Rap Poetic Grenades ni kundi la wachanaji ambalo chimbuko lake ni Arusha. Crew hii imeundwa Na vichwa vitatu.
Leo tumepata fursa ya kuongea na theluthi moja ya kundi hili, ambaye ni J Yank ili tuweze kupiga naye story na kuweza kumfahamu yeye, kundi lake na harakati zao.
J Yank ni a down to earth brother ambaye ni rahisi kuongea na kushauriana naye hivyo basi gumzo letu lilikuwa freshi na niliweza kujifunza mengi toka kwake.
Karibu ufahamu na ujifunze toka kwa huyu kijana toka A-town.
Karibu kwenye kipindi cha handakini, kabla ya yote naomba ututajie majina yako halisi
Asante sana. Kwa majina yangu halisi mimi ninaitwa Joseph Pantaleo Msechu.
Je ulianza lini kujihusisha na hip hop na kwanini ikawa hip hop na sio rnb wala haina nyingine ya mziki?
Nilianza kitambo kidogo kwenye Mwaka 2007 na 2008 hivi, ndo nilianza kujihusisha na harakati hizi za Hip Hop na nilipenda kujihusisha na utamaduni kutoka na kuchimba na kugundua huu utamaduni unamuhusu mtu mweusi na kwa ujumla unahusu maisha yetu halisi haswa.
Ni emcee gani walikuvutia kwa nyumbani na nje ya nyumbani mpaka ukapenda na wewe kufanya unachokifanya kwa sasa?
Emcee wa nyumbani aliyenivutia sana kwa kipindi cha nyuma hapa Tanzania alikua ni Professor Jay kwa wakati huo miaka ya nyuma sana pia kuna marehemu Complex, Faza Nelly, Kwanza Unit na wengine wa jamii hii ya Hip Hop kwa kipindi hicho haswa Miaka ya 90’s kuja 20’s. Msanii wa Nje ya Nchi kipindi hicho alikua ni Nas, Eazy E, Tupac, Notorious B.I.G. na kundi la Lost Boyz sana.
Emcee ni kioo cha jamii, je taswira ya mziki wako ni ipi kwa jamii inayokutazama?
Taswira ya mziki wangu ni kulenga haswa maudhui yenye maadili mema na kuleta Uchanya tu na kufundisha pia ili kuepusha ile dhana ya watu wanavyosema kuwa aina hii ya muziki ni wa kihuni na haufai katika jamii.
Kupitia jibu hili, kipindi au zama tulizopo emcee wengi sana track zao ni battle, una maoni gani kuhusu hili ikiwa jamii bado inahitaji elimu ya ukombozi wa fikra?
Hapa inatakiwa emcees wabadilike kidogo maana nyimbo nyingi siku hizi ndo kama unavyosema ni battle tu ambapo hii inashawishi jamii kuamini kuwa muziki wetu ni wakihuni au wavuta bangi au kuonekana inahamasisha ugomvi ndo maana unakuta ni ngumu sana miziki ya Hip Hop mingi kwa sasa ni ngumu kusikika hata redioni mara kwa mara au watu wakisikiliza. Tubadilike (Tutoe Elimu na Burudani).
Quality Brothers Crew yenu bado ipo?
Crew yetu ipo kama kawaida, ila kwa sasa hatujiiti Quality Brothers kama ilivyozoeleka hapo zamani.
Embu tuzungumzie kidogo na kwa kirefu kuhusu Quality Brother's na mipango yake ya mwaka huu na jina lenu jipya. Kwanini mmelibadilisha kutoka quality Brother's kuwa lililo sasa?
Kwa sasa hatuitwi wala hatutumii Jina la QB au Quality Brothers kama ilivyozoeleka. Kwa sasa tunatambulika kama RPG ambapo kirefu chake ni Rap Poetic Grenades na mipango yetu kwa mwaka huu baada ya kutoa Album ya ‘Grenades From North’ iliyotoka mwaka jana kwa sasa tuko jikoni tukiandaa album ya member mwenzetu ambaye ni Slai ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika na itawajia hivi karibuni ambayo inafanyikia palepale Studio za NorthBlock Records chini ya producer Luis.
Kwa nini mlijibatiza hivi?
Tuliamua kujibatiza hivi kutokana na Jina letu la QB (Quality Brothers) kuibiwa hivyo tukaona haina haja ya kuamua kuendelea kubishana na kugombania jina ndo uamuzi ukawa wa kubadili na tukapata jina jingine hili ndo tukaamua kujiita RPG (Rap Poetic Grenades).
Je ni watu gani wametumia jina lenu la QB? Kwani jina lenu halikusajiliwa mpaka hao wengine wakaiba na kulimiliki wao? Na je kama hamkusajili wakatokea watu wengine wakaiba na jina jipya la RPG mtafanyaje? Au ndio mtakuwa mnafanya kazi ya kubadilisha majina kila mnapoibiwa si itakuwa mnawapa usumbufu mashabiki wenu?
Jina la QB halikua limesajiliwa kwa kipindi chote hicho japo tumelipigania na mpaka asilimia kubwa ya watu walilielewa na mpaka na leo wapo watu wananiita QB tu.
Jamaa walioliiba hili jina sijajua haswa walichipukia wapi ila ilitokea ghafla tu tulianza kuona mitandaoni kuna jamaa anajiita Geofrey QB, na mwenzake anajiita Imma QB na katika kuchunguza tukaja kujua kuwa wale ni wasanii wa producer wa kujiita Dupy Beats, nadhani watu wengi wanamjua au wameshamsikia.
Na baada ya kuiba jina na kuanza kujitangaza ilitokea zogo kiasi flani katika mitandao ya kijamii kuhusiana na hilo jina, ila ikafikia mahali sisi tukaamua kukaa chini na kushauriana kuhusiana na hili maana wale jamaa nao ilifikia mahali wanasema tunatafuta kiki.
Hapo ndipo niliposhauriana na kuwashirikisha baadhi ya Ndugu zangu katika Utamaduni akiwemo Adam Shule Kongwe na Benny Ole Ngenyiki na kaka mkubwa LC (Lucas Malali) katika swala la kushiriki kubadili jina ndipo lilipotokea jina hilo la RPG sasa na ndo linalotumika na pia jina RPG lipo katika zoezi la kusajiliwa sasa hivi hivyo hapatatokea swala la wizi wa jina tena. Taratibu za usajili zinaendelea.
Memba mwenzako Joe Mic naona anadili sana na poetic kuliko michano, na wewe kuna kipindi ulikuwa unadili na kutengeneza midundo, RPG lengo kubwa la kundi ni nini katika jamii yetu ya kitanzania?
Hapana, iko namna hii Joe Mic ndo anadili sana na midundo japo katika uandishi pia bado anahusika na mimi pamoja na Slai tunahusika katika uandishi kwa asilimia kubwa kuliko midundo. Japokua mimi binafsi nnauwezo kiasi wa kufanya kitu pia katika midundo hivyo nashirikiana na Joe Mic pia katika hili.
Mziki unaoufanya una faida kwa jamii yako inayokuzunguka au wanapata faida gani kupitia RPG?
Muziki nnaoufanya una faida kwa jamii kwa sababu nyimbo nyingi ambazo tumefanya na kuzitoa karibia asilimia 90 huwa ni za ujumbe sana. Hivyo jamii huwa inaelimika kupitia huu muziki tunaofanya.
J Yank wewe ni emcee pia vile vile ni producer, katikati ya hapo wapi unapopendelea zaidi?
Mimi ninapendelea kubaki kama Emcee kwa kiasi kikubwa kwa sababu ndo kitu ambacho nnamini nnakiweza kwa asilimia kubwa zaidi.
RPG ni kundi la memba wangapi mpaka sasa?
RPG ni kundi lenye watu watatu tu ndani yake
Ambao ni:
1. Slaiyank
2. J Yank (Mimi)
3. Joe Mic
Joe Mic - J Yank - SlaiYank
Tutegemee album lini na mtawapa collabo ma emcee gani katika album yenu?
Baada ya Album ya Grenades From North iliotoka mwaka jana ambapo iliwashirikisha watu kibao wakali ndani yake kama Nash Mc, Wise Man, Adam Shule Kongwe, Fred Lou na Neno Wa Kwanza, Album inayofuata kwa sasa ni album ya emcee mmoja pekee kutoka katika kundi letu ambaye ni Slaiyank kisha baada ya hapo tutakaa chini na kuafikiana tena kuhusu tufanye kipi kati ya album au mixtape ya kundi tena.
Tueleze kidogo kuhusu albam yenu ya mwisho mlioitoa Grenades From North? Nini maudhui ya albam hii? Je mashabiki waliipokea vipi kazi hii?
Maudhui ya album ya Grenades From North yalilenga sana sana kwenye kuwasilisha ujumbe wenye kutia hamasa na nguvu zaidi katika nyanja mbalimbali haswa kwa jamii zinazolenga mafanikio na kupambana katika hali moja ama nyingine katika maisha kujikwamua kiuchumi na kiutamaduni na kupinga baadhi ya mambo ambayo si sahihi yanayozikabili jamii hizo hivyo ililenga kumkwamua mtu kifikra vilevile…
Na kwa ujumla jamii inayoamini katika utamaduni iliipokea vizuri album hii kulingana na hadhi yake na maudhui kwa ujumla.
Unazungumziaje ufanyaji kazi wenu chini ya North Block Records chini ya producer Louis? Je mpo chini ya management ya North Block Records?
Ufanyaji wetu wa kazi ndani ya studio za NorthBlock chini ya Producer DR. LOUIS ni mzuri sana na haijawahi kutokea kuleteana shida au utata kati yetu maana kwanza tunaheshimiana sana na pia tumekutana sote tunapenda hiki tunachofanya hivyo hakuna tatizo kabisa katika hili.
Kuhusu swala la kuwa chini ya Management ya NorthBlock Records ni hapana hatuko katika Management hiyo bali tunafanya kazi kwa makubaliano na maafikiano ya pande zote mbili kwa pamoja.
Ma producer waliohusika katika mradi wenu mpya ni akina nani? Unazungumziaje mkono wa Louis kwa production?
Ma producer waliohusika katika mradi mpya ni Dr. Louis mwenyewe akishirikiana na High Smoke pamoja na Dels Beats basi… Nikizungumzia mkono wa Louis kwa upande wa production kwa kweli huyu brother ni producer mkali sana wa beats za HipHop na kazi za HipHop kwa ujumla kuwahi kutokea hapa jijini Arusha.
Unauzungumzia vipi mziki wa handaki kwa hapa Bongo, kuanzia mafanikio na changamoto zake, na kama kutakuwa na changamoto tunaomba mapendekezo ya nini kifanyike?
Kwa kweli muziki wetu wa handaki hapa bongo kwa sasa kiasi flani watu wanaendelea kuelewa elewa japo mashiko hayajawa makubwa kiviile na ni kutokana na inabaki jamii chache ya watu wanabaki kuaminishana ujinga. Na maoni yangu katika hili ni tuzidi kukaza tu, maana nnamini mafanikio yapo katika kujituma kwa bidii.
Changamoto zipo kwa upande wa kurekodi na pia katika utoaji wa kazi za wasanii na kuzisambaza pia (hapa support ya ununuzi wa tapes ni ndogo mnoo) hii inapelekea wana kibao kukosa kipato hata kidogo tu cha kujikimu, tunaishia kuchukuliana poa tuu alafu tunasema tunakaza… Pia kuna wimbi kubwa sana limeibuka la baadhi ya mashabiki wa huu Muziki na wao kutokea na kujifanya ni Emcee na wanafanya muziki pia hivyo hii ni changamoto na ni uzibe kwa wale Real Emceez katika kazi zao.
Katika kurekodi changamoto kubwa ni katika swala la production. Mixing ya ngoma zetu nyingi sana kutoka handaki ni mbovu hapa inabidi watu wakae watulie wafanye kazi serious sio mzaha au kuchukulia poa (kwakuwa ni Hip Hop).
Kati ya "HIP HOP BASE" na "FID STYLE" Ni kipindi kipi ungependa kirudi hewani, na kwa sababu gani?
Hip Hop Base ndicho kipindi nilichowahi kukipenda sana kuliko vipindi vyote vya hapa bongo vinavyohusisha harakati za Hip Hop na ningependa sana kirudi maana kilikuwa kimebeba uhalisia sana na kilikuwa na mizuka mingi kwa mambo mengi na pia kilikuwa ni cha muda mfupi na kikatoweka ghafla mpaka leo hii.
Je shabiki/mfuasi wa utamaduni wa Hip Hop akitaka kazi zako au za kundi anaweza kuzipata kwa njia gani?
Mtu anaweza kupata kazi zetu kwa njia ya CD kwa zile zilizokuwa tayari kimauzo na kwa zile zilizoachiwa bure kama mitandaoni atazipata kwa njia hata ya WhatsApp au Email anicheki tu nitamtumia bila wasi wasi.
Kwa kumalizia unawaambia nini baadhi ya emcee na mashabiki wengine wa utamaduni wa Hip Hop kuhusu ubishani uliopo wa kusema flani ni Hip Hop flani sio Hip Hop?
Huuni ujinga kubishania kitu ambacho hukijui kutokana na mtu unayembishania. Na huwezi kulazimisha kumuaminisha mtu pia kwasababu kuna baadhi ya watu walishaaminisha watu kuwa wanafanya Hip Hop na jamii ikaelewa lakini mwisho wa siku wamekuja kuzingua na kuongopa na kufanya aina nyingine za kazi ambazo hazihusiani na HipHop Halisi.
Hivyo basi wakati mwingine mimi huwa nnaona kila mtu abaki na kile anachoamini na mwisho wa siku ukweli utabaki daima kwamba ni nani na ni yupi na anafanya nini ili heshima ibaki milele.
Shukrani kaka kwa mda wako pamoja sana, natumai tutajuzana zaidi juu ya kazi zako na za kundi pindi inapotakiwa kujuzana. Pia watajie majina ya account zako katika mitandao ya kijamii kwa wale ambao watapenda kufatilia kila unachofanya katika mziki wako?
Asante… Nimeshaweka Tracks zetu kadhaa tulizoziachia ambazo zinapatikana katika Album Yetu ya Grenades From North ili kwa ambao hawajawahi kuzipata waweze kuzipata na kuzisikiliza pia.
Mimi katika Mitandao ya Kijamii natumia majina haya
Facebook: J Yank RPG
Twitter: J_Yank_Rpg
Instagram: J_Yank_Rpg
Iko hivyo.
Asante sana kwa mda wako