Double Y aka Mnyama Double ambaye amejijengea jina kama mtayarishaji shupavu wa Hip Hop anayepatikana kule Dodoma Tanzania. Jamaa ana midundo ya kibunifu na kazi zake zimeskika kutoka kwa wakongwe wa Hip Hop na chipukizi wa hivi karibuni. Wimbo wake pia umetumika kama soundtrack kwenye kampeni iliyo anzishwa na Rais wa Muungano Wa Tanzania, Dr. Samia Suluhu Hassan, The Royal Tour. Twendeni tour ya gumzo letu mumfahamu mnyama huyu.
Karibu kaka Mnyama Double hapa Micshariki Africa. Unaitwaje rasmi, unatokea wapi na unajishughulisha na nini?
Kwa majina yangu halisia naitwa Yasini Yahya lakini jina maarufu najulikana kama Double Y au wengi wao hufupisha kwa kuniita Double. Mimi ni mzaliwa wa mkoa wa Dodoma na ninaishi Dodoma pia najishughulisha na utayarishaji muziki (producer) pia mtayarishaji wa matangazo ya biashara “voice over” na mengineyo mengi.
Tuanze kwanza kufahamu historia yako, ulizaliwa wapi, mpo wangapi kwenye familia yenu, ulisomea wapi kwanzia shule ya msingi, upili na umefikia wapi kimasomo, tukiongelea mifumo ya shule hapa?
Mimi ni mzaliwa wa Dodoma katika familia yetu tupo watoto 6 na shule ya msingi nilisomea Dodoma shule moja inaitwa Uhuru na Secondary nilisomea Dodoma pia katika shule moja inaitwa Jamhuri secondary School na elimu yangu ni Form 4.
Je hizi mbanga za utayarishaji ulianzaje? Uligunduaje kama una talanta ya muziki na utayarishaji na ulifanikiwa vipi kukuza kipaji hadi kufikia hapa ulipo ambapo ndio inakuwekea msosi mezani? Je unakumbuka mdundo wako wa kwanza kumuundia msanii ulikua upi, wa msanii gani na wimbo unaitwaje?
Mimi kabla ya kuwa producer kwanza nilikuwa msanii kwa muda mrefu ambapo nilikuwa nikirekodi kwa brother angu mmoja aliyekuwa Dodoma ana studio anaitwa Jomary kwa jina maarufu alikuwa anaitwa Dope. Huyo ndio mtu pekee ambaye alianza kunionesha njia kwenye muziki na kuanza kunifanya kupenda kuwa producer, heshima sana kwake.
Niligundua nina talanta ya muziki baada ya kufika secondary ambapo nilikutana na marafiki zangu Boni na Amani ambapo tulipelekea kuunda kundi la muziki tukiwa shule secondary mwaka 2003 lililoitwa B.A.Y ambalo lilikuwa maarufu na huo ndio ulikua mwanzo wa kujua vitu vingi kwenye muziki kiujumla na kupenda muziki na kadri muda ulivyo kwenda kutokana na maisha basi tukajikuta kwenye kundi wengine wazazi wao walikuwa ni waajiriwa wa serikali basi wakapelekwa mikoa mingine kwa hiyo nikabakia mwenyewe ambapo nikaanza safari mpya ya kujitafuta.
Hapo ndipo nilipojikuta napenda u producer na usanii japokua haikuwa rahisi kufikia malengo maana kwa kipindi kile familia zilikuwa na fikra za vijana wakianza kujihusisha na mambo ya muziki tu basi ni uhuni kwa hiyo ilikuwa ngumu sana lakini haikunifanya kuacha kufanya ninachokiamini na juhudi zilikuwa kubwa na ndio maana nilifanikiwa mpaka kufikia hapa nilipo na leo ndio imekuwa kazi yangu.
Ngoma yangu ya kwanza kuiproduce official ni ngoma ya kundi moja Dodoma linaitwa Central Zone na wimbo ulikuwa unaitwa Hasilazimisheni na haikuwa rahisi maana sikuwa nafahamu vitu vingi kwenye production lakini nilishangaa niliweza kufanya kila kitu mwenyewe kuanzia beat mixing mpaka mastering mwenyewe na wimbo ukawa na ubora mpaka uliweza kuchezwa kwenye vituo vya mbalimbali vya redio. Hatua ile ilinipa nguvu Sana 💪🏽.
Ni watayarishaji gani walikuhamasisha na wanakuhamasisha kila kukicha ndani na nje ya Tanzania?
Kwa miaka ya nyuma maproducer walionihamasisha kwenye production ni P Funk na Duke.
Mnyama Double, mbona sio Mnyama Single😀? Hili jina lako lilikujaje na linamaanisha nini?
Hahahahaha Mnyama Double limetokana na Double Y ambapo ni mchanganyiko wa herufi mbili zinazofanana kutoka kwenye jina langu na la mzee wangu, Yasini Yahya. Hizi Y, iliyopo kwangu na kwa jina la mzazi wangu ukizichanganya zinakuwa Y mbili ambapo tukiziweka kwenye lugha ya kigeni Inakuwa Double Y. kwa hiyo wengi wao huwa wanafupisha kwa kuniita Double tu wakaona pia sio kesi kwa kuniongezea jina lingine la Mnyama Double 😆.
Hili jina langu lilikuja baada ya kuwaza ni kwa nini nisichanganye na jina la baba yangu kwa sababu nampenda sana mzee wangu ndio nikaona basi kwenye jina langu ili likamilike ni lazima na jina la mzee wangu na ndio nikaamua kujiita Double Y kwani hapo ukilitaja jina langu la kazi jua umenitaja na umemtaja na mzee wangu pia na ndio maana hata baraka hazikai mbali na sisi 😆.
Tueleze historia yako na Watengwa, mlianzaje kufanya kazi na mmeunda miradi gani ya pamoja mpaka sasa?
Historia yangu mimi na Watengwa ilianzia kwa brother ChindoMan miaka kadhaa nyuma ambapo tulifanya wimbo wa kwanza nae ambao ulikuwa unaitwa Kipaza Tunacho Sisi ambapo alishirikishwa na Black Desert alitokea kuupenda sana huo wimbo na pia aliona kitu kikubwa ndani yangu na chemistry kati yetu basi kutokea hapo akawa na imani na mimi na kuanzia hapo tulifanya kazi nyingi zikiwemo za kwake solo na hata baadhi za kundi na nje na kazi Chindoman ni mtu aliyenisaidia sana kufikia malengo yangu shukrani kwake 🙏 .
Kando na Watengwa umeshafanya kazi na wasanii gani na kwenye kazi zipi iwe ni EP, Mixtape au album? Je singles si ni za kumwaga tu?
Nje ya Watengwa nimeshafanya kazi na wasanii wengi sana,(KadGo-Albam Kiutuuzima) (Songa-Albam Hisia za Moyoni), (Nash Mc-Pambana), (Mansuli - Albam Love Life), ( Ghetto Ambassador Nina Haja Nawe), (Chaba - Washawasha & Fungulia Maumbwa), (Memo-Ujuzi), (Mkoloni-Mori) Host Zee - One Step), Watawala Na Ukoo – Hizo pesa Za Kwetu) (Mturu - Mama), (Kanja Wizzle - Kungfu Kanja), (Ashunga - Albam Uso Na Ubongo), Elly wa Uswazi - Dom ID, kiukweli ni wengi sana siwezi kuwamaliza wote aisee ni wengi hao ni baadhi tu…
Nieleze kuhusu chemistry yako na ChindoMan inapokuja kwenye kazi maana kazi mkifanya pamoja inatoka freshi sana...na pia ulihusika pakubwa sana kwenye uandaaji wa album yake Kijenge Juu….
Kwanza sitakuwa mtu wa busara kama nisipomwambia brother ChindoMan shukrani sana maana ukimzungumzia Chindo unakuwa unauzungumzia muhimili wa muziki wa Hip Hop Tanzania na role model wa vijana wengi wa Tanzania na dunia kiujumla.
Mi nadhani ni Mungu tu kaamua kutukutanisha ili tukikutana tuweze kufanya kazi ambazo zikiwafikia watu zitakuwa zinawagusa na watazifurahia. Pia nadhani Chindo ni msanii pekee ambaye kama wasanii wengine wangebeba roho yake huyu mtu basi tungepata vijana wengi ambao wangefanikiwa nje na muziki, Chindo ni msaada mkubwa sana kwenye safari yangu, mambo mengi sana amenisaidia. Chindo ni definition ya Hip-Hop kiuhalisia kabisaa 💪🏽.
Jingle yako inayokutambulisha kwenye kazi ulizozisimamia hua inasemaje na ilikujaje?
Jingo ile huwa inasema "Double happene on dis one" na ilifanywa na msanii mmoja alikuwa anaitwa Slogan Lecture ambaye siku hizi kawa mwalimu. Yeye aliisema tu kwenye wimbo wake niliokuwa namtengenezea, mimi nikaipenda, nikakipenda nikakitengeneza ndio ikawa jingle yangu official
Mnyama pia unaimba si mchezo kwani nimekuskia kwenye chorus za ngoma kadhaa ulizoziunda, hili nalo vipi?
Yeah, namshukuru Mungu kanipa uwezo mkubwa sana wa kuimba na hata kurap na ikumbukwe pia kabla ya kuwa Producer nilikuwa mwanamuziki wa kuimba.
Wimbo wa Nuru Mturu, "Mama" ulimuwezesha Nuru kujinyakulia tuzo ya mwezi September 2022 ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards. Hii ngoma ilikujaje na je ulijiskiaje kuona moja ya kazi uliyoiunda kutambulika na kupewa tuzo?
Kwanza niseme shukrani sana kwa Micshariki Africa kwa Tuzo, ushindi wa Nuru Mturu ni ushindi wangu pia na hii imempa nguvu Nuru na mimi pia kwenye uandaaji wa nyimbo zenye maudhui mazuri na yenye kufundisha jamii.
Tueleze kuhusu D Sound Records, mnajishughulisha na nini pale na je ni miziki ya Hip Hop inapigwa pale au pia aina nyingine ya miziki?
D Sound Records ni studio inayojihusisha na kila kitu Gospel, Bongo Flava, Trap, Hip-Hop Nyimbo za Asili nyimbo za Dance Pamoja na utayarishaji wa matangazo ya Redio na Tv.
Tueleze mchakato wa kuandaa mdundo na ngoma toka upate wazo liwe ni lako au la msanii, huwa unakuaje?
Kwanza kujua ni aina gani ya muziki anataka tuufanye, kusikiliza idea yake na kuanza utengenezaji mpaka kukamilisha.
Kama mtayarishaji je chaka hili linakulipa na linakupa heshima unayo stahili?
Mi nadhani kwanza kwenye maisha ukifanya kitu unachokipenda huwa kinakupa amani na furaha wakati wote ila pia naendesha maisha kupitia kazi hii ila pia kazi hii inanipa marafiki na maadui pia kwa hivyo kuna watakao kuheshimu na watakao kukosea heshima maana kila mtu ana mtazamo wake.
Muziki unakulipa bro au pia unapiga mishe zingine ili kuweza kujikimu?
Unatulipa kwa kiasi ndio maana mpaka leo tunafanya ingawa inakuwa tofauti na nchi zilizoendelea ambazo mifumo yao ni tofauti na mifumo yetu ila pia najishughulisha na ufungaji wa sound proof sehemu zozote zinazohitaji kuwa na soundproof kwa ajili ya kelele za nje kuingia ndani au kelele za ndani kutoka nje.
Kila kazi na changamoto, zako kama mtayarishaji?
Changamoto ni nyingi wakati mwingine tunapata vijana wengi wenye vipaji lakini wanakosa watu wa kuwawekezea nguvu ili kufikia malengo yao na tunajitahidi kuwafanyia vijana kazi nzuri lakini zinakuwa ngumu kupata nafasi kwenye redio kwa sababu ya mifumo iliyopo sasa, ubinafsi, ujamaa na hela.
Una neno gani kwa ajili ya wasanii chipukizi ambao wanataka kujitosa mazima kwenye Sanaa na Muziki?
Mi nadhani kwa sasa ni vyema vijana wakaweza kufanya muziki huku pia wakiwa na kitu kingine cha kufanya ambacho kitakuwa kikimuingizia kipato maana muziki wa sasa unahitaji kuwekeza Zaidi.
Neno la mwisho na watu gani ungependa kuwagotea ambao wamekua nawe kidete kwenye hii safari yako ya muziki.
Kikubwa cha kuwaambia watu wangu nawapenda sana na shukrani sana kwa kupenda ninachokifanya na pia shukrani kwa baba na mama yangu kwa kunisapoti wakati wote. Shukrani kwa watu wote wanaopenda ninachokifanya.
Tumalize kwa kupata mawasiliano yako na anwani unazotumia kwenye mitandao ya kijamii.
Namba yangu ya simu ni +255719818136 au nicheki
Instagram: mnyama_double
Email: yassinyahya44@gmail.com
Shukran kwa mda wako.
Shukran kwa mda wako pia.