Ukaguzi Wa Albam: Sankofa II
Msanii: Gego Master
Tarehe iliyotoka: 01.07.2020
Nyimbo: 15
Ma Producer na Wapiga Midundo: Sigga, Steve, Bano, A-M-O-C, De La P,
Mchanganya Sauti na Midudo: Sigga,
Studio: Paradise Apple, Digg Down Records
Baada ya kujenga msingi mzuri kwenye mradi wake wa kwanza Sankofa mwaka mmoja baadae emcee Gego Master alirudi tena na sehemu ya 2 ya series ya Sankofa na kutupatia Sankofa 2 tarehe moja mwezi wa saba 2020 ambayo ni mwaka mmoja kamili baada ya mradi wake wa kwanza.
Mradi huu unaanzia kule tulipotoka kwa Sankofa kwenye single ya mradi huu iendayo kwa jina hilo hilo Gego Master anaonesha vile mradi wa kwanza ulikua hatua kubwa ambao umemuwezesha yeye kupiga hatua nyuma na kujitazama na kisha kuweza kupiga hatua mbili mbele kwa kupitia mradi huu akisema,
“Ashanti Fulani Zulu na Dogon/
Igbo Chaga Maasai na Ngoni/
Twende Usukumani Wamakonde wa kusini/
Kenya Kalenjin Luo na Kikuyu/
Nchini Uganda Bahamba na Baganda/
Banyarwanda Songea kwa Wamanda/
Mtoto Wenu niko hama vya zamani navitaka/
Nimefundishwa na Akan ni seme Sankofa/
Koffi Annan kule alipotoka/
Na kama hujui ulipotoka hujui unapokwenda/
Na hiyo ndio Sankofa/
Najua mnaipenda ni Sankofa ya pili/
Ya kwanza imenijenga/
Scientist emcee nafanya mnachopenda/
Nachukua maneno nayasaga kwenye blender/
Kwame Nkurumah tujifunze daima/
Sankofa inatutuma tujifunze ya nyuma/
Kwenye mradi huu Gego Master hajacheza mbali na formula iliyomsaidia kufanikisha mradi wake wa kwanza ambao ni K.I.S.S yaani Keep It Simple Stupid kwani yeye ana uwezo wa kuandika mashairi simple yanayobeba mawazo complex.
Mradi huu ambao una nyimbo 15 una madini kibao na nyimbo nyingi ambazo mimi binafsi nilizipenda. Mradi unaanza na wimbo uitwao Ile Siku ambao ni moja ya nyimbo zinazokutia nguvu na kukupa matumaini kando na kukupa ujasiri wa kukabili ishu yoyote inayokusumbua maishani mwako. Nyimbo nyingine yenye nia hii ni kama Kila Siku Mtaani, Hard Time, pamoja na Mwaka Mpya.
Miradi mingi ya Hip Hop inapofika kwa interlude au muda wa mapumziko huwa wanatupatia ka skit ka dogo ila Gego aliamua kutumia mda huu kufanya kitu tofauti. Kwenye interlude mbili kwenye mradi huu Gego anageuka The Teacher au mhadhiri wa chuo kikuu na kwa dakika tano ya kila kipindi anatupiga Lecture na Lecture 2 ambazo zote zinaongelea historia ya utamaduni wa Hip Hop nchini Tanzania kama utangulizi wa kitabu chake cha Uelewe Utamaduni Wa Hip Hop.
Na mada hii ya utamaduni wa Hip Hop ameiwakilisha vyema kwenye mradi kwenye nyimbo zifuatazo; Classic akiwa na Ado Mo pamoja na Saint Pio, Wapenda Rap, No More Drama, HIP HOP pamoja na Mimi Na Wewe.
Mimi Na Wewe unapiga vizuri sana wakati Gego anapongelea mapenzi yake na utamaduni wa Hip Hop na historia ya mapenzi yake na Hip Hop toka akutane na mpenzi huyu hadi sasa. Mdundo na kiitikio pia vimegonga freshi sana kwenye wimbo huu.
Kwenye wimbo Classic Gego akishirikiana na Ado Mo pamoja na Saint PO wanakumbuka miradi pamoja na wana Hip Hop waliokuwa wakiwaangalia na waliowakubali.
Mada ya mahusiano imeguswa kwenye nyimbo kadhaa kama vile Gego The 3rd akiwa na Mau Kolimba, Rafiki Zangu pamoja na Tunawakumbuka akiwa na Mau Kolimba tena. Kwenye Gego The 3rd emcee huyu anaamua kumuimbia kijana wake wa kwanza kwenye wimbo mzuka sana ambapo kijana akizidi kukua atakuta hapa kawachiwa madini ya tanzanite na dhahabu. Mau Kolimba akitumia sauti yake nyororo anampiga Gego kampani nzuri sana.
Kwenye Tunawakumbuka Gego anashirikiana tena vizuri sana na Mau Kolimba kumwaga mvinyo kwenye ardhi akiwakumbuka watu wake wa karibu waliotutangulia mbele za haki. Wimbo ni mzuri asilimia 100 na umetumia akili 100 ili kuufanikisha; A-M-O-C kaandaa mdundo mzuka sana ambapo kinanda kinapiga freshi pamoja na ki violin flani ilhali Gego kachana kwa hisia sana wakati Mau Kolimba kapeleka dua zetu kwa muumba kwa niaba ya wafu akitumia karama ya sauti yake nzuria sana kama kawa.
Sankofa 2 imepiga tofauti na inaonesha vile Gego anazidi kunoa ubunifu wake kimashairi, ki mada pamoja na uchanaji wake. Pia unataji wake kwa midundo kwenye mradi umeanza kukolea kama rangi kwenye kitambaa cha kaniki. Turudi Kush na Kemet kupitia Sankofa 2.
Kupata nakala yako ya mradi huu wasiliana na Gego Master kupitia;
Instagram: Gego Master