Kaa Feel, Ndio maana halisi ya Handaki!
Tunapozungumzia handaki kwa haraka haraka akili za mtu huenda kwa shimo au mtaro flani unaotumiwa na mtu kujificha au kujikinga sana sana wakati wa vita. Hivyo basi tunapozungumzia Hip Hop ya handaki tunazungumzia ile Hip Hop ambayo inapatikana mfuasi anapochimba chini kwenye “ardhi” ya Hip Hop kutafuta madini yalipofichwa.
Katika kuchimba kwangu nilipata fursa ya kuskia mradi wa Hip Hop Handaki wa emcee flani anayejiita Kaa Feel. Pale ndipo niliposkia kuwa “Kaa Feel ndio maana halisi ya handaki…”.
Hivyo basi niliona ni vyema nimualike emcee huyu kwenye jukwaa la Micshariki Africa ili kuweza kuona huyu handaki anafanyaje.
Karibu usome gumzo letu na Kaa Feel ili uweze kupata elimu kuhusu Handaki.
Karibu Kaa Feel kwenye jukwaa la Hip Hop Micshariki Africa. Kwanza tuambie jina lako rasmi
Shukran sana (Micshariki). Mimi jina langu rasmi ni William Donatus Kyanyali ila kutokana na michakato na harakati ndipo lilipo ibuka jina la Kaa Feel
Kaa Feel unatokea au kupatikana wapi na unajihusisha na nini ?
Mimi kwa sasa napatikana Temeke, mitaa ya Yombo. Najihusisha na biashara tofauti tofauti, street entrepreneur..
Tueleze historia yako ya nyuma ki mziki.
Mziki tulianza kupenda tukiwa watoto enzi hizo miaka ya 2003, 2004 ndio tulizidi kuchenguka zaidi na Hip Hop mpaka sasa tunaweza kulisimamisha handaki vile inavyohitajika.
Mbona unajiita Kaa Feel?
Kaa Feel ni jina ambalo lilitoka kwa “General” Kiraka Rado USO na hiyo ni kutokana na aina ya rap ninayofanya kwamba ukikaa kuiskiliza lazima uta Feel. Hapo nyuma nilishatumia majina tofauti tofauti nilipokutana na kamanda alipendelea jina liwe hilo, Kaa Feel.
Una miradi mingapi hadi sasa?
Mpaka sasa nina miradi miwili; mmoja ambao nishauwachia tayari unaojulikana kama Handaki na ni handaki kweli kweli, maana halisi ya handaki, kuanzia ujumbe, midundo iliyotumika, style ya ku rap ni handaki, handaki kweli kweli.
Mradi wa pili ni Damu ambao na tarajia mpaka mwisho wa mwaka huu(2021) utakuwa umeachiwa. Damu nayo pia itakua albam iliyo shiba handaki kweli kweli pia. Kwa hiyo mpaka sasa nina miradi miwili, yep.
Mimi naona we una represent hardcore Hip Hop flani ya bongo au nimekosea? Nini kinachokusukuma kufanya sio tu Hip Hop ila underground/handaki Hip Hop ?
Ni kweli mimi ninafanya underground Hip Hop, Hip Hop ya handaki na kinachoniskuma kufanya hivi ni vingi; cha kwanza ni kulinda utamaduni wetu wa Hip Hop kwa sababu wewe mwenyewe ni shahidi kwani umeweza kuona mkondo mkuu (mainstream) yanayofanyika. Maigizo ni mengi sana huko juu na kuna mda wengi wanalazimika kuigiza ili waweze kukaa kule juu kwenye mkondo mkuu. Hivo hata style zao wanazotumia kwenye rap unaweza ukaona zina mabadiliko hazifanani na utamaduni, uandishi wao, jumbe zao na zingine hazina jumbe kabisa ila huku tulipo sisi handaki we mwenyewe ni shahidi wa kile kinachotoka huku, lazima kiwe na uzito ndani yake.
Na ndio maana huku albam zetu hua tunaziita vitabu yani kwamba unapozisikiliza lazima utajifunza vingi vingi, vingi vya kupanua ubongo. Chakula cha ubongo kinapatikana handaki, huku tulipo sisi.
Huku ndipo misingi inapotunzwa, na ni moja ya vitu vinavyo nishawishi kuendelea kuwakilisha handaki.
Nilikuja nikaona video flani raw ukiwa na Kiraka Tosh, chem chem sana. Nini kilicho waskuma kwa moment ile kuunda ile video?
Kwa kipindi kile kama Watunza Misingi tulikuwa tushafanya audio nyingi sana. Sasa kutokana na audio kuwa nyingi na kuna muda pia watu hupenda kukiona kitu katika muonekano wa picha kwa hiyo hicho ndio kilichotusukuma sisi kufanya video ile ya Tutaendelea Kubisha.
Handaki Vol 1. Tueleze kudogo kuhusu mradi huu.
Handaki ni albam na ni kitabu kilichoshiba sana maana halisi ya handaki. Ukihitaji kujifunza kuhusu handaki kile ni kitabu tosha kabisa, kuna elimu tosha kuhusu handaki.
Na kama bado hujaiskiliza albam ya Handaki unaukosea ubongo wako, unaunyima ubongo wako haki. Handaki ni vita kubwa sana.
We ni mmoja wa Watunza Misingi. Watunza Misingi ni nani na wanajihusisha na nini ?
Watunza Misingi ni jumuiya ya wana wenye nia moja ya kimapambano, wanaharakati kutoka handaki, underground Hip Hop.
Watunza Misingi ni mjumuisho wa makundi mengi sana karibu Tanzania nzima na magenge sehemu tofauti tofauti yamejikusanya yenye nia moja ya kimapambano, nia ya kiukombozi, wapambanaji, wavuja jasho wameamua kupambania taifa lao na kupambania taifa lao kwa ujumla. Kwa hiyo Watunza Misingi ni jumuiya ya wana mapinduzi kutoka handaki.
Ni magenge mengi sana nikianza kuyaorodhesha; tupo sisi Viraka, MaKaNTa, Wasadikaya, Wanaboma na magenge mengi mengi na wengine pia ni solo artists pia wanaishi kwenye misingi sana. Watunza Misingi ni jeshi kubwa, jeshi kutoka handaki. Nikianza kuwaorodhesha wote hatumalizi sasa hivi. Ni jeshi kubwa, kwa hiyo saluti kwa wana wote wanaoitunza misingi.
Tunapoongelea Hip Hop ya handakini tunamaanisha nini?
Hip Hop ya handaki. Tunapo zungumzia Hip Hop ya handakini tunazungumzia Hip Hop ambayo imebaki inafanywa na wale wana ambao wamebaki katika nguzo na misingi ya utamaduni wa Hip Hop pasipo kuyumbishwa na chochote kuanzia kwenye maisha yao halisi kwani wamejitolea kupambana, wanajeshi kamili wenye nia ya dhati wasioyumbishwa na udhalili wowote unaofanywa na watu wowote katika kuuzima ukweli uliopo huku handaki.
Ni watu waliojitolea, wasio endeshwa na mihemko, wasiotegemea kuipata pesa kwa kupitia tu ku rap rap tu vitu ambavyo havi make sense na havi fanani na mazingira yetu halisi. Watu waliobaki wameshikilia misingi.
Hiyo ndio Hip Hop ya handaki kuanzia kwenye ujumbe, midundo mpaka style zao za ku rap zime baki kwenye utamaduni. Hao ndio wana handaki.
Mashairi unaandika mwenyewe au unandikiwa? Je emcee akiandikiwa mistari kuna tatizo lolote? We mwenyewe ushawahi kuandikiwa au kuandikia mtu mashairi ?
Mimi sijawahi kuandikiwa mashairi, ninaandika mwenyewe na kwa emcee kuandikiwa sio tatizo kama kutakuwa kuna sababu ya msingi ila ni tatizo kama itakua ni kitu chake cha kudumu kwamba hawezi kabisa kuandika ila kama labda imetokea mada anaona kwake ina ugumu kidogo kuandikiwa sio tatizo ila kama hawezi kabisa nafkiri anaweza akajaribu kupambania kuliweza hilo kuliko kutegemea maandishi ya mtu.
Mbona wana handaki hampendi kutumia teknolojia kunadi miradi yenu kwani wachache ndio wameweka miradi yao kwenye streaming apps ?
Sio kwamba hawapendi ila nafkiri kila mmoja ana sababu zake tofauti tofauti. Yaweza kuwa ni uzembe, yaweza kuwa mazingira ya maisha yanayomzunguka hayamruhusu kufanya hivyo kwa mda huo, au bado hajaona umuhimu wa hilo, kwa hiyo kuna sababu tofauti tofauti ila sio kwamba hawapendi.
Watu wa handaki wanapenda na wanaamini kwamba huko pia wana watu wao kwa hiyo watu wana sababu zao tofauti tofauti sio kwamba hawapendi.
Kando na mziki Kaa Feel unajishughulisha na nini kingine ili kuweza kujikimu kimaisha? Je pia una vipaji vingine kando na kuchana na unaweza kupiga chombo gani cha mziki?
Kama nilivyosema mwanzo kando na mziki mimi najihusisha na biashara ndogo ndogo zinazoweza kunikimu kidogo kidogo kulingana na maisha yangu ninayoishi.
Mbali na kuchana pia ninaweza kufanya graffiti lakini kwenye swala la vyombo vya mziki sipigi chombo chochote.
We naona ni strictly Boombap. Unaongeleaja midundo na uchanaji wa Trap, mumble rap pamoja na Drill ambazo ndio zinapigwa sana siku hizi?
Sio tatizo kwa watu kuamua kufanya aina nyingine ya mziki tofauti tofauti. Yaani rapper anapo amua kufanya hiyo Trap sijui na miziki gani mingine hiyo sio tatizo.
Tatizo ni kuwaaminisha jamii kwamba Hip Hop sasa ndio inatakiwa ifanyike hivyo. Kwamba zama zimebadilika kwa hiyo watu tunatakiwa kufanya hivyo. Tatizo linaanzia hapo.
Kwa hiyo mimi nafkiri tungepeana tu nafasi wao wangebaki kwenye style zao, ma rapper wabaki na style zao zozote wanazotaka, vyovyote wanavyotaka wao na ma emcee tubakie kwenye utamaduni wetu na wote tupewe nafasi ya kufikisha jumbe zetu katika hata hizo sehemu zao wanazopeleka watu wa mkondo mkuu(mainstream). Waruhusu mabomu kutoka handaki, bunduki kutoka handaki zikapambane kwenye uwanja huo.
Hata wale ambao walikuwepo handakini na wameamua kufanya mambo yao mengine basi wasiendelee kujitangaza kama bado wapo huku, waendelee tu huko na upande wao na hivyo tupeane nafasi watu wa misingi tuendelee kusimamisha misingi.
Nini kifanyike ile Hip Hop ya handaki izidi kupanua soko na kupata waskilizaji zaidi bila ya kupoteza uhalisia wake?
Mimi nafkiri sasa media zingeruhusu kidogo mawazo kutoka huku chini handakini yaka sikilizwa na watu. Waruhusu mawazo yaskilizwe na watu, haijalishi anapinga utawala, haijalishi yanapinga watu ambao labda kwao ni msaada, ila wajaribu kupokea mawazo ya watu tofauti, yakiwa chanya, yakiwa hasi wajaribu kuyapokea ili waweze kupata vitu vingi ambavyo viko huku chini na huku kwao haviskiki kwani watu wanaskia kila siku ujinga ule ule.
Vitabu vilivyobeba elimu vinaendelea kubaki handakini. Hata wale wanaojiita wadau wakikutana na watu kutoka huku wawaruhusu waendelee kufanya aina ile ile ya mziki walioendelea kufanya na wawekeze na kama wanavyofanya kwa ile miziki mingine, wawekeze pia kwenye mziki wetu huu wa misingi. Matokeo yatakuwa ni mazuri sana.
Wasiwashawishi watu kufanya vitu kama flani kwa kuwa flani kafanya na anaonekana labda ameenda sana. Waki push hichi pia kitapendwa kama vile vilivyo pendwa vingine.
Dj Alice ni mmoja wa wageni waliopo kwenye mradi wako. Mimi binafsi simfahamu ila niliona baraka sana kuwa akina dada pia wanakubalika na mnafanya mao kazi ? Kwa nini akina dada ni wachache kwenye mziki wa Hip Hop sio tu kwa upande la uchanaji bali hata kwa ushabiki? Tunaweza kufanya nini zaidi ili kuzidi kuwavutia wa support Hip Hop ya handaki?
Wakina dada ni kawaida yao kwani ki asilia sio watu wa kuchimba sana. Kwa hiyo hata vitu wanavyovisikiliza vinatoka kwenye hizo media ambazo tayari hazitaki kuona aina hii ya mziki ikienda.
Hivi hata wanapojaribu kuingia wanajikuta moja moja lazima waje katika style zile ambazo wanaziona kila siku kwenye tv, wanaziskia kwenye radio na wanahisi sasa ndio zitakazokuja kuwapa hela.
Hata anapopata nafasi ya kuskiza hii ya handaki anakuwa kabisa alishawahi kuambiwa kuwa hiyo haiwezi kukupa mafanikio na wao mafanikio wanayaangalia kwenye tv, wanayaangalia mafanikio kwenye mitandao, ndivyo wao wanavyoyapima mafanikio kwa upeo wao
Hivyo akina dada inakuwa ni ngumu sana kwao kuelewa hiki.
Nafkiri kuwavutia narudia tena ni media ziendelee kuruhusu haya mavuguvugu ya mapambano yaendelee kuskika na wengi ili wapambanaji wengi waweze kuonekana. Waendelee kuruhusu sauti kutoka handaki ziweze kuskika hivyo hata wao wataweza kuskiliza na wataweza kuelewa maana ya huku tulipo na kuelewa faida ya huku tulipo sisi na hata huku tulipo pia watu wataanza kupata faida kupitia tunachokifanya.
Nini cha mwisho unaweza kutueleza ambacho sijakuuliza?
Cha mwisho ninachoweza kukuambia ni kuhusu mradi wangu wa pili niliouzungumzia wa Damu. Albam ya damu pia ni vita kubwa zaidi, na mapambano yanaendelea, mapambano makubwa, akili kubwa imetumika kuandaa mradi huo, ufanisi mkubwa umetumika hivyo imebeba uzito mkubwa sana. Damu ni kama bomu kwa mamluki, bomu kwa mabepari, ni bomu kwa wote wanaojaribu kuzuia njia ya mawazo chanya yanayotoka kwa wanaojitolea kupambana.
Damu ni bomu la ushindi la kumaliza maadui vitani. Albam ya Damu ni njia sahihi kabisa, ni mwelekeo, ni dira. Damu ni chakula cha ubongo. Hivyo mkae tayari kwa ujio wa albam toka kwa Kaa Feel ya Damu. Mwezi wa 12 taarifa zitatoka. Damu ni funzo kubwa, chem chem sana!
Kiraka Kaa Feel, Watunza Misingi, Viraka EnterBrainNet, Full.