EP: Africa Revolution
Msanii: K Voo
Nyimbo: 6
Tarehe Iliyotoka: 07.12.2019
Ma Producer na Wapiga Midundo: 10th Wonder, Rama Genius, Miracle Noma, Bin Laden
Studio: AJ Records, Killers Records

Kelvin Chaulo au ukipenda K Voo ni mzaliwa wa Dodoma mjini, Tanzania. Baada ya kuangusha My Life EP kwanza hapo awali, 2019 alikuja na mradi mwingine ukiwa ni EP vile vile iendayo kwa jina la Africa Revolution.

Baada ya kuwa kwenye game kwa muda, K Voo aligundua kuwa wasanii pamoja na wachenguaji wengine kuna mada ambazo walikuwa hawaziongelei au kama walikuwa wanaziongelea basi walikuwa hawazitendei haki mada hizo.

Mojawapo ya mambo haya ni kuhusu bara la Africa na changamoto zake. Hivyo basi K Voo ambaye alianza mziki toka akiwa shule ya msingi alishika penseli na kuanza kuandika mistari kwenye daftari lake; mistari iliyokuwa na nia ya kuongelea yanayoendelea Afrika, mazuri na mabaya.

Nia ya mradi huu ni kufungua akili za waskilizaji wake na kuwafanya watafakari kuhusu bara la Africa ndani ya dakika 15.

Mradi unafunguliwa na simulizi kwa lugha ya ung’eng’e inayotupa kumbukumbu kuhusu Afrika ilivyokuwa zamani na vile tulikuwa ni wafalme na kulikuwa na malkia pamoja na changamoto za wakati ule. Japokuwa wafalme na ma malkia hawa wa kitambo walibobea kwa kuwa na falme na miliki nyingi na kubwa, kizazi chetu cha wafalme na ma malkia watakuwa wamiliki ki ujasiriamali kwa kuungana vizuri na wenzao.

Dibaji ndio wimbo unaotupa mwongozo wa nini tutarajie toka kwa mradi huu wa Africa Revolution. Anasema K Voo,.

“Karibu nikuliwaze kwenye yangu EP/
Naona fahari kuzaliwa Afrika sijutii/”

Akimalizia vesi anasema hatumii longolongo au mazingaombwe kukufanya umsikie,

“Abra-ca-da-bra huwezi kuzikuta hapa/
Maelekezo sahihi skiza track inayofuata/”

Kama alivyosema K Voo kwenye mdundo ufuatao uitwao “Uhuru” ulioundwa vizuri na 10th Wonder wakishirikiana na Bin Laden, madini yanamiminika toka kwa emcee huyu na wosio toka kwa viongozi wa sasa na wa nyuma wa Afrika kama Julius Malema na Robert Mugabe unaskika. Mdundo umetumia sampuli za guitar na sauti toka nyimbo za Afrika Magharibi hususan Mali. K Voo anatukumbusha kinaya cha maisha ya Waafrika anaposema,

“Nafichua vilivyofichwa, hizi tungo mizizi/
Wakija kwetu watalii, tukienda kwao wakimbizi/”
10th Wonder na Rama Genius wanashirikiana kutupikia mdundo wa singo iitwayo “Waafrika” inayo enzi bara letu na uafrika wetu. K Voo anatueleza ujumbe wake kwenye mradi wake ni huu,

“Iliidhinishwa June 16, 91/
Sipendi ulimbukeni na zama moja kwa moja/
Waafrika tupendane tusije kuwa vioja/
Nawahamasisha raia kila chocho, kila boda/
Kwa imani yangu naomba mizimu inilinde/
Iniepushie mitihani, majaribu na mbilinge/
Kwanini ninyamaze upuuzi wenu nisiimbe/
wino wa peni ni silaha ya jadi kama upinde/”

Askari wa jadi walitumia silaha, K Voo anatumia wino wa peni kupigana vita vya kisasa.
“Mjenzi Huru” ni singo ya tano ambayo Rama Genius anatumia vizuri sampuli toka kwenye wimbo wa muimbaji Nneka uitwao “My Home”. Pia sampuli toka kwa shairi la dada Mwende “FreeQuency” Katwiwa, Mkenya anayeishi America liitwalo “The Gospel of Colonization” linatumika vizuri kwenye singo hii kama kiitikio. Shairi hili linazungumzia vile mzungu alitumia dini kututoa kwenye reli kwa kudai wametuletea “Mungu” kana kwamba sisi tulikuwa hatujui kama Mungu yupo ilhali walichokuwa wanakilenga ni kuchukua ardhi yetu yenye rutuba na raslimali zetu.

Pia K Voo anatupa tahadhari kutomnyooshea mzungu kidole cha lawama kwa changamoto tunazo zipitia bila kukubali makosa yetu na kujirekebisha ili tujinasue toka kwa mtego wao. Anasema K Voo,

“Sababu ya umaskini ni Waafrika wenyewe/
Ukarimu umetuponza mpaka sasa tuonewe/”
Anazidi kwenda ndani zaidi kutuonyesha mbinu walizotumia hawa wakoloni kutumiliki,

“Usingizi sipati, natafakari/
Wametuachia dini na kuiba rasilimali/
Wazungu na Warabu, vibaraka wa majini/
Utumwa hautakwisha kama hatutaziacha dini/
Tatizo sio upimbi ila ni ubinadamu wetu/
Media zimekuja potosha jamii yetu/
Wazee wetu walikaribisha wanyama wakidhani watu/
Kumbe wana roho mbaya, wanakula nyama za watu/”

Kwenye wimbo wa “Siasa Chafu” K Voo anaonesha hasira yake dhidi ya wanasiasa wanaotumia siasa kutumiliki na kutuharibia maisha wakati wao wakinufaika. Anakashifu wanavyonunua vifaa vikubwa ambavyo hatuvihitaji na pia kujenga miradi mikubwa ilhali wananchi wanalala njaa. Ujasiri wa K Voo unaonekana wazi anapoongelea mada ambazo marapa wako wa kawaida hawawezi kuzigusa ili wabaki upande sahihi wa ki siasa.

Ujasiri wa K Voo unaonekana dhahiri pale anapoamua kusema haya,
“Mnamiliki vitambi, majumba na kupombeka/
Nafungua mdomo na sihofiii kutekwa/
Mara ununuzi wa radar, mara sakata la EPA/
Ubinafsishaji wa mali za umma na visirani/
Mauaji ya wananchi 22 visiwani/”

Mradi huu umepikwa vizuri japokua ni mfupi ila Africa Revolution ni mradi wenye ukweli mwingi wa kukufanya wewe kama muafrika au mtu mwenye utu kutafakari historia ya muafrika, shida za muafrika na kuanza kuwaza nini unaweza kufanya kujinasua toka kwa mitego ya kibepari na kuanza kuishi. African Revolution ni mradi wa kimapinduzi unao pindua dhana zako kuhusu Afrika na Muafrika.