Binafsi nilianza kumfahamu Rama Wise pale aliposhirikiana na ma emcee wenzake Amphoteric, Trayo Version pamoja na Blad Key kwenye wimbo ART. Kutoka hapa nikafuatilia kazi zake za awali kama vile Sifichi, Ujana akiwa na Bless P na nyingine nyingi.
Rama Wise sasa anakaribia kutupatia mradi wake mkubwa wa kwanza rasmi ambao ameupatia jina Mimi Ni Huyu. Tukisubiria kazi hii nimeona ni vyema kuwaletea mahojiano nae yaliyo fanyika kwenye group flani la WhatsApp, Muziki Na Maisha.
Karibuni!
MkoKeNya
Rama Wise karibu dimbani....
Shukran sana.
Jina lako kamili unaitwa nani na kwa nini ulijiita Rama Wise?
Kwa jina ni Ramadhani Hamadi Swalehe.
Rama Wise ni jina ambalo nilipewa na washkaji zangu kulingana na vile nilivyo au ambavyo wameona niko kila niwapo nao na mambo yangu kwa ujumla.
Yap Yap tueleze...
åRama ni kabila gani!?
å Mtoto wa ngapi!?
åKazaliwa wapi na amekulia wapi!?
å Kiwango cha elimu Kama hutojali
Hapa tumjue Ramadhan Hamadi Swalehe...
Inaonekana umekulia kwenye familia ya kidini vipi haikuwa changamoto kwa hizi harakati zetu!?
Rama ni Mjita kutoka Mkoani Mara, Manispaa ya Musoma. Mtoto wa pili katika familia ya watoto saba. Nimezaliwa hapo hapo mkoani lakini nimekulia Mwanza sana Musoma pia na Morogoro.
Imekuwa changamoto kiukweli lakini ilifikia wakati ilibidi tu wanielewe na kukubaliana na hali na ndio ikawa hivi mpaka sasa.
Binafsi napenda sana unachofanya na kwa nini ulichagua kufanya mziki wa hip hop na upande mwingi umekua ukiandika jumbe za hamasa kwa jamii nini siri juu ya hili?
Juu ya jumbe ndio target yangu hasa na nimejikita zaidi huko sababu naona ni sehemu ambapo watu wengi wanapakimbia siku hadi siku namimi nikaona ni fursa kwangu na hisia zangu huendana sana na hicho kitu sababu huakisi mazingira halisi ya maisha tunayoishi kwa jamii iliyotuzunguka.
Morogoro pale kulikuwa na MYT (Moro Youth Talent) na kaka mkubwa XP Xperience Peter Claver. Vipi ushawahi kushiriki kwenye zile harakati!?
Yeah na ni harakati ambayo nilishiriki mara ya tatu; mara ya kwanza ilikuwa Musoma iliitwa Masstown Movement, baada ya hapo nilipita pia Mwanza pale Gogo Vinu kwa akina Jeff Jerry, mara ya tatu ndio ilikuwa Moro (Morogoro) na kipindi hicho ilikuwa ni Kipaji Ni Ajira kabla ya kuwa registered na kuwa Moro Youth Talent.
Na ni msanii gani aliyekuwa na ushawishi kwako kupenda na hata kufanya muziki ilhali ulikuwa katika mazingira flani ya kidini kwa sana!?
Imetokea lakini sababu nyingine nilipendelea kufanya baada ya kuona ndio kitu naweza zaidi sababu kabla ya kufanya hii kitu nilianza nikiwa naimba lakini haikunifanya kuwa huru sababu sikuwa niki enjoy kama ambavyo nikichana na nimeanza kuchana nilipoanza kurecord kwa mara ya kwanza kabisa studio.
Siku waliyojua kwanza sikutegemea, walihamaki na hawakuamini kama ni mimi waliduwaa na kunishangaa ingawa magombezo hayakuwa mbali sana. Lakini mwisho wa yote nilimwambia mzee, “Mimi kijana wako unataka niwe nani, maana kila ninachofanya na kuona kinanipa furaha na amani we hutaki unataka siku usikie mwanao ni mwizi” maana ukiacha mziki naruka sarakasi kitu ambacho mzee hakutaka pia. Alidai nitakuwa mwizi kwani nilikua nacheza mpira pia na hakutaka na kila nilipoumizwa mpirani kauli yake ilikua ni kunisema niache.
Nashukuru hatimaye alikubaliana na nnachokifanya mdogo mdogo kwa kusimuliwa na watu wa pembeni juu ya uwezo wangu.
Kwa upande wa ma emcee walionipa motisha ni kama akina Sugu, Jay Moe, Prof Jay na ilitokana na baba zangu wadogo niliokuwa nikiishi nao kupenda kusikiliza sana nyimbo zao nilijikuta napenda kidogo kidogo mpaka hatimaye nami nikaingia miguu yote.

Unaposema ulianza kuchana ulipoanza kurekodi kwa mara ya kwanza kabisa studio una maanisha nini hapa? Wimbo wako wa kwanza kurekodi ulikuwa ni wimbo gani? Na mazingira yake yalikuwaje mpaka kwenda kuufanya?
Namaanisha wimbo wa kwanza wakati wa kurecord siku hiyo jamaa yangu mmoja ndio tulijichanga tupige ngoma moja pamoja baada ya kurecord ye hakupendezwa na alivyoisikia sauti yake akaahidi kuacha mziki siku hiyo na kuniambia ni record mwenyewe mimi pia nikaomba beat nyingine ndio nikachagua beat ya hip hop nikaenda kuandikia nami ndio nikabadilikia hapo hapo mpaka leo.
Kwa wasiokujua vibes zako zinatokea wapi unapopanda steji maana mzee hautumii sigara kubwa wala pombe halafu wewe pia ni swala tano haikutoi kwenye reli na lini umepanga kuacha gemu na kurudi kwa mola wako (chagizo)?
Kuhusu vibe nafikiri ni mapigo/beats tu maana mi nikisikia beats hisia zikaoana na kuwa familia hupata mzuka wa kufanya kitu juu yake ni hivyo tu kaka.
Yeah hii pia inanibana wakati naandika na sio kwamba kuna mtu anakuwa ananipangia namna ya kuandika hapana inatokeaga tu inakuwa hivyo na nimeshajizoea pia kuwa wa hivyo hivyo.
Je Rama Wise ni producer (pia) na je ofisi yako ipo maeneo gani?
Mi sio producer ni msanii tu kama wasanii wengine bro.
Yapi ni matarajio uliyonayo katika sanaa yako?
Kwa upande wa faida nafikiri kuifurahisha nafsi yangu si kitu kidogo hasa inapopelekea na nafsi za watu wengine kuvutika na nnachokifanya hii kwangu ni kubwa nafikiri kilichobaki ni upande wa pili huu tunaoita upande wa shilingi ili nifaidike zaidi na zaidi kwa kukibadilisha nilichonacho kuwa hela.
Nafikiri ni siku ambayo mimi mwenyewe siijui ila huwa naona kabisa kila dalili huko mbeleni
Nitajie wasanii watano wa hip hop unaowasikiliza sana
Nipatapo muda Dizasta namsikiliza na yule One Incredible wa nyuma 2016 kurudi nyuma Jay Moe pia. Adam Shule Kongwe namsikiliza zaidi ule wimbo wa Nyumba Yangu haunichoshagi kusikiliza asee.
Ushawahi kuwa katika kundi au chini ya usimamizi wa mtu?
Nimewahi kuwaza kaka ila sijawahi kuona sababu ya kufanya hiyo kitu kabisa labda kwa siku za mbeleni naweza kupata sababu ya kufanya hivyo.
Si enjoy kuwa alone lakini bado sijaona kabisa ile nguvu ya ushawishi kwangu kufanya kazi na management.
Tueleze kuhusu maandalizi yako ya albamu yako, imefikia wapi? Itakuwa albamu ya aina gani!? Nini umekusudia kufikisha kwa jamii kupitia hiyo package? Lini itakuwa tayari na imeshirikisha vichwa gani!?
Kwanza kwa sasa mbele yangu niko katika maandalizi ya album yangu ya kwanza na maandalizi yako mwishoni nafikiri kupitia hili kuna mengi na mengine yatatokea na kunipa njia na mwanga ikiwa matarajio mengine ni kuwafikia kama sio kuwafikishia kila nilichojaaliwa kuwa na uwezo wa kukifanya kupitia talanta yangu.
Nahitaji sana sapoti maana hii safari ina vipando vingi kiasi naona mwenyewe siwezi. Nahitaji kusapotiwa kwa namna yoyote kama hivyo nimejitutumua nakuja na album mni supoti.
Changamoto zipi unakutana nazo binafsi na vipi unakabiliana nazo…
Changamoto hazikosi ni nyingi hasa katika suala la uwezesho katika ufanikishaji kazi, sapoti bhana ni changamoto nyingine unakuta unapata nafasi za kurecord sehemu au mtu wa kukupiga tafu lakini anataka akubadilishe unavyoimba akuswitch. Yaani unashangaa mtu kakukubali kwa unavyofanya lakini ili akupush anataka akubadilishe. Kingine baadhi ya wasanii ukitaka kufanya nao basi anajichukua kana kwamba ukifanya naye ndio umeshapiga pesa vile.
Mapokeo ya kazi zako unayaonaje?
Mapokeo ni mazuri na hili nililiona tangu naanza kabisa sababu kila nilipokuwa nikirap nilikua nikiambiwa mimi siwezi kuandika mashairi kama hayo naambiwa nime copy hii lilinifanya nijue nina kitu ndani yangu ambacho ni kikubwa kuliko hata mimi mwenyewe.
Kwa kuangalia kuanzia umeanza mpaka sasa, safari ya kufikia malengo yako itafikiwa baada ya muda gani?
Kukadiria safari ya malengo itafika baada ya muda gani ni uongo ila nnachoamini ni kwamba sitatoka kapa na sina kitakachonifanya kujutia hata kama sitafikia sababu kitendo cha kufanya tu na nikajisikia nimefanya naona nimefikia malengo yangu.
Na jamii itakapopata elimu somo au darasa kupitia nnachofanya kwa namna nnavyoizindua kila nipatapo fursa ya kufanya hivyo naona nayasogelea malengo yangu.
Kuacha alama ni moja kati ya malengo yangu bro.
Umekuwa katika utamaduni kwa kipindi kirefu ni mambo gani ya kimiyeyusho yeyusho unayoweza tuhimiza kuepuka sisi kama manigga Hip Hop?
Kitu cha msingi nafikiri ni kukijua vizuri kitu kabla ya kukifanya…
Kila kitu huwa na matokeo yake sasa basi tusipende kufanya vitu kwa mizuka na mikumbo kisa fulani yuko katika utamaduni anafanya hivi basi na wewe ufanye ndio uonekane uko katika utamaduni. Uhuni ni tabia binafsi tusihusianishe kabisa hii kitu na utamaduni hii itatusaidia mimi pia nipo humu ndani ya utamaduni ila muda mwingi nautumia kujifunza kuliko hata nnavyofanya yanayohusiana na utamaduni.
Masuala ya msingi naona yote tulishauliza na yamejibiwa kiufasaha sana. Shukran kwenu, kwa kushiriki Dimbani na kufuatilia Dimba. Hope leo angalau tumemfahamu kimtindo ndugu yetu Ramawise. Amani kwako Rama Wise.
Shukran sana kwa muda wenu.