Uchambuzi Wa Kanda Mseto: Undisputed
Msanii: Genry UK+
Tarehe iliyotoka: 13.01.2021
Nyimbo: 19
Muunda Midundo/Mtayarishaji/Mchanganya Sauti Na Midundo: Mdachi
Studio: Wadachi Music Africa
Hip Hop ya handakini kama mnavyo ifahamu inatuletea vipaji kibao kila iitwapo leo. Ma emcee hawa baada ya kuchana mbele ya familia zao au washkaji inafika mda wanaona kuwa itapendeza kama watu wa nje wangepata fursa ya kuwaskia. Hivyo basi kwa kuamini kuwa ana talanta ya kipekee anaenda studio na baada ya kuachia singles kadhaa anaamua kuachia mradi wake wa kwanza iwe ni EP, Kanda Mseto au hata Albam. Kwenye kundi la ma emcee hawa kuna mmoja kachipukia kule Mbeya kwani jina Genry Uk+. Tofauti yake na ma emcee hawa wanaozidi tokea kule handakini hadi yeye kwa kujiamini sana na kua hana wa kumpinga aliita kanda mseto yake Undsiputed Mixtape.
Mradi huu ambao umeundwa asilimia mia chini ya usimamizi wa Wadachi Music mmiliki wa Wadachi Music Africa unaanza na Intro toka kwa Lugombo MaKaNTa. Mradi huu moja kwa moja Genry UK+ ameuunda na nia ya kuonesha ubabe wake kwenye Hip Hop ya Handakini kwani kwenye wimbo uliobeba jina la albam Undisputed akiwa na Dimo anasema malengo yake ni kujikita handakini wakati wa kufanya sanaa yake na kuhakikisha yuko real.
Mradi huu ukiuskia utaona vile emcee huyo ana uwezo wa kutumia ubunifu wake kuongelea mada tofauti pamoja na kuongelea mada ngumu kwa njia nyepesi kwa uelewa wa mashabiki zake. Pia emcee huyu ana uwezo wa kukusimulia story ukacheka, ukatafakari na ukasikitika pia.
Nyimbo zinazoonesha uwezo wa kupiga story kwenye mradi huu zipo kibao kama vile, Bado Natafuta akiwa na Pizzo Madawa ambao unaanza na salamu za Kinyakyusa kabla ya Genry kutueleza kuhusu historia yake akisema kuwa kilichomvunja moyo kutopenda elimu ni kuwa walikuwa wanapofunza wapi hela zinapopatikana. Nyimbo nyingine za hadithi ni kama Dream akiwa na T Breaker, Usaliti akiwa na Alvin, Mkasa Wa Mlevi pamoja na Mtemi Junka. Jamaa yuko vizuri sana kwenye uandishi na uchanaji wa storytelling. Mkasa Wa Mlevi utaona ucheshi wa kamanda pamoja na mashairi yake freshi.
Ili kutuonesha vile handaki imekolea ndani mwake kachana kwenye nyimbo kadhaa kuhusu mada hii; Interview, na Dreamer, Maswali Na Ushauri, Control pamoja na Handaki. Mission 6 O’clock (Cypher) ni cypher la kibabe linalokamilisha mradi kiujumla ila inakuonesha uwezo wa Genry kung’ara bado akiwa na ma emcee tofauti kwenye booth.
Kwa upande wa mahusiano, emcee Genry ameongelea mada hii kwa upana kwenye nyimbo kadhaa kama Rafiki Shida (Belaciao) ambao mdundo unatumia sample ya Belle Ciao toka kwa La Casa De Papel . Pia kuna Mwanangu akimshirikisha Clarence, Usaliti akiwa na Alvin, Nikupambe unaotumia sample za mziki toka kwa Backstreet Boyz(Shape Of My Heart) pamoja na Nakupenda wa marehemu Brenda Fassie. Kwenye Sijamjua ametumia vizuri pia sampuli toka kwa wimbo wa Marijani Rajabu(Georgina) ambapo kwenye kiitikio emcee huyu ameamua kutumia mahojiano kati ya watu wawili wanaotafuta vigezo vya mwanamke wa kuoa. Mdachi amempatia mwana midundo freshi na, cheki Mwanangu na Usaliti na nyingine kibao.
Nyimbo nyingine ambazo ni chanya sana kwenye mradi huu zenye mitazamo tofauti kama kukutia moyo pamoja na kuongelea changamoto za maisha yetu ni kama Kaza, Msanii Mwenye Kiu , Wema pamoja na Ghetto ft Clarence. Kwenye Wema unatumika sampuli nzuri sana kwenye mdundo pamoja na magita wazimu sana wakati Genry akimsifia Wema kama vile mpenzi,
‘Tangu nikujue nimejifunza vingi/
Sio kila nipendacho mie nitalipa kwa shilingi/
Hey kama utani tulipoanza msingi/
Nina mengi ya kufanya ila ndo ndio ya msingi/
Kwani nimependa vyote vizuri toka kwako/
Na ikibidi tufe wote nikiwepo kando yako/
Wema kwa kweli yani unastahili sifa/
Sikuachi nikafeli milele mpaka na kufa/
Umenifunza vizuri kuishi niwe na kiasi/
Tabia mbaya sio vizuri ina urafiki na hasi/
Wa Ukokola mimi kwangu wewe ni kila kitu/
Sitasahau maishani unavyouthamini utu/
Bila kujali rika heshima ni ngoma draw/
Mpaka nafarijika kunipenda hardcore/
Wema jamani uzuri wako hauelezeki/
Kama ungeuzwa dukani kila mmoja ange make it/
Baki kuishi na mimi sitokuacha asilani/
Wanasema tuwe ndani nawaambia unaishi moyoni/
Mwangu daima tayari umekita nanga/
Sishangai wakisema eti unaringa!/
Kiukweli mradi ni moto sio tu kwa utunzi wa mashairi bali hata kwa uwasilishaji, midundo iliyotumika pamoja na wageni waalikwa kufanya yaliyowaleta. Genry Uk+ anawania kuwa Undisputed kuna wa kumpinga? Karibu ndani ya ring.
Kupata nakala yako ya mradi huu wasiliana na Genry kupitia
Facebook: Genry Mwankemwa
Instagram: mwankemwagenry
WhatsApp: +255 789 435 354