Uchambuzi Wa Mixtape: Mambo Bado
Emcee: Igee Afrikka
Tarehe iliyotoka: 02.04.2021
Nyimbo: 14
Mtayarishaji: Risco Black
Mixing & Mastering: Igee Afrika
Studio: Malik Music

Nyimbo Nilizozipenda: Igee In The House, Roga Na Strings 2, Itabidi, Coup d’état, Fireplace

Igee Afrikka

Mapema mwaka jana nilipata taarifa kuhusu mradi wa Igee Afrikka uitwao Mambo Bado ambao ni mixtape aliyoiachia sokoni ili kuweza kujitambulisha kwa mashabiki wa muziki na utamaduni wa Hip Hop. Emcee huyu ambaye anatokea kule Kasarani, Nairobi alibatiza mradi wake Mambo Bado kwa sababu mbili; kama njia ya kumuenzi babu yake aliependa kumtia moyo kwa kumwambia “Mambo Bado” na pia kuwajulisha mashabiki zake kuwa pilika ndio bado zinaanza hivyo wakae mkao wa kula.

Mixtape hii ambayo aliisimamia yeye mwenyewe akisaidiwa na Risco Black imetumia midundo ya wasanii tofauti na hili ni sawa ukiangalia ni mradi ambao sio rasmi. Kazi inaanza na Intro ambayo inatupeleka hadi Igee In The House ambao unatumia mdundo wa Kriss Kross Jump.

Baada ya hapa emcee huyu ana anaamua kuFanya kwenye mdundo mzuka kabla ya kukwambia Nimekam kwenye mdundo flani wa kucheza na anajikuta anarudia mdundo huu tena kwenye Nimekam Remix.

Mradi huu ambao emcee huyu ameingia booth mwenyewe bila usaidizi wa emcee yoyote yule una mashairi mepesi kiaina sawia na mada zinazogusiwa huko. Mradi japokua umejaa punchlines na double entendre kibao naona kinachokosekana ni mtiririko wa mawazo kwenye mashairi yake.

Ila kando na hayo kijana anajikakamua kwenye mradi huu pia kutupatia mistari yenye ucheshi na pia ni fursa ya wana Hip Hop kutoka East Africa ambao wanapenda kujifunza lugha ya sheng kuskia misamiati mipya toka lugha hii.

Roga Na Strings 2 ni muendelezo wa Roga Na Strings 1 ambapo emcee huyu anachana juu ya ala za gita peke yake ila changamoto naona ni zile zile za kutokuwa na mada maalum kwenye ngoma.

Igee Afrikka kaachia mradi wake wa kwanza sokoni na ni hatua toka kwa kwake ila  naona kuwa Malik akizidi kujinoa zaidi  naamini atatuletea kazi nzuri mbeleni kwani Mambo Bado.

Mfuate Igee Afrikka kwenye mitandao ya kijamii;

Facebook: Igee Afrika
Instagram:
igee_afrika
Twitter:
@AfrikaIgee