Ukaguzi wa albam: The Verteller
Msanii: Dizasta Vina
Tarehe iliyotoka: 27.12.2020
Nyimbo: 20
Wapiga midundo na ma producer: Ringle Beats, CjaMoker, Jcob, Dizasta Vina,
Mixing & Mastering: CjaMoker, Ringle Beats
Studio: MV09, Dreambooth
Dizasta ni neno lililotafsiriwa moja kwa moja toka kwa neno la kiingereza disaster linalomaanisha shida kubwa inayotokea kwa muda mfupi au mrefu ambayo husababisha upotezaji wa binadamu, nyenzo, uchumi au upotezaji wa mazingira ambao unazidi uwezo wa jamii iliyoathiriwa au jamii kuweza kutumia rasilimali zake.
Vina ni silabi zenye sauti ya namna moja zinazotokea katikati au mwishoni mwa kila mshororo wa kila ubeti wa shairi.
Unapounganisha maneno haya mawili Dizasta na Vina unampata Dizasta Vina ambaye ni msanii wa Hip Hop, mwandishi wa nyimbo, mtunzi wa hadithi, composer na beatmaker na pia ni mpiga vyombo aliyezaliwa mwanzoni mwa miaka ya tisini. Anajulikana rasmi kama Edger Vicent Mwaipeta. Jina hili Dizasta Vina alipewa rasmi na dada flani DJ na mtangazaji wa radio anayeitwa Divanji aliyekubali uchanaji wake.
Baada ya kujitosa kwenye ulimwengu wa muziki wa Hip Hop 2010, Dizasta alifanikiwa kuachia single yake ya kwanza Harder, 2012 kabla ya kuachia compilation CD-Jesusta pamoja na mixtape yake The Wonder Boy. Baada ya kuachia singles kadhaa Dizasta Vina alifanikiwa kuachia debut albam yake The Verteller.
The Verteller ni nani? Albam inaanza na Intro nzuri ambayo ni simulizi ya dakika tano ambapo Dizasta anatupatia somo la historia kuhusu mwandishi na umuhimu wake kwenye jamii. Anaonesha vile msimuliaji yupo tayari kulipa gharama zozote kupata na kukupa taarifa sahihi. Kwa maana hii Dizasta anajitambulisha kama the narrator, the story teller au pia kama The Verteller!
Dizasta Vina ametumia uwezo wake mkubwa wa kutunga hadithi kama njia yake kuu ya kuelimisha na kuburudisha. Kwenye mradi huu nyimbo nyingi zinaanza kama simulizi za hadithi flani ambazo zimejaa mafumbo, taharuki, misemo, methali, sitiari, jumbe wazi na zile zilizofichwa.
Hadithi hizi kwenye mradi huu zinapatikana kwenye nyimbo kama Kibabu na Binti, Tatuu ya asili, pamoja msururu wa nyimbo nne zinazoanza na neno Confessions pamoja na Hatia IV, Money na Wimbo usio bora.
Hadithi kwenye nyimbo hizi zinagusa mada tofauti tofauti zikiwemo mahusiano na changamoto zake(Kibabu na Binti), gonjwa la ukimwi na ubakaji(Tatuu ya asili), umuhimu wa kuchukua tahadhari kwa kila jambo(Confessions of a mad man), kifo(Confessions of a mad philosopher) na pia upendo wa Dizasta Vina kwa mamake (Confessions of a mad son).
Hadithi hizi zimeundwa ki ustadi na japokuwa zote ni nzuri Confessions of a mad man ndio ubunifu wake uliniteka vilivyo pale biti linapoisha. Wakati mad man anapotenda unyama wake juu ya binti, sauti za binti akipumua zinaskika kwenye speaker.Mdundo pia umeundwa ki ustadi sana ukipiga bass guitar zuri sana na kinanda freshi.
Ubunifu unazidi kuonekana zaidi pale Dizasta anapoamua kuzungumzia changamoto wanazozipitia jinsia zote mbili za binadamu kwenye wimbo wa Mascular Feminist unaopiga kwa dakika tisa mfululizo.
Kwenye albam ambayo pakubwa Dizasta kasimama mwenyewe,Vina aliweza kushirikiana na waimbaji wawili wa kike akiwemo Dash kwenye single ya kwanza kwenye mradi huu Mwanajua pamoja na TK Nendeze kwenye Almasi. Nyimbo zote mbili zimesimama kiutunzi, ki midundo, kimashairi na pia waalikwa wote walitendea haki mialiko hiyo.Kwenye Hatia IV nayo alishirikishwa dada Nasra ambaye ni msimulizi msaidizi kwenye hadithi ya John.
Mada nyingine zinazopatikana kwenye mradi huu ni kama vile mahusiano na ndoa kwenye nyimbo ya Ndoano, Wimbo usio bora, Ulemavu, pamoja na Almasi. Ndoano imejaa madini kibao kwa ajili ya wanandoa au wenye mipango ya kujitosa kwenye ndoa…
“Ndoa ni ile iliyoandikwa na sheria au dini?/
Au shuruti baada ya hatia ya kuzini?/
Ni jukumu unalovishwa baada ya ugoni?/
Au bashasha unalojivika usoni?/
Watu wajue umeridhia makubaliano na riba za njaa/
Ahadi ya kuwa pamoja kwenye shida na raha/
Ahadi inayovunjwa ka' sheria inavyopindwa na jamaa/
Ndoa si akiba ni sanaa, ndoa ni.....””
Series ya Nobody is safe inaendelea pia kwenye sehemu ya tatu na inagusia maswala ya majigambo kiushairi kama vile wimbo wa Maabara ambao amewashirikisha ma emcee Bokonya,Wakiafrika na Adam Shule Kongwe.
Kesho na Kifo ni nyimbo zinazotamatisha albam hii. Nyimbo hizi zote mbili zinakupa matumaini na ujasiri wa kuishi. Kesho unamkuta Dizasta akitamba kwenye mdundo mzuka sana. Wimbo unazidi kuonesha kwa nini yeye ni miongoni mwa washairi wazuri wa kizazi hiki,
“Kesho nafasi ya kuanza upya/
Kumaliza kuishi nafasi ya kuanza kufa/
Kuivunja sheria nafasi ya kufata ruksa/
Kuikumbuka jana au kuanza kuifuata future/
Future ni leo ni siku ambayo miti hukimbia/
Jua hushuka upendo marafiki hufifia/
Hufifia, wimbi la wanafiki huingia/
Kesho ya tumaini hubakia/
Tumaini shika walao shika walao/
Na ujifunze kuziba kombe pindi anapopita nyang’au/
Akishapita tenda wema alafu kisha sahau/
Na uchunge unaponena watakuzika wadau/
Wadau walikuwa uchi ukawavika mavazi/
Nyumba yako ikavunjika wakakunyima hifadhi/
Je utasamehe utasahau kulipa kisasi/
Au kesho itakukuta umeshika risasi/”
Kwenye Kifo ambapo watu wengi huona kifo kama kitu cha kuogopesha Dizasta anakiona kama kitu cha kawaida. Anamketisha kitako bwana kifo na kuanza kumuongelesha akisema hivi,
“Nagundua we kilema huna hisia/
Watu wanavyolia unaridhika mwenyewe/
Haujui haupo huru ujue hii kazi utaipiga milele/
Wanasema hujakamilika kama hujafa, ntakamilika/
Asiyekamilika ni wewe/
Hauna maisha haujui malengo/
Hauna familia hivyo haujui upendo/”
Mradi huu kwenye rap game ya Africa Mashariki ni wa kipekee. Kipaji cha Dizasta Vina kimenikumbusha kuhusu emcee Sticky Fingaz wa kundi la Onyx. Nikiwa denti chuo kikuu niliweza kununua solo debut albam yake Black Trash: The Autobiography of Kirk Jones ambayo ilikuwa albam revolutionary kwenye handaki ya Hip Hop kule America kama ulivyo mradi wa The Verteller.
Dizasta kama vile Sticky Fingaz ana uwezo mkubwa wa kukupigia story ambayo ndani imejaa ucheshi na kilio, furaha na masikitiko, woga na ujasiri, kuvunjika moyo na matumaini, utofauti pamoja na usawa. Dizasta haogopi kuwa emcee mwenye style tofauti, mwenye uwezo na uhuru wa kuongelea chochote na yupo tayari kulipa gharama zozote ziendazo na maamuzi haya. Dizasta Vina mabibi na mabwana ni The Verteller!
Mpate Dizasta Vina kwenye mitandoa ya kijamii:
Facebook: Dizasta Vina
Instagram: dizastavina
Twitter: dizastavina
YouTube: Dizasta Vina