Uchambuzi Wa Album: Mwanangu
Msanii: Hafee Mauwezo
Tarehe iliyotoka: 18.05.2021
Nyimbo: 13
Watayarishaji: Dexter, Canty, AB Touch, Hafee, DTouch, Bin Laden,
Studio: B Base Records
Nyimbo Nilizozipenda: Mwanangu, Ukibadilika, Nikipendacho, One Day, Mungu Baba, No Fair, Kifo, Dear Ex

Hafee

Hafee Mauwezo nilimtafuta mwaka jana ili niweze kununua album yake Mwanangu. Miradi ya kuichambua ni mingi ila leo nimeamua nitulie na mradi huu kwanza.

Mradi huu ambao midundo yake mingi imepigwa na Dexter, umebarikiwa na midundo toka kwa ma producer wengine kama AB Touch, D Touch, Bin Laden pamoja na Hafee mwenyewe ambaye kwenye pitapita zangu mitaa ya Mitandao Ya Kijamii nimeona pia ni muunda midundo anayejiamini.

Wimbo Mwanangu ndio uliobeba jina la album ambapo Hafee amemshirikisha Chad Music. Kwenye wimbo huu Hafee anaongea na mwanae akimsimulia mazingira ya ujio wake ambayo yalimfanya Hafee kubadili mtazamo wake kuhusu maisha. Kwenye kiitikio Chad Music kabariki wimbo vizuri sana.

Hafee kwenye mradi huu aliamua kugusia mada kadhaa ambazo aliona ni muhimu kizazi cha baadae kujua kama vile Kifo akisaidiana na Mantiki Barz kwenye ngoma inayotumia sampuli toka kwa wimbo wa Remmy Ongala Sura Mbaya, Kifo. Pia mada hii ya kifo imeguswa vizuri kwenye Kama Nakuona akiwa na One Six kwenye kiitio.

Mada ya imani zetu imeguswa vizuri kwenye wimbo mzuka uitwao Mungu Baba akiwa na Chad Music na kama kawa Chad kauwa sana kwenye kiitikio hadi unaweza hisi upo ibadani. Vinanda vinapiga freshi sana kwenye ngoma hii.

Nyimbo kadhaa zimegusia mada ya mahusiano kama vile Nikipendacho, One Day akiwa na Bammy pamoja na Dear Ex akiwa na Chad Music tena. One Day ni wimbo mzuka sana unaoonesha vile Hafee alimpa shavu mwana akapata mke ila akabadilika kwenye mahusiano na kumtesa huyo mwanadada hadi akafariki. Hafee ana uwezo wa kuwakilisha hadithi freshi.

Kwenye nyimbo kadhaa emcee huyu kachana kuhusu upendo wake na mziki wa Hip Hop pamoja na uwezo wake wa kughani kama vile Ukibadilika akiwa na Bammy, Niwafundishe Kidogo, No Fair pamoja na Arobaini Za Mauwezo. Kwenye Ukibadilika emcee huyu anachana kuhusu vile watu wanajaribu kumshawishi aachane na misingi ya Hip Hop ili aweze toka;

“Hafee mambo vipi nafurahi tumekutana/
Mi ni wako shabiki wa mziki wako mwana/
Najua we ni mkali unawafunika wengi sana/
Ka ukibadilika utasogea mbali sana/
Twist kidogo kwenye flow unayo pita/
Mbona utawabamba radio nyingi zitakwita/
Hauwezi kosa shavu hata show watakupa/
Watakuweka level flani uko bomba uwe supa/
Tatizo lako mwana unachukulia poa/
Wakati ukibadilika kuna watu utawaondoa/
Inaonekana hautaki kupiga pesa/
Tuna date watoto wakali magari kuyaendesha/
Hautakiwi kua hapo ulipokua/
Si unamuona Msodoki kabadili katusua/
Ukikaza na ulipo utaambulia stresi/
Jaribu kubadilika japo pita ka Weusi/”

Hafee amejitahidi sana kwenye mradi huu; mashairi mazuri, uchanaji mzuri, uwasilishaji mzuri pamoja na midundo mizuri. Mradi huu mzuri sana Mwanangu.

Kupata nakala yako ya mradi huu cheki na Hafee kupitia;

Facebook: Hafidh Salum
Instagram: hafeemauwezo
WhatsApp: +255757763939