Kwa kawaida mtu anaposikia neno Black Ninja picha inayokuja fasta akilini mwake ni ya mtu aliyevaa nguo nyeusi mwili mzima na pia kuziba uso wake wote isipokuwa macho yake ili kuzuia watu wasimuone sura na kumfahamu. Pia mtu huyu mara nyingi hubeba upanga mgongoni ambao ni silaha yake kuu anayoitumia kujilinda na kulinda jamii yake.

Kwenye ulimwengu wa Hip Hop,Tanzania kuna Black Ninja ambaye yupo tofauti kidogo. Kitu ambacho ni cheusi pekee mwilini mwake ni ndevu zake zinazong’aa kwenye kichwa ambacho mara nyingi kanyoa upara. Silaha yake kuu ni kinanda, kinasa, kipaza na studio inayomuwezesha yeye kufanya kazi ya kusaidia wana Hip Hop kuunda miradi yao. Black Ninja huyu ni producer toka  studio za Boombap Clinic (B.B.C) Dar Es Salaam.

Kazi zingine alizoziandaa Black Ninja;

12code - Nicas
Amphoterick Tz - Zungusha
Nikki Mbishi - #999
Olulock x Naah - Thanks Lord
Black Ninja ft Black fire - Tofauti

Leo tumepata fursa ya kufanya mahojiano na Dr. Black Ninja, karibu umfahamu...

Black Ninja ni nani, kazaliwa wapi na anatokea/kupatikana wapi? We ni muunda Midundo tu/beat maker au producer?

Black ninja ni DJ pamoja na producer pia ni music engineer by professional kutoka Chuo kikuu cha Dar Es Salaam (uDSM), mimi nimezaliwa Mbeya mjini -Ilolo natokea Mbeya.

Jina lako la kwenye kitambulisho ni nani ?

Kwa majina ramsi naitwa Shakur Leonard Mussa Matonga.

Kwanini unajiita au unaitwa Black Ninja? Jina lilikujaje na linamaanisha nini?

Black Ninja ni jina alilonipa marehemu mama yangu Binti Sophia kwakuwa nilikuwa napenda sana video za ki Ninja. Watu toka utoto wangu pale Mbeya waliniita Ninja mweusi nikiwa na miaka 12 hadi leo.

Kwanini wajiita Doctor Black Ninja, ulihitimu na phd ?

Dr kwakuwa natoa tiba kwenye zahanati. Eeeh dingi mie ni Dr by professional pia na music engineer kutoka Chuo kikuu cha mlimani(akicheka!)

Ulianzaje shughuli ya u producer na ni kipi kilichokupatia motisha kubaki hapo?

Mziki bhana haikuwa ndoto yangu ni shida tu zilifanya niwe kwenye muziki lakini naweza sema mwisho ikawa kama destiny yangu. Nimefundishwa muziki na Kibabu wapoteen pamoja na Duke Tachez hao ndio walioniingiza humo. Kwa kuwa producer ni mtu accurate pia genius kwahiyo ni rahisi kufanikiwa.

Je unatengeneza aina gani ya miziki?

Natengeneza mziki wa Rap na RnB.

Ulishawahi kuwa na shaka kuwa utafanikiwa kwenye hili?

Sijawahi kuwa na shaka juu ya hili.

Ni kipi kilichokusukuma usiache fani hii ?

Kwa kuwa  jukumu la kuijenga jamii kifikra na kuikomboa ni la kila mtu mwenye uelewa, kwa hiyo hii sio fani tu, ni jukumu langu juu ya jamii yangu.

Ilikuchukua muda  gani hadi  kuanza kusikika na kutambulika kama producer?

Ilinichukua miezi mitatu kuwa producer mkali.Yote ni kwa sababu ya shida na elimu ya ubamizaji toka kwa mwalimu wangu Kibabu.

We hupata vipi wateja wako?

Napenda kutumia vijana wapya kwenye game wanaoamini uwezo wangu pia kuwasikiliza juu ya mfuko wao inanisaidia kuwapata na kujikimu.

Ungetoa ushauri gani kwa yoyote anayependa kufuata nyayo zako?

Awe yeye tu asiwe mie.

Ushawahi kupata kazi kutoka wasanii wa nchi za nje?

Yeah nimefanya kazi na Havoc toka Mobb Deep, Npaz.  Nilifanikiwa kumuuzia mdundo marehemu DMX kabla ya kifo chake na pia nimefanya joint nyingi na wadau wa nje pia Kenya, South Afrika pamoja na Uganda.

Nini unachokiona kilicho tofauti kati ya Hip Hop ya mamtoni na hii ya East Africa? Ni kipi wao wanachokifanya tofauti ambacho sisi tunaweza kujifunza toka kwao?

Hip hop haina tofauti ni ile ile ila watu ndo wako tofauti wanaofanya rap music ni lazima wawe tofauti kwa kuwa tupo tofauti.

Umeshafanya kazi na ma emcee gani na kwa miradi gani?

Nimefanya kazi na Nikki Mbishi, P The Mc, One The incredible, Songa, Mansuli, Zaiid, Mex Cortez, Cado Kitengo, Watunza Misingi, Baby Boy,Maujanja Saplayaz, Xp, Prime Number, Homan, Plate Mdaijasho,, TK Nendez, Bassat,Mbize The Poem Kid, Phina The Truth, Fivara, Rabi James, Dibo Emcee, Bad Ngundo, Papa Frege.  Ma emcee zaidi ya 300 pia ngoma zaidi ya 500 kwa handaki wengine siwezi kumbuka wako wapya zaidi ya 60. Miradi pia ni mingi mingine sikumbuki. Kay Wa Mapacha (Og), Mbize The Poem Kid (The seed EP), Rabi James (Ep and album) sikumbuki maana ni mingi pia zaidi ya 100!

We upo chini ya umiliki wa studio ya mtu au unamiliki studio yako mwenyewe? Tueleze kuhusu B.B.C, Historia yake kidogo?

Niko chini ya ofisi yangu mwenyewe . Boombap clinic ilianza 2015. Mi mwenyewe ndo niliyeunda na kuwaza kwa lengo la kuwa na zahanati ya Boombap baada ya mwaka fulani hapo Boombap kupoa ila nashukuru sasa nipo na wasanii pamoja na producer mwingine 10th Wonder. Wasanii  ni Trickson, Rabi James, Dibo Mcee, Fedoo BoyCa, Bad Ngundo pamoja  Papa Frege.

Ile sign tune Yako ya “BBC once again” ilikujaje?

Ile ilikuwa 2018 niko na Phina The Truth(dadake mdogo) studio akaipiga. Sasa nilipo kuwa naisikiliza alivyo ingiza nkaona mbona kitu chenyewe na baadae mke wangu akasema, "Hii B.B.C once again tamu sana!”.

Boom Bap Clinic (B.B.C)

Je unaelezeaje mtindo wako wa kufanya kazi na msanii?

Napenda kufanya kazi hapo kwa hapo kuanzia mwanzo ili tupate kitu kizuri.

Je wewe ni mdonoaji? Udonoaji na ubamizaji ni nini?

Mimi nahusika na udonyoaji. Udonoaji ni usampulishaji(sampling) katika Boom bap. Ubamizaji ni kupiga midundo

Ni wimbo gani au mradi gani unaoupenda sana ambao uliufanyia kazi?

Kazi zangu zote nazipenda sana kuzidi kitu chochote kwa kuwa nafurahia ninacho kifanya.

Gharama zako kwa kazi hii ni kiasi gani?

Laki moja kwa wasanii wachanga laki 2 kwa wasanii wa kiwango cha kati.

Umekuwa ukiskiliza mziki wa aina hivi karibuni?

Sifuatilii juu ya hilo.

Je ni jambo gani moja ambalo kila wimbo lazima uwe nalo ili uwe thabiti?

Uwasilishaji umbo la wazo la huo muziki ulio kichwani ndo uthabiti.

Ni nani mtayarishaji bora wa muziki anayefanya kazi katika tasnia hii leo unaye mkubali?

Wote wanao piga Boombap beats nawakubali sana.

Nje ya muziki Black Ninja hujishughulisha na nini?

Muziki only. music ndo taaluma, ndo kazi, ndo maisha.

Ni watayarishaji gani,waimbaji au wasaniii waliokupa motisha yako ya msingi?

Havoc wa Mobb Deep, DJ Premier, Peter Rock, Kibabu Wapoteen, Duke Tachez.

Unazungumziaje game ya underground hip hop /handakini toka Tanzania na Africa Mashariki?

Sina neno kwa kuwa sioni cha kusema naona bado mapema.

Je ni masomo gani muhimu ambayo umejifunza juu ya kutengeneza midundo ambayo ma producer pamoja na wasanii chipukizi wanaweza kujifunza?

Music theory, piano instructions, selection of instrument.

Una miradi yako binafsi iwe ni EP, mixtape and albam ambayo ulishawahi iachia sokoni?

Yeah ipo kuna EP tatu sasa, The Compound, Balibaza, Watema Rhymes  na kila mradi unapatikana kwa elfu Tshs 3000/= tu!.

Niliona mna mpango wa kufanya kazi na Tenth Wonder, hili unalizungumziaje?

Ni producer aliye Boombap Clinic (B.B.C)

Tutegemee nini toka kwa Black Ninja na team yote ya B.B.C hivi karibuni na baadaye?

Tutegemee ulinzi na uzalendo juu ya kutunza nguzo na utamaduni wa Hip Hop na Boombap.

Ni nini cha mwisho unachoweza kutuambia ki ujumla ambacho sijakuuliza?

Naipenda Hip Hop hicho ndo ulisahau kuniuliza.

Peace yooh!

Wasiliana na Black Ninja kupitia mitandaoa ya kijamii:

Facebook: Blaq Ninjh(Black Ninja)
Instagram: black_ninjaah
Boombap Clinic(B.B.C) - boombapclinic