Ukaguzi Wa Albam: Sankofa
Msanii: Gego Master
Tarehe iliyotoka: 01.07.2019
Nyimbo: 10
Ma Producer na Wapiga Midundo: Abby MP, A-M-O-C,
Mchanganya Sauti na Midundo: Abby MP
Studio: Digg Down Records
Wiki hii nilikuwa nimeamua kuchambua mradi wa Gego Master Sankofa 3 ila nikaona ili kuweza kuuchambua vizuri mradi huu lazima nianze Sankofa (1). Hivyo nikapekua mtandao na kwa bahati nzuri nikakuta Gego kaweka Sankofa (1) pale Bandcamp ili uweze kuuskiza wote na ukiupenda, uununue.
Hiyvo basi moja kwa moja nikapiga mbizi ndani mradi ili kuweza kuona kilichopo. Kwanza kabisa tuanze kwa kufahamu Sankofa ni nini? Neno Sankofa linatokana na watu wa Akan wa nchi ya Ghana. Ni neno la Kiakan linalomaanisha kihalisi “kurudi na kukichukua.”Moja ya alama za Adinkra kwa Sankofa inaonyesha ndege wa kizushi akiruka mbele na kichwa chake kimegeuzwa nyuma. Hivyo basi emcee huyu kwa kupitia mradi huu anataka kuturudisha nyuma ili tukachukue…
Mradi unaanza na utangulizi mzuri toka kwa Gego Master akitueleza kidogo kuhusu maana ya Sankofa kama nilivyofanya kwenye utangulizi wangu pia. Kando na kutukumbushia maana ya Sankofa kiujumla Gego anatuonesha vile mradi huu ni special sana kwake kwani ni jaribio lake la kwanza la kutuonesha uwezo wake wa kughani baada ya kujifunza kufanya hivyo. Pia kafanya mradi huu kwa ajili ya yoyote anaependa utamaduni wa Hip Hop.
Mradi huu kulingana na vile nilivyouskia mimi umegusa mada kadhaa kuu zikiwemo, historia kwa mtazamo wa “kurudi, kuchukua na kuthamini” tulipotoka, imani, mahusiano, utamaduni wa rap na pia mawazo chanya ya kutujenga.
Kwenye nyimbo mbili za kwanza, Guidance akiwa na Jadah MaKaNTa pamoja na Wonderful World Gego anatupatia historia na kugusia maswala ya imani vizuri na kutuonesha kwa nini pia anajiita Scientist Emcee. Guidance unapiga vizuri sana ki mdundo, kimashairi na kwenye kiitikio sauti ya Jadah MaKanTa inaimba vizuri sana hadi unabarikiwa. Gego anatema madini ya kiroho akisema,
“Muumba Mbingu Ardhi na watu/
Ameniumba mimi wewe na chatu/
Tumeumbwa tofauti kila kitu/
Na Akaumba Mchana pia Usiku/
Naomba kwa niaba ya Ndugu zangu/
Eeeeeh Mungu saidia hawa Ndugu/
Waambie kwamba upo ndani yao/
Ili waache kukutafuta nje yao/
Penda kujifunza kila siku/
Hebu Tenda bila kulipwa hata kitu/
Hebu Nenda popote walipo watu/
Hebu ona Thamani kwa kila mtu/
Jiulize ukweli wa Historia yako/
Jifunze toka kwa babu zako/
Jitukuze na huo Uafrika wako/
Elewa Melanin ni nguzo juu yako/”
Mashairi yake yako rahisi sana kuandika ila yana madini kibao kama unavyoona. Moja ya nyimbo nilizopenda kwenye mradi huu. Wonderful World nao unatumia vizuri sampuli ya wimbo What A Wonderful World wa Louis Armstrong na kutupatia mdundo pamoja na mziki mzuri sana. Kupitia wimbo huu unasafiri dunia ya kale na ya sasa kupitia mashairi ya emcee Gego
Mada ya mahusiano ipo kwenye wimbo wa Gego The 2nd akiwa na Jay Mbili ambao ni wimbo aliomuimbia shemeji yetu. Ni wimbo unaoishi huu ambapo Gego anatufungulia pazia ili tuone kidogo kuhusu maisha yake ya familia pale anapotusimulia kuhusu alipompata shemeji yetu, mapenzi yao kukua hadi wao kuanzisha familia na ujio wa mtoto wao Gego The 3rd. Wimbo mzuka sana
Nyimbo kama vile Zaidi ya Rap akiwa na Dark Master pamoja H.I.P H.O.P akiwa na Magenge ni nyimbo zinazoongelea utamaduni wa Hip Hop. Zaidi ya Rap inatukumbushia kuwa Hip Hop ni zaidi ya kughani kwani wana Hip Hop ni wajisiriamali, wanajihusisha na machata pamoja na graffiti na pia ni watu wanaopenda kusoma ili wapate elimu.
Kando na wimbo wa kula bata House party nyimbo zilizobakia ni nyimbo za kukutia moyo na kukujenga. Acha Waseme akiwa na producer Abby MP ni wimbo wa kuwabeza wale wavunja moyo waliopo maishani mwenu kwa kuweka bayana vitu ulivyoweza kufanikisha maishani mwako tofauti na matarajio yao na yale walikua wanasema dhidi yako.
Pia kwenye Tunaflow akiwa na Fivara ma emcee hawa wanatuonesha vile kila kitu huanza kikiwa kidogo hadi kukua na kukamilika akisema,
“Chumvi inakua sukari/
Asali inakua shubiri/
Mistari inakua nyimbo/
Na nyimbo inakua jingle/
Na kisha tuna make bingo/”
Mambo yanakua mambo/
Ule msongo wa mawazo/
Nilishausahau kitambo/
Na bado tupo bongo/
Ni international ila local/
Smart sio kitoto/
Na hatunaga longolongo/”
Kila siku hatua dua kwa hiyo kila siku Tunaflow. Tega Skio pia ni wimbo chanya ambapo Gego anakutia moyo kwa yoyote magumu unayoyapitia akikutia moyo kwenye wimbo ambao anatema beti za nguvu.
Mradi huu ni mzuri na mashairi ya Gego ni mepesi kuelewa kwani yameandikwa kwa mtindo wa moja kwa moja. Hata kwa upande wa kughani Gego amejitahidi sana ukiangalia ya kuwa yeye mwenyewe kasema kuwa mradi huu ndio wake wa kwanza unaokua kama ushahidi kuwa yeye pia anaweza kughani. Huu ni msingi mzuri kwa ajili ya santuri za Sankofa zinazofuata.
Kupata nakala yako ya mradi huu wasiliana na Gego Master kupitia mtandao wa kijamii:
Instagram: Gego Master