Ukaguzi wa albam: Fikra Ni Vazi La Rap
Msanii: Fivara
Tarehe iliyotoka: 22.11.2018
Nyimbo: 13
Wapiga midundo na ma producer: Mikono (Ya Kazi), 9th Baba (Producer Baba), Sheem King, Jegalla Konducta Kusini,
Mixing & Mastering: Mikono (Ya Kazi)
Studio: Touch Music, Lutiz Records, Kibaha Hass Records

Unaposkia mtu akikwambia kuwa, “Fikra Ni Vazi La Rap” basi kwa haraka haraka unaweza anza kufikiria msemo huu unamaanisha nini. Na ndio maana leo tumeruka na mradi wa Fivara ambao ulitoka takriban miaka mitatu iliyopita ili kuweza kukagua mradi huu ili kuona maana fiche na banaya wa mradi huu.

Fivara kwa kifupi ni Fikra Ni Vazi La Rap hivyo basi  jina la debut albam hii moja kwa moja ni jina la msanii huyu.

Nimepata fursa ya kuiskia Albam hii mara kibao na kusema kweli sijawahi kuchoshwa nayo kwani ni mradi ulioundwa ki makini na mawazo ya ziada yalitumika kuhakikisha kuwa mradi tutakao upokea kama waskilizaji utawacha alama ndani ya masikio na mioyo yetu.

Mradi huu unanza na mdundo mzuri uliundwa na 9th Baba akishirikiana na Professor Ludigo, Zao. Hakuna njia nzuri ya kufungua albam zaida ya kuwaundia wimbo unaotoa shukran na unaoonesha mapenzi kwa waliokutangulia kwenye game. Fivara anachana mashairi mazuri sana akitukumbusha wale walioweka jiwe la msingi kwenye Hip Hop ya Bongo na maishani mwa Fivara pia. Juu ya mdundo mzuri ambao violin inapiga taratibu Fivara anatema,

“Zao la Prof. Jay, zao la Mr. II/
Zao la Kwanza Unit, kwa kifupi KU/
Nadata kwa ushairi sio mapozi ka’ Bluu/
Zao la Chindo man kutoka Kijenge juu/
Zao la J.C.B acha nilenge tu/
Ukiskia Pah! Imekukosa panda taxi twenzetu/
Zao la Fid Q, zao la Dandu/
Sina makosa, unaua gemu ndio masomo yangu/…”

Ukweli ni kuwa kama sio hawa ma legendary waliotuachia msingi mzuri emcee huyu anakiri hata yeye pengine hangekuepo au hata kuskika kama emcee.

Kama nilivyotangulia kusema hapo awali mradi huu ulikuwa kama utambulisho wa Fivara kwa mashabiki zake na wana Hip Hop kiujumla na hili unaliona wazi kwenye nyimbo kadhaa zikiwemo Katika ubora wangu, Mama (Interlude),Shangazi, Mawazo, Msongo Wa Mawazo. Kwenye midundo tajwa hapa utapata fursa ya kumfahamu Fivara kwani anatupa upenyo tuchungulie maisha yake na fikra zake private.

Mawazo ambao ni wimbo mmoja wapo favourite unamkuta emcee huyu akifunguka hisia zake juu ya changamoto zinazomzonga hadi sasa ameugua gonjwa la depression (Msongo wa mawazo). Chini ya dakika mbili Fivara anatema nyongo akituachia mistari kwenye mdundo ilioekewa na Mikono akisema,

“Navyowaza ni tofauti na kuota /
Maana kuna mawazo, mi mwenyewe nayaogopa/
Mfano mzuri ni kuwazia kushindwa/
Huwa inapunguza asilimia ya Ubingwa/
Utawaza waza mwishowe haujiamini/
Kitete kingi, moyo unadunda kama nini/
Unaikosa kazi, unarudi ghetto unawaza/
Unakata tamaa ila roho inasema Kaza/
Pia ukiwaza nyumbani una young brothers
Shemu ana mimba unaelekea Mbaba/
Ndio maisha ya sasa kuwaza kuwazua/
Hadi kichwa kinazingua, kinavyokunwa na kuungua/
Mwenzenu nilishawaza kwenda nje ya dunia/…”

Na mada hii inaendelea kwenye Msongo Wa Mawazo ambao ni wimbo soulful sana na wa kusikitisha sana.

Mama(Intelude) uliopigwa na Mikono pamoja na Sheem King unatumia sampuli ya wimbo wa Christoper Martin Mama na Fivara anautendea haki aki show love kwa bi mkubwa. Wimbo huu pamoja na Shangazi zinasimulia maisha ya Fivara.

Kwenye mradi huu Fivara amegusia historia ya Africa kwenye wimbo aliowashirikisha wasanii EXP wa D.EXP pamoja na Big Solo uitwao Africa Yetu.

Mada zingine zilizozungumziwa kwenye mradi huu ni kama chagamoto za elimu na wajibu kwenye wimbo wa Elimika Uwajibike, ujasiri wa kukabiliana na chochote maishani mwetu kwenye wimbo Tayari, changamoto za simu, teknologia na mitandao ya kijamii kwenye  Ushamba Wazi, utafutaji kwenye 24/7 pamoja na changamoto za unyanyasaji wa kijinsia kwenye wimbo Fataki akiwa na Davos unatumia sampuli ya mziki wa Reggae Give Me A Call toka kwa Mitch.

Asante (Outrometry) ni wimbo unaotufungia albam hii Fivara akitupa sneek ya maisha yake tena anapomkumbuka kaka yake aliyemuacha ambaye alikuwa kama pacha Tafari.

Kusema kweli fikra ndio vazi la rap, na kusema kweli tumeliona hili kupitia mistari na mashairi ya Fivara ambaye amejitahidi kuhakikisha kuwa kila tone la wino linalotoka kwa bic yake au kipande cha graphite kinachotoka kwa penseli yake kinatendewa haki kwa kutupa mistari mizuri tutakayoienzi. Amelifanikisha hili emcee FiVaRa kwenye Fikra Ni Vazi la Rap.