AFYA YA AKILI ni suala mtambuka, linaakisi mambo mengi. Unapoongelea gari, kwa mfano, haimaanishi kwamba, gari ni matairi pekee, au ni injini tu; hili halihitaji ufafanuzi zaidi, ni sawa tu na mwili wa binadamu, kiumbe kingine chochote, au hata kitu, ndiyo hata kitu!

Naamini kila kitu chenye nafasi, kinaundwa, kutengenezwa au kuwezeshwa na jambo zaidi ya moja. Hili nimeliandika kwa kufikirika tu, tafiti wakati mwingine huwa zinaanza na fikra. Hebu jiulize! Jiwe kama jiwe, unadhani halina muunganiko au mkusanyiko wa vitu tofauti na muonekano wake, vinavyofanya liwe jiwe?!

Mwili wa binadamu haujakamilika kama hauna mikono, miguu, macho, mdomo, kichwa au kiungo kingine chochote kinachofanya mwili ukamilike. Hii mantiki inatosha kumaanisha kwamba, afya ya akili ni hoja inayoakisi mambo mengi yanayojumuisha nyanja mbalimbali za maisha tunayoishi, iwe ni kiuchumi, kisiasa, kijamii, kisaikolojia, kitamaduni na kadhalika.

Nyanja yoyote kati ya hizo, ikiwa na changamoto inaweza kusababisha tatizo linaloweza kupelekea kwa changamoto ya afya ya akili kwa mtu husika, japo sio kwa kila mtu, na hii ni kulingana na namna tunavyotofautiana hasa kisaikolojia linapokuja suala la kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Fikra zetu, hisia, na matendo yetu, hutegemea afya ya akili, ambayo kwa mantiki hii, pia inachangia kwa kiasi kikubwa kwa afya ya mwili. Kuna watu wenye matumaini, na ari ya kutokata tamaa kimaisha, japokuwa hii haifanyi wasipitie changamoto zinazoweza kuwakatisha tamaa kiasi cha kuwayumbisha kisaikolojia, kulingana na hali halisi, kwa mfano mazingira ya kazi, mahusiano, magonjwa, na kadhalika. Unaweza ukaanza siku ukiwa na furaha, ila ukaimaliza ukiwa huna amani, na kwa mfano huu, mtu anaweza kujikuta kwenye changamoto kama za wasiwasi, huzuni, matumizi ya madawa ya kulevya, n.k., hivyo afya ya akili, kama ilivyo kwa afya ya mwili, sio suala fixed, na badala yake hutegemea hali halisi tunazopitia, na mara nyingi sio moja tu.

Uelewa kuhusiana na afya ya akili ni muhimu hasa ukilinganisha na mfumo wa maisha tulionao, kwa mfano, tatizo la ajira, na ugumu wa maisha kwa ujumla, yanapelekea watu wengi kushindwa kukabiliana na changamoto husika, na hivyo kusababisha baadhi yao kufikia maamuzi yanayoacha simanzi kwa ndugu, jamaa na marafiki. Utumiaji wa vilevi uliokithiri, ongezeko la watu wenye wasiwasi, na wenye sonona kuhusu mustakabali wao, ndugu jamaa, na rafiki zetu wanaoamua kutoa uhai wao, yote kutokana na changamoto tajwa, na nyingine nyingi.

We ni mwanaume kwa mfano, umeajiriwa, na una familia inayokutegemea, ila fikiria kitakachotokea endapo utasimamishwa kazi, au kufukuzwa kabisa. Sio peke yako utaathirika, ni familia yako nzima, na madhara huenda yasiishie kwenye kuta za nyumbani kwako; kuna mazingira yanayowazunguka, na kuna mazingira yanayohusisha wanao/mkeo. Assume wanao ni wanafunzi, matokeo ya wewe kupoteza kazi huenda yakawaathiri hadi wao, na sio tu kushindwa kuwalipia ada, ila pia kifikra, kimasomo, na inawezekana isiishie hapo, hata mahusiano yao na wenzao huenda yakawa na changamoto, kiasi cha kuongeza madhara zaidi, mfano mahusiano mabaya, achilia mbali kushindwa kuzingatia masomo hata kufeli. Unaweza ukafikiria zaidi hiyo chain reaction, na ni kumaanisha kwamba, sio wao na mazingira yao pekee, bali hata wewe na mazingira yako, na hata mazingira yenu wenyewe huathirika, wakati mwingine hata familia kuvurugika kutokana tu na hiyo changamoto.

Ishu inaweza isihusishe masuala ya kazi peke yake (kama huo mfano), ndio maana nikaainisha nyanja mbili tatu kati ya nyingi za kimaisha, mfano kuna changamoto za kimapenzi, unyanyasaji, na nyinginezo, na pengine kuna ambazo hujazisoma hapa, ila we binafsi ushawahi kukumbana nazo zikapelekea upate changamoto za afya ya akili.

Chester Bennington.

Kwa wafuatiliaji wa muziki wa Rock, hili sio jina geni; lengo sio kukusogezea historia yake kwa undani, ila kwa kifupi jamaa alikuwa mwanamuziki wa bendi inayojulikana kama Linkin’ Park. Mashabiki wao waligubikwa na mshtuko ulioambatana na majonzi, mi mmojawapo, baada ya kupokea taarifa za kifo chake. Alifariki Julai 20, 2017, akiwa ana umri wa miaka 41, na aliacha watoto sita, na aliyewahi kuwa mkewe, Talinda.

Mwendazake Chester

Katika baadhi ya mahojiano yake na vyombo vya habari, aliwahi kusema mara kadhaa kuhusu historia ya utoto wake, hasa akiihusisha na changamoto za afya ya akili alizokuwa anazipitia akiwa mtu mzima. Hapa unaweza pia kujifunza jambo kwamba, kuna mambo huwa tunayabeba tangu tukiwa wadogo, na madhara yake hudhihirika baada ya muda mrefu, na mara nyingi hali kama hii huwatokea wale wenye kawaida ya kuficha changamoto wanazopitia; Chester alikuwa mmojawapo, na hii si kwa watoto tu, hata ukiwa mtu mzima ni vyema kushea changamoto kama hizo kwa wataalamu, au kwa mtu wako wa karibu unaemwamini.

Jamaa hakuficha kwamba, akiwa mdogo, aliwahi kuwa na urafiki na jamaa aliyekuwa kamzidi kiumri, ila alikuwa na kawaida ya kumfanyia vitendo vya kikatili, ikiwemo ulawiti, wakati mwingine akilazimishwa kufanya mambo ambayo alikuwa hataki kufanya; alianza kukumbana na huo uovu akiwa na umri wa miaka saba.

Ni uovu ambao hakuwahi kuufichua, aliubeba kwa takriban miaka sita. Huku akiendelea kupitia hizo changamoto, wazazi wake walitalakiana, wakati huo akiwa na miaka 11, ila aliendelea kuishi na baba yake, ambaye naye kutokana na mazingira ya kazi yake, hakuwa anatumia muda mwingi kuwa naye; pia hakuwahi kuficha hisia zake kwamba wakati huo alihisi kutengwa na kutelekezwa na wazazi wake, na bado vile vitendo vya yule mshenzi viliendelea kumuandama from time to time.

Akiwa na miaka 13, alipata nafuu ya kuepuka uovu wa yule jamaa (sidhani kama aliwahi kumtaja; sio kwa vyanzo nilivyopitia), ila madhara ya kisaikolojia aliyoyapata yalimsumbua sana, kwa kumdhoofisha kiasi cha kufanya aishi kwa kutokujiamini, na kujiona hafai, hali iliyopelekea aanze kujihusisha na matumizi ya madawa ya kulevya, ili kuepukana na hizo changamoto; kama ilivyo kwa kila mwanzo wa uraibu, ni mara chache mtu huanza na matumizi na madawa yenye madhara makubwa, kwa mfano, ni kawaida mtu kuanza na uvutaji wa sigara, kisha kuendelea na bangi na kuishia kwenye unga; unaweza ukaitazama hii kwa jicho tofauti, ila elewa nilichomaanisha.  Chester aliishia kwenye uraibu wa cocaine na methamphetamines, achilia mbali mitungi.

Akiwa mtu mzima, aliwahi kusema kwamba, kumbukumbu za vile vitendo vichafu zilikuwa kama zimefutika, ila siku moja alienda kumtembelea mama yake, na alipofika nyumbani kwake aliona picha iliyokuwa ukutani aliyopigwa kipindi akiwa mdogo, tena nyakati zile vile vitendo vikiwa vimeshamiri, kitendo cha kuiona ile picha kilipelekea kurudi kwa kumbukumbu za ule uovu, ila kitendo cha kuendelea kukaa kimya mpaka akawa mtu mzima vile kiliendelea kumuumiza, na ndivyo uraibu ulivyoendelea kukithiri, na hakusita kuongeza kuwa, ishu ya yeye kuchezewa vile ndiyo ilimfanya awe mteja, na mtu mwenye huzuni kupitiliza.

Matumizi ya madawa ya kulevya yaliendelea hata alipoanza harakati zake za muziki na kundi lake, na hakuwahi kuficha namna alivyokuwa anatumia kiasi kikubwa cha madawa kiasi kwamba hadi akawa anatumia madawa mengine, mfano opium ili kupunguza stimu za madawa mengine (cocaine na methamphetamines).

Jamaa hakuwahi kuponea uraibu uliomuandama mpaka siku anaondoka duniani; mbaya zaidi changamoto ziliongezeka alipompoteza aliyewahi kuwa rafiki yake, ambaye nae alikuwa anafanya muziki kama wake, na kibaya zaidi, nae aliaga dunia kwa staili kama yake; jamaa aliitwa Chris Cornell, alifariki miezi michache kabla ya Chester (Chester alifariki Julai, Chris alifariki Mei). Bennington alikua akimsikiliza Cornell tangu akiwa mdogo hadi akawa shabiki wake mkubwa, mpaka akaanza harakati zake, na kubahatika kufanya naye kazi na kuwa marafiki, achilia mbali kuwa wasanii wazuri. Kifo cha Chester kiliacha maswali mengi, kwa sababu tarehe aliyoondoa uhai wake ilitakiwa iwe ni siku ya kuzaliwa kwa Chris, ila yote kwa yote ilithibitika kilichopelekea kifo chake zilikuwa ni changamoto za afya ya akili.

Wote walifariki kwa kujinyonga.

“Heavy.”

Sikumbuki ni lini hasa nilianza kusikia neno ‘JIKUBALI’, ila ni kitambo sana, na sio tofauti na maneno mengine mengi tunayojifunza bila kujua, kama vile tunavyojifunza kuongea na/au kuzungumza kabila au lugha zetu za kwanza. Mtu akisema anajikubali anachomaanisha kwanza, kinaanza na anavyojichukulia, na huko kujikuchukulia kwenyewe kunahusisha mambo mengi ikiwemo kujiamini, ila tusisahau kujiamini kwa mtu husika haina maana sawa kwa kila mtu, ndio maana usishangae kuona mtu mwenye kiburi, na dharau za wazi ila naye anakuthibitishia kujikubali kwa jinsi alivyo (ndicho nilichomaanisha namna tunavyojichukulia/tunavyojiona [Self-image/self-concept]).

Ningependa nikusihi tuliangalie hili in a positive way, kwa mfano ibaki tu kwamba anayejikubali ni yule anayejiamini, asiyejikweza, anayeishi kulingana na mazingira, asiyekwazika kirahisi, anayejipenda na kujithamini, mkweli, muwazi, na mwenye sifa nyingine kama hizo, ikiwemo anayetambua umuhimu wa afya ya akili; mpaka hapo we mwenzangu sijui vipi! Unajikubali ama? Naamini mpaka sasa una uwezo wa kuelewa mtu asiyejikubali ana sifa zipi, ila kama bado unapata utata, basi elewa tu kwamba, mtu asiyejikubali ni moja ya wale wasiojua wala kuelewa umuhimu wa afya ya akili. Kibongobongo ukisema, ‘fulani hajipendi’ ni sawa na kusema ‘fulani hajikubali’, kuna wenzetu wanaelewa hii ishu kama self-hatred au self-loathing, sio kitu poa kabisa.

Wakati Linkin’ Park wanaanza kuandika “Heavy.” Chester aliweka wazi hali yake halisi; hakuwa sawa kisaikolojia. Hivi ushawahi kunywa vikombe, say baharini, ziwani au mtoni? Kwa wale wasiojua kuogelea, na wamepitia hiyo ishu wanajua balaa lake, ndicho alichomaanisha; “...too much stuff is just happening to me. I just feel underwater…” nimemnukuu kwa mujibu wa kauli ya Shinoda, walikuwa wakifanya kazi pamoja, na hiyo ilikuwa ni sehemu ya mahojiano yake na moja ya waandishi wa habari.

“I don't like my mind right now.” ni mstari anaoanza nao, na ni dalili ya kutokujikubali. Self-hatred huchangiwa na mambo mengi, ila mojawapo ni trauma. Vitendo alivyokuwa anafanyiwa akiwa mdogo ni mfano mmojawapo, mingine ni kama kushuhudia mwenzio anafanyiwa ukatili usiomithilika, au we mwenyewe ukipitia changamoto na ikakuacha na kilema cha kudumu, na mifano ya mengine kama hiyo, matokeo yake ni mtu kujiona hafai (low self-esteem), na hisia za namna hiyo sio nzuri, na ili kuzipotezea ndio tunaanza kutafuta namna za kujisahaulisha maumivu, mwisho wake ni madhara mengine zaidi.

Sehemu nyingine anasema, “I wanna let go, but there is comfort in the panic.”

Moja ya namna ya kupotezea fikra za kutokujikubali ni utumiaji wa vilevi, hili linajulikana na nishalionyesha, ila mara nyingi mtu asipoponea mapema, matokeo yake ni uraibu; mwana naye ilikuwa the same, ukiwa na sonona, na ukawa mtumiaji wa hizo mambo, wakati unavesha unafarijika sana, ila stimu zikikata mzunguko unakuwa uleule. Alichokuwa anaimba ndicho alichokuwa anapitia, na ndiyo ilikuwa staili yake (kuimba mapito yake binafsi).

Pia anaimba, “And I drive myself crazy, thinking everything is about me.”

Sehemu ya pili ya huo mstari inaakisi madhara mengine ya self-hatred. Mtu mwenye changamoto za namna hiyo, kwa mfano, anakuwa anahisi kufuatiliwa na kila mtu (paranoia), kutomuamini mtu; kila kinachofanyika kama hakiko sawa, anahisi kimefanyika kwa ajili yake, anahisi kutetwa sana kutokana na jinsi alivyo, hata akikutanisha macho na mtu kwa bahati tu, anahisi yeye ndio alikuwa anakodolewa, yani haachi kujishtukia, na mara nyingi inakuwa ni kutokana na jambo linalomsumbua, mfano uraibu. Asilimia kubwa ya mateja wako hivyo. Msisitizo ni, suala huwa sio uraibu pekee.

Kazi nyingine inayowahusu Linkin Park, na bado muimbaji akiwa Chester (actually, jamaa ndiye alikuwa lead vocalist), inajulikana kama “Crawling.” na kimsingi inahusu madhara ya madawa ya kulevya, hasa aliyokuwa anayapata kutokana na matumizi ya Meths, ila mwisho wa siku ni kazi inayomhusu kila anayepitia changamoto za uraibu wa madawa ya kulevya, kama alizokuwa anapitia.

Bottom line

Ni muhimu sana kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kimaisha bila wasiwasi, huku tukiimarisha mahusiano yetu na kila mtu, kwa namna isiyoathiri maisha yetu ya kila siku; kama ni mfanyakazi au mfanyabiashara, basi kazi au biashara husika zifanyike kwa ufanisi, hii ni kwa kila mtu. Najua sio rahisi kama inavyosomeka, ila uwezekano upo, na ndio maana kumekuwa na vyanzo, pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha suala la afya ya akili linazingatiwa, ili harakati zetu ziwe za mafanikio.

Kitu kimoja ambacho binafsi nilichelewa kugundua ni mtazamo chanya kuhusu maisha, bila kujali hali halisi nayopitia. Miaka kadhaa nyuma niliwahi kuugua kifua kikuu, nikapona baada ya mwaka halafu ugonjwa ukanirudia tena, nikasota kwa takriban miezi 8 [soma zaidi hapa]. Kwa takriban miezi 6 nilikuwa nikihangaika kwenda huku na kule, kwenye hospitali mbalimbali, ili kujua tatizo ni nini bila mafanikio, ni moja ya vipindi nilivyowahi kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu maisha, kiasi kwamba siku tatizo lilipogundulika nilipata ahueni hata kabla ya kuanza matibabu rasmi, na hata nilipoanza matibabu nilihamasika kufanya kila nilichopenda kufanya, kiasi kwamba ukawa ndio wakati pekee niliofanikiwa kutoa mradi wangu wa nyimbo 10, jambo ambalo sikuwahi kulifanya nlipokuwa mzima, na ndio wakati niliowahi kutunga wimbo naoupenda mpaka leo. Pia ulikuwa ni wakati nilioanza kuandika kitabu (riwaya) ambacho nimeshakikamilisha, yote kwa sababu niliamua kuwa na mtazamo chanya wa maisha.

Ukweli ni kwamba mpaka leo maisha huwa nayatazama positively hata nikwazike vipi. Kuwa na mtazamo wa maisha wa namna hiyo ni msingi wa kukabiliana na changamoto, na huo ndio mwanzo wa kulinda afya ya akili. Bado sio rahisi, hata mimi from time to time mpaka leo, huwa najikuta nakuwa stressed, ila mwisho wa siku nikifikiria uhai, na uzima nilionao, sometimes kwa kukutana na wenzetu wengine wenye changamoto za wazi, na bado wanamudu kuonesha tabasamu, na kuwa na amani isiyo na chembe ya unafiki, huwa najikuta nahamasika kupiga moyo konde, kunyanyuka na kuendelea kusonga, haijalishi kwa mwendo gani, uwe wa farasi au kinyonga (s/o kwa Kikosi cha Mizinga).

Unaweza ukajiuliza unawezaje kuwa na mtazamo chanya kwenye haya maisha wakati umefiwa na mpendwa wako (Wapumzike kwa Amani wazazi wangu), huna ajira, ni muathirika, say wa UKIMWI, au saratani, au una ulemavu wa kudumu, au huna mvuto kama wenzako, au mpaka leo huna mtoto, na umri umesogea, unaweza ukawa na mlolongo wa sababu zinazokufanya uchukie maisha kwa kutokujikubali, ila mwisho wa siku BADO UNAISHI. Sekta ya afya inatumia gharama kubwa sana kwenye tafiti za kitabibu, na matibabu kwa ujumla ili kuhakikisha tunaishi, na kuna magonjwa mtu akipita bado matibabu yake ni gharama kubwa kiasi kwamba hadi kuna wenzetu wanaamua kupitisha mabakuli ya michango wapambanie uzima (wasife), imagine that!

Kuna sehemu kwenye moja ya kazi yangu moja niliandika “...kufa ndio kupona.”nilichomaanisha kisanii, sio ujiue ili uponee, ila ni kumshukuru Mungu hata tunapofiwa na wapendwa wetu, badala ya kusononeka ajili ya mtu aliyepumzika (kapona) kwa amani, ilhali we bado unaishi, na ukweli ni kwamba haupendi kufa kama aliyetangulia mbele ya haki. Nadhani kwa huu mfano wa kufiwa na wapendwa wetu (bereavement), inatosha kukupa picha kwa nini inabidi tujitahidi kuwa na mtazamo chanya kwa kila jambo ili ustawi wa afya ya akili uwe na manufaa kwetu.

Unapokuwa na mtazamo chanya, ishu kama kushea masaibu yako kwa unaowaamini, au wataalamu wa masuala ya afya ya akili, huwa ni suala la kawaida. Wakati mwingine unaweza usiwashirikishe changamoto zako, ila kutokana na huo mtazamo ukajikuta tu mwenyewe unatafuta namna za kukabiliana na sononeko, wasiwasi, na mengine kama hayo; uzuri teknolojia imetusogezea taarifa za kutosha kwenye kila jambo, japokuwa pia umakini unahitajika unapozitafuta, kwa sababu sio kila taarifa ya mtandaoni ni sahihi.

Kila namna inayotusaidia kulinda afya ya akili ukiiangalia kwa undani chimbuko lake ni mtazamo chanya wa kimaisha, iwe kuishi kwa matumaini, au vyovyote vile.

Kuna siku nilikuwa na rafiki yangu wa karibu (true story), nilikuwa kwenye lindi la changamoto usipime, na kiukweli kesho yangu haikuwa ni wakati niliouzingatia sana kwa sababu sehemu kubwa ya maisha yangu nimekuwa nikipambana kuwa huru, hasa kiuchumi, na karibu kwenye kila nyanja nyingine muhimu za kimaisha. Mwenyewe anajua nilivyopambana mpaka siku nakutana nae, na mpaka muda huo tayari mwana ana familia, ana kazi, mi sina familia wala kazi, na sielewi, na sijawahi kushea changamoto zangu kwake kwa hisia vile kama siku ile, na umri tumelingana, (inaumiza si ndio? Najua hii haimuumizi kila mtu, ila binafsi ilikuwa inaniumiza, tena sio kidogo); kwa kuongezea tu, chanzo kingine kinachofanya mtu asijikubali ni kujilinganisha na wengine, hasa unapojilinganisha na mtu/watu waliokuzidi kimafanikio, haifai kwa afya ya akili.

Kufupisha stori, baada ya kumweleza changamoto zangu, ambazo nyingi hazikuwa ngeni kwake, hakusita kunitia moyo, na zaidi alisema, “shukuru kwa kila jambo Shilinde.” kisha akanivuta pembeni kwa sababu tulipokuwa tumechill, hapakuwa private sana. Kilichofuata alinielezea changamoto yake moja tu ambayo hakuwahi kuniambia kwa muda mrefu tangu aipate, na ni changamoto ambayo binafsi naiogopa vibaya mno, kiasi kwamba nikikumbana nayo, pamoja na ninavyojitahidi kukabiliana na changamoto za sasa, bado itaniyumbisha; nilijiona sina matatizo, and yet mwana alikuwa ananichana huku akitabasamu, na mara nyingi hua haachi kutabasamu na kufurahia kila anapopata wasaa wa kujiachia.

Mtazamo wangu ulibadilika ghafla mithili ya siku niliyoambiwa nina maambukizi ya kifua kikuu. Sikuwahi kufikiria kuacha sigara wakati huo (ulikuwa unaenda mwaka wa tisa nikiwa mvutaji mzuri tu), japo nilikuwa natamani kuacha, hadi niliwahi kutumia dawa za mitishamba za Kimasai lakini wapi, ila siku nilipogundulika nina huo ugonjwa, niliacha na sikuwahi kuwa na cravings mpaka leo, ndivyo mwana nae alibadilisha mtazamo wangu kimaisha, mtazamo ulionirudishia matumaini niliyonayo mpaka leo.

Sababu, na namna za kuzingatia afya ya akili ni nyingi, ila kimsingi huanza na mtazamo chanya wa kimaisha, tujitahidi sana eneo hilo, kwa sababu kiuhalisia changamoto hatarishi kwa afya ya akili zinaongezeka kila uchwao, taarifa za watu kufanya vitendo vinavyoashiria athari katika afya ya akili ni nyingi. Hali siyo nzuri.

USIKAE KIMYA, KAMA HUWEZI KUVUMILIA.

Shilinde.