Ukaguzi Wa Albam: Moro Jazz
Msanii: Fredrick Mulla
Tarehe iliyotoka: 12
Nyimbo: 11.06.2021
Wapiga Midundo: Gihcue, Aby Bangladesh, Migi
Mchanganya Sauti na Midudo: Gihcue
Studio: Digital Vibez (Morogoro, Masika, Tanzania)
Mara nyingi ninaponunua mradi wa msanii yoyote yule huwa nina hamu ya kuskia kilichopo ndani. Kama vile kitabu kipya hunadiwa kwa kuonesha jalada la mbele lenye picha inayokupa taswira ya nini utarajie toka kwenye kitabu basi pia jalada la mbele la albam ya mziki lina uwezo huo huo wa kukuonesha nini utarajie kwenye mradi endapo utaununua.Vile vile jalada la nyuma la kitabu hukupa mukhtasari wa kilichopo ndani ya mradi sawia na jalada la nyuma la albam kwa kupitia majina ya nyimbo hukupa mukhtasari mzuri wa nini utegemee ndani ya mradi.
Hivyo basi niliponunua mradi wa Moro Jazz toka kwa Fredrick Mulla nilikuwa na matumaini makubwa kuwa inaweza ikawa albam nzuri kwani huu ndio ulikua mradi wake wa kwanza mimi kununua baada ya kuskiliza kazi zake kadhaa pale YouTube.
Mradi unaanza na wimbo uliobeba jina la albam ambayo pia ndio single rasmi ya kwanza toka kwa mradi huu, Moro Jazz. Wimbo huu unamkuta Mulla aki reminisce na kujivunia kuhusu chimbuko lake na maisha yake kule Morogoro kwenye mdundo laid back ambao umeundwa na producer wake anayemkubali GQ akionesha ukaribu wao akisema,
Nikiwaga Mo town hua ni raha tu/
Sms kwa GQ, “Yo I’m back fool”/
Like Yo, “Uko studio, I wanna come through”/
“Kichwa kimejaa ma mistari nataka rap tu”/
Like Yo, “Uko town tokea tu”/
“Midundo kibao kama vile nimetokea ju"/”
Hapa ndipo unaelewa ukaribu wa GQ na Mulla unatoka wapi na unaelewa kwa nini Gq kahusika pakubwa kwenye uandaaji wa albam hii. Msingi wa aina ya ngoma utakazopata kwenye albam hii unawekwa kwenye wimbo huu wa kwanza sio tu ki mashairi bali hata kwa upande wa viitikio pamoja na midundo. Mradi huu wenye nyimbo 12 umeweza kugusia mada tofauti tofauti kama kama vile mahusiano, imani, majigambo na pia kutiana moyo.
Day Uno akiwa na Shentete pamoja na Marafiki ni wimbo unaotoa shout kwa marafiki wake wa karibu na umuhimu wanao cheza kwenye maisha yake. Kama umeshazoea ma boombap Mulla kwenye mradi huu yupo tofauti kwani wakati mwingine madini anatema kwa kuimba tu kwa sauti nzuri sana. Marafiki ni wimbo mzuka sana ambapo anaonesha upendo wake kwa wana na umuhimu wanaocheza katika maisha yake akisema kwenye wimbo wenye vesi moja,
“Mi na wanangu forever/
Ndio walifanya niamini naweza/
Hatubadiliki yo we still here kama utabiri wa weather/
Nikijisahau nikizingua hawanifichi wananieleza/
Ukiwepo msosi juu ya meza niku split half kama leather/
Washkaji wengi hatuongei ila kwangu nyi bado ni best half/
Maisha yanafanya hatuonani wanangu nyi bado wanangu till next life/
Najua sana sionekani kitaani nina majukumu and that’s life/
Mambo za kuringa ringa kukataa wana mnajua wana mi sio that type/
Yo wait minute a trick chuki zako kaziitie Uber please/
Utajiri wa kwanza marafiki nikiwakosa naweza kua lunatic/
Nikiwa na nyinyi huwa navimba kila kona mzani hauwezi pima hii/
Nina ushkaji ambao ukizingua dakika mbili washarusha ngumi free/
Kwenye kiitio Mulla kaua na vocals zake safi sana akisema,
“Happy days yeah, with my friends/
Hata tukiwa down we still friends/
We still friends till the end/
Tukikosana we make amends/”
Ni baraka sana tukiwa na marafiki wa kweli.
Mada ya mapenzi imegusiwa kwenye nyimbo kadhaa zikiwemo, Love Song, Ukikubali, My Ex’s pamoja na Anasema akiwa na Brian Simba. My Ex’s unanikumbusha wimbo wa marehemu DMX What These Bitches Want.
Mada ya imani imeguswa kwenye Dear Lord akiwa na Beda Andrew. Hapa Mulla katupeleka ibadani kwenye wimbo safi sana unaopiga vinanda freshi sana ilhali sauti za kwaya zikimsaidia Beda kwenye kiitikio. Mdundo wa wimbo huu mzuri umeundwa na Aby Bangladesh aka Steez.
Kings and Queens pamoja na Muda akiwa na Kay Zaddy ni nyimbo za kuinua wana kwa kuwatia moyo na kuwaonesha kuwa wanaweza kufanikisha chochote wawazacho kwani wao ni wafalme na ma malkia na wanachohitaji ni muda ili kuweza kufanikisha ndoto zao. Nyimbo mbili chanya na mzuka sana.
Ili usimuone wa hivi hivi kwa sababu hajagongea ngoma zake kwenye midundo ya ki boombap Mulla anaamua kukunja shati na kurusha ngumi za majigambo kwenye wimbo wa Heavyweight akighani mwanzo mwisho kwenye wimbo wa vesi moja kua ana uzito wa juu kama Professor J wa Mitulinga.
Mradi huu ulikua ki tofauti ila mimi binafsi niliupenda kwani umeweza kuniletea Hip Hop ki tofauti sana. Umenikumbusha mradi wa marehemu G.U.R.U ulioitwa Jazzmattaz ambao kama Fredrick Mulla alitumia midundo ya Jazz na kuweza kutupatia mradi mzuri na tofauti sana ki Hip Hop. Tusisahau pia kuwa Morogoro ndio nyumbani kwa Morogoro Jazz Band illiyokua chini ya usimamizi wa Mbaraka Mwinshehe hivyo basi mradi huu ni kama njia moja ya kuenzi vya nyumbani.
Uthubutu wa kuwa tofauti nimeupenda japokua mada naona zingeweza kuongezeka zaidi ili kuangazia agenda nyingine zaidi. Nimefika tamati ya uchambuzi na sina budi kama vile wimbo wa mwisho wa mradi huu kusema Asanteni kwa kusoma makala haya na karibuni muiskilize Moro Jazz.
Kupata nakala yako ya albam hii wasiliana na Fredrick Mulla kupitia
Twitter: FredrickMulla
Instagram: fredrickmulla