Duppy Beatz

Duppy Beatz ni mmoja wa watayarishaji wakali kutoka nchini Tanzania. Mtayarishaji huyu kando na kuwa music producer ni mwandishi wa nyimbo, mhandisi wa mixing & mastering, anapiga kazi za voice over, ni copywriter, ni tv host, ni artists manager pamoja na C.E.O wa Uprise Music Empire.

Karibu sana Micshariki Africa kaka Dupy Beats. Kwanza tungependa kukufahamu majina yako rasmi, unatokea wapi na unajihusisha na nini?

Kwa jina langu la kuzaliwa naitwa James Salvatory Relai. Ni mkazi wa Mbagala Chalambe, Dar Es Salaam Tanzania. Kabila ni Mwera wa Lindi, Mkoa wa Lindi Kusini. Najishughulisha na shughuli za uzalishaji sauti pamoja na uhandisi sauti na utayarishaji, sauti, muziki, ni producer wa muziki na pia natengeneza sauti au voice over za matangazo mbali mbali, identity za radio na images za radio na pia TV host, kipindi elsio cha TV lakini pia ni meneja wa artists. Kuna artists wawili ambao nawasimamia; Waddy B na Mullah The Matrix.

Pia ni mixing and mastering engineer, huwa nafanya final kwenye muziki wa kila aina.

Playlist ya Dupy Beatz hii hapa (gusa link)

Tupe historia yako ya nyuma kidogo, kaka ulizaliwa wapi, ulisomea wapi shule za msingi na upili na baada ya hapo uliendelea hadi wapi? Kwenye familia yenu mpo wangapi na utoto wako ulikuaje?

Mimi ni mzaliwa wa Dar Es Salaam, nimezaliwa Muhimbili pale miaka thelathini na kitu iliyopita na pia ni mwenyeji wa mkoa wa Lindi kwa upande wa baba (kabila ni Mwera) ila kwa upande wa mama kabila ni Muhaya eeh wa Bukoba, Kaskazini.

Mimi pia nimeanza elimu ya Chekechea kipindi nipo Sinza, Sinza Makaburini, miaka hiyo ya tisini lakini baadae nilianza shule ya Mapambano, darasa la kwanza mpaka darasa la nne. Baadaye tulihama kutoka Sinza mpaka Mbagala, Charambe, ambapo niliendelea na shule ya msingi katika Shule Ya Msingi, Msasa na baadae kuweza kufaulu kuingia shule ya upili ambayo ilikuwa ni Dar Es Salaam Secondary School kwa ajili ya O-Level. Kipindi hicho tulikuwa na msanii mkubwa tu Mr. Blue, na kina Ben Pol na pia Stereo Singa Singa na wasanii wengine mbalimbali.

Baada ya O-Level niliendelea advanced na kusoma pale Jitegemee JKT na baadaye chuo ambacho kwa bahati mbaya nili drop out, nilisoma pale CBE.

Kipindi cha utoto wangu nilikuwa napenda sana vitu vingi vya asilia vya Tanzania, michezo ya kitoto ya kitanzania ambayo sidhani kama watoto sasa hivi wanaimba kama vile “Kombolela”, “Kidali” na vitu kama hivyo lakini pia back then nilikuwa napenda sana simulizi.

Nakumbuka kipindi kile naishi Sinza kulikuwa na utaratibu wa mgao wa umeme ilikuwa miaka ya tisini basi shangazi yangu na dada yangu mkubwa walikuwa na utaratibu wa kutuhadithia hadithi. Walikuwa wanatuweka pale, tunakaa wanatuhadithia hadithi na vitu kama hivyo.

Lakini pia kulikuwa na show za TV ambazo nilikuwa nazipenda sana kutoka kwenye nchi mbali mbali hususan Marekani kwa mfano, “The Living Single”, “21 Jump street” kulikuwa na movie kama vile “Wamaasai Na Ng’ombe Zao” ya marehemu Anachia, watu wengi hiyo movie watakuwa wanaikumbuka. Tamthilia kama za Dr. Cheni, zamani sana kabisa naona kabla ya “Kaole”, “Mambo Hayo”, akina Bishanga Bashaija, “Richy Richy” enzi zile, kulikuwa na vitu ka “King Majuto”, kulikuwa na show kama “Life Goes On” na vitu kama hivyo. Vitu vingi sana, back in the 90’s si unajua tena, “Fresh Prince (Of BelAir)” na vitu kama hivyo vilikuwa vimenijenga sana na ukicheki na pia kucheki ma katuni ya Disney, Hollywood. Moja ya ndoto yangu ilikuwa kuja kutengeneza filamu na katuni Tanzania.

Safari yako ya muziki ilianzia wapi na lini, tupeleke way back kaka ili tuweze kufahamu chimbuko la huu utayarishaji wako?

Actually safari yangu ya muziki rasmi ilianzia baada ya siku moja nilipokuwa mdogo na ku tune kwenye TV nikamuona Tupac kwa mara ya kwanza alikuwa aki peform “California Love” na Dr. Dre. Kisha baadaye nikaja kumsikiliza mwanadada hayati Aaliyah pamoja na Timbaland, nilikuwa napenda vile midundo inavyokwenda, kwa hiyo ikawa kwenye damu yangu na mimi siku moja nije nijifunze vile midundo inatengenezwa. Safari yangu ilianzia hapo.

Kwa hiyo nikawa napenda kupiga beat tu mdomoni, beat boxing na nini kipindi nikiwa mdogo, baadaye nilikuja kuingia kwenye band ya shule ya msingi kama band master msaidizi lakini pia baadaye ndoto zangu kubwa ni kuja kuwa mtayarishaji mkubwa wa Tanzania. Kwa bahati nzuri kulikuwa na watayarishaji wengi Tanzania ambao walikuwa wanafanya muziki kama vile P-Funk “Majani”, Master Jay, marehemu Roy na wengine mbali mbali.

Kwa hiyo nilikuwa napenda kukaa muda mwingi nasubiri kuskiliza midundo ya bongo flava. Eehe pamoja na ndoto yangu ambayo kidogo inahuzunisha nilikuwa nimepanga kua siku nitakayomaliza O-Level nitaenda kumtembelea producer marehemu hayati Roy ila kwa bahati mbaya alifariki kabla sijakutana nae.  Hivyo basi nikaendelea kujifunza kupiga instrumentation mimi na kijana mmoja ambaye anaitwa Saddam lakini baadaye nilipata nafasi Juma Nature aliniskia akanikaribisha studio kwake then kama wanavyosema the rest is history.

Lakini baada ya hapo niliendelea kujishughulisha kuendelea na uundaji wa muziki kwa sababu ni kitu ambacho nilikuwa napenda sana, nilikuwa inspired sana na ma producer mbali mbali kutoka nje na ndani ya nchi.

Mbona unatumia jina la kazi, Dupy Beats, lilikujaje na linamaanisha nini?

Jina langu mimi la awali nilikua naitwa J. Lee ambayo ilikuwa ni initial ya jina langu yaani James Lilai. Lakini later on nilikuwa na rafiki yangu anaitwa Leo Mysterio ila jina lake rasmi anaitwa Haji Mwalimu, yeye alikuja kujiita H Lee mimi nika change jina kutoka J Lee nikawa najiita J Lizo lakini baadaye Leo alikuja kunibadilisha jina na kuja kuniita Dupy.

Dupy ilikujaje? Dupy ilikuja kipindi kile wakati tunajifunza kuunda midundo 2005 kutokana na midundo yangu ilikuwa inamvutia sana leo akanipa jina la Dupy. Mara ya kwanza nilijaribu kulikataa lakini akanielezea maana yake ni “Diamond Unique Producer for Years” kutoka initial zake ndio limetoka neno DUPY lakini later Beatz, ikaja DUPY Beatz

Pia nafahamu kuhusu studio ya Uprise Music. Tueleze kuhusu chimbuko la studio hii nini kilichokusukuma kuifungua, changamoto ulizozipita wakati ulipoanza na nini mnakifanya hapo Uprise Music. Gharama za kazi zikoje?

Yeah, chimbuko la Uprise lilikuwa kama masihara, tulikuwa tuko chumbani tukitoka shule na nini, wajua kihela kidogo unabana, ukipata kidogo unaenda kununua subwoofer, kipindi hicho unajua hata ku afford computer ilikuwa ngumu.

Lakini baada ya passion ya mda mrefu ya mimi kupenda kutayarisha mziki, nitoe pongezi kwa marehemu mama yangu (Mungu Alamlaze Pema), yeye ndio mtu wa kwanza ambaye aliona kuna kitu ndani yangu katika utayarishaji wa muziki ingawa yeye hakufahamu utayarishaji wa mziki ni nini. Alichokuwa anajua nilikuwa nampigia kelele tu, “Mama nahitaji computer”.

Kwa bahati nzuri au mbaya kuna hela flani iliingia kwa wazazi wangu lakini mama alichokifanya alijaribu kuchomoa hela kidogo katika zile hela za baba akanikabidhi akaniambia, “Mwanangu unataka computer, shika hii hela kanunue computer.” So nilivyoenda kuchukua ile hela kununua computer, safari yangu ya mziki ilianzia hapo rasmi.

Baadaye tukaanza kufanya beats, nikawa nafanya beats nyumbani na yule rafiki yangu Saddam alikuwa anafanya beats kwao, kwa hiyo tukawa tunashirikiana sana.

Lakini mimi wakati ule sikuwa na jina la studio, Saddam alikuwa na studio yake ya chumbani alikuwa anaiita Prising lakini mimi baadae niliweza kupata "fund" katika zile hustle zangu na kufungua studio. Ubaya nilikuwa sina jina, nikamwambia Saddam, “Saddam, inakuaje mimi nikachukua hili jina la Prising?” Saddam akaafiki kwani japokuwa alikuwa anapenda kugonga beat hakuwa na interest ya kuwa producer mkubwa kwa sababu yeye tayari alikuwa ana njia yake nyingine ya kufanya maisha yake hapo baadaye.

Saddam alinipatia lile jina la prising lakini baadaye nilichokuja kukifanya mimi, nili edit kidogo kutoka Prising na kuiita Uprise Music Empire ndio likaja jina la studio yetu.

Gharama zetu sisi ni za kawaida. Kwa mfano sasa hivi kuna huduma mbali mbali hapa studio za Uprise Music kwa mfano utengenezaji mziki, utengenezaji matangazo, utengenezaji voice over na vitu kama hivyo. Lakini kwa kawaida bei ni ya kawaida ya msanii mkubwa kurekodi ni Tshs 1,000,000.00 lakini kwa msanii upcoming, chipukizi ni laki tano. Lakini pia kwa huduma ya mixing na mastering  ni laki mbili, lakini bei ya matangazo ni ya kukaa na kuzungumza.

Changamoto za kufungua studio nilikutana nazo nyingi sana. Wengi watu hawakuweza kuamini kuwa naweza kufungua studio kama huku kwetu Mbagala, Charambe na ika survive kwa sababu huku kuna studio nyingi sana zishafunguliwa na zikafa lakini moja ya studio ambayo imeweza kukaa mda mrefu Mbagala ni Uprise Music. Studio kubwa Mbagala na Temeke ni Uprise Music lakini kuna studio nyingine nyingi tu zipo ila moja ya studio ambayo ni kubwa ambayo imefika mbali sana kutoka Mbagala ni Uprise Music

Jingle inayokutambulisha kwetu ya “Haha, Uprise Music Baby!” ilikujaje?

Nikizungumzia studio tag au jingle yetu ya studio ambao inaanza kama kicheko cha mdada mwenye sauti nzuri na kusema lile neno la “Uprise Music”. Huyu dada kwa jina anaitwa Wilansia Bless Lema. Ni mmoja wa marafiki zangu wakubwa sana, ni rafiki yangu zaidi ya miaka kumi na tatu sasa hivi.

Ni mtu ambaye nilikutana naye mwanzoni kabisa kipindi nafungua studio ya Uprise Music 2010. Alikuwa amekuja kufanya collabo ya mtu mwingine lakini kutokana na uwezo wake alivyokuwa anajua kuimba ndipo nikakaa nikamuomba, “Dada kwa nini usiweze kunifanyia jingle?” Mimi ndio nilimpa maelekezo kuwa acheke mwanzoni halafu ataje studio title yangu pale, Uprise Music Baby na vitu kama hivyo. Nilikuwa nimemwambia aitaje in a sexy way ndio ikatokea hiyo jingle ya Uprise Music Baby!, mpaka kuja kuona studio kibao nazo pia zinaiga lakini it’s all good, kwa sababu mwisho wa siku it’s all about the money!

Kwa hiyo hapo ndio jingle ilipotokea. Shout out kwa dada Wilansia Bless Lema kokote alipo.

Wakati ukianza kama mtayarishaji je ni mdundo au ngoma gani uliyoiandaa ambayo unaweza kusema ndio ilikufungulia milango ya mafanikio yako kama mtayarishaji?

Ngoma ni nyingi sana ambazo nilikuwa nimezifanya ukizingatia kuwa studio baadae ilikuja kufanya kazi na wasanii wakubwa. Kwa kipindi kile tulifanya kazi na msanii mkubwa kama AT, tulifanya kazi na WCB, tulifanya kazi na Yamoto Band na wasanii wengine mbali mbali kama Izzo B.

Lakini ngoma ya kwanza kabisa kuweza kutambulishwa radio nilikuwa na kundi langu ambalo lilikuwa linaitwa Chikwaso na ilikuwa ni mixtape inaitwa “Chikwaso Mixtape” kwa hiyo tulifanya ikatambulishwa lakini baadaye singo ambayo ilienda viral, mbali kidogo ilikuwa ni wimbo wa “Tummoghele” ambayo tuliifanya na Izzo Bizness na ushirikiano wa Master Jay.

Je kutoka enzi zile uanze kama mtayarishaji mpaka sasa, nini kimebadilika kwenye utayarishaji wako pamoja na miundombinu ya utayarishaji na imeathiri kazi zako kwa kiasi gani?

Mabadiliko, kuna mazuri kuna mabaya, wajua hii ni safari. Back in the days sikuwa na utaalam mwingi sana ukilinganisha na sasa, hivyo niliweza kujifunza taaluma ya utengenezaji mziki na uboreshaji wa kazi za sanaa ikiwemo kuweza kukaa na baadhi ya ma producers wakubwa na kunishauri.

Pia kuweza kutumia mda wangu mwingi kusoma YouTube na vitu kama hivyo na kwa hiyo changamoto ni nyingi sana nimekutana nazo, milima na mabonde. Nilikuwa na vifaa hafifu lakini sasa hivi namshkuru mwenyezi Mungu kwa hapa nimefika na vitu ambavyo nipo navyo, naendelea kutengeneza legacy.

Changamoto ni nyingi sana nikisema nizielezee hapa itakua hadithi ndefu sana, people come and go kwenye biashara ila namshkuru Mungu tunaendelea kupambana na hizi mbanga.

So wakati ukianza je wana familia walikuchukuliaje au walikupa sapoti kwenye hii safari yako ya muziki tokea hapo mwanzoni?

Ah kwa bahati nzuri kipindi naanza hizi harakati za muziki, familia ki ukweli ilinipa sapoti 100% kwa sababu waliamini kwamba ndio kitu ninachokipenda na basi wao wakakunjua moyo wakanipa sapoti zote, familia yangu yote ilinipa sapoti kwa hiyo hakukuwa na changamoto zozote kupitia familia yangu tofauti na kuendelea kunitia moyo na kuendelea kuniombea.

Una zaidi ya muongo mmoja kwenye hili game kaka…kwanza tuanza kwa kufahamu wasanii ambao umeshawahi kufanya nao kazi…

Wasanii ambao tushawahi kufanya nao kazi hapa katika studio ya Uprise Music ni wengi sana. Kuna wasanii wengi ambao hawafahamiki lakini pia nakumbuka nishawahi kufanya kazi na Nameless na Baby Madaha japokuwa haijawahi kutoka, nimefanya kazi na kundi langu la Chikwaso, tumefanya kazi na Stamina, Songa, AT, Harmonize, pia kuna collaboration ya Harmonize na Daimond, tumefanya kazi na Izzo Bizness, tumepiga kazi na Shaa! Pia tumefanya kazi na Mansu Li, tumepiga chaka na Nuhu Mziwanda, tumefanya kazi na Lady Jaydee, H Baba na wengine wengi wengi tumepiga nao kazi kupitia studio ya Uprise Music.

Pia ningependa kujua ni kwenye miradi gani na ya wasanii gani ulishawahi kufanya kazi nao iwe ni EP, Mixtapes au hata albums

Wasanii ambao nimefanya nao EP ni Izzo Bizness, Nuhu Mziwanda, Mansu Li na pia H Baba. Na wasanii ambao nimefanikiwa kuwepo kwenye album zao au kuwahi kuhusika kuunda album zao ni Lady Jaydee, Mansu Li pamoja na Izzo Bizness.

Inapokuja kwa miradi yako binafsi je ipo, inaitwaje na ilitoka lini?

Actually miradi yangu ipo ila kwa sasa hivi sidhani kama ni muda rasmi wa kuzungumzia hilo, niwie radhi lakini miradi binafsi ipo na itakuja na kwenye right time watu wataweza kuijua na ntaweza kui expose kwa jamii ili waweze kuifahamu.

Kwa mtazamo wako ni tofauti ya wana muziki waliopo mkondo mkuu (mainstream media) na handaki na kitu gani kinachangia huu mgawanyo kwenye Hip Hop music ya bongo?

Kikubwa ni support na mtaji. Unajua wasanii wengi ambao wapo mainstream unakuta wana support kubwa sana. Utakuta kuna wadau labda wanawashika mkono, wanawekeza pesa katika kazi zao na vitu kama hivyo, lakini undergrounds wengi wanakuwa wanakosa watu wakuwa support na kuwa fund kwenye kazi zao.

Katika industry yoyote ya muziki lazima kuwe na funding, uwekezaji wa pesa ili watu waweze kufika mbali na kufanya kitu kikubwa. Lakini kama hakuna kitu kama hicho na upatikanaji wa pesa unakuwa pia ni mgumu basi tofauti itakuwepo kubwa kila siku kati ya mainstream na handaki.

Je unaona kama wewe kama mtayarishaji unapewa heshima unayo stahili?

Kiukweli sisi hatupewi heshima inayostahili kutokana pia na mgawanyiko mkubwa sana wa mapato baina ya msanii na producer. Ukicheki kama hivyo msanii anakuwa anapata kipato au asilimia kubwa kushinda yule mtayarishaji.

Kwa hiyo huo uwiano bado haupo sawa ingawa bado tunaona watu wanaendelea kupambania na vitu kama hivyo kuwe na usawa katika mgawanyo wa haki, lakini bado, kiufupi bado! Ila huko siku za usoni mambo yataweza kukaa mswano.

Inapokuja kwenye maswala ya utayarishaji, mchakato wako ni upi toka muwasiliane na msanii hadi kukamilisha wimbo?

Kwa ufupi tu utaratibu wangu wa kufanya kazi msanii anapokuwa amenicheki, tunazungumza maybe anataka kukutana na mimi, kwani wengine wanapenda tukutane ana kwa ana tupige gumzo na vitu kama hivyo. Pia kuna wengine tunaongea kupitia njia ya mtandao, kwa kunipigia simu na tukapanga na nikaweza kumuuliza aina gani ya muziki ambao anapenda kuufanya na vitu kama hivyo.

Kwa hiyo tunaweza tuka meet studio na kuzungumza na tukafikia mwafaka, basi for the first time tunaweza kuona kama msanii ni chipukizi na kuna vitu havifahamu nami namsaidia labda kufanya instrumentation kisha nampa demonstration (demo) kwa ajili ya kwenda kufanyia mazoezi na kwenda kuboresha uandishi wake.

Then tunapanga ratiba ya kupanga tena session, tunacheki mashairi kama bado hayajakaa vizuri, tunaweza tukamuita mtu akaja kumsaidia kwa ajili ya kuweza kuboresha wimbo wake then baadaye ikiwa imekaa sawia tunamrekodi na kisha tunaacha wimbo kwa ajili ya mixing and mastering ambayo hiyo inaweza ikachukua hata 3 days.

Then baadaye tunampigia huyo msanii tunakutana nae tunaskiliza ile kazi kama kuna marekebisho yoyote ya wimbo tunafanya marekebisho then baadaye tunatoa ile product, tunampa ile product. Lakini pia inategemea na gharama ya msanii pia. Kama ametoa gharama changamfu kidogo basi tunamsaidia pia kusambaza huo wimbo au kazi ya sanaa husika.

Umeshafanya kazi na Izzo Bizness...hii chemistry yenu ilikujaje? Tueleze kuhusu hii album yenu ya majuzi kati "Trust God" maana ulikuwa mradi mzuka sana.

Kama inavyojulikana mimi na Izzo tuna chemistry kubwa sana. Tuna chemistry zaidi ya miaka kumi sasa, ni mtu ambaye ni wa karibu sana kwangu, ni a very close friend of mine, ni family friend pia na mshkaji wangu sana.

Chemistry yetu as always ipo "fire" na album hii tumeiandaa kwa mda mrefu sana, sio chini ya miaka sita mpaka imekuja kutoka. Namshkuru mwenyezi Mungu mapokezi yalikuwa mazuri ingawa hatukupata time nzuri sana ya ku promote kwa sababu Izzo alipata safari ya kwenda Marekani. Hivi sasa ninapozungumza bado yupo  Marekani lakini bado tunaendelea kuwasiliana kwa ajili ya projects nyingine.

Kwa hiyo tulishindwa kufanyia promotion kubwa ila mapokezi yalikuwa makubwa kutoka kwa mashabiki wetu na project inaendelea kufanya vizuri katika digital platform na sehemu zingine.

Pia umewasajili wasanii wawili kwenye label yako ya Uprise Music; Waddy B pamoja na Mullah The Matrix. Tueleze kuhusu wawili hawa, kazi zao na ni nini tutarajie kutoka kwenu wana Uprise?

Nina wasanii wawili Mullah The Matrix msanii wa kiume na Waddy B, msanii wa kike. Ndio wasanii ambao tupo nao hapa Uprise. Aah unajua pia nimejaribu kumsign msanii wa kike kwa sababu hii industry ina uchache sana wa wasanii wa kike kwa hiyo ndio maana nimejaribu kumsign Waddy ili kuweza kuleta challenge katika hii industry ya muziki haswa kwa upande wa rap wa akina dada.

Naamini she has a lot to offer kwenye hii industry. Recently tumeachia hii EP yake inaitwa “The Coming” ina nyimbo saba. Kwa hiyo tuna matarajio makubwa sana kwa dada Waddy kuweza kufika mbali, kufikia malengo yake ya kutikisa hii industry ya Bongo!

Lakini pia tuna kaka Mullah The Matrix ambaye pia tumeachia naye kazi nyingi hapo awali kabla hatujaanza kuwa pamoja kibiashara nami kuwa meneja wake. Lakini pia recently hapa tunaachia wimbo nadhani sio chini ya wiki mbili zijazo, wimbo mwingine rasmi kwa ajili ya kufungia mwaka, ambayo itakuwa collaboration.

Kwa hiyo ni mtu ambaye ninamuamini ambaye ana uwezo mkubwa sana ku flow na naamini ataleta chachu katika hii industry yetu ya bongo as well as Waddy B pia ambaye ni fresh blood ambaye ndio sasa anakuja kwenye industry hivyo kikubwa naomba Watanzania muweze kumpokea pamoja na Africa Mashariki kwa ujumla.

Kaka Dupy wewe pia msemaji wa Tanzania Producers And Composers Association (TPCA), hivi mnajihusisha na nini hapa?

Hichi ni chama kinachohusiana na watayarishaji wote na watunzi wa muziki hapa Tanzania. Nia na lengo la chama hiki ni kuleta umoja katika watayarishaji wa muziki Tanzania na pia kuweza kupambania haki za ma producer na watayarishaji wote wa muziki Tanzania ili wote waweze kufikia malengo.

Ikitokea leo hii kuna changamoto imetokea labda ya kimaslahi ya producer na pengine na msanii au kampuni flani basi TPCA ni sehemu moja ya kuweza kukimbilia ikishirikiana na BaSaTa kuweza kutatua changamoto mbali mbali za sanaa kupitia upande wa producers.

Tukimalizia kaka tungependa kujua ni nini ambacho hatujakuuliza wewe ambacho ungependa kutuambia?

Kitu ambacho umesahau kuniuliza ni family man. Ni family man nikiwa na maana kwamba nina mke mmoja na watoto wawili, Ivan and Ian, mmoja ana miaka minne mwingine ana miaka miwili. Eeh kwa hiyo mimi pia ni family mana bana, kwa watu wengi ambao hawajui. I’m not single, I’m taken!

Tupe mawasiliano yako na wapi unapatikana kwenye mitandao ya kijamii

Instagram: Dupy Beatz
Facebook: James Dupy Lilai
Twitter: DupyBeatz
Instagram: Uprise Music Empire

Simu: +255712183001
+255625517796

Email: producerdupy@gmail.com
Uprisemusic2000@gmail.com

Shukran sana Dupy Beatz kwa mda wako, baraka tele.

Shukran sana pia kwa mahojiano mazuri and  you are all welcome!