Uchambuzi Wa EP: Street Motivation
Emcee: Gamba Junior
Tarehe iliyotoka: 07.05.2022
Nyimbo: 5
Watayarishaji: Mika Man, Hanto Beatz, Magical
Studio: City Of Sound
Wimbo nilioupenda: Mtafutaji
Tarehe 7 mwezi wa pili mwaka 2022 ndio siku ambayo mradi wa kwanza toka kwa Gamba unaingia sokoni. Mradi huu umetengenezwa na kutayarishwa na Mika Man, Hanto Beatz bila kumsahau mtu mzima Magical.
Ambao wamepata shavu kwenye huu mradi ni Rudo, Msouth pamoja na Jaheem. Huku upande wa kava akisimama Zee Maya sambamba na Boothwear.
Sikio la Beberu limepata bahati ya kusikia huu mradi na kuchambua wimbo mmoja mmoja kwa kutoka kwa Gamba mwenyewe kijana anayewakilisha Mwanza. Humu tumezungumzia kuhusu EP yake Street Motivation.
Embu tuzungumzie kuhusu hii EP yako kabla ya kupitia wimbo mmoja mmoja, embu zungumzia ni EP ya namna gani na kuna nini ambacho kinaweza kumshawishi mtu kuinunua?
Humo ndani nimejaribu kuongelea changamoto ama mambo yanayotokea kila siku kwenye mitaa tunayoishi na maisha yetu ya mtanzania wa kawaida kabisa.
Natazama kava ya EP yako hii ya Street Motivation, je hii kava inasadifu kilichomo kwenye nyimbo zilizomo au inakuwa inamaanisha nini?
Cover inasadifu kilichomo kwa maana jina la EP na kilichoimbwa ndani vinawiana.
Hii ni EP yako ya ngapi toka umeingia kwenye utamaduni wa Hip Hop?
Ndio EP yangu ya kwanza, initambulishe kisha baada ya hapo nitakuja na album pia.
Tutegemee kupata kitu gani kwenye hii EP yako ambayo umeingiza sokoni?
Kwanza nategemea mapokeo mazuri ya wadau wa muziki, pia maoni yao chanya watakayotoa yatanipa fursa ya kujijenga zaidi na kuandaa miradi yangu inayofuata kwa ubora zaidi.
Naomba kuwafahamu watengenezaji wa huu mradi na emcee ambao umeshirikiana nao katika nyimbo zako na kwanini uliwachagua hao kuandaa hii kazi yako na EP yako ya kwanza?
Kwanza kabisa walioshiriki humo ndani ni wasanii ambao kwa hapa Mwanza ni wakali sana wanavipaji vikubwa nikaona sio mbaya kufanya kitu na watu ninaowakubali katika kazi zao, Kwenye wimbo uliobeba jina la EP ndio nimewashirikisha hao humo kuna Jaheem, Msouth na Rudo.
Ep imebeba nyimbo 5 naomba tuanze na huu wimbo wa kwanza Chidi, kitu gani kilikusukuma kuandika huu wimbo na pia unahisi jamii imepata elimu gani kupitia huyu Chidi? Bila kusahau unaweza kutuambia mdundo wa huu wimbo kafanya nani?
Wazo la wimbo wa Chidi ni kisa cha kweli kabisa huku mtaani kwetu. Kuna miaka ya nyuma Mwanza ilipitia changamoto sana vijana wengi kujikita katika makundi ya wahuni na waporaji, ilikua mbaya sana hio hali na niliwahi kuwa shuhuda.
Sasa ikanisukuma kuandika huo wimbo, ila wengi wamezoea kwamba mtu akiwa mhuni basi mwisho wake ni jela ama kifo , kumbe kuna nafasi nyingine ya kubadilika na kuwa mtu mwema kwenye jamiii.
Mdundo wa huo wimbo ulitengenezwa na rafiki yangu mmoja hivi anaishi ujerumani anaitwa Hanto hua ni producer wa muziki na anasomea maswala ya uhandisi wa sauti. Lakini tukaja kuifanya utayarishaji kwenye studio za City of Sound hapa Mwanza chini ya usimamizi wa mtayarishaji anaefahamika kwa jina la Magical. Huyo Hanto ni raia wa Marekani lakini anaishi Ujerumani katengeneza midundo 3 humo ukianza na Chidi, Mtafutaji na Street Motivation, kaitengeneza hio midundo.
Twende wimbo namba 2 ambao umeupa jina 13hood hii inawakilisha nini au ni code ya kitu gani ambacho unataka kutuambia?
13Hood kwanza inawakilisha tarehe yangu ya kuzaliwa. Nimezaliwa 13 August. Wazo la huo wimbo nimejaribu kuelezea mambo yaliyowahi kunikuta kuanzia mtaani nikiwa na marafiki zangu namna tunavyoishi na watu wa karibu tofauti tofauti. 13hood ni code ya siku yangu ya kuzaliwa.
Wimbo namba 3 umeupa jina Ndoto huu wimbo nimeusikiliza vizuri unasema watu wapiganie ndoto(malengo) yao waweze kufika wanapopawaza ukirudi wimbo namba 2 wenye jina 13hood unazungumzia pia maisha ya street japo kiujumbe kuna utofauti je kwa aina ya nyimbo zako wewe mwenyewe kupishana hauoni kama zinashindwa kuonesha msimamo wako umesimamia wapi?
Hio inanipa uwanda mpana kujifikirisha kimuziki ndomana nyimbo hizo mbili zimeongea vitu tofauti ila lengo bado liko vilevile kuna maisha tunaishi na pia kuna malengo kati yetu kama binadamu sasa lazima tuweze kujikwamua kwenye kila changamoto inayotokea.
Wimbo namba 4 Mtafutaji ni moja ya nyimbo zangu bora toka kwenye hii EP yako. Niambie wazo la huu wimbo limetokana na nini kitu gani kilikusukuma ukaandika huu wimbo?
Wazo la huu wimbo aisee! Si unajua tena vijana mambo ya mahusiano kwenye moja na mbili kuna mdada alitokea kunipenda sana, alafu mi kipindi hicho sina hata mchongo mambo yangu kiuchumi yalikua magumu, alafu alikua na binti yake mdogo anaitwa Nicole akawa anataka mimi niwe kama baba wakambo hivi nianze ku pay bills kitu ambacho kilikua kigumu sana kwangu yaani kuhudumia mtoto ambae sio wangu. Ilifika mda mahusiano yakaisha, yeye alidai mimi sina msaada kwake , ila kuna nyakati nilikua na msaidia kila ninachoweza.
Wimbo namba 5 na wa mwisho ni huu uliobeba jina la EP, Street Motivation. Jina la wimbo linatakiwa liende sawa na kile kinachoimbwa Kwenye mistari ya wimbo kuna line imeleta ukakasi kidogo. Mtu anasema akikosa nafasi mjini arudi kijijini akawe mkulima. Swali je ukiwa kama Mr Street Motivation ukulima unauchukuliaje au ni kwa ajili ya watu walioshindwa maisha au ni kazi kama kazi zingine?
Hio line kwamba hapo sio kila maisha yapo mjini tu, kuna nafasi nyingine pembezoni mwa miji tunaweza fanya na tukafanikiwa sio kila mafanikio yapo kwenye mazingira yako, kuna namna inakulazimu utoke ili ufanikiwe.
Unazizungumziaji hizi platform za mziki je zinalipa au ni miyeyusho maana nimeona EP yako hii umeweka yote katika platform mojawapo huku ukisema mtu akitaka kununua achangie Tsh3000 na kwenye platform unajua mtu anasikiliza free, je kuna faida gani unapata kwenye kusikiliza free?
Hizo platform kuna baadhi miyeyusho siwezi kuzitaja kwa sababu za kibiashara, hapa nilipoweka kazi yangu naona patanilipa zaidi kwa tafiti nilizofanya kabla ya kuweka muziki wangu hapo swala la mtu akitaka anunue kwa Tshs 3000/= ni kwamba kila mtu asikilize ama akikosa hio elfu 3000/= basi anaweza kupata hata 1000/= akaweka bandle na ku stream online, lakini lengo kubwa hasa ni kupata waskiilizaji wa aina tofauti kwenye career yangu ya muziki naamini ili upate lazima uwekeze "Invest before you earn" anasema the late Nipsey Hussle R.I.P .
Je mtu akitaka kupata hii EP na kazi zako zingine zilizotangulia anazipata kwa njia gani?
Zote zinapatikana katika digital platform ya Audiomack, hapo ndio mtu anaweza kupata kazi zangu zote zilizopita pamoja na EP ipo hapo pia.
Tutegemee kitu gani kitafatia toka kwako baada ya hii EP kuingia sokoni?
Baada ya mradi, nitakuja na album baadae.
Tupitie kusapoti Hip Hop toka kwa Gamba.
Facebook: Gamba Junior
Instagram: Gamba138