Wasanii: Duke na Bokonya
EP: Beat and Rhymes EP1
Tarehe iliyo toka: 01-08-2020
Nyimbo: 5
Utayarishaji wa beat: Duke Tachez
Studio: MLab Records
Japo kua mwaka wa 2020 utakumbukwa sana kwa maambukizi yalioikumba dunia hii ya Uviko 19 yaliyo anzia China, kuna kirusi kilicho tokea Tanzania mwaka huu pia. Kirusi na madaktari wawili walio bobea kwa fani zao, “Dr.” Duke Tachez (Phd, Beats Productions) na “Dr.” Bokonya (Phd, Emcee Handakini).
Wawili hawa waliungana na kutupa kirusi kiitwacho B&P-EP1 ambacho ishara moja wapo ya kuonesha kua umedhurika ni ku rudia rudia mistari ya EP hii wakati ikichezwa na pia kichwa cha aliedhurika kutikisika pole pole kuonesha ngoma za EP kirusi zimepenya hadi moyoni.
Harakati za kutengeneza kirusi hiki kilichopewa jina B&P-EP1 kilianza kutengenzwa kama ifuatavyo,
1. Tunaset
Kutoka kwa formula za beat ya nyimbo hii unapoanza kudondoka toka kwa madaktari hawa wawili wanapo kua maabara ya MLAB unaashiria kua kinachofuatia ni uvumbuzi hatari. Wanaanza kukutahadharisha kua mpira wa mapenzi hauwezi kuzui hichi kirusi,
“Condomu usiziamini sana/
Punguza kuwavua chupi/
Ukweli mzuri ila ukifikishwa vibaya unabiua chuki! /
Bokonya anaangusha mistari ya msingi kuonyesha nia yao ni “kusambaza ujumbe kila kona!” Bokonya anaachia madini muhimu kwa watu wa kila umri,
“Akiba ni muhimu sana usipo weka /
Utapata tabu, yani utajichoresha/
Ukubwa chuo kikuu, wengi wanajisomesha/
Mitihani migumu sana kuliko NECTA!”
Tahadhari pia anatoa kwenye huu wimbo akisema,
“Jitoe kwenye danger zone/
Ukiona ukweni kuna kiwanja, usishoboke, jenga home! /”
Umakini wa mistari hii inaonyesha vile Bokonya yupo makini na anacho kichana..
Setting ilikua ya ustadi wa juu toka kwa ma “doctor” hawa wawili ki Beat na ki Rhyme
2. Usipende wakimshirikisha TK Nendeze
Duke ana anza beat kwa tarumbeta inayo jirudia rudia kama neno “usipende” kwenye huu wimbo wenye beats nyororo ambazo zinataka kusisitiza ujumbe. Ujumbe huu lazma uta taja kitu kimoja ambacho unakifanya maishani mwako ambacho si kizuri, hadi unaweza hisi pengine Bokonya amekufahamu mda mrefu. Kiitikio tu ni onyo tosha pale anapo imba kwa sauti nzuri dada TK Nendeze akisema,
“Usipende kaa upande wa uwongo/
Usipende roho ya kinyongo/
Usipende kuharibu michongo,
Usipende dhuluma, tumia ubongo !”
Kwa vesi ya kwanza anaanza kutoa amri kama Musa mlimani Sinai akisema,
“Usipende kuhukumu/
Usipende kusengenya/
Usipende kudhulumu/
Usipenda kukaa na duku duku!”
Na wakati aki washauri polisi, anamkumbusha raia wa kawaida majukumu yake pia,
“Polisi usipende kutuwinda/
Kwani ninavyojua mimi, wajibu wako ni kutulinda/
Usipende rushwa, usitoe wala kupokea/”
Kwenye vesi ya pili anaanza kwa kuongea na mashabiki wa hip hop akikumbushia haya,
“Hip hop ni shule usipende kutoroka/
Kua mkweli nakushauri usipende kuongopa!”
Je dada zetu wanashauriwa chochote na Bokonya? Ndio,
“Binti ji hadhari na vishawishi/
Ukitongozwa usipende kukubali kirahisi!”
Nyimbo ina vesi tatu na imejaa madini kibao kushinda mgodi wa Mwadui. Lazma itakugusa atakapo taja mapungu flani ambayo unaweza kua nayo.
3. MC
Japo kua Bokonya ndie “Doctor” alie gundua kirusi cha B&R-EP1 kwa wimbo huu anataka kukumbusha kua yeye ni MC kwanza. Anaonyesha vile yeye ame enea kila mahali kama Covid pale anapo anza vesi yake,
“Mi ni sauti ya mtaa, MC balaa/
Ujuzi umenijaa, hadi najishangaa/
Na burst zaidi ya tairi, kila mdundo naufaa/
Mimi sio kiti, ila kwangu hua na kaa!”
Pia Bokonya anatuonyesha kua kirusi hiki ambacho chanzo chake kikuu ni Hip Hop genes kimemuathiri akisema,
“Wana niita Bokonya MC, muathirika wa rap/
Nasambaza ngoma kwa jamii!”
MC ni nani?
“Mi ni MC, MC, mi ni Mc, naitoa gizani jamii/
Mi ni MC, MC, mi ni Mc, nafundisha, utadhani nabii”
Wanavyo endana Duke na Bokonya kwenye hii EP ni kama Ying na Yang au kama walivyokua ma legendary wa Hip Hop Gangstarr - Guru na DJ Premier.
4. Bokonya Barz
Skiza hii
Wimbo huu ndio mfupi kuliko nyimbo zote zilizopo kwenye EP hii. Chini ya dakika tatu Bokonya hapa anaachia mistari bila kiitikio ili kukueleza yeye ni nani kwa mfano,
“Usicheze na mimi, ala ala, /
Wakali wako wachumba, nunda na wanawa/
Sina budi kuwa bamba mashabiki/
Mi ni nyota inayong’aa kwenye anga ya muziki/
Sishindani na watoto wajuzi/
Waloanza ku chana baada ya Ngwair na Langa kufariki! /
Mkali wakupanga maandishi /
Napita kama nyoka kwenye shamba la Mitiki/
Natamba juu ya biti,
Kutema vina kwangu ni simple kama ngedele kudanda juu ya miti!
Hua situlii, naranda kila streeti/
Mhangaikaji natafuta mkwanja ili niishi/
Na nikizipata nazichanga, najidhiki/
Mwisho wa siku lazima kibanda ni miliki!”
Bokonya ni MC mwenye malengo.
5. Super Sub
Kwenye soka Super Sub ni mchezaji anae weza kubadili matokeo ya mchezo. Bokonya hasiti kujiita Super Sub maana anaamini uwezo wake wa uandishi unaweza kubadili game la Hip Hop!
Anaanza kujisifia hivi,
“Kudada deki, mi ni mchafu kama mzibua choo/
Ukileta zakuleta na kuzingua bro/
Hii game sipotezi, wala haiwezi kua draw/
Niimejipanga msimu huu, nachukua doo! ”
Pia anamalizia kuonyesha vile B&P-EP1 ni kirusi noma kwa kusema,
“Mchizi wa mistari, kilinge kwangu ni concert/
Style yangu ngumu, iige upate tonsils! “
Je upo tayari kwa kirusi hiki hatari kilicho achiwa toka maabara ya MLAB kukuambukiza? Ukiambukizwa lazma utabaki ukienzi na kuthamini vile mahandaki ya Hip Hop ni muhimu kwa utamaduni huu wa Hip Hop.
Kupata nakala yako ya mradi huu wasiliana na Duke Tachez kupitia;
Facebook: Duke Gervalius
Instagram: duketachez