Uchambuzi wa EP: Spit EP
Msanii: Producer High Smoke
Tarehe iliyotoka: 24.05.2021
Nyimbo: 5
Wasanii Waliohusika: Kaa La Moto, Dazzle, Mama C, Chaca, Jcb(Watengwa), D Wa Maujanja, Ibra Da Hustla, Boox, Alex, G-Love
Muunda Midundo/Mtayarishaji/Mchanganya Sauti Na Midundo: High Smoke
Studio: Kichacani, Northblock Records
Japokua sikuwahi kumskia producer High Smoke hapo awali, kazi yake ilisogezwa na wana na kusema kweli niliipenda sana. Mradi wake ambao ulinitambulisha kuhusu producer huyu ulitoka katikati ya mwaka huu na ulijulikana kama Spit EP.
High Smoke kwenye mradi huu amewashirikisha ma emcee tofauti toka maeneo tofauti kama vile Kaa La Moto(Mombasa, Kenya) Chaca na JCB, D Maujanja, Ibra da Hustla(Tanzania) na wengine wengi. Pia High Smoke amemshirikisha Mama C ambaye ana support mradi kwa njia ya uimbaji wake akitumia lafudhi yake ya wa America.
Neno Spit kwa tafsiri ya moja kwa moja kwa lugha yetu ya Kiswahili linamaanisha “tema”. Na kusema kweli kwenye mradi huu watu wanatema bars na si kitoto.
Mradi unaanza na wimbo Kwa Nini ambao unapiga mdundo mzuka sana unaowawezesha ma emcee Kaa La Moto, Chaca, JCB pamoja na D Maujanja kuchana freshi wakati Mama C akiwapiga company kwenye kiitikio.
Kwenye wimbo wa pili Me N You ambao ni wimbo wa mahusiano kati ya wawili wanaopendana High Smoke anafanya kazi na Ibra Da Hustla, G Love, Alex na Boox.
Mama C na Kaa La Moto wanashirikishwa tena kwenye wimbo maridadi sana Spiritual Warrior. Wimbo huu unapiga vizuri sana ki mdundo na bass gita lake noma sana kwenye woofer yako pamoja na vinanda vizuri na flute au filimbi nzuri sana ikiskika taratibu juu ya ngoma. Wimbo umejaa ma punchlines kibao wakati mama akibariki ngoma kwa uimbaji flani wa kiroho wa kiafrika.
“Hii ni ngumu babu unaweza tobolea sikio/
Nahisi freshi hata ikibuma au isipofika kwa radio/
Tushaona ma star walo jengwa na uwezo sio/
Siku hizi sio talanta unaweza tu uka trend tu kwa kalio/
Matokeo talanta inakatwa unaishiwa bundle/
Wanaona sio mbaya kutafta kiki kuanzisha scandal/
Kando kando zitaskika story za uwongo na ukweli/
Wameshafeli kwa kuwa alingoja kubebwa na ferry/”
Ibra Da Hustla anashiriki vizuri kwenye Vibe na anaonesha kuwa bado yupo vizuri kimashairi na uchanaji pia.
Wimbo ambao ulinikosha sana kwenye EP hii ni Maasai ambapo kachana Dazzle. Emcee huyu anaenzi mila na tamaduni zetu za kiafrika kwa kuchana kuhusu tamaduni za wa Maasai. Mdundo baraka sana pamoja na uchanaji akisema emcee Dazzle,
“Pita Ngorongoro uone maisha yetu/
Twende Simanjiro Mata nyumba zetu/
Arusha yetu na mashuka nguo zetu/
Molel mpaka Lizer nkoo zetu/”
Bonge moja la mradi toka kwa High Smoke na ma emcee wamejitahidi kumpa producer High Smoke mashairi na uchanaji unaoendana na midundo waliyopewa.Spit EP ndio mpango mzima.