Uchambuzi Wa EP: Chapter Of Love
Msanii: Ghost The Living
Tarehe iliyotoka: 31.03.2021
Nyimbo: 5
Watayarishaji: KC, Teez
Studio: Neptone Records

Nyimbo nilizozipenda: Mtoto Mchanga, Binti Mdogo, Jiandae, Malkia

Ghost The Living

Ghost The Living ni emcee ambae nimekua nikifuatilia kazi zake kwa karibu sana. Binafsi nilianza kumskia baada ya kupata mahojiano aliyofanya na mwandishi Beberu La Mbegu wakiongelea wimbo wake Hatari Isiyojulikana tulioupatia Nukuu Iliyonukuliwa hapa hapa Micshariki Africa. Baada ya hapa ndio nikaweza kuskiza ngoma zake zingine kama R.I.P Roberto, Koboko, Taxi Driver na No Formula.

Mwaka jana alitoa EP yake ya kwanza rasmi na sikua na budi kupata nakala yangu iliniweze kumskia emcee huyu vizuri na kwa ukaribu. Chapters Of Love ndio inapiga toka kwenye speakers zangu leo.

Ghost The Living ambae jina lake unaweza kulitafsiri kwa Kiswahili kumaanisha Mzimu Unao Ishi kwenye mradi huu amejikita kwenye mada ya upendo kwenye nyanja tofauti. Mradi unaanza na wimbo wa kwanza, Hakuna Upendo ambapo kando na kuchana tu anakuonesha pia anaweza kuimba kama tunavyoona kwenye kiitikio. Wimbo huu unaongea kuhusu upendo kutopewa thamani unayo stahili au kutokuwepo kabisa.

Wimbo Binti Mdogo akiwa na OB D unaonesha uwezo wa Ghost kutuchania hadithi. Wimbo huu ambao unaopiga kwenye mdundo wenye hisia ya kusikitsha unamkuta binti flani akimsimulia Ghost historia ya maisha yake na sababu zilizo msukuma yeye akawa kahaba.  Kwenye wimbo huu wenye beti Ghost anachana bila kupumzika mwanzo mwisho hadi pale OB D anachukua doria kumalizia wimbo.

I’m Sorry akiwa na Davoo ni wimbo wa mahusiano na mapenzi kati ya Ghost na mpenzi wake akiongelea changamoto wanazokabiliana nazo zikiwemo wabaya wao kuwataka wa achane. Na japokua wanapitia mengi emcee huyu anasema haya;

“Tunaishi maisha yote iwe tabu au njaa/
Hatukua na mboga saba ni ugali kavuu dagaa/
Still upo nami kama nyayo na bapa/
Tofauti na wengina ambao wao wana achwa/
Najiuliza bila wewe ningependwa na nani/
Moyo ungevunjika ningewekwa rehani/
Nikiwa nawe mami ni raha tupu/
Nioneshe utamu wote tukiwa room vaa nusu/
Wenye chuki wanywe sumu wajinyonge/
Vile bora vile hai waje humu wajikombe/

Nikutunze kwa makini kama sahani za wageni au vikombe/

Nikutunze venye fiti majirani hawahemi/
Wenye wivu eti, “Steve siku hizi umeoa?”/
“Ndio nina mtoto!” Na nyie sikuhizi mna boa/
Baby wee hujui tu navyo kupenda nakuhitaji/
Kwangu ni zaidi nakupenda nakuhifadhi/”

Mtoto Mchanga akiwa na Davoo tena ni wimbo mzuka sana unao onesha zaidi uwezo wa Ghost kusimulia hadithi. Wimbo unaongelea vile Ghost akiwa bado kapera anayejipanga maishani mwake anakuta mtoto katupwa nje na mlango wa chumba alicho panga yenye hadhi duni. Anaamua kumchukua mtoto huyo na jamii inamgeuka na kumuuzia kesi kua mtoto huyo inawezekana niwake kaachwa na mmoja wa wapenzi wake ambapo siyo kweli. Davoo anamwaga hisia kwenye kiitiko akisema,

“Nyamaza kulia mwana simjui mama/
Na mimi ghetto nashika tama hiyo/
Mbele sioni nahisi kiza kimetanda (yeah yeah yeeaa)/
Mtoto mwenyewe bado mdogo/
Ghetto mi nakula msoto/
Ntampa nini yeye hafurahi…yeye afurahi…./

Wimbo mwingine mzuka sana wa mahusiano ni Malkia Wangu akiwa na OB D kwenye mdundo mzuka sana unaopiga vinanda freshi sana.

Ghost The Living yupo hai kwenye Chapters Of Love.

Kupata nakala yako ya EP hii kwa buku 5 (Tshs 5000) wasiliana na Ghost The Living kuptia;

Facebook: GhostThe Living
Instagram: ghost_the_living
WhatsApp: +255 759 339 884