Fredrick Pius maarufu kama Fedoo ni msanii wa Hip Hop kutoka Tanzania. Yeye ni mchanaji, mwandishi wa muziki, professional outdoor leader. Anawakilisha Mkoa wa Kilimanjaro na Moshi ambapo alizaliwa na kukulia.
Mpaka Sasa ana Extended Playlist (EP) moja (Mangi Sabas) 2022 na nyimbo kadhaa zikiwemo Ngumu Kutuhimili, Kaboka Mchizi, Nicheki, Ngoma Ngumu na baadhi ya collabo alizofanya na Black Ninja.
Fedoo ni jina la kukumbukwa, inabidi watu wawe na hili jina kichwani.
Karibu Micshariki Africa kaka Fedoo. Utangulizi kwanza, Fedoo ni nani, majina ya serikali na unafanya nini?
Asante sana kaka. Naitwa Fredrick Pius Shio. Kupitia Sanaa ya Muzuki nafahamika kwa jina la FEDOO. Fredrick au Fedoo ni msanii wa Hip Hop (mchenguaji) anayeliwakilisha taifa la Tanzania. Pia ni mwanafunzi kwa sasa nasomea kama Professional Tour Guide and Outdoor Leadership. Kiufupi ni balozi mzuri katika sekta ya utalii hapa Tanzania.
Jina lako la kisanii lilikujaje na linamaanisha nini?
FEDOO ni jina ambalo nilipewa na watu wangu wa karibu kipindi tupo shule ya sekondari Majengo kule Moshi. Mwanzo nilikuwa natumia jina jingine kabisa lakini niliona asilimia kubwa walishindwa kulisahau jina la Fedoo.
Maana halisi ya Fedoo ni ufupisho wa jina Fredrick, na kwa maana yangu mimi Fedoo ni Feel Dough (Doo). Nahisi pesa kila muda na ndio maana halisi ya Fedoo.
Nilikufahamu kwa mara ya kwanza uliposhirikishwa kwenye Mixtape ya Adam Shule Kongwe CHI. Je, ulijiskiaje kufanya kazi na mmoja ya wachanaji bora wa handaki kutoka Tanzania?
Dah! Kwanza kabisa heshima nyingi kaka Adam Shule Kongwe moja kati ya wachenguaji mahiri Tanzania kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kushiriki kwenye kanda mseto yake 'CHI' ambayo nimehusika wimbo namba 18, Ngoma Ya Bata. Ni nafasi kubwa sana kwangu kwani inanijenga na kunifanya nizidi kujifunza ili imani waliyonayo kwangu isipungue. Kuwepo kwenye mixtape ya 'CHI' kwangu ni nafasi ya thamani sana kwani nilifurahi sana pia kuwepo kwenye kazi moja na mmoja kati wa wachenguaji ninaowapenda sana Javan (Chuna Ngozi).
Safari yako ya muziki ilianza vipi na imekuwaje hadi sasa?
Safari yangu ya muziki ilianza kwa hatua za Kuskia Kusikiliza Kukariri Kuigiza Na Mwisho Wa Siku Kutunga. Kipindi mdogo nilikuwa nawasikiliza watu tofauti kama Nikki Mbishi, Fid Q, Chindo Man, Professor Jay na Marehemu Langa. Hawa ndio wasanii niliokua nawasikiliza sana na kuweza kuchana mistari yao yote bila kusita. Baada ya hapo nikawa najiandikia mistari yangu peke yangu na kuichana mpaka siku nilipokutana na marehemu Andre K na ku record wimbo wangu wa kwanza. Safari Bado inaendelea na kila siku najiona nazidi kukua na kuongezeka.
Umeweza kutoa nyimbo kadhaa ambazo zilikutambulisha kwa mashabiki. Je ulijisikiaje ulipoingia kwenye studio mara ya kwanza? Je wimbo wa kwanza unaitwaje na mashabiki waliupokea vipi?
Dah! Mara yangu ya kwanza kuingia booth ilikuwa tofauti kidogo kwani nilikuwa kama sio mgeni kutokana na watu niliokuwa nao. Nilichokuwa nawaza ni kuwa nitasikika vipi. Ilikuwa kama bahati sana kwani siku ya kwanza naingia booth mtayarishaji alikuwa ni Tenth Wonder ambaye anafanya vizuri sana kwenye kuandaa ngoma hapa Tanzania. Nilifanikiwa kufanya ngoma ya kwanza kabisa inayoitwa Ngumu Kutuhimili nikiwa nimeshirikisha Andre K na Eddy Mc.
Ilikuwa nzuri sana na niliifanya kwa ujasiri na munkari kwani siku nakutana na Andre K ndio siku alinikutanisha na 10th Wonder na siku hiyo hiyo ndio siku tulirekodi Ngumu Kutuhimili. Ngoma ilipokelewa vizuri sana sana tofauti na nilivyokua nadhani. Pia heshima sana Kwa kaka Lucas malali (LC), mradi wake wa 24barz ulinitambulisha vyema sana kwa wafuatiliaji wa muziki wa Handaki.
Mwaka jana ulikuwa na shughuli nyingi pia. Ulitoa nyimbo kadhaa na ukafanya kazi na Black Ninja wa Boombap Clinic, hii ilifanyikaje na ulijiskiaje kufanya kazi na mtayarishaji huyu aliyebobea?
Kufanya kazi na Black Ninja kwangu ni nafasi kubwa sana naweza nikasema. Black Ninja ni mtayarishaji mkali kabisa hapa Tanzania kuwahi kutokea katika kizazi chetu.
Mitandao ya kijamii ndio iliyonikutanisha na Black Ninja mpaka tukafikia kufanya kazi pamoja. Ukaribu uliendelea ambapo ikapelekea Black kuja Moshi na kufanya baadhi ya kazi ambazo zipo kwenye mradi wa Watema rhymes pamoja na Juu Chini Chini Juu.Miradi ilinitambulisha zaidi Kwa watu na kuniunganisha na wachenguaji kutoka mikoa tofauti.
Niseme tu heshima sana kwa Black Ninja na BBC kwa ujumla, najiskia amani sana kufanya nao kazi , na bado kazi zitaendelea kufanyika cha msingi ni wadau kuwa tayari kwa mengi mazuri.
Pia ulitoa mojawapo ya EP bora zaidi za mwaka wa 2022, Mangi Sabas. Tuambie kuhusu mradi huu, wazo la jina na mradi, watayarishaji waliohusika na wasanii walioshirikishwa katika mradi huo.
Asante sana Kwa kuitambua Mangi Sabas EP kama moja ya mradi bora Kwa mwaka jana.
Wazo la mradi lilikuja kutokana na asili yetu. Mimi ni Mchaga upande wa Uru Kaskazini na kwenye historia walitokea machifu baadhi walioweza kuiongoza Uru Kaskazini akiwemo Mangi Laiseri, Mangi Kisarika na Mangi Sabas. Kwa Nini Mangi Sabas? Ni Kwa sababu ninapoishi kwa sasa KCMC Moshi ndio sehemu pekee Mangi Sabas anakumbukwa maana kuna shule ya sekondari iliyopewa jina lake. Ile ni shule yetu na mimi sikuwa na namna ilitakiwa tu EP iitwe Mangi Sabas. Ni jina la shule, Chifu pia eneo langu. Mradi umelenga kunitambulisha mimi Fedoo kama Mangi Sabas na pia umegusia maswala ya kiuchumi na mihangaiko ya kila siku.
Mradi una Nyimbo 5 zikiwa ni;
- Nicheki
- MONEY ft. Nigger P
- Mapichapicha
- Oldskul Haswa
- Vichwa Vichwa ft. Bad Ngundo na Fivara
Mtayarishaji alikuwa Dr. Luis kuanzia midundo na uchanganyaji, vocals zote zilifanyika Northblock Records na tarehe 20.12.2022 ndio siku mradi ulitambulishwa rasmi na unapatikana kwa bei ya Tshs 5000 tu. Heshima Kwa wote walioweza kuunga mkono na wanaoendelea kununua mradi huu.
Asante kwa Fivara na Bad Ngundo kwa beti kali zilizojaza thamani kwenye mradi huu, asanteni kwenu.
Je, EP hii ilikuwa ni hatua gani muhimu katika safari yako ya kukua kama mwana Hip Hop?
Kwa kweli Mangi Sabas EP ina umuhimu mkubwa sana kwangu kama msanii wa handaki ninayechipukia. Mradi umepokelewa vizuri kiasi unanifanya niwaze kuandaa miradi mingi mingine kutokana na ujasiri niliopata baada ya matokeo ya mradi huu.
Mangi Sabas kwangu ni kitu kikubwa sana na watu watarajie kazi nyingi mwaka huu ikiwemo mixtape yangu ya kwanza, cha msingi tu ambao hawajaipata wanaweza wakawasiliana na mimi wakaipata na wakasikiliza huku wakisubiri kazi nyingine kutoka kwangu.
Je, ni changamoto zipi ulikumbana nazo kama mwanafunzi na pia msanii? Je, unawezaje ku balansi muda wako kati ya vitabu na maikrofoni?
Kwangu inakuwa rahisi kwani ratiba ndio kila kitu kwenye maisha ya kila siku. Pia kwangu ni vyema kufanya kitu sahihi muda ambao sio sahihi. Naweza kujigawa na nikafanya vyote bila kukosa amani.
Tunaweza kutarajia nini kutoka kwako mwaka huu?
Kama nilivyosema watu watarajie vitu vingi sana kutoka kwangu huu mwaka. Mangoma yapo yanakuja, pia kikubwa mwaka huu nitaachia mixtape yangu ya kwanza kabisa, swala ni watu kuzidi kunifuatilia ili waweze kujua itatoka lini na jina la mixtape pia.
Pia mwaka huu wategemee kunisikia nikiwa nimeshirishwa kwenye ngoma kibao tu za ma emcee wakali hapa Tanzania na Kenya.
Unajisikiaje kufanya kazi na Micshariki Africa na K Dawg kwenye albamu yao inayokuja ? Mashabiki wetu wanaweza kutarajia nini kutoka kwa mradi huu?
Binafsi kwangu ni faraja sana kuwa mmoja wa washiriki kwenye mradi huu mkubwa wa Micshariki Africa. Kuhusika kwenye album hii inayotoka hivi karibuni (Mashariki Ya Fikra) kwangu ni jambo kubwa sana kwa kweli kwani kuna wachenguaji wengi mahiri na kuwa muwakilishi katika wote kwangu ni imani kubwa sana.
Nawasihi tu watu wakae tayari kwa kuburudika na kuelimika. Mradi huu umegusia sehemu tofauti kama dini, siasa, uchumi na utamaduni wa watu wa Afrika Mashariki ambapo ni Kenya na Tanzania. Mimi na Msito tunawaahidi watu wa Kenya na Tanzania wategemee burudani na elimu ya kutosha kutoka kwenye Mashariki Ya Fikra album.
K Dawg pia nafurahi sana kuwa mmoja kati ya watu niliofanya nae kazi kwani ni mmoja kati ya watayarishaji wazuri kutoka Kenya. Midundo yake na namna yake ya kumalizia nyimbo vilinifanya niwe na hamu sana ya kuja kufanya nae kazi siku moja. Kupitia Micshariki Africa imewezekana na ninaamini tutazidi kufanya kazi kubwa zaidi.
Je ilikuaje kufanya kazi na Msito mmoja wa wana Hip Hop chipukizi wazuri anayekuja kwa kasi kutoka Kenya?
Kufanya kazi na Msito ni kama shule kaka. Nimejifunza mambo mengi sana kutoka kwake. Msito ana uzoefu na booth pia ana kazi nyingi sana kunizidi. Hii kwangu naichukua kama mtihani na nimeufaulu, Msito kanifanya nimekuwa na munkari (energy) sana kipindi narekodi na vingi nimejifunza kwake ikiwemo swala la ufundi na jinsi anavyotiririka na midundo, pia kuhusu time management Msito amekuwa mwalimu wangu mkuu. Yooh Msito popote ulipo heshima kwako, nakupenda sana kaka na unafahamu. Tegemeeni kazi zangu na Msito baada ya hii album, hatujamaliza.
Asante kwa wakati wako, mawazo ya mwisho?
Asante sana kaka. Mwisho ningependa kuwaambia watu, wadau wanaofuatilia hizi harakati wasichoke, pia wazidi kutuunga mkono bila kuchoka ili na sisi tuzidi kufanya kazi bila kuchoka pia.Muhimu kabisa ni tarehe 13.03.2023 watu wawe tayari kwa hiyo siku. Ndio siku rasmi album itatoka na watu wataweza kufaidi na kusikiliza kilichowasilishwa na Fedoo, Msito, pamoja na Micshariki Afrika. Cha msingi ni wewe kutufuatilia kila mahali kama Micshariki Africa uweze kuwa karibu na mchakato huu.
Asante.
Mfuate Fedoo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii;
Facebook: Fredrick Pius Cheddar
Instagram: F_E_D_O_O