Elisha Elai

Moja ya ma emcee wa kizazi kipya ambaye anakuja kwa kasi sana ni Elisha Elai. Emcee Elisha Elai amejijengea jina handakini Kenya kutokana na mashairi yake ya kijanja, ya kibunifu na ya kuelimisha jamii. Toka Kitambo Bazenga huyu amekuwa kwenye hii rap game na leo amekuja kuwajuza kuwa yeye ni “A Man On A Mission”.

Karibu sana Elisha Elai hapa Micshariki Africa. Kwanza kabla ya yote mbona “Toka Kitambo” tukiangalia ni majuzi tu umeachia album yako ya kwanza "Man On A Mission"...

“Toka Kitambo” ni slogan ilitokea nikifanya cypher flani ya DJ TinTin around 2018 kama introduction before nianze kurap, ilikuwa ya kutaarifu mashabiki kuwa rap nilianza zamani, then ikakuja ikawa popular mpaka sasa.

Sasa tuzame kwenye utangulizi ila watu wajue tupo na nani na unajihusisha na nini? Majina yako rasmi?

Majina kamili ni Elisha Odhiambo known as Elisha Elai, ni msanii wa Hip Hop kutoka Kenya nikiwakilisha Dandora.

Tupeleke nyuma sasa, Toka Kitambo... ulizaliwa wapi, mpo wangapi kwenye familia yenu. Pia tungependa kujua ulisomea wapi shule za msingi na upili na hapo baadae pengine kama ulijiendeleza kimasomo.

Nilizaliwa Dandora phase 4, kwa familia tupo watoto saba. Shule ya msingi nilisomea Tom Mboya ilhali shule ya upili nilisomea pale Jupiter High School Dandora. Hapo ndio nilimalizia masomo yangu

Dandora Music ilikuwa na mchango gani kwenye sanaa yako? Je unaongeleaje hatua walizopiga memba wa kitambo wa kundi hili? Hapa nazungumzia Msito na Franso.

Dandora Music ilinisaidia sana kimziki, hapo ndio nillianza  kunoa kipaji changu na  kuelewa biashara ya mziki pia.

Safari yako ya mziki ilianzaje, toka ugundue una kipaji cha uchanaji mpaka hapa ulipofikia kuachia album yako ya kwanza?

Safari ya mziki ilianza 2011 nikiwa shule ya msingi, nilivutiwa sana na walichokuwa wanakifanya  Ukoo Flani Mau Mau.

Tueleze kuhusu mara yako ya kwanza kuingia studio, ilikuwaje na ngoma gani ulirekodi na marafiki na mashabiki walipokeaje kazi yako ya kwanza? Ngoma inaitwaje?

Mara ya kwanza kuingia studio ilikuwa 2011 nikiwa na kundi flani linaitwa Wakuu na tuliunda ngoma flani ilikuwa inaongea kuhusu amani, ilikuwa inaitwa “Amani Lazima”.

Mpaka sasa mimi mafahamu kuwa una miradi miwli mikubwa, hapa nazungumzia EP na album. Tueleze kuhusu kazi hizi

Mpaka sasa nina EP inaitwa “Bazenga” ambayo niliitoa 2019 na album ambayo inaitwa “Man On A Mission” ambayo nimeitoa mwaka jana 2023 mwezi wa Desemba.

Tueleze kuhusu watayarishaji pamoja na wasanii uliofanya nao kazi humu. Nani aliunda cover la mradi wako?

Albamu hiyo ina nyimbo 17 ambazo zilirekodiwa, kutayarishwa na kuchanganywa katika studio za BigBeats Afriq Studio na Aress 66. Pia kuna watayarishaji wengine walioshirikishwa kwenye mradi huu ambao ni Luidgi, Afrvka Beats, Dillie, Eyu Chino na Lilbeats.

Elisha Elai amewashirikisha wasanii wanne bora kwenye albamu yake ya kwanza ambao ni Wyre Da Lovechild, Dyana Cods, Jasper na Motra The Future kutoka Tanzania.

Jalada liliundwa na Robert Wesley.

Tuzame zaidi kuhusu kazi yako mpya... Kwanini "Man On A Mission"?

Tangu nianze mziki nimekuwa na mission ya kubadilisha mtaa wangu Dandora ujulikane kwa vitu chanya, kwa sababu Dandora imekuwa ni mtaa unajulikana kama mtaa wa wezi na malaya. So hii album "Man On A Mision" ni ya kuweza kubadilisha taswira ya mtaa wangu ili uweze kuangaliwa kwa mtazamo chanya, kwamba vijana tuna vipaji kando na mawazo hasi yaliyojaa vichwa vya watu wanaposikia jina Dandora.

Niliona kazi moja pia mlifanya na mchanaji kutoka Tanzania, Motra The Future. Hii ilikujaje na unazungumziaje kazi kama hizi zinazounganisha badala ya kuwagawanyisha wasanii pamoja na mashabiki?

Motra The Future tulipatana 2022 Arusha nikafanya video shoot na tukawa marafiki sana.Kwahiyo ilikuwa rahisi kumshirikisha kwa album yangu kwa sababu ya mahusiano mazuri kati yetu tayari.

Kazi hii uliamua kuiuza binafsi badala ya kuweka kwenye digital platforms ili mashabiki waweze kuiskia kule. Mbona hivi? Je kazi inapatikana kwa njia gani na kwa gharama gani?

Album "Man On A Mission” niliamua kuuza nakala 1000 moja kwanza kwa shilingi za Kenya 1000 (TZS 16,000.00) na unaeza ipata virahisi ukinicheki kupitia mitandao ya kijamii ila baadaye nitaiweka kwa streaming platforms nikianza kuunda videos.

Pia niliona kazi zako uliofanya na Umoja Sounds kule Tanzania, inapokuja kwa ujuzi je hizi international collabos zina umuhimu gani sio tu kwa sanaa  yako bali hata ukuaji wako kama msanii?

International collabo zinasaidia upande wa networking, na fanbase ya different location pia…

Ni changamoto gani ulizozipitia na ulikabiliana nazo kwa njia ipi?

Changamoto ya kwanza ni maswala ya hela. Muziki ni kama biashara zingine kwani inahitaji mtu awekeze ndio mambo yasonge. Pili ni muda, album inahitaji muda mwingi ili kuweza kukamilisha, sio kama kanda mseto (mixtape) au EP.

Umepiga kazi sana na mtayarishaji mtu mzima Aress. Aress mli link up naye vipi na amechangia kiasi gani ukuaji wako kama msanii? Je una mkataba na kaka Aress?

Aress tulipatana na yeye 2019 tukizindua EP ya DJ TinTin  pale club Muze baada ya Dandora Music kuchukua muda wa mapumziko... Mpaka sasa amekuwa mtayarishaji wangu na mshauri pia.

asa baada ya mradi kutoka, Je una mipango ya kutembelea vyombo vya habari kwa ajili ya promo na pengine kuandaa matamasha ili kuweza kukutana na mashabiki zako?

Mpango kwanza ni ku shoot video kadhaa za album, kisha baada ya hapo ndio nitakuwa nikitembelea vyombo vya habari kadhaa ili kuskuma agenda ya mradi wangu.

Tukimalizia unawashauri nini wasanii chipukizi ambao ndio sasa wanajitafuta na wanataka kufanikiwa kwenye muziki kama wewe?

Muziki si rahisi, inataka mtu ambaye amejitolea, lazima uwe tayari kujituma na kukabiliana na kupambana na changamoto ambazo zitajitokeza kwenye safari yako.

Unapatikana wapi kwenye mitandao ya kijamii

Mitandao ya kijamii kila mahali ni Elisha Elai

Shukran sana kwa mda wako Elisha Elai, Toka Kimbokta

Shukran pia!