Jedikouga alikuwa mtu wa watu aliyependa kutumia sanaa yake kuinua, kubadili, kuonya na kufunza jamii yake. Kando na kuwa emcee, kaka Martin Mokiwa kama alivyojulikana rasmi pia alikuwa ni mwana sanaa aliyependa mambo ya ubunifu na uchoraji.

Kaka Martin pia alikuwa mwanaharakati aliyependa kutumia sanaa yake kupiga vita dhidi ya madawa ya kulevya. Yeye pamoja na kundi lake la Ngamia Wa Jangwani wakishirikiana na wana MaKaNTa walianzisha kundi lililoitwa P.A.N.D.E (Push Art Not Drugs Exhibitors) ambalo lilihamasisha ma yanki kuzamia ndani ya sanaa badala ya kujihusisha na madawa ya kulevya.

Japokuwa Mokiwa hayupo nasi tena ametuachia vitu kibao ambavyo tunaweza kujifunza ikiwemo haya mahojiano waliyofanya na Don Dee Dion kabla hajatuacha. Cheki gumzo upate elimika pia.

-Kefa N Mkombola

Asante sana Martin Mokiwa(Jedikouga)

Nini kilikusukuma mpaka ukaandika huu wimbo wako wa Sauti?

Sauti-imejazwa mengi ya kuongea nahisi pia bado nina mengi ya kuongea.... kilichonisukuma ni uwasilishaji wa mada husika, "sauti" kuwa na mengi ya kuongea kwa wakati mmoja

Ulitumia muda gani kuanzia kuandika mpaka kuingia studio na kurekodi huu wimbo?

Sauti niliandika toka 2015 nikaunganisha na mashairi ambayo niliona kwangu ni mapya na yanaweza kukaa. Mwaka 2016 ndio nilirekodi hii kazi na kuitoa 2017 kwenye album ya Rbg Afrika moja!

Wimbo umefanyika katika studio gani chini ya producer gani?

Studio ni MaKaNTa records (sauti na mixing) -ilikuwa mwezi wa 12 mwaka 2017, na mtayarishaji anaitwa Aziz Muyombo (Aziz Midundo), jamaa anakaa Dodoma, mwaka 2016.

Hebu tuzungumzie maudhui ya huu wimbo wako wa Sauti; yapo vipi kuna neno kama kermet nimeliona. Kwanza kermet ni nini maana litakuwa neno jipya kwa wale wengi wasiojua kermet ni nini?

Maudhui ya wimbo yamekaa kisiasa, kijamii na upande wa historia pia...!!!

Kemetic/Kemet ni jina la kwanza la nchi ya misri likimaanisha ardhi ya watu weusi kabla haijabadilishwa na Wagiriki ilikuwa inaitwa hivyo…

Je unafikiria hii sauti au niseme huu wimbo wa Sauti jamii itakuwa imekuelewa kile ulichokusudia wakielewe na je kama hawajakielewa utatumia njia gani kuwapa elimu wapate kuelewa kuhusu Sauti?

Naamini jamii imewafikia vizuri kwa wale waliosikiliza ila wanahitaji kwenda kina kwa vitu vingine nilivyowasilisha vinahitaji kuweza kuelekeza nini namaanisha au nilikuwa namaamisha.....

Mfano:"Natazama Faluja kwa taswira ya Abuja"- hapa nilikuwa nimelenga tukio lililotokea Faluja la kuuawa  kwa watu wasiokuwa na hatia kwa mlipuko wa bomu, ndilo pia limetokea Abuja nchini Nigeria mwaka 2011 na kuua watu wasiokuwa na hatia........ ukiangalia hii ni mikakati ambayo imesukwa kwa lengo moja.

Elimu kwa jamii ni kupitia ufafanuzi wa mashairi niliyoandika, kuna mengine yako wazi, mengine nimeweza kuyaficha ili kuifanya hadhira iweze kuwa na kiu na kudadisi fanani kasema kitu gani....

"Imeandikwa mwenye haki ataishi kwa imani"  hapa ni sawa na kusema "kwa maana haki ya mungu imedhihirishwa ndani yake toka imani ata imani, kama ilivyoandikwa mwenye haki ataishi kwa imani"~Warumi 1:17

Huu ni wimbo wa ngapi kutoa na je unaamini huu wimbo utafikia malengo yako uliyokusudia kabla ya kuutoa au utaishia njiani?

Huu ni wimbo wa pili kutoa, ambao nafanya kazi zangu nje ya kundi langu.....

Kwa hatua moja au nyingine naamini utawafikia kwa kuwa huu wimbo uko kwenye album kubwa ya pamoja ya Rbg Afrika Moja

Kitu gani kilifanya mpaka ukaamua kumpa collabo Jadah Makanta?

Jadah MaKaNTa ni moja kati ya wasanii ambao nina wakubali sana kwa kuwa na sauti ya kipekee kwenye uimbaji na pia kutokana na mdundo ulivyowekwa nikasema nahitaji mtu wa kuweza kupiga back up itakayoendana na mdundo vizuri....... heshima kwa Jadah MaKaNTa.

Maudhui gani unapenda kuyatumia katika kuandika nyimbo zako?

Maudhui ninayoyapenda katika uwasilishaji huwa nagusa siasa, historia, na falsafa za dini na maisha.......

Baada ya wimbo huu wa Sauti kutoka, jamii na mashabiki zako wategemee nini kutoka kwako na kundi lenu kiujumla?

Baada ya wimbo wa Sauti kuna single inaitwa Shuhuda itatoka na pia album yangu nategemea kuachia mwezi wa 6 inaitwa Deni. Nafikiri watu wategemee kupata kujifunza mengi....

Kwenye album yako utakuwa umewapa shavu/collabo watu/mc's gani?

Album: Darkmaster, Kiraka Rado, MaKaNTa, Majanta, Abc ujamaa na ndugu zangu toka familia ya Ngamia wa Jangwani

Jedikouga mpaka ulipofikia ni kitu gani kinakukwaza katika mziki au tungo za emcees wengine?

Kitu kinachonikwaza ni wengi wa emcee kuwa na uwanja mpana wa majigambo kuliko uwasilishaji wenye maana… ni hilo tu.Ingawa kila mtu ana njia zake za uwasilishaji hilo nalo silipingi...

Je mtu akitaka kupata huu wimbo na kazi zako zingine ulizofanya atumie njia gani kuweza kupata kazi zako au za kundi?

Wimbo wa Sauti unapatikana kwenye album ya RBG Afrika Moja, na pia upo tovuti ya Africanmusic na Audiomack.

Mziki unaofanya unakupa faida gani tukiachilia kujulikana kwa wale wapenda Hip Hop ya handakini?

Faida ni kuungana na wana na kutanua wigo wa wasikilizaji wa kazi zangu. Bado naamini mbeleni utakuja kunipa faida kubwa kwa kuwa muziki ni bidhaa na bidhaa lazima iende sokoni na kununuliwa....

Baada ya kutoa huu wimbo fan base yako umeonaje imekua au imeshuka?

Fan base imekua, nashukuru kwa watu ambao wako makini kunisikiliza nini namaanisha kwenye uwasilishaji wa nyimbo zangu.

Vipi kuhusu kufanya video ya wimbo wako wa Sauti?

Video nitakuja kufanya... nikitoa remix yake.. ambayo itakuwepo kwenye album ya Deni.

Kouga una mkakati gani wa kuzunguka mikoani na kushare harakati zako na kujifunza mapya?

Mkakati upo comrade. Ukiacha hili suala la muziki, sisi tuna jumuiya yetu inaitwa P. A. N. D. E tuko na ndugu zangu, MaKaNTa pia wakiwemo... P. A. N. D. E(Push Art Not Drugs Exhibitors) -tuna mkakati wa kutoa elimu ya suala zima la madawa ya kulevya kupitia sanaa, ambayo itahusisha uuzaji wa bidhaa kwa wajasiriamali na wanasanaa.

Kwa hiyo hii lazima tutengeneze njia zaidi ya kuwafikia wengine mikoani na kujumuika nao kwa kuandaa magulio tofauti na kujumuika na taasisi zinazohusiana na madawa ya kulevya. Tuko mbioni comrade... nashukuru kwa swali.

Na je unakabiliana vipi na kupambana na harakati za madawa ya kulevya na ile project yako mpaka sasa umeshafanya harakati gani mtaani za kukomesha Madawa? Na Je, unasapoti vipi mateja walioathirika na drugs katika kuwakwamua kiuchumi? Na je ofisi yako imeajiri vijana wangapi uliowatoa kwenye uteja na kuwarudisha kwenye Sanaa?

Ile project sio ya kwangu tuko na familia. Mimi ni kama mmoja wa waratibu na ofisi ni ya familia ya P.A.N.D.E.

Project ya P.A.N.D.E imeanza mwaka jana, na mwaka huu ndio tumepata ofisi ambayo tuko sisi kama sisi....

Suala la kuwakwamua watu waliojiingiza kwenye drugs tumeshajaribu kuweka ushawishi sana especially kwa ndugu wa karibu walioathirika na kuacha hivi vitu na kuwashawishi kuwa pamoja kwa kuwa sisi tunasimamia  vipaji na hatupendi kuona vipaji vikipotea.

Ajira bado hatujatoa, ila sisi wenyewe tumejipa ajira na kuamini baadae tutaweza kuwaajiri wengine pia! Ila tunakaribisha ndugu yeyote mwenye maono ambaye anaweza kuona kama P.AN.D.E inaweza kumfaa tukajumuika pamoja.

P.A.N.D.E ina project kibao ambazo ziko nyuma ya pazia ikiwemo project inaitwa "TAE"(Talent And Education) -hii inalenga utoaji wa elimu katika suala zima la maswala ya madawa ya kulevya katika kuua vipaji/sanaa. Inahusisha zaidi watoto umri wa miaka 4 hadi 12 tukiamini kuwa hawa wako kwenye kipindi cha ukuaji. Motto "Prevention of drugs for the new generation"

Sawasawa na kabla hamjaja huku mikoani je mazingira yanayowazunguka mmeshayamudu katika kukabiliana na hii changamoto ya madawa? Na mpaka sasa ni vjana wangapi mnawasaidia kimaisha toka muanze kutokea hadharani na hii harakati ya P.A.N.D.E na kujihusisha katika baadhi ya matamasha kwa kuuza bidhaa?

Kwenye suala la madawa tumejaribu kujipa elimu sisi wenyewe na kujimudu. Kwa sasa hatuna vijana wowote ila kuna watu ambao tushawa-approach kujiunga na sisi ikiwemo rafiki zangu wa karibu ambao waliangukia kwenye uteja...!!! na mojawapo ni yule jamaa niliyekuwa nae kwenye lile tukio la RUF tulilokutana.....

Swali la mwisho toka kwangu, ilikuaje ukaamua kuchagua kuwa emcee na sio mwimbaji kama wanavyoimba wengine wanaitwa wabana pua?

Emcee kwangu mimi lina maana pana "Microphone Controller"- kwa hiyo unapopata kinasa lazima ukihimili kwenye suala zima la uwasilishaji, nikimaanisha "ugawaji wa maarifa"....

Upande wa kuimba naweza kuimba ila sina sauti kama wengine, nikaona bora nidumu kwenye kuchana. Heshima kwa wanaoimba pia, wamebarikiwa sauti zinazoendana na midundo husika.

Asante kwa muda wako Jedikouga siku nyingine ukiwa na lolote unaweza kutuambia na sisi tutasapoti vile tunavyoweza

Nashukuru sana kwa kuweza kunipa nafasi kuwasilisha vitu vyangu humu na muda wako wa maswali na wana wote.... Hizi ratiba nzuri tungependa kuona zinaendelea kwani tunajengana sisi kwa sisi..... nashukuru!

R.I.P Jedikouga