Msanii: Fikrah Teule
Album: Azania na Wanawe
Tarehe iliyotoka: 31 Oktoba 2020
Nyimbo: 12
Ma Producer: HR The Messenger, Teknixx, J Synth, PMG
Mchanganyaji sauti na vyombo: HR The Messenger

Miaka ya themanini kule Nairobi, Kenya alizaliwa mtoto kwa jina la Orang’i Sibanda na baada ya miaka miwili familia ya mtoto huyu ilihamia Mombasa ambapo alipokulia na kusomea. Kando na masomo ya shuleni kumuelimisha kijana huyu, mitaa aliyokuwa anaishi ilimfunza mengi, ilimfungua macho kwa changamoto zake na pia ikamfanya agundue talanta itakayomuwezesha kuwakilisha mambo haya kwa jamii. Kijana huyu kulingana na mawazo, mitazamo ya maisha na fikra zake kufunguliwa aliamua kujiita Fikrah Teule.

Fikrah Teule ni emcee ambaye uandishi wake ni tofauti; hafuati kanuni na sheria zinazotoa muongozo kuhusu tunavyopaswa kuandika. Yeye hupendelea kuandika kwa mfumo wa “abstract” au dhahania kwa Kiswahili. Mziki wake unalenga sana kuhamasisha jamii, kuwatia watu motisha maishani mwao na pia kueleweka kirahisi na vijana wa rika lake pamoja na jamii kiujumla.

Kimziki Fikrah Teule alianza kujulikana rasmi 2007 wakati akiwa na kundi liitwalo Angazetu wakiwa pamoja na Mizani na X-O. Enzi hizo alipata fursa kufanya kazi pamoja na kundi kongwe la hip hop lililo chimbukia Mombasa liitwalo Ukoo Flani. Akiwa na jeshi hili alizidi kunoa penseli yake ya uandishi kwa kujipima uzani ki uchanaji na magwiji kama Chizzen Brain, R.I.C (wawili hawa walibobea na wimbo wao uitwao Hoi), Shalen Musa na N.J.E wa Ufuoni Records. Hawa ndio wasanii ambao walimpa Fikrah Teule motisha na ari ya kusukuma gurudumu la mziki. Pia Fikrah Teule ni mwanafunzi wa ma emcee tofauti tofauti wakiwemo akina Kalamashaka, Fid Q, KRS 1, Rakim, Nas, Talib kweli, Jadakiss na kundi la kitambo la hip hop, Gangstarr na wengineo.

Firkrah Teule hadi sasa ameshatoa miradi kadhaa; akiwa na Angazetu walitoa albam iitwayo “Angazia” na mixtape mbili ziitwazo “Nyayo za Shujaa” na “Wengi wape”. Akiwa peke yake 2014 Fikrah Teule aliachia mradi wake wa kwanza kwa jina Falsafa za mwenda pole.

Mwaka wa 2020 ulikuwa mwaka wenye changamoto nyingi duniani; Corona iliibuka kule China, nzige walivamia mashamba mengi Afrika Mashariki na pia mito, maziwa na madimbwi ya maji yalijaa na kuleta madhara makubwa. Kwenye mazingira haya magumu na pia “lockdown” ya miezi mitatu nchini Kenya emcee Fikrah Teule alipata mawazo ya kutengeneza album yake ya pili. Ilipofika Oktoba Fikrah Teule akatupatia album ijulikanayo kama “Azania Na Wanawe”

Azania ni jina la kitambo lililotumika sana maeneo ya kusini-mashariki ya Afrika yakiwemo pwani inayochomoza toka Somalia hadi Kenya na kidogo hadi eneo la kusini mwa Tanzania. Maeneo haya kitambo yalikuwa makazi ya makabila makuu ya wa Cushites kabla ya wa Bantu kuanza kuyamiliki.

Hivyo basi kwenye mradi huu wa Azania Na Wanawe, Fikrah Teule ameamu kuzungumza na watoto wa Azania, Afrika na waafrika kiujumla. Jaladio la mradi unakukaribisha na picha ya rangi nzuri ivutiayo macho ya rangi ya damu ya mzee kwenye nguo iliyomfunika bibi anayesikilizwa kwa umakini na wajukuu zake iliyochorwa na msanii Yonah Mudibo toka Mombasa. Picha imesadifu utamaduni wetu wa kiafrika wa kusimulia hadithi kama anavyofanya Fikrah Teule kwenye album hii.

Album hii iliyosimamiwa kwa asilimia nyingi na producer HR The Messenger inaanza na utangulizi ambapo ameshirikishwa Van Jan akikuahidi Fikrah Teule kuwa utakachokipata ndani ni, “good music kwa speaker…” HR toka mwanzo anaweka msingi mzuri wa midundo yote kwenye mradi.

“Nami Napiga” inafuatia pale ambapo Fikra, Shadihi na Trabolee na producer HR wanapigana vita takatifu ili kuhakikisha kuwa mawazo yao hakuna atakayeweza kuyaua. Singo hii iliyoundwa na J. Synth ni kati ya nyimbo nne pekee zilizoundwa na ma producer tofauti na HR The Messenger.

Kwenye wimbo huu anasema Shahidi “Xcalibur”
“X- the traveller,mind yangu ni tour to far lands/
Vitu marvelous nikacheki na ku zi transform tu words/
Nika condense the words to ink drops kwa pad/
Nika collect ma scars, ma scalps niki zuru earth/
A student and a teacher, journey ya knowledge ni circles/
Ndio na dai ku roam nijaze wino kwa passport/
Nijitambue, nisiwe kondoo, dogi ya Pavlov/
It’s only fair nikitumia mic kama means ya transport/”

Hakuna emcee au muimbaji aliyealikwa kwenye mradi huu bila kukidhi vigezo kama wanavyo ng’aa ma emcee wote kwenye “Nami Napigana”.

Fikrah Teule anaongelea mapenzi kwenye nyimbo mbili zilizoundwa ki “Neo Soul” kwenye “Wewe”akimshirikisha muimbaji GJB100 na “Nataka Tujuane” akimshirikisha Victoria Gichora na zote zimepikwa vizuri na HR The Messenger. Waimbaji hawa wawili wanalainisha sauti ngumu ya Fikrah Teule ambayo iko ki “Jadakiss” hivi.

“Jua” akiwa na emcee Kaa La Moto na muimbaji Vique ni wimbo wa historia yetu ya Afrika na umuhimu wa kuwa na matumaini kuhusu siku zetu za usoni. Wimbo mwingine wenye maudhui haya ni “Nikiwa Free”. Vique anatupa matumaini akisema,

“Jua litang’aa,
Ikija ile siku, tunayoitazamia”

Kwenye “Najitahidi” akiwa na Nafsi Huru na Shari Afrika, Fikrah anatukumbushia vile mtu anapopata msongo wa mawazo anachanganya ma faili akisema,

“Nasahau ninayopaswa kumbuka /
Ila nakumbuka ninayotaka kusahau/
Huihataji kuokota uchafu huitwa akili pungwani/
Wala kuzivua nguo hadharani/
Ubaki uchi ila basi tu/
Leo na wapa ukweli mtupu/
Yeyote anaweza dhurika nini chanzo? /
Vipi ataisaidika/
Unahisi jamii imekutenga/
Ndugu hawafaia tena/
Jawabu lisiwe kuondoa uhai/
Usife moyo, hauko peke yako/
Sahii tuongee, hakuna la kuficha/
Mwishowe majonzi tukitazama picha/
Mazungumzo yanaweza tatua/
Familia na walio karibu…./”

Anaimba Shari Afrika kwenye kiitikio, “Wanipa presha/ Wanitesa/Usinitese/”
Wimbo huu unazungumzia unyogovu na wasiwasi kwenye maisha yetu ya kila siku. Hili ni tatizo kubwa ambalo watu wanapitia kimya kimya ilhali madhara yake ni kua mtu anaweza kujiua.

“Baadhi ya Matukio” akimshirikisha Victoria Gichora tena ni hadithi kuhusu changamoto wanazopitia watu tofauti. Umeandikwa kwa ustadi mkubwa.

“Wako Mwaminifu” ni historia ya mapenzi ya Fikrah Teule na binti Hip Hop ambapo Fikrah anamuongelea binti huyo kule Kenya na alivyokuwa na mahusiano na ma emcee wengine kabla ya Teule kuteka Fikrah zake. Hii nyimbo imeandikwa ki “Common” alivyosema. “I used to love her”.

Nyimbo zinazomalizia mradi ni “Tusonge Mbele” na “Azania na Wanawe” iliyobeba jina la album. Tusonge Mbele inapigwa na nyuzi za kifaa cha mziki toka Mali kiitwacho “Kora” ilhali Azania na Wanawe inashirikisha ma emcee toka Kenya, Uganda na Zambia na wote wanaimba kwa lugha zao za nyumbani. Ma emcee wanachana kwa lugha za Shona, Baganda, Gikuyu, Gusii na Luo. Tarumbeta linapulizwa kuashiria pengine kuwa mbiu ya mgambo inawakumushia turudi tulipo toka, turudi kwa Azania na Wanawe.

Fikrah Teule feat. GJB100 - You (Video)

Fikrah Teule ft. Kaa La Moto & Viquee Ofala-Jua (Video)

Fikrah Teule ft HR The Messenger, Witness, Xcalibur & Trabolee (Audio)