kuimba, naweza nikazipenda pia ngoma za kuimba kwa kuwasikiliza wanaojua kuimba ila me siwezi kuimba. Na napenda Hip Hop zaidi.

Toka mwaka 2002 mpaka sasa 2021 ni miaka 19 imetimia toka uanze kupenda Hip Hop na kuwa ndani ya Hip Hop, je ni nyimbo ngapi umeachia au Ep, album ngapi zipo sokoni?

Nina mixtape moja, na EP mbili. Moja ikiwa ni ya kushirikiana ambayo ilishatoka. Album 2 hazikufanikiwa kutoka mpaka sasa ziko studio kwa bwana Black Ninja moja na nyingine kwa bwana Stim Master wa Nexus Studio japokua ma producer ni tofauti tofauti.

Taratibu za utoaji zilikumbana na muingiliano wa mambo kidogo lakini zitatoka. Kwa miaka ile kuanzia 2002 mpaka miaka ya hapa katikati ilikuwa ni ngumu sana kuachia hizo mambo kutokana na uhalisia wa game.

Utamaduni wa handaki na muunganiko wa familia ya handaki umesaidia sana kuamsha morale za kuachia packages. Awali ilikuwa ni ku rap tu na ku perform kupigiwa makofi baaaas!

Jina Papaa mbona kama linatumiwa sana na watu wa mziki wa dansi kwa sana mfano utasikia Papaa Beberu mume ya mbuzi, je jina hili halikupi wakati mgumu pindi ukiwa unajitambulisha kwa maniga kwa kuanza na Papaa?

Hapana man! Papaa inaweza kuwa ni wadhifa na sio jina rasmi la watu wa aina flani! Binafsi halinipi wakati mgumu kwa sababu katika utamaduni wetu wale wanaonifahamu huniita hivi wakifahamu ni nini nafanya pia. Kwa hiyo linabaki kuwa jina. Ambao huona ni refu kutamka tu Frege.

Changamoto gani unakutana nazo kwenye mziki unaofanya?

Changamoto kubwa ni kwamba kile ninachowasilisha huwa natamani kiwafikie watu wengi zaidi ya wale kinaowafikia. Pia makundi makundi kwenye utamaduni pamoja na ushikaji ushikaji kwenye ufanyaji wa kazi na kusogeza kazi binafsi huwa naona kama ni changamoto pia.

Dhima kuu ya hip hop ni kuelemisha na kuburudisha na ndani ya dhima hizo kuna vipengele kama conscious rap, hard-core rap, gangster rap na vingine vingi. Je kwa vipengele vichache hivyo wewe unasimama kwenye kipi? Unafanya muziki aina ya hip hop? Au kwa vile niko mbali? Sijawahi sikia hata moja, nitapataje albamu yako?

Conscious rap kwanza napendelea zaidi kisha hard core rap. Napenda aggressiveness pia kwenye kuwasilisha

Tuzungumze kuhusu WABETI. Hebu tuambie kuhusu WABETI ni kina nani na nini wanafanya kwenye huu utamaduni wa hip hop na wapo memba wangapi kwenye kundi. Idadi ya memba wa familia ya wabeti mpo wangapi mfano tukisema Yunani Empire wapo 11 wachanaji 8 watayarishaji watatu?

WABETI ni watunzi wa Beti. Kama tunavyofahamu maana ya UBETI kwenye Kiswahili.

WABETI ni familia lakini kwa sasa tulioonekana ni Frege na Bad Ngundo lakini pia wakati ukifika tutasikia uwakilishi wa WABETI kutoka kwa Members wengine pia wa familia. Kwa hiyo maandalizi mazuri yanafanyika ili uwakilishi uwe wenye tija ukiwafikia wana.

Frege kuna kufanana kwa ki mtindo kati yako na Trubadour George?

Trubadour George ni ndugu yangu tuliyekua wote tuliyesoma wote, tuliyekaa dawati moja, tuliye rap pamoja na mpaka sasa tuko wote na hata katika mashairi yake au yangu tumeshaandika mengi sana tukiwa pamoja.

Anaweza akaandika akanitumia nika edit, nikaandika nikamtumia aka edit. Mwisho wa siku tunapata kitu kimoja. Labda ndo sababu ya kufanana pia. Hili nadhani umenipata kamanda nimelitolea ufafanuzi.

Kuna kolabo umetugusia kule Facebook, tunaomba utueleze, inaitwaje? Walioshiriki kina nani? Inatoka lini na imefanyika studio gani?

Hii kolabo nitataja jina pindi itakapotoka ila video tayari imeshafanyika na washiriki ni Frege, One The Incredible, Bad Ngundo, Mex Cortez pamoja na Cado Kitengo. Mdundishaji ni Black Ninja na editing ya video inaendelea. Siku si nyingi itatoka.

Tumekuwa tukikuona kwenye Agro Hip Hop vipi hii movement imeishia wapi na mipango yake ilikuwa nini? Kuna muendelezo au?

Agro HipHop movement inaongozwa na Plate Mdaijasho na mimi ni kama mwana familia. Kwa hiyo mipango haijafa, ipo na imeendelea kusimamia maandalizi ya kazi mbali mbali. Kuna EP mpya ya Plate Mdaijasho pia ni chini ya Agro Hip Hop. Kwa hiyo iko hai hii movement na matukio kibao Kahama yatafanyika siku si nyingi.

Ugusie hii Project kuanzia Idea, Utunzi na ushiriki wake kiujumla (Balibaza).

Mtunzi wa hizi kazi ni mimi mwenyewe na mtayarishaji ni Black ninja ambaye baada ya kuimaliza tuliingia makubaliano tukamalizana mi na yeye na umiliki wa uuzaji ukaendelea kuwa wake. Mtayarishaji wa ngoma zote alikuwa ni Black Ninja.

Igusie na hii pia na upatikanaji wake(Ukubwa EP).

Hii ni EP ya Wabeti ambayo tumeifanya mimi pamoja na Bad Ngundo. ilitoka mwaka huu (2021) pia. Inapatikana YouTube bure.

Unaweza share link/wimbo mmoja tusikilize. Nje na mziki unadili na mbanga zipi? Maana inajulikana wazi ni ngumu sana kuendesha maisha kupitia mziki hasa underground hip hop kwa nchi yetu?

Link nimeshea hapo juu ya baadhi ya nyimbo na nje ya muziki mi ni muajiriwa kwenye serikali ya Mama Samia. Kiufupi ni Economist. Kwa hiyo huwa kuna wakati harakati zinaingiliana na majukumu ya ofisini na kusababisha ukimya kidogo japo sio sana. Ni kwa muda mchache sana.

Unatumia vipi kinasa kuwasilisha nguzo zingine za hip hop ambazo sehemu nyingi ya jamii yetu hawazijui?

Uwasilishaji wangu zaidi ni kwenye nyimbo ninazofanya hivyo basi hata kwenye ngoma ninazofanya hupenda pia kuhubiri nguzo nyingine pia pale ninapotakiwa kufanya hivyo.

Unaitazama vipi underground hip hop ya Tanzania toka ilipoanza mpaka ilipo sasa na inapoelekea?

Naitazama chanya sana na kwa sasa kila mtu anaona jinsi handaki ilivyoamka na inavyozingatiwa na watu wengi. Hata waliopo mainstream kwa sasa wanafahamu na wanajua yaliyopo Handaki. Kwa hiyo binafsi na appreciate sana jitihada za kila mwana kwenye kila kinachofanyika. Imeinua sana Underground Hip Hop katika ardhi yetu ya Tanzania pia.

Mipango yako ikoje katika mziki wako kuanzia wewe mwenyewe mpaka Wabeti?

Mipango iliyopo ni kuhakikisha malengo tuliyojiwekea kama Wabeti yanafikiwa. Mi napenda zaidi malengo ya familia kuliko mmoja mmoja. Familia ikisogea basi kila mmoja amesogea. Kwa hiyo malengo yetu ni kuendelea kufanya kazi na kuziwasilisha kwa jamii lengwa mpaka tuhakikishe kuwa yale tunayotaka yasikike yanasikika na kama kuna namna jamii itaelewa yale tunayoyafundisha. Akitokea hata mmoja au wawili wakaelimika basi tunashukuru. Yule mtu ataendelea kutukumbuka pia

Mfano kazi kama hii.Tuna imani wakisikiliza watu 100 basi kuna hata watano watakaobadilika mtazamo.

Tuzungumzie mixtape na ep ulizotoa mapokezi yake yalikuwaje kwa jamii uliyokusudia? Je lengo lilitimia au ndio ulitoa kuonesha kuwa unaweza kutoa mixtape na ep kama wanavyotoa wengine?

Lengo lilitimia ukiangalia kazi hizo ni moja ndo niliingia mkataba na Black Ninja tukamaliza akauza yeye lakini kazi nyingine tulitoa bila kuuza yaani bure. Lengo lilikuwa ni kutoa tu zile jumbe nilizokusudia zitoke katika wakati huo. Sio kutoa ili kuonesha watu kwamba naweza kutoa EP au mixtape au album, hapana. Ingekuwa ni hivo basi hata album zilizopo studio ningezitoa tu ili watu waone.

Umekuwa ni muumini wa upendo kwa Mimi navyojua, je unaamini bifu za wanamuziki zinasaidia sanaa yetu kukua?

Sasa hapa kuna kukua kwa majina ya wasanii na kuna kukua kwa sanaa. Wakati mwingine beef inaweza ikakuza majina ya wasanii husika huku inaua dhana ya sanaa. Kwa hiyo siwezi kataa beef zisiwepo kwa sababu zipo tangu tunakua na tumezikuta kwa hiyo upande zina matokeo chanya na kuna wakati hazina matokeo mazuri.

Upatikanaji wa kazi zako uko vipi iwapo mtu akiwa anahitaji kusapoti kile unachokofanya? Je umefanikiwa kusambaza kazi zako mikoa mingapi mpaka sasa?

Kazi zangu zote zipo kwenye digital platforms na kwa yeyote ambaye anaona ni vyema kunipata niko Instagram: Papaa_frege  niko Facebook: Papaa Frege updates zote huwa zinakuwepo pale.

Oi frege nini kilikusukuma kuandika hii track? Moja ya track zangu bora toka kwako.

Hii ni kutokana na baadhi ya mifano ambayo ukisikiliza beti ya pili utaona kuna baadhi ya mifano niliitoa na hiyo ni moja ya maswali ambayo nilijiuliza kabla ya kuiandika. Kwa hiyo nikaanza umiza kichwa kaka maana nilikuwa naamini ni kitu ambacho ni valid.

Ulishawahi kumblock (kwenye mitandao ya kijamii) shabiki yako mliyetofautiana mawazo kwa maana nimeona baadhi ya wasanii waki block mashabiki? Na unalionaje hili katika mtazamo huu?

Hapana sijawahi kumblock shabiki kaka.

Inawezekana ikawa sawa au isiwe sawa. Kama shabiki anakupa challenge ya kuongeza juhudi sio sawa kumblock ila kuna mashabiki hutukana tu bila sababu wao ni kutukana tu. Sasa wasanii nao wana mioyo na wanatumia nguvu nyingi na resources pia kujifikisha mahala walipo. Kwa hiyo inakata stimu anapojitokeza shabiki wa namna hiyo.

Papaa Frege, teknolojia ya ku stream kazi za wasaniii ndio habari ya mjini, we binafsi unatumia hizi apps na umeweka kazi zako kule? Kwa nini?

Kazi zangu zote zinapatikana huko kwa sababu upigaji wa magoti kwenye media huwa siko tayari. Naamini pia katika streams zetu za handaki.

Una ushauri gani kwa mchenguaji anayepanda jukwaani akiwa bwii au mpepe umemzidi kwa mashabiki wake waliolipa kiingilio?

Hahaa hawa wanastahili maombi na wakibisha ni adhabu kali inawafaa ni suala la mtu binafsi kuji control na kujua watu wanataka nini na sanaa yake inamtaka afanye nini.

Je unachokifanya kinaendana na ulichowekeza na unachokivuna?

Hapana. Na hili si kwangu tu.

Akitokea mtu akakwambia Frege wewe ni waki hutunzi misingi utamjibu nini?

Kama hii ndo itakuwa definition ya wacky then kwa mtazamo ntamjibu tu "SAWA". Manake huwezi kumpangia mtu jinsi gani akuongelee wewe.

Asante kwa mda wako Frege naona mda unasepa tuache ufanye mengine na tuwapishe wengine wafanye yao humu.

Asante!