Ukaguzi Wa Albam: Handaki Vol. 1
Msanii: Kaa Feel
Tarehe iliyotoka: 20.08.2020
Nyimbo: 15
Ma Producer na Wapiga Midundo: Jegalla OG
Wachanganya Sauti na Midudo: Paul Loops
Studio: Misingi Studio

Kaa Feel

“Lazima tutambue handaki ni nini…” ndio kauli inayotufungulia mradi wa Kaa Feel kwenye debut albam yake Handaki Vol 1 kwenye utangulizi wa albam. Uzuri wa utangulizi huu ni kuwa emcee Kaa Feel mwenyewe anatuoredheshea vigezo anavyotakiwa kuwa navyo mtu ila aweze kujigamba kuwa yeye ni wa handaki kindakindaki. Kutumia vigezo alivyovianisha yeye mwenyewe ambavyo mimi mwenyewe nilifanya utafiti nikagundua ndio vigezo vya aliye handakini tutavitumia kukagua albam hii ili kuona kama kweli ni mradi wake ni wa handaki pia.

Mradi huu ambao asilimia mia moja umeundwa na producer Jegalla OG ni boombap za ki old school mwanzo mwisho ambazo kwa kusema kweli emcee Kaa Feel amezitendea haki. Pia nilichokipendea kwa mradi huu ni kua asilimia  95 ya ngoma zote Kaa Feel kachana akiwa solo ila ma emcee waliobahatika kuwa kwenye mradi huu ni Kiraka Tosh, Miracle, Rado, Javan, Eddy Mc pamoja na DJ Alice.

Mada ya handaki imekolea kwenye mradi huu kwa asilimia kubwa na nyimbo nyingi zinazo piga humu zimeongelea handaki kwa upana. Nyimbo kama vile Amua, Toka Naanza, Maana Halisi Ya Handaki, Na Ahidi na Sisi  ni nyimbo zilizoshiba madini ya handaki mwanzo mwisho. Toka Naanza akiwa na Kiraka Tosh kwenye kiitikio unaonesha historia yake na handaki akitema hivi kwenye vesi ya kwanza,

“Toka naanza niko makini/
Nilitambua kiini nilitambua nataka nini/
Imani yangu niliamini/
Sijawai kulegalega ni hatari nikiwa kazini/
Ukinihisi naona shega naongeza wingi wa mapini/
Toka naanza naupinga sana umaskini/
Kwenye nchi tajiri tunakwama wapi tathmini/
Nilianza na ngumu kigumu sikuwaza jina/
Sikutangaza anasa ni sumu cha kwanza heshima/
Sikutamani fani kisa nasifiwa na wajinga/
Toka nazama ndani misingi yangu nailinda/
Sikutamani fani kisa nasifiwa na wajinga/
Toka nazama ndani misingi yangu nailinda/
Sikutamani umaarufu nilipendezwa na handaki/
Sio kuchanachana tu(Nilipendezwa na harakati)/
Wanatusaka hawatupati/
Mitego yao haitunasi/
Niliamua kuuza roho siku ongozwa na wasiwasi/
Sikuogopa kuitwa muasi ukweli nausimamia/
Hata wote munipinge misimamo itabakia/”

Mistari aina hii ndio inaonesha uwezo wa Kaa Feel wakati emcee Kiraka Tosha anayemuelewa vizuri Kaa Feel anampa kaka support na kiitikio cha nguvu.

Maana Halisi Ya Handaki ambao ni wimbo wa nne kwenye mradi huu naweza sema ndio wimbo uliobeba jina la albam hii japokua jina la wimbo lipo tofauti na jina la albam ila sio kwa umbali. Wimbo wenyewe umepikwa ki ustadi na Jegalla OG na Kaa Feel anatuonyesha kuwa yeye ni handaki na mfano wa mtu anayeiwakilisha handaki akichana mistari kama risasi hewani na sauti yake nzito. Kiitikio kinakupa mukhtasari mzuri wa maana halisi ya handaki akisema,

“Wanagombea kutoka sisi chimbo tumebaki/
Tunatokea chini piga juu mafataki/
Kaa Feel ndio maana halisi ya handaki/
Sisi ndio maana halisi ya handaki/”

Kuonesha umuhimu wa knowledge au maarifa handakini Kaa Feel anashirikiana tena na Rado Kiraka kwenye mdundo flani old school sana uitwao Ruhusu Maarifa wenye kinanda mzuka sana. Nondo kama kawa toka kwa Kaa Feel akisema,

“Nimepita hatua nyingi na mengi niliyokabili/
Vigingi haviyumbishi misingi ya Kaa Feel/
Sina unusu nusu nishajitusu kiukamili/
Maarifa nayaruhusu nayapokea kwenye akili/
Ruhusu maarifa uwe na fikra yakinifu/
Upende kujifunza ili ukuwe mbunifu/
Nishaona ma ibilisi wanaigiza utakatifu/
Wanasema wameokoka na hawapati ukamilifu/
Jifunze jinsi ya kuishi na raia wanaokuzunguka/
Jifunze kuwa na usawa usiongozwe na mizuka/
Kuwa na imani we uliyeanguka/
Kuna siku utainuka/
Ruhusu maarifa ili ubongo uweze funguka/
Wana roho za kutu magumu yetu hawajali/
Bora uthamini utu hatuziki mtu na mali/
Usichoke kujifunza mbinu za ma jenerali/
Ruhusu maarifa utaiona afadhali/”

Na kiitikio je? Kama kawa madini wakisema Kaa Feel na Tosh,

“Ruhusu maarifa ili ukuwe ki ufahamu/
Usiyumbishe fikra tumia vizuri kalamu/
Daima hauzeeki utaalamu/
Ruhusu maarifa ujikomboea binadamu/”

Kusema kweli mashairi ya emcee huyu yanaandikwa ki ustadi na kimalengo flani na kutokana na hili unakuta vina vinapangika kwa uliani bila kufosi kabisa. Nadhani anayetaka kujua mashairi ya handaki yapo na utofauti gani na mkondo mkuu mradi huu ni case study nzuri.

Changamoto wanazopitia sio tu wanahandaki bali hata wananchi wa kawaida zimeguswa kwenye wimbo wa kijeru flani hivi, Tushazoea ambapo Jegalla kapiga violin fresh kwenye mdundo wa boombap na ukatoka vizuri sana. Wimbo huu ni kama somo la chuoni, Handaki Vol 1: 101 kwa ajili ya yoyote anayetaka kujaribu kuwa mwana handaki ajitayarishe kwa haya;

“Kupata stress almanusra kudata/ (tushazoea)
Kukaza roho na kuandamwa na ukata/ (tushazoea)
Nasogesha kiujasiri hichi kipaji/(tushazoea)
Kuishi bila kipato cha kukidhi mahitaji/(tushazoea)”

Maisha ya handaki lazima ujiandae kupitia magumu kama kweli wataka kubaki huku.

Pia kingine nimependa toka kwa mradi huu ni aina ya sampuli za mziki zilitotumika kwenye mradi huu ili kuongezea thamani mashairi ya Kaa Feel kama vile kwenye Imani Yangu ambapo kwenye mdundo kunapiga solo gita safi sana. Pia kwenye Nathubutu ambapo mdundo unatumia sampuli toka kwa wimbo wa Martial Pa’nucci akiwa na Biz Ice toka Congo uitwao Black Is Beautiful.

Maskio ya Jegalla na Kaa Feel kuchagua midundo sahihi kwa ajili ya mradi huu inakuonesha vile midundo pia ni muhimu sana na inasaidia vizuri uwasilishaji wa hoja au mada kwa jamii. Uchimbaji wa madini unaendana vizuri na uchimbaji wa midundo.

Mradi huu kama sawia na malengo ya handaki unakupa ushauri kutoruhusu umaarufu kukuongoza, unaupa kipaumbele ufahamu wa mtu, unathamini elimu ya mtu binafsi, una hamasisha nguvu ya raia na pia unaonesha umuhimu wa mapinduzi yoyote yale kuanzia chini, mashinani . Kaa Feel ndio maana halisi ya handaki na ukitaka kujua A – Z ya handaki hakikisha unapata nakala yako ya kitabu cha Handaki Vol 1.

Kupata nakala yako ya albam hii wasiliana na

Nyeke Da Nyiki kwa njia ya simu/WhatsApp:

+255 765 686 821

+255 785 031 074