Ukaguzi Wa Albam: Sankofa III – The Trilogy Of Knowledge
Msanii: Gego Master
Tarehe iliyotoka: 01.07.2021
Nyimbo: 13
Ma Producer na Wapiga Midundo: De La P, Sigga
Mchanganya Sauti na Midundo: Sigga,
Studio: Paradise Apple

Gego Masta - Sankofa

Ili vitu viwe imara mara nyingi huja kwa utatu. Kwa mfano ukimwangalia binadamu ana akili, mwili na roho au dunia nayo kadri unapochimba kwenda ndani utaona pia ina safu tatu ambazo kwa kingereza zinaitwa crust (ipo kwa nje hadi umbali kiasi kwenda ndani), mantle ambayo ipo ndani zaidi kabla hujafika core ambayo huwa ni uji uji unaofahamika kama lava wakati wa volcano.

Hivyo basi Gego Master alijua kwamba ili kuelewa vizuri hili somo la Sankofa lazima atatupatia mradi mmoja tena ili kukamilisha principle ya utatu wa utulivu na hivyo basi tarehe 01.07.2021 alifanikisha hili kwa kutupatia Sankofa III – The Trilogy.

Mradi huu unaendeleza ile mada ya Sankofa inayosema “Turudi nyuma tukakichukue” ila wakati huu anaanza kwa kutupeleka nchini Japan ili tuweze kujifunza toka kwao kuhusu Ikigai ambayo inamaanisha “kitu kinachompatia mtu hisia ya kusudi la kuishi”. Kwa kupitia mdundo mzuka wa Sigga anatuelemisha kuhusu concept hii kwa kutupa watu wanaoishi Ikigai na kutupa mifano na akisema kwake binafsi Hip Hop ndio Ikigai yake. Anatuambia hivi,

“Kuwa bosi wa maisha yako hiyo ndio Ikigai/
Kupata na kufanya kazi unayo ipenda, ambayo inakupa fedha hiyo ndio Ikigai/
Kulala unapotaka Kuamka unapotaka hiyo ndio Ikigai/
Nenda ndani ya nafsi yako toka na kitu chako/
Kujiangalia mwenyewe na kuangalia wenzako hiyo ndio Ikigai/
What’s your Ikigai? Ajira sio Ikigai/
Shtuka amka fasta find your Ikigai/”

Kama vile miradi ya awali Gego anaendeleza formula ya mada zilizofanikisha miradi ya awali ambapo mada za mradi zimegawanywa kwa makundi kadhaa, utafutaji wa maarifa, nyimbo za mahusiano pamoja na Hip Hop.

Kando na kutudokezea kuhusu Lifestyle yake akiwa na Kugu Gego anatutia moyo tutafute maarifa kwenye vibao kama vile Every day, SOMA akiwa na Songa, Giza akiwa na Della P pamoja na Mwanzo. Kwenye SOMA ambao umeundwa vizuri sana na Sigga ma emcee hawa wanakwambia elimu haina umri, jinsia wala kikomo. Wimbo mzuka sana ambao unakupa motisha kuwa mtafiti na mtu wa kupenda kutafuta madini yaliyofichwa kwenye vitabu.

Kwa upande wa mahusiano Gego anatoa shout kwa shemeji yetu tena kama kwenye Sankofa(1) kwenye Kwa Ajili Yako akiwa na Masiah na tena kuwakumbuka waliotuacha kwenye Ni Mchizi Tu akiwa na Geof Master.

Pia kama ilivyo desturi yake anakumbuka waasisi wa Hip Hop kwenye Wakongwe pamoja na kutukumbushia historia yetu kwenye Giza akiwa na Della P kabla ya kutufungia mradi na Mwanzo akiwa na Della P tena pamoja na Mau Kolimba ambao unagonga vizuri sana.

Sankofa 3 ipo vizuri ila kwangu mimi haikufika vigezo vilivyo wekwa hapo awali kwenye Sankofa 1 na 2. Ila nadhani ni hatua moja nzuri kwa Gego Master kuzidi kuuwakilisha utamaduni wa Hip Hop sio tu kama mwana historia anayetupatia vitabu tulivyovizoea bali hata kwa njia ya kinasa. Safari ya kilomita alfu moja huanza na hatua moja, na Sankofa ya utatu ni hatua ya tatu nzuri.

Kupata nakala yako ya mradi huu wasiliana na Gego Master kupitia:
Instagram: Gego Master