Msanii: Kaa La Moto
Album: KESI
Tarehe iliyotoka: 15.07.2019
Nyimbo: 15
Ma Producer: NJE Pro, Sango, Okoth Oyiera & Teknixx, Kaa La Moto
Studio: Ufuoni Records international, Malindi Records, Kubwa Records & B Records
Mchanganyaji sauti na vyombo: Chizn Brain
Producer mkuu: Kutto "Bantu Pai" Mwagaradi

Mara nyingi watu wanapokuwa na kesi huwa wanakimbilia aidha kwa wazee, polisi au hata kortini ili waweze kupata suluhu juu ya changamoto zinazoletwa na kesi hizo. Tunaposubiria maamuzi ya mahakimu hawa huwa tunajua kuwa tunaweza shinda kesi, tunaweza shindwa kesi au kesi inaweza kutupiliwa mbali na mahakama.

KESI ni album iliyoundwa na msanii wa Hip Hop toka Mombasa aendaye kwa jina Kaa La Moto. Kaa La Moto anajulikana rasmi kama Kesi Juma Mohammed na anatokea pwani ya Kenya, Mombasa toka kwa jamii ya wa Mijikenda. Emcee huyu pia anajulikana kama “Kiumbe”.Kwa hiyo jina lake anapokuwa jukwaani analolitumia ni Kaa La Moto Kiumbe; Kaa La Moto likiwakilisha vitu visivyoishi ilihali Kiumbe likiwakilisha vitu vinavyoishi.

Kaa La Moto ni msanii aliyejivika kofia nyingi; ni mchenguaji au emcee mahiri, ni mwana ndondi na mtaalam na mwalimu wa Shotokan Karate na pia ni baba wa familia.
Baada ya kuachia mixtape kadhaa na album moja hapo awali, mwaka 2019 ndege ya KLM ilipaa tena na kutoa mradi mwingine tena ulioitwa KESI.

KESI ni album yenye maana mbili; Kesi, jina rasmi la emcee huyu na pia KESI kumaanisha mambo yanayo zungumziwa ndani ya albam hii ni mambo yatakayoibua mijadala tofauti toka kwa wasikilizaji.Kwa mfano ukiskia nyimbo inayobeba jina la album KESI, Kaa La Moto anaona kuwa kuna uwezekano mtoto wake aliyemzaa nje ya ndoa na binti fulani ana uwezo wa kuwaunganisha wapenzi hao wa kitambo.

Albam ya KESI ni albam iliyoundwa kwa ustadi wa hali ya juu na iliwashirikisha ma producer toka Mombasa, Nairobi na pia nchi jirani ya Tanzania. Mkono wa Chzn Brain aliyezaliwa Mombasa na anaishi Tanzania unaonekana kila mahali kwenye mradi huu.
Album hii inaanza kwa mwendokasi akituambia Kaa La Moto “Hands Up” akitufungulia mradi kwa kutuamrisha tusalimu amri kwa kinasa chake na beat la wimbo huu. Wimbo huu wa ku party unaendana sawia na wimbo uitwao “Kidogo”. Kwenye Hands Up emcee huyu anakumbushia kuwa hata akiwa kwenye party hasahau jukumu lake ni nini anaposema, “Watoto wa Hijabu wamekuja kumcheki Nabii”.

Gita zinapiga mdogo mdogo kwenye wimbo wa “Mtoto wa Mama Saumu” kwenye wimbo ambao Kaa La Moto anajielezea kuwa yeye ni nani, historia ya maisha yake kiujumla na kimuziki, chimbuko lake ki kabila na maisha yake enzi hizo kule Mombasa akisema,

“Madogo wananienzi mtaani kaa Ukoo Flani/
Upande wa pili wanaoenzi ni ngumi za mjapani/”

“Msafiri” ni wimbo unaoongelea changamoto za maisha ya kila siku anayopitia Kiumbe. Kwenye vesi ya pili ya wimbo huu anasema hivi,

“Naskia mwanangu akiulizia, mwambieni nipo salama/
Wala sijakimbia, malishoni alishwe ndama/
Wa kwanza kwa familia, ilibidi nimtunze mama/
Na kuhakikisha wadogo zangu pia wanasoma/
Namuombea uhai, kesho haina uhakika/
Sitaki aje pitia maisha ya kudharaulika/
Mpe malezi bora, asije akadanganyika/
Wengi ngono za mapema, ziliwafanya wakasahaulika/”

Msafiri anaona kuwa kwenye haya maisha kuna kupanda na kushuka.

“Kijiweni” ni wimbo unaochora picha halisi ya maisha yetu ya uswahilini na wimbo unao tupatia kumbukumbu kuhusu umuhimu wa vijiwe vyetu. Anasema hivi bwana Kesi,

“Kijiwe wewe ndiye ulipangiwa tarehe ya harusi/
Ulizungumziwa msiba na mipango kuhusu mechi/
Stori za visasi na vita kijiwe ulihusika/
We ndio ulikuwa unajua demu gani bado bikra/
Nani kaachika, nani kapewa talaka/
Nani kaavya, nani ana mimba, nani ndio tasa/
Ugomvi na siasa/
Habari za Mombasa/
Nilipokuwa hapa kwenye kijiwe niliona future kuwa rapper”

Kijiwe ndicho kilimkuza, kumnoa na kumtoa nabii huyu. Tusikidharau kijiwe.

“Kenda” ni wimbo uliokwenda shule unaozungumzia makabila na tamaduni za ma Emcee Kaa La Moto na mkongwe wa muziki wa Hip Hop Kenya toka kwenye kundi la Kalamashaka, Kamaa. Wawili hawa wanapitishiana kinasa wakiongelea mataifa yao; Kaa La Moto, MijiKenda (Miji 9) ilhali Kamaa akiongelea makabila 9 ya Wakikuyu waliotokea nyumba ya Mumbi. Sauti za wazee wa ki Mijikenda zinaskika vizuri pamoja na maombi ya Kamaa akisema, “Thai, Thathaiya Ngai Thai!”

Nyimbo nyingine zilizojisimamia vizuri kwenye mradi huu ni kama, “Malenga” unaotuhamasisha kukumbuka na kuenzi magwiji, wanafalsafa, wahenga na malenga wetu wa jadi. Salu T toka Tanzania ana fungua wimbo na vesi ya moto sana.

“Mungu Saidia” akiwa na Vivonce, “Old vs New” akiwa na Chizn Brain, “Kumbukumbu” akimshirikisha Songa toka Tanzania pamoja na “Sawa” ni nyimbo zilizosimama kwenye mradi na ninazozipenda sana kwenye albam hii.

“Sawa” ni wimbo poa sana unaogusa changamoto walizo na wanazopitia ma emcee toka Mombasa akisema KLM kua,

“Utaskia mbwembwe wakiongea kwenye anga zao/
Hakuna rapper aliyebobea kwenye mji wa mwambao/
Ukoo Flani ilivuma uhuru wachukue Mau Mau/
Cannibal, Sokoro na Maduke wa Farao/”
Kisha anaendelea akisema,
“Ku hit mjomba, fika Nairobi/
Mombasa hawana nyumba wasanii wanagongea makodi/
Hawajui biashara wanaimba kuhusu hobby/
Wengi wazee wa ndumba wanaishi juu ya showbiz/”

“Ma Niggaz Hip Hop” Ndio “singo” inayofunga rasmi mradi huu.

Albam hii imeshinda KESI na maamuzi ni kuwa mradi huu ni muhimu kwenye utamaduni wa Hip Hop sio Mombasa tu bali Kenya nzima, Tanzania na kwenye ulimwengu wa Hip Hop Na Rap ya Kiswahili. Mombasa kupitia mradi huu iliweza kurudisha heshima yake kama chimbuko la Hip Hop kwenye ramani ya Kenya.
Kesi ameshinda na KESI.