Ukaguzi wa albam: DIRA
Wasanii: Dom Down Click (D.D.C)
Tarehe iliyotoka: 20.05.2020
Nyimbo: 17
Wapiga midundo na ma producer: Qwitch, Bin Laden, 10th Wonder, Pallah Midundo
Mixing & Mastering: Bin Laden
Studio: Killers Records, Tongwe Records

Kwenye historia ya binadamu, kumekuwa na msukumo flani maishani mwake unaomwambia kuwa kwa eneo alipo kwa sasa hawezi kupanuka zaidi na inabidi atoke alipo na kwenda pahala kwingine ili aweze kukua zaidi. Msukumo huu hugusa maeneo tofauti ya maisha yake; ukuaji wake ki utu, ki roho, kifedha, ki talanta na kisiasa pia.

Na ili kukamilisha matamanio haya vizuri binadamu anahitaji dira itakayomuongoza maishani mwake. Dira hii inaweza kuwa Mwenyezi Mungu, ushauri toka kwa wazazi, wanafamilia au marafiki pamoja na elimu. Pia dira ni kifaa ambacho kwa lugha ya kimombo kinajulikana kama compass ambacho kina uwezo wa kukuonesha ulipo na kukuwezesha kujua kule unapotaka kwenda.

Dom Down Click (D.D.C) ni kundi linaloundwa na ma emcee toka maeneo tofauti Tanzania kama vile Mwanza, Singida, Dodoma na kadhalika. Ma emcee hawa baada ya kukutana kwa upendo kati yao na kile wanachopenda kukifanya, kughani, waliamua kuunda kundi lao rasmi D.D.C ambapo jina hilo alilitoa Lucas Malali (LC). Kundi hili linaundwa na ma emcee wafuatao; Adam Shule Kongwe, Salii Trejo, Goda Mc, Miracle Noma, Kanja Wizzle, Javan (Chuna Ngozi) pamoja na Andre K (R.I.P).

Kundi hili lilifanikiwa kutoa singles pamoja na EP, Mixtape na albam kadhaa hapo awali kama vile The Element Vol. II (2014), Mechanism (2015) pamoja na Fasihi Simulizi (2016). Baada ya kimya cha mda mrefu mwaka wa 2020 wana D.D.C walivunja ukimya wao na wakatupatia albam yao ya pamoja baada ya miaka minne DIRA.

Mradi huu unaanza na utangulizi mzuri toka kwa Adam Shule Kongwe akituonesha hoja utakazo zipata ndani ya albam hii kama vile hoja za kiuchumi, kisiasa, kijamii, kijamii na pia kutabiri yajayo yatakuwaje.

Wimbo wa DIRA ndio umebeba jina la albam hii na umeundwa vizuri sana na producer 10th Wonder, ikipiga percussions na tarumbeta nzuri kwenye wimbo huu. Kaka Goda Mc kwenye vesi ya pili anatema madini ya muongozo freshi sana,

“Kabla hujagusa taifa kwa vinavyo shusha uchumi/
Shuka kabisa na uanzie nyumba kumi/
Shuka tena hadi ufike ngazi ya kaya/
Uuone huu mfumo ulivyo tu tight vibaya/
Imeshakua mbaya na kwanini isiharibike/
Au tuweke midahalo kuhusu nini kifanyike/
Imeshawekwa mingi na mingi tumeshiriki/
Makongamano Utitiri dhidi ya wa magharibi/
Nadhani swala sio maneno magumu/
Naamini msala ni maneno matupu/
Kengele zipo wakumfunga hakuna/
Watu wakiambiwa vitendo wanaugua wanaumwa/
Wanabaki change gonna come tu/ Na Future Ya Nyanja Zote ni nyeusi tu/
Kotekote naona pini kibao/
Sipati picha miaka kumi ijayo/”

Mada ambayo imeongelewa kwa upana kwenye mradi huu ni kuhusu changamoto za maisha yetu ya kila siku pamoja na kutiana moyo. Nyimbo zilizobeba hoja hizi ni Matatizo, Jipange, Sababu, Mnatakaje, pamoja na Tabasamu. Nyimbo zote ukiziskiza utajipata kichwa chako pamoja na moyo wako vikiguswa na kuachwa ukiwa chanya zaidi kuliko ulivyokuwa kabla ya kuskia nyimbo hizi.

Kaa Mbali na Andalio ni nyimbo zinazonuia kutupa tahadhari au onyo juu ya maisha yetu tunayoishi. 10th wonder pia kashikilia mpini tena kwenye Andalio kwenye wimbo unaomkuta Kanja Wizzle, Salii Trejo na Goda Mc wakichana yenye madini kibao!

Kanja Wizle anasema,

“Ngoja nianze kuzungumzia marafiki/
Wale wanafiki/
Wanaokupatia vishawishi/
Kama dawa ya kulevya, ujambazi pia na wizi/
Mwisho wake hua ni uchizi au chini ya ulinzi wa polisi/
Najua sio rahisi ila ni vyema kujiepusha/
Maana maisha tunayoishi ni leo hatujui future/
Kesho na kesho kutwa anaepanga ni maulana/
So usiwe unakurupuka kwa kile unachofanya…”

Mada nyingine iliyogusiwa kwenye mradi huu ni majigambo kwenye Manahodha (Ma Captain) ambapo wana D.D.C wanapiga vifua kuhusu uwezo wao kwenye wimbo ulioundwa kiustadi sana na producer Qwitch.

Kuonesha vile wanavyothamini historia pamoja na vitu vya asili ma emcee pia kwenye mradi huu wanatukumbusha kuhusu maisha ya Babu yetu kwenye wimbo anao chana Miracle Noma pekee ilhali Adam Shule Kongwe akiwa na muimbaji Papah kwenye mdundo wa Hip Hop-Reggae ulioundwa na Bin Laden uitwao Halisi anatusifia vile,

“Natambua msingi ni furaha/
Mother yuko fiti mpaka ma binti wanamshangaa!”

kisa na maana anatumia vyakula natural.

Kama tunavyojua kazi na dawa ndio mpango mzima hivyo kwenye wimbo Madebeni wana D.D.C wanapata fursa ya kula bata. Kama wasemavyo wahenga wa kisasa, “Bata batani/Kuku kibandani”, kila emcee anabaki ndani ya mada bila kuyumba kama anavyofanya kwenye mradi wote huu,
Sali Trejo anaonesha ucheshi wake akisema,

Mizinga sipigi oya oya/
Mirimba ni mingi ona ona/
Mziki nikicheza ni dakika nakaa/
Dj ananirusha na ratiba inafaa/
Juu najiachia ka na parachuti/
Watwana hawana vyao wanaona kama hapakuchi/
Wako jiko ila wakiarifiwa wanakua na baridi/
Wanarudisha chenchi ka wametumwa na bahiri/
Anaejidai mtata nae amekutwa mara mbili/
Ulinzi ka mbinguni au nimekuja na waziri/
Pigo za kihaya ukizileta ni mbaya/
Sana utajipresha,
Malaya wanabusu savana/
Mbwembwe zao zote zinahusu cassava/
Maji hayo marefu we una buku saa saba/
Fanya daka toyo sio kututazama./

Kwenye Sanaa Sali Trejo anapatikana solo kwenye wimbo mzuka sana ambao kiitikio ni sauti ya ki Acapella inayopigwa na Adam Shule. Sali anatuelimisha umuhimu wa sanaa sio tu maishani mwake bali kwa wote.

“Nikiwa na kipaji huwa na enjoy na ni ajira/
Basi nastahili kuajiriwa na hadhira/”

Pia kama alivyosema Lupe Fiasco kua Hip Hop saved my life Trejo nae anaonesha vile sanaa imekua muhimu sana kwake akisema,

“Sanaa umeniokoa umeniokoa sanaa/
Siwezi sema sina kazi wakati naukomboa mtaa/
Mshahara unadumaza/
Biashara zinafanya tunakaza/”

Mwana D.D.C Andre K japokuwa hayupo nasi tena amekumbukwa vyema kwenye mradi huu kwenye skit iitwayo G.S.A (Gangsta Still Alive) akiwa na Marehemu Ramso na kwa kweli wawili hawa bado wanaishi kwenye mradi huu. Japo kuwa skit ina furaha ndani yake inatuachia huzuni tukijua wawili hawa hawapo nasi tena!

Kaka Goda Mc anashika doria kwa wimbo unaozungumzia rasmi mshikaji wao Andre K. kwenye wimbo uitwao Mjue Mwana. Kwenye huu wimbo ndio utamjua mwanetu Andre K vizuri kwenye wimbo unaopiga mdo mdo sana.

Kupitia mradi huu wana Hip Hop na watu kiujumla wamepata chombo kipya cha kuwasaidiwa wajue wapi waelekee. DIRA hii itakutia moyo pale utakapohitaji kutiwa moyo, itakuonya pale unapotakiwa kuonywa,itakupa darasa pale utakapohitaji elimu, DIRA hii imeacha alama kwenye game la Hip Hop la Africa Mashariki.

Wasiliana na Dom Down Click kwa kupitia mitandao ya kijamii;

Facebook: Dom Down Click -Ddc
Instagram: domdownclick