Msanii: Javan
Album: Kifamilia Zaidi
Tarehe iliyotoka: 26.12.2020
Nyimbo: 15
Beats: Joe Mic, Bin Laden, Miracle (Noma), Abby Bangladesh, Qwitch
Studio: Killers Records
Toka kwenye kundi la Dom Down Click (D.D.C) kuna ma emcee waliowahi tangulia kutoa album, EP na mixtape zao binafsi hapo nyuma wakiwemo Andre K (RIP), Adam Shule Kongwe na Miracle Noma. Mwaka Jana (2020) Javan pia aliamua kuachia rasmi albamu yake ya kwanza iitwayo Kifamilia Zaidi. Jina lake rasmi ni Said Mashaka Javan ila kwa uchanaji wake pia anaitwa Chuna Ngozi.
Kabla ya mradi huu Javan alikua ameshikiri miradi ya pamoja na kundi la D.D.C na pia akiwa pamoja na Adam Shule Kongwe waliwahi kuachia album ijulikanayo kama Chini Kabisa.
Javan ambaye alizaliwa miaka ya tisini kule Dodoma Tanzania ni mtu mwenye vipaji vingi; ni mchoraji mbali na kuwa mchanaji. Kwenye album yake ya Kifamilia Zaidi Javan anatuchorea picha halisi na kuchana kuhusu maisha yetu ya kila siku kwenye familia zetu.
Album hii ya Kifamilia Zaidi iliundwa Dodoma kwenye studio za Killers Records. Ni album ambayo Javan amewakaribisha wenzake ili wakae kifamilia na kuuskiliza mradi huu pamoja ili kuona vile mambo tofauti tofauti ya kimaisha yanavyotugusa sote kama jamii moja. Hivyo basi kutokana na mwaliko huu mimi pia nilikaa kitako mkekani kuuskiliza mradi huu na sijutii kufanya hivyo kwani mradi wenyewe kama inavyoonesha jaladio (cover) la album linasisitiza heshima, usalama, kujithamini, uwazi, upendo na utayari kwenye maisha yetu ya kila siku.
Album inaanza na utangulizi mzuri na hotuba ya baba wa taifa la Tanzania hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anayefungua mradi huu kwa bashasha akishukuru wana familia kwa fursa nzuri ya kutoa maoni yake kama anavyonuia kufanya Javan akisisitiza Mwalimu kuwa lazma tujue tunatoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi na tufanyeje ili tufikie tunapotaka kwenda.
Album inaanza na wimbo uitwao “Dos and Don'ts” ulioundwa na Joe Mic wa kundi la RPGs. Huu ndio wimbo wangu bora kwenye album hii pamoja na “Jiongeze Ujongee” na “Sintofahamu” na “Kaka Mkubwa”. “Dos and Don’ts” aliomshirikisha tag team yake toka Chini Kabisa, Adam Shule Kongwe unakupa tahadhari kuhusu maamuzi yako ya kila siku kwa vitu unavyofanya. Anasema Javan,
“Chochote unachofanya zidisha ufanisi/
Usikate tamaa eti kisa hufahamiki/
Maadui wakisogea, usisimame/
Ongeza speed ila usishindane/
Usimwamimi snitch usimpe siri kamwe/
Kaa nae mbali, haswa akitaka mshirikiane/
Yupo radhi kukupa tuff ili ukwame/
Dhumuni ki maisha msilingane/
Mfano msela hakupi diko/
Ila anasimamia bill mkanywe/
Anakupa hela ila hakupi dili mfanye”
Kwenye “Kaka Mkubwa” Javan anaongelea changamoto za ujana pale jamii inapokuangalia tofauti kama wewe ni mdogo ki umri kisa huna fedha hivyo basi familia inaweza kukudharau na kukuona hauna maana ila kama anavyosema marehemu Andre K kwenye kiitikio, “kaza mjomba, usije ukaomba ufe!” Bin Laden alikua doria kwenye hili beat na kama kawa alikuwa makini ki utunzi.
Pia kuna nyimbo za mapenzi kama “Lisa”, “Kizungumkuti” na “Hisia huru”. “Ujana Wetu” iliyoundwa na Qwitch ndio single iliyobeba mradi na imesample vizuri “Forever Young” ya Alphaville na ni onyo toka kwa Javan kuwa ujana ni maji ya moto. Pia mada anaendelea nayo kwenye wimbo kama “Panya Road”.
Albamu hii ina mafunzo mengi kwa ajili ya jamii nzima. Ni album inayokupa mtazamo chanya kuhusu changamoto za maisha yetu ya kila siku na kama unapitia magumu yoyote maishani hii ndio album ya kukupa msukumo mzuri wa kufikia mafanikio yako. Javan kwenye hii album amesimama kama Mwalimu Julius na ni mshauri mzuri wa jamii bila kuzingatia umri wake mdogo.
Kupata mradi huu kwa Tshs 10,000.00/Kshs 500.00 mcheki Javan kupitia;
WhatsApp: +255629528090
Facebook: Javan Geuvara
Instagram: Javan Guevara