Karibu Fivara katika Karibu kwenye mahojiano yetu hapa Micshariki.
Shukrani sana.
Tunaomba majina yako kamili.
Naitwa Jordan Wilson Zabron.
Kwanini uliamua kujiita FIVARA, na FIVARA ni jina tu au linamaanisha nini?
Fivara ni kifupi cha Fikra ni Vazi la Rap. Ni jina nililotengeneza mwenyewe kutoka kwenye jina Joddafivara baada ya kuunga jina langu Jordan na majina ya wanaharakati wawili ninaowakubali ambao ni Gaddafi na Che Guevara. Mwisho wa siku nilitoa Jodda kutokana kwamba ilikuwa inakaribia jina langu halisi hivo ikabaki Fivara.
Unapatikana wapi na unafanya nini nje ya mziki?
Sasa hivi napatikana Mwanza. Nje ya muziki nimeajiriwa kwenye kampuni moja ya kuuza vifaa vya umeme, najihusisha pia na ujasiriamali wa kuuza bidhaa zenye logo ya Hatua ambapo tuna T-shirt, Masweta, Pull over na kofia.
Kwa hiyo wewe ni mzawa wa Mwanza au unawakilisha wapi?
Ndio, mie nimezaliwa na kukulia Mwanza. Baba ni mtu wa Kigoma, Muha na mama ni mtu wa Mbeya, Mnyakyusa.
Kwa maana hiyo unawakilisha Mwanza, Kigoma na Mbeya au Mwanza peke yake.
Msukuma?
Nawakilisha Mwanza asee, japo sio msukuma.
Ulianza lini kujihusisha na utamaduni huu wa Hip hop, na kwanini Hip hop na sio Bolingo au Zouk?
Nilianza kujihusisha rasmi na utamaduni wa Hip Hop 2010 sababu zikiwa ni baada ya kuwa mpenzi wa muziki kwa muda mrefu nilikuja kugundua ukweli kuhusu huu utamaduni na nikajikita zaidi, kwenda kwenye matamasha na baadaye movement zangu binafsi.
Ili kuweka kumbu kumbu vizuri ni matamasha gani ambayo umeweza kuhudhuria na yakaweza kukuimarisha?
Sprite Freestyle battle, S.U.A ndo nayakumbuka.
Ni emcees gani waliokuvutia au kukushawishi kusimama katika upande ulionao kwa hapa bongo na ughaibuni?
Wengi tu..
Kati ya wengi wapo ambao wako akilini mwako ni vyema ukawataja hao
Mbele kina Immortal, Black Thought, Nas, KRS One, Rakim, Masta Ace, Sean P, Common, Biggie, J Cole, Kendrick Lamar nk Bongo, Hasheem Dogo, Salu Tee, Fid Q, Professor J, Langa, Chid Benz, Adili, Nash Mc, Nikki Mbishi, nk.
Ulianza lini ku record track yako ya kwanza na uliipa jina gani, na mpaka sasa una tracks ngapi, je una Albums / Mixtape ngapi na kama zipo zinakwenda kwa majina yapi?
Track yangu ya kwanza kurekodi ilikua Yote Maisha, 2013. Nilirekodia Mwanza kwa jamaa anaitwa Man Shiba…beat ikiwa ya Sallii Teknik. Mpaka sasa nina tracks nyingi kiukweli, kujua idadi kamili sijui afu nina mixtape moja Alpha Mixtape niliyoachia 2016 katika mitandao ya Audiomack, Soundcloud… Ilikua na ngoma 06 moja intro, moja poem na nne ngoma. Pia niliachia album yangu ya kwanza mwaka 2018, inaitwa Fikra ni Vazi la Rap ambayo ni utambulisho na ilielezea falsafa yangu.
Muongozo: Pia ni vyema ungeweka links ili ambao hawajawahi kukusikia wakusikie.
Audiomack: https://audiomack.com/fivara
YouTube: https://youtube.com/c/Fivara
Mdundo: https://mdundo.com/a/193875
Apple Music: https://music.apple.com/tz/artist/fivara/1566531039
Spotify: https://open.spotify.com/artist/5R7ok1Pq2SkDkznzIBoMjF?si=5JBxxrupTvqyDOSElHtdqw&dl_branch=1
Deezer: https://deezer.page.link/2ScCeZFvBj5QCBuw9
Fivara, una plan gani kutoka ulipo na kwenda mbele zaidi kimuziki?
Mpango wangu ni kuandaa miradi mingi Zaidi yaani Albums, Eps na Mixtapes pia kuandaa bidhaa za kijasiriamali ikiwemo Hatua na nyingine. Mpango wangu mwingine ni kuikuza lebo yangu ya mziki Pie Muzik na kufikia kuwasaini wasanii wengine wenye uwezo na vipaji.”
Kuna track yako moja inaitwa Zao hii idea uliipataje?
“Hii idea ilianza kwa vesi moja ambayo niliwaza kuwatambua waasisi, wahusika na vichwa walioshiriki katika kusukuma Hip Hop ya Bongo. Miaka ya nyuma tulienda studio moja aliyokuepo Prof Ludigo, ilikua Kibamba…Tumefika kuingia Studio kumchania Ludi nkachana vesi ya kwanza ya Zao, akaipenda sana akasema tutaanza kuirekodi. Hivyo niliporudi mtaani nkamalizia vesi ya pili. Itakuja pia Remix yake, ntawashirikisha wana.
Nakumbuka ulikuwa kwenye Crew ya MBWA WAKALI MINYORORO MIBOVU pamoja na Meddy Samurai almaarufu King Swagger.. Je hii ilifikia wapi, kuna kazi ambazo mlifanikiwa ku release , kama bado mna mpango gani?
Mbwa Wakali sa hivi haipo afu tulikua wengi zaidi ya wawili yaani Stan Rhymes, Meddy, Ill Moshi, Mimi. Baadae Meddy aliongeza wanae Tanga tukawa tisa baadae tukapungua na baadae akajiunga Mas Stanza.
Alipojiunga Mas Stanza tukajihesabu watano yani Stan Rhymes, Meddy, Ill Moshi, Mimi na Mas Stanza. Watu wengi wanajua tuko wawili kwa sababu sisi ndo tulikua active na Mbwa Wakali, kina Stan na wana wengine walikua busy na Solo project zao sana.
Kabla ya Mbwa Wakali mi na Meddy Tulikua na crew yetu Negro Creators ambayo tuliikaushia baada ya kuundwa Mbwa Wakali. Stan na Meddy ndo waliunda Mbwa Wakali na mi nilpotoka likizo nikaikuta crew nikajiunga na movement zikaendelea.
Mwaka jana tulipogundua hii movement tuko wa 2 sana front kati ya wengi tukaona tuirudie Negro Creators ila sasa tukaiita Negro Shiettaz. Mbwa Wakali hatukufanya track ila mi na Meddy tuna projects kama Nuksi, Umimi, nk
Nyongeza: Project za Negro Shiettaz zitakuja ila kwa sasa Meddy yuko chuo Moshi hivo ni mpaka akimaliza pengine…Kuhusu Mbwa Wakali labda ije itokee Reunion.
Tueleze kuhusu kundi lenu la Ngome ya Chuma? Ni nani waliopo ndani ya crew hii, ilianza lini na pia kuna miradi mmefanya pamoja na ipo sokoni?
Ngome ya chuma sio kundi ni umoja mimi, Mantiki Barz na Rabi James ambapo tulianza kwa kufanya miradi miwili; Ngome ya chuma na Wanufaika wa mfumo. Ngome ya chuma ni wimbo ambao ulitoka rasmi 2018 na upo kwenye baadhi ya platforms.
Pia umoja huu tulipanga kwamba tutaandaa miradi ikiwemo mixtape, albam na kadhalika ila bado hatujalifanikisha hili ila umoja bado upo na sisi bado ni washikaji ambao bado tunawasiliana mara kwa mara.
Unauzungumziaje mziki wa handaki hapa bongo tukianzia mapungufu na uimara wake na vitu gani vinatakiwa vifanyike ili tuweze kusonga zaidi ya hapa tulipo?
Mapungufu ni ujuaji, utengano, unafki…uimara ni kwamba siku zinavosogea watu wanazidi kupata uelewa handaki ni nini. Cha kufanya ni kuzidi kuelimishana, kuambiana ukweli, kukosoana, kukumbushana, kuungana na tuwekeze.
Je mipango yako ya mwaka huu ni ipi? Kuna miradi mipya tutegemee toka kwako?
Kwa mwaka huu nina mpango wa kuachia album yangu ya pili mwisho wa mwaka huu lakini kabla ya album naachia wimbo kila mwezi ikiwa ni utaratibu niliojiwekea mpaka album itakapotoka.
Unaweza kutueleza kidogo kuhusu brand yako ya Hatua pamoja na studio yako/yenu ya Pie Muzik?
Hatua ni brand yangu ya mavazi niliyoanzisha rasmi 2020 ikifuatia wimbo wa Hatua nilioachia 2019. Ni brand ambayo inaelezea Hatua ambazo anazipitia mtu katika maisha kwenye nyanja mbalimbali kuanzia kazi, mahusiano, elimu, biashara, ukuaji nk.
Pie Muzik ni lebo huru ya mziki ambayo niliianzisha rasmi 2020 ambapo inahusika na kazi za mziki na kazi zangu zote sasa hivi zinatoka chini ya lebo hii. Kwa sasa nipo msanii mwenyewe kwa sababu bado tupo katika hatua za mwanzo za kuiunda lebo hii.
Ipo team ya watu nyuma wenye majukumu mbalimbali katika lebo hii. Malengo ni kuja kusimamia wasanii wenye vipaji na uwezo, kusambaza kazi za mziki, kufanya marketing na branding kwa wasanii na wanamziki mbalimbali.
Fivara upo busy sana maana una miradi mingine kama vile Hatua Book Club, Tz Hip Hop room pale kwenye app ya Clubhouse nk. Tueleze kidogo kuhusu hili na ongezea pia shughuli zako zingine ambazo pengine sikuzitaja
Hatua Book Club hii ni jamii/club ya watu wanaopenda, wanaoanza au wanaotaka kusoma vitabu. Tumeanza na group la WhatsApp lakini malengo ni kuja kuwa na website kwa ajili ya kuuza, kupakua na kupandisha vitabu. Pia tunatarajia kuwa na harakati za kuhamasisha usomaji wa vitabu katika jamii yetu, kuandaa na kujenga maktaba katika maeneo tofauti tofauti Tanzania na nje ya nchi.
TZ Hiphop ni club niliyoanzisha katika mtandao mpya wa kijamii uitwao Clubhouse. Kwenye hiyo club huwa tunakua na session mbalimbali kuhusiana na Hiphop/Rap ya Tanzania na nje ya nchi. Tunakuaga na vipindi kama Album Reviews ambapo huwa tunachambua album mbalimbali za wasanii wa Hiphop hapa Bongo, kuna discussions ambapo huwa tunajadiliana kuhusu mada mbalimbali zinazohusu utamaduni na Rap Kiujumla, kuna kipindi pia Megamix ambapo huwa tunapiga ngoma mbalimbali za Rap kutoka Bongo na bila kusahau huwa tuna kipindi cha Michano.
Mwaka huu umeachia wimbo mpya kila mwezi kando na ma freestyle kibao, je ni nini kimekusukuma ukafanya hivi?
Kilichonisukuma kufanya hivyo ni kutengeneza mwendelezo (Consistency) kwa kazi zangu. Wakati mashabiki zangu wanasubiri album hizi kazi za kila mwezi zitawapa kampani mpaka pale album itakapotoka. Kazi hizi pia zinanisaidia kulijaribu soko, kuongeza mashabiki na pia kubaki katika rotation maana mambo ni mengi siku hizi kwa hiyo ili uwepo kwenye mzunguko ni lazima uwe na maudhui ya mara kwa mara. Lengo jingine ni kuchangamsha game na pia kuchangamsha platform ambazo nimeweka kazi zangu Pamoja na mitandao ya kijamii.
Je kwa maoni yako unaona kama Watanzania wanathamini Hip Hop ya handaki toka bongo?
Watanzania bado hawaipi thamani Hip Hop ya handaki kwa sababu watu wenyewe wa Handaki hatuipi thamani hivyo wao ni vigumu kuweza kuipa thamani.
Kwanini uliamua kuweka mziki wako kwenye streaming apps? Mziki wako upo kwenye apps zipi?
Nimeweka kazi kwenye streaming apps ili niweze kuwafikia watu wengi zaidi duniani pia niweze kuongeza mashabiki na ikiwezekana nipate kipato kutoka kwenye hizo platforms.
Je mziki ukiweka kwenye streaming apps unalipa?
Ndio inalipa lakini mpaka uwe umefikisha vigezo vya wewe kulipwa maana kila app ina vigezo vyake ili mtu aweze kulipwa. Kikubwa ni kuwa na maudhui mazuri, kupromoti vizuri na kuwa na mwendelezo hapo utaona faida yake hizo apps. Kitu kingine usiwe na haraka inahitaji muda maana sio jambo la kuamka tu ukawa unalipwa, lazima ujipange na ujiandae.
Hitimisho: Asante kwa time yako karibu tena MicShariki.
Mpate Fivara kupitia mitandao ya kijamii:
Facebook: Fivara Nyati(Kimpa Vita)
Instagram:fivara
Twitter: fivara_