Jay Moe

Juma Mohamed Mchopanga enzi hizo akijiita Ex-Mayhem, alianza kufahamika katika ramani ya muziki akiwa katika kundi la Sewer Celibacy, kundi lililoundwa na yeye Jay Moe, Mchizi Moxie, Jaffarai na Calvin Kimali.

Mwaka 2000 katika ukumbi wa Mambo Club, kulikuwa na shindano la kusaka vipaji na washindi walikuwa ni "Sewer Celibacy, Solothang, Mack 2 B na Lady Lou, kwa pamoja wakaona sio kesi wao kama wateule wa shindano wakaunda kundi rasmi na wakajiita Wateule.

Baada ya kufanya kazi kadhaa za kundi, Jay Moe akafanya solo projects na kufanikiwa kuachia albamu yake "Ulimwengu Ndio Mama" na baadaye Tena albamu ya "Mawazo"

Jay Moe – Mawazo

Jay Moe ana a.k.a nyingi sana ila kuna hii ya 'Mawazo' a.k.a ambayo ilikuja kubeba albamu yake ya 2 ya kuitwa Mawazo.

Zaidi ya kuwa a.k.a Mawazo ndio ikawa benchmark ya muziki wake kuanzia enzi hizo mpaka leo hii.

Jay Moe alitengeneza falsafa hii na kuanza kuiishi. Ikawa ndio urali kwa kila wimbo wake na hii ilifanya awe msanii wa kuchimba, kuchimbua na kuchambua mada/idea anazoandika kwa kina sana.

Sikiliza Ulimwengu Ndio Mama, Majukumu, Bishoo, Mvua Na Jua, Maisha Ya Boarding, Kama Unataka Demu, Pesa Madafu, Famous, Hili Game nk, kila wimbo upo kwa msingi huo wa "Mawazo".

"Mawazo" ilimfanya JayMo akae mbali na idea nyepesi.

Hata nyimbo alizofanya za kuparty kama vile Kimya kimya, Cheza Kwa Step bado unaona zipo kwa urali ule ule wa “Mawazo".

Jay Moe alianza game akiwa chalii tu, njia ya Mawazo haikuwa rahisi vile ilihitaji aumize sana kichwa kuishi kwa msingi huo lakini alifanikiwa. Leo hii Jay Moe amekuwa mtu wa makamo pamoja na hivyo BADO ngoma zake za kitambo zinamfiti vizuri tu, tena vizuri pengine kuliko hata jana na juzi. Hii ni kwa sababu, nyimbo zake zilikuwa za umri mkubwa kipindi yeye bado ana umri mdogo tu.

Mara kadhaa nimesikia kwenye media akiulizwa "hivi uliwaza nini kuandika wimbo huu?’ hawajui, hawajui kuwa 'Mawazo' ndio msingi na muongozo wa muziki wake. Wangejua wasingemuuliza 'Mawazo' aliwaza nini sababu yeye mwenyewe ndio 'Mawazo'.

Mawazo huibua idea pale ambapo mtu hakudhani kama kuna idea. Hukuwaza kama "Mvua Na Jua, Bishoo nk” zinaweza kuwa idea kali, yeye aliwaza na kuziibua. Hukuwaza kuwa "Nisaidie Kushare, Pesa Madafu" zaweza kuwa idea za kufanyia ngoma, yeye aliwaza na kuziibua. Idea zake ni za namna hiyo, "Twende Kwa Mganga, Maisha Ya Boarding nk.

Pale anaposema anaachia ngoma unawaza "Atakuja na idea gani?” Hata jina la wimbo likitoka utawaza "Humo ndani kazungumza nini?" kwani huchelewi kuwaza kulia alafu yeye akapita kushoto.

STORY TELLER

Kuna waandishi wengi wakali katika mtindo wa simulizi (story telling) alafu kuna Jay Moe, yeye ana aina yake ya uandishi wa ‘nyimbo za simulizi’. Uandishi wake wa Story ni wa kipekee.

Sikiliza “Story 3” tofauti. Mkasa wa Ahmed, Mariam na nani sijui yule aaaahgh! Ni Story ya aina yake!

Achana na “Story 3”. unaikumbuka ‘Ni Mshamba’? Story ya mkasa wenye wahusika wa 3.Usichanganye, ile ya akina Inno ni “Story 3” tofauti na hii “ Ni Mshamba” ni story 1 yenye wahusika wa 3. Jikumbushe ile verse pale mwanzoni anaposema

“Mkasa wenye wahusika watatu, Jaymo, Kidosho/
Na Mr Lover mmoja (yukwapi?) kalamba chocho/
Tumuache kwanza, pili tuache muhtasari wa habari/
Twende kwa Jay Moe na kidosho ambaye ndio shory/”

Umeona hii Simulizi hapo mwanzo inaposhonwa? Umeona tekniki hizo katika simulizi. Ni story ya aina yake.

Sikiliza “Maisha Ya Boarding”, ubeti wa 1 ameanza kama simulizi za wengine akitumia nafsi ya kwanza umoja akijizungumzia yeye kuanzia primary hadi anaenda boarding. Verse ya 2 akagusia nafsi ya kwanza kisha akaanza kukuchanganyia nafsi ili kuuondoa ule u ABC wa simulizi uliozoeleka na akaendelea kusimulia kwa namna nyingine bila kujigusa tena yeye kama alivyoanza. Ni story ya aina yake!

Zake sio zile story tulizozizoea kwamba, flani kazaliwa, akahangaika na maisha kisha akafa! Zake ni story za aina yake.

Sikiliza ‘Long Distance Lovers’, sikiliza ‘Tutaonana Tena’ ile namna anavyowasilimua wale jamaa, jamaa hawataki hata kutembeza kijiti. halafu mwishoni pale anasimulia na simu inaita kumbe ndio shory anayemsimulia kwa wana anapiga simu. Ni story ya aina yake.

Sikiliza ‘Bishoo’ jinsi anavyopita mle ndani na simulizi yake ya ubishoo.

Uandishi wake huu huwa anautumia hata kwenye nyimbo ambazo sio za simulizi kivile, sikiliza Majukumu, Ulimwengu Ndio Mama na ngoma zake nyingine utaona kuna upitaji wa kistoribstori flani hivi, kama hujanielewa vizuri nenda kasikilize “Kama Unataka Demu” kuna tekniki flani mule, ametaja majina ya mabinti katika mtindo wa kastori flani hivi

Amini kwamba, haikuwa kwa bahati mbaya kushirikishwa kwa story ya ‘Ukisikia Paah! Kwani yeye ndio mjuzi wa hizo michoro.

Siku nyingi zimepita ila Jay Moe bado yupo, bado mkali kama jana na juzi. Makali yake hayazeeki ila yamezidi zaidi. Hakika, Jay Moe ni Mkongwe asiyezeeka.