Goda MC

Goda MC nilianza kumfahamu baada ya kuchukua nakala za miradi ya DDC. Kwenye miradi hii cha kwanza kilichonifanya nimfahamu Goda MC ni sauti yake nzito na ya kipekee pamoja na mashairi yake yenye uzito kama suati yake ilivyo.

Baada ya kufanya miradi ya jumla na wanae wa Dom Down Click, Goda amekuja na EP yake mpya TUFE. Tulipiga nae gumzo kuhusu safari yake ya muziki, teknolojia na mradi wake mpya.

Karibu sana Micshariki Africa kaka Goda MC. Kwanza kabisa hongera kwa EP yako ulioachia hivi majuzi TUFE EP. Kabla hatujaenda mbali na kuanza kuongelea kazi hii, ningependa kukufahamu majina yako rasmi, unatokea wapi na unajihusisha na mishe zipi?

Asante sana, ninaitwa Andrew Michael Mihayo, nje ya muziki.  Mimi ni mtunza takwimu (data manager), katika idara ya afya ya wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.

Tupe historia yako kaka, ulizaliwa wapi, ulisomea wapi shulezya msingi na upili na baada ya hapo uliendelea hadi wapi? Pia utoto wako ulikuaje?

Nilipata elimu ya msingi katika shule ya msingi Mwadui, baada ya hapo niliendelea na msomo yangu ya sekondari katika shule ya Shinyanga Secondary iliyoko mkoani Shinyanga na baadae kumalizia masomo katika shule ya Jitegemee Secondary iliyoko jijini Dar Es Salaam, na nilipata masomo ya stashahada ya Information Technology katika chuo cha University Of Dar Es Salaam Computing Centre (UCC).

Goda MC alianza kujishughulisha rasmi na muziki miaka ya 2000 mwanzoni akiwa anasoma katika shule ya Sekondari Shinyanga iliyojulikana sana kwa jina la Shybush pamoja na wenzake watatu waliounda kundi la Bega Crew ambao ni Chizzo B(Essau Musakanka), Faso B(Bonifasi Mfutakamba) na Mtemi Jirani(Gervas Nyaringa), enzi hizo akifahamika kama Ammyson.

Pamoja na kutopata nafasi ya kurekodi wimbo hata mmoja walijipatia umaarufu mkubwa kutokana na kuhudhuria matamasha mbalimbali yakiwemo ya kiushindani na kuibuka washindi mara nyingi zaidi, huko Shybush, Mwadui, Maganzo pamoja na Shinyanga mjini kiujumla. Kundi lilisambaratika miaka ya 2003-2004 mwishoni baada ya kila mmoja kumaliza shule kwa muda wake na kurudi nyumbani.

Kuanzia mwaka 2005 katikati Goda MC akijulikana kama Andre_7,alibahatika kukutana na wanamuziki kama Masta Vepa aliyewahi kuwa katika kundi la Joint Mobb pamoja na TMK Wanaume Family kwa vipindi tofauti na aliyewahi kutamba na kibao kama Mtani Jirani alichomshirikisha Juma Nature akiwa na Joint Mobb.

Baada ya kukutana na Goda MC (Andre_7 kipindi hicho), Chat B na Mmasai waliamua kuanzisha kikundi chao na kukiita Tmk Watukazi na ndipo Goda MC (Andre_7) alipopata nafasi ya kuanza kurekodi katika studio za Sound Crafters ambapo walifanya kazi kadhaa chini ya mtayarishaji Henrico, Mark 2b (R.I.P), pamoja na mkongwe Drez Chief.

Baadhi ya nyimbo walizofanikiwa kuzi rekodi kama Tmk Watukazi ni pamoja na, Niacheni, Huwezi Kuzuia ft. Juma Nature pamoja na Sara ft. Banana Zorro ambazo hazikupata nafasi ya kuwika. Kundi hili TMK Watu Kazi lilisambaratika miaka ya 2007 kutokana na majukumu mbalimbali  yaliyokuwa yakiwakabili wanafamilia na Goda MC kurudi shule akisoma maswala ya IT pamoja na Graphics Design.

Mwanzoni 2008 Goda MC alikutana na James Msafiri (Umbwa), Stopper The Rhymmeca(Waturutumbi) katika studio za Jaz Records pamoja na Az(Azizi Kipingu) aliyekuwa mmiliki wa studio za Jaz Records chini ya producer Q The Don pamoja na Tuddy Thomas kwa vipindi tofauti hapa akiwa graphic designer na alifanikiwa kutengeneza logos za t-shirt za Jaz Records na logo ya t-shirt ya mocumentary kwenye mradi wa documentary ya Jay-Moe iliyokwenda kwa jina la Mocumentary pamoja na hapo alifanikiwa kurekodi nyimbo mbalimbali ikiwemo Usupastar ft. Linex ambayo haikufanya vema pia kwa kipindi hicho.

Baada ya Jaz Records kufungwa miaka ya 2009-2010 ndipo Goda MC alipohamishia makazi yake Dodoma rasmi na hapo ndipo alipokutana na Lucas Malali(LC),Adam Selemani(Adam Shule Kongwe), Andrea Kimolo(Andre_K R.I.P), Saidi Javani(Chuna Ngozi) pamoja na Saidi Yahaya (Miracle Noma) ambapo walikuja kuunda kundi lijulikanalo kama Dom Down Click(Ddc).

Wakafanikiwa kurekodi albam kadhaa ikiwemo The Element Vol 2, Mechanism, Fasihi Simulizi Pamoja Na Dira ambazo zote ziliachiwa. Goda MC akiwa kama solo artist nimeachia Tufe EP, ni mradi wake wa kwanza na rasmi kama solo mc, asante.

Kuhusu utoto, wakubwa wanasema nilikuwa mtundu sana kiasi kwamba wanashangaa jinsi nilivyokuja kugeuka mpole na mtaratibu, nilikuwa nikitokea mtaani lazima usikie watoto wanalia, nimeshawapiga makwenzi na ninakimbizwa na mama zao.

Goda MC, jina lilikujaje na lina maana gani? Pia nimekuona unajiita DoxCity kama aka, hii nayo vipi?

Jina la Goda, nilipewa na jamaa yangu wa karibu sana ambae mara kadhaa nilipokuwa nikichana alipenda kusema kutokana na uandishi wangu kutofautiana na ma mc wengi, alipenda kuniambia, "Sasa wewe ndo the Great Of Dodoma Area" hiyo moja kwa moja ikazaa jina Goda.

Doxcity imetokana na jina la mtaa wangu ninaotoka au ninaopatikana hadi sasa unaoitwa Mailimbili Mnada Wa Zamani, hapa ndipo mnada maarufu wa nyama ulipokuwepo kabla haujahamishiwa maeneo ya Msalato-Dodoma. Kutokana na mnada kuwa kitaani kwangu pia kulikuwa na machinjio, basi mtaa huo ukawa maarufu sana ukiitwa Dox, hadi leo hii ukifika Dodoma panda daladala ya kwenda Chuo Cha Mipango mwambie konda, “Shusha Dox”, atakushusha nyumbani.

Kutokana na hilo sambamba na michano kwenye mstari wangu mmoja katika wimbo ulioitwa Mistari Vitisho niliofanya na Andre_K(R.I.P) pamoja na Adamu Shule Kongwe(Old School), nilimaliza verse kwa kusema, “Mimi ndo Doxcity kada”, kwa maana mimi ni kada wa Dox, na hapo ndipo lilizaliwa jina hilo Doxcity.

Goda MC safari yako ya muziki ilianza lini? Nini kilichokuskuma mpaka sasa umefanikiwa kuwa emcee kwenye utamaduni wa Hip Hop?

Kuwepo kwenye huu utamaduni ilitokana na kupenda walichokuwa wakikifanya ma brother waliotangulia mfano, brother Sugu Jongwe, watu kama HBC (Hard Blasters Crew), Wateule (Jay Moe na Solo Thang), pia nilimpenda sana alichokuwa akifanya Fanani wa HBC.

Nakumbuka nilikuwa naweza kuchana verse zake karibu zote, nilijifunza vitu vingi sana kwake na nikawa nabadilika kadri muda ulivyokwenda hadi leo hii G.O.D.A. Pia kwa ujumla ninapenda sana muziki unaoelimisha jamii, kuijenga jamii kwa mawazo chanya, kuhamasisha watu kufanya kazi, kupinga yasiyofaa n.k. Nachukia sana nyimbo za wasanii zisizo na maadili na zinazopotosha jamii, nadhani hii ni sababu moja kubwa iliyonifanya mimi kuupenda utamaduni huu.

Binafsi mimi nilianza kukufahamu nilipoanza kununua miradi ya wana D.D.C (Dom Down Click). Kwanza tueleze kuhusu historia ya DDC, mlianzaje na wewe mwenyewe ulijikutaje ndani ya kundi hili? Nani ma emcee wanaopatikana kwenye kundi hili? Ni miradi mi ngapi mmeachia mpaka sasa, EP, Mixtape na album, ilitoka lini na inapatikana wapi?

Baada ya kuwa kila mmoja amefanya kazi zake kadhaa na kazi nyingi pia za kushirikishana,hapo ndipo lilipokuja wazo la kuanzisha kundi. Nakumbuka siku hiyo Gheto kwangu tukiwa pamoja na Lucas Malali(LC), Adam Old School pamoja na Andre_K(R.IP.),tulipendekeza majina mengi na baadae tulilipitisha jina la Dom Down Click(DDC)na baadae ma emcee wengine ,Javan Chuna Ngozi, Miracle, Kanja Wizzle, Sali Trejo walikuja kujiunga na kundi hili.

Miradi tuliofanikiwa kufanya kama DDC mpaka sasa ni pamoja na

  1. The Element Vol.2
  2. Mechanism
  3. Fasihi Simulizi
  4. Dira

Albam ambazo zote zimekwishatoka.

Goda kama solo artist pamoja na kusikika kwenye ngoma nyingi zilizoko kwenye miradi ya ddc kama kundi, mfano: Tamisemi (The Element Vol.2).

Mauaji (Mechanism), Mitambao (Fasihi Simulizi), Kaa Mbali, Andalio, Mjue Mwana, Dira n.k zilizomo kwenye Dira albam. Nina single nyingi pia mfano; Nitaacha Kitu Gani, Vita Ya Fasihi, Mistari Vitisho na nyingine nyingi, lakini Tufe EP ni mradi wa kwanza na mipango iliyopo ni kutoa albam mwishoni mwaka huu pamoja na mixtape ambayo itatoka mwaka huu pia.

Kutoka kwa album ya DDC, Dira kuna mgoma flani pale ulichana solo unaitwa Mjue Mwana ambayo nilifahamu kuwa ilikuwa dedication kwa Andre K aka Rap Suleiman (RIP). Tueleze kuhusu mchango wa huyu mwana kwenye kundi lenu na nini kilichokusukuma kuandika ngoma hii?

Nilisukumwa kuandika wimbo wa Mjue Mwana kutokana na ndoto nyingi kubwa alizokuwa nazo Andre_K (R.I.P) mwenyewe ambazo kwa bahati mbaya hazikutimia kutokana na kifo chake. Hapa lengo lilikuwa kumuenzi, kumkumbuka na ambao hawakumjua basi wapate nafasi ya kumfahamu alipokuwa hai hadi leo hii hayupo.

Nilikuwa nasema Andre_K alikuwa msanii mkali sana kuwahi kutokea na mpaka leo hii hajatokea kama yeye, alikuwa muandishi mzuri sana na mwenye mitindo mingi mizuri ya kughani "masta wa mitindo" au Dar Es Salaam Killer ni baadhi ya a.k.a zake ametuachia pengo kubwa lisilozibika.

Siku hizi nimeona members wengine wa DDC mmeanza kuchangamkia miradi ya kibinafsi. Je kundi lipo salama au ndio ishara kuwa kila mtu anaenda kivyake? Adam ana miradi kadhaa binafsi, Javan nae, Kanja Wizzle katoa Mixtape, Miracle Noma nae ana miradi kadhaa na wewe sasa na EP yako.

Kuhusu members wa DDC kufanya solo projects kila mmoja ni utaratibu ambao tumejiwekea na tunapohitaji kufanya project ya DDC kama kundi huwa hakuna kipingamizi ni swala la kupanga, kukutana na kufanya kazi. DDC ni familia kwa hiyo hata mmoja anapofanya solo project huwa anapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa members wengine.

Pia umeachia ngoma mpya hivi majuzi na Miracle Noma ambae nimeona mmeshirikiana pamoja vizuri kwa miradi kadhaa. Hii chemistry yenu ilikujaje?

Kuhusu kufanya kazi mara kadhaa na Miracle Noma ni kutokana na kuwa karibu nae kwa sasa kuliko members wengine ambao wametawanyika sehemu mbalimbali kutokana na majukumu ya kimaisha.

Kuhusu ukemia ukifuatilia utakuta wana DDC wote tuna ukemia, yani Goda na Kongwe, iwe Miracle na Chuna, Chuna na Kongwe, Kanja na Miracle na hii imetokana na kufanya kazi pamoja kwa miaka mingi sasa.

Tufe EP ilidondoka miezi kadhaa hapo nyuma. Mbona Tufe? Jina lilikujaje na linamaanisha nini?

Kuhusu Tufe EP kwanza jina lenyewe kama lilivyo"tufe"; tufe lina umbo la duara ambalo linafanana na umbo la dunia. Katika tufe nilijaribu kuzungumzia maisha ya binadamu na  hatima yake duniani, ni jinsi gani mwanadamu anatakiwa awe pamoja na changamoto zake.

Mfano track no.1: Nimebadilika inaonesha ni jinsi gani binadamu anaweza kupotea njia au kupotoka na kufanya matendo mabaya na ya kuchukiza wengine na hata kumkufuru Mungu na watu kumkatia tamaa kabisa.

Lakini katika nimebadilika inaonesha ni jinsi gani binadamu huyo wa hovyo anaweza kubadilika, kuwa mwema kutenda matendo ya kumpendeza mungu na hata kufanya makubwa zaidi yaani ukiamua kuwa unavyotaka kuwa inawezekana.

Track no.2: Bega Kwa Bega - Hii inazungumzia ni jinsi gani jamii inaweza kuishi katika maadili mema pamoja na kuheshimiana kwa dhati kwa wakubwa na wadogo na hii ni kutokana na misingi ambayo jamii imejiwekea.

Track.no 3: Kidume - Hii inahamasisha zaidi vijana kujituma katika kazi bila kukata tamaa, bila kusikiliza wakatisha tamaa n.k ili tu kuweza kufanikiwa na kujikimu kimaisha.

Track no 4: Njama Za Siri - Track hii ni mahususi kwa kumfungua akili binadamu kwamba kazi au vitu vya maendeleo anavyofanya,sio wote wanaofurahi kumuona akipiga hatua au kujikwamua kwa hiyo lazima ujue maadui wapo na hawaishi, cha msingi ukishawajua basi hawatakusumbua. Ni wimbo unaohamasisha kupambana pamoja na vikwazo vya watu hao wabaya na kuhakikisha unawashinda ili usiwape nafasi au kisitokee wanachopenda kutokea ili wacheke.

Track no 5: Akiba Ya Maneno - Hii inatufundisha kuwa na akiba ya maneno pindi tunapoudhiwa au pindi tunapokuwa na furaha kupitiliza,kwani unaweza msemea mtu maneno ya hovyo na ya kumdhalilisha bila wewe kufahamu kwamba mtu huyo huyo ndie anaweza kuwa msaada kwenye tatizo lako la kesho liwe dogo au kubwa. Wimbo unafundisha mtu kutafakari kabla ya kuzungumza, kuchagua lugha ya kuzungumza kutokana na mazingira n.k.

Track no 6: Wataasisi - Humu umeoneshwa ufundi wa kughani na kuandika yaani mitambao pamoja na kunata na mdundo.

Hiyo ndo Tufe EP.

EP hii ulianza kuindaa lini, ilikuchukua mda kiasi gani kumaliza? Je ma emcee na watayarishaji waliohusika kwenye EP hii ni akina nani?

EP hii nilianza kuiandaa Mwezi December 2022 na ilinichukua takribani miezi mitatu. Watayarishaji waliohusika katika TUFE EP ni Producer 10th Wonder, aliyepiga midundo yote kasoro bonus track Sumu Na Dawa iliyopigwa na Producer Bin Laden kutoka Tongwe Records. Mixing pamoja na Mastering ilifanywa na mtaalamu Producer Jors Bless kutoka Bless Music.

Ma emcee walioshirikishwa kwenye TUFE EP ni pamoja na Adam Shule Kongwe, Miracle Noma na Kanja (Wizzle) kutoka DDC. Wengine ni K-Voo Mkakamavu, BCP (Wage) kutoka Swahili Genge( SGK) pamoja na Young CHI.

Uandishi wako hupata msukumo kutoka wapi na wewe hupenda kuangazia hoja gani sana kwenye mashairi yako?

Uandishi wangu hupata msukumo kutoka kwenye jamii maskini na mashairi yangu hulenga katika ukombozi wa kifikra na kuleta usawa katika jamii, zaidi hulenga katika kuelimisha jamii, kuijenga jamii kwa mawazo chanya n.k

Kando na muziki unafanya mishe gani nyingine za kisanaa na pengine kazi ili kuweza kujikimu?

Kando na muziki mimi ni mtaalamu wa takwimu katika idara ya afya, wilayani Chemba mkoani Dodoma. Pia ni baba wa familia, nimeoa na nina watoto wawili.

Baada ya miradi yako hii mipya mashabiki zako watarajie nini kutoka kwa Goda MC?

Baada ya miradi yangu hii mipya ya Tufe EP pamoja na Track ya Suka mashabiki zangu wategemee kupokea albam yangu kama Goda MC mwishoni mwa mwaka huu lakini hapa katikati kabla ya albam nitaachia track zingine mbili ambazo sitozitaja majina kwa muda huu.

Hip Hop ni utamaduni unaowavutia watu wengi sana...kitu gani kilichokuvutia kwenye utamaduni huu na nini kinachokufanya ubaki kua mfuasi kila kukicha?

Kilichonivutia katika utamadani huu ni kutokana na kujipambanua kwake kwa vipaumbele vyake hasa utetezi wa wanyonge, kusimamia haki pamoja na ukombozi wa jamii kifikra kwa ujumla wake. Nimekulia katika utamaduni huu na sasa nimewiwa kuwa mwalimu wa jamii nzima. Sijiskii kukaa kimya huku nikiona mambo yakienda kombo na nina sehemu ya kusemea kupitia utamaduni huu wa Hip Hop.

Neno la ushauri kwa wadau wa utamaduni huu wanaokusoma popote walipo nje na ndani ya Africa Mashariki?

Kwa ma emcee wenzangu bado nawasisitiza zaidi kwenye kuandika zaidi kwenye mashairi ya kuelimisha jamii kwani ni mambo mengi sana hayako sawa na yanahitaji kusemewa na sisi wana hip hop,kuanzia kwenye jamii, mmomonyoko wa maadili, maasi, maovu yanazidi kukithiri, changamoto kwenye nyanja za kisiasa, maswala ya kiuchumi n.k. Waepuke sana utunzi unaoweza kwenda kupotosha jamii hasa kuwaharibu kifikra na kimtizamo watoto wadogo.

Akina nani ungependa kuwasalimu ambao wamekua na wewe kwenye safari hii ya muziki?

Kwa kweli ni wengi sana lakini baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu basi niweze kuwasalimu wachache wawakilishe maana kuwataja wote hapa hapatoshi naomba niwashukukuru, Masta Vapour(Joint Mobb),Chizzo B, Mtemi Jirani, Faso B(Bega Crew), Abuu AJ Rec, Lucas Malali(LC), Shule Kongwe, Javan,Andre_K(R.I.P), Bin Laden, 10th Wonder, Az-Jaz Rec, Stopa The Rhymmeca na wengine wengi tu.

Pengine kuna chochote ambacho sijakuuliza ambacho ungependa kutuambia?

Nadhani mengi tumezungumza tayari

Neno la mwisho?

Neno la mwisho bado nawasisitiza ma emcee wenzangu kujikita zaidi kwenye kuelimisha jamii ni kama walivyosema Msito na Fedoo, "Every Artist Should Teach”.

Shukrani sana kaka Goda MC kwa mda wako na kila la heri kwenye mbanga zako

Asante sana na kazi njema pia.