Kambona ni rapa/mtengeneza filamu wa kujitegemea kutoka Nairobi, Kenya ambaye anatangaza ujio wake katika ulimwengu wa Hip Hop akiwa na mixtape ya kweli iliyoundwa kwa bajeti ndogo ila ikawekezewa na moyo mkubwa.
Kambona ni mwanafunzi wa Sinema na Rap anayejituma sana ambaye hivi karibuni aliacha kandamseto yake ‘MARiACHi’ ambayo ilitumia wazo kutoka kwenye filamu ya kitambo ya Robert Rodriguez inayokwenda kwa jina la El Mariachi.
Kama mstari wa kwanza wa wimbo wake unaobeba jina la albamu unavyosema, Kambona ni mtu mwenye malengo anafanya kazi ndani ya bajeti. Katika mradi wake wa kwanza, yeye ametengeneza kanda inayobeba maumivu pamoja na majivuno huku akichana kwa midundo kutoka kwa marapa na watayarishaji mashuhuri. Tunapaswa kutambua kuwa, Mariachi, kwanza, ni hadithi ya mtu aliyeacha hofu na aliyekamata ndoto zake na hataki kuziacha
Karibu Micshariki Africa kaka Kambona. Naomba ujitambulishe kwa mashabiki zetu, Kambona ni nani, unatokea wapi na anajihusisha na nini?
Kambona ni rapa/mtengenezaji filamu huru kutoka Nairobi, Kenya. Wakati sipo bize kuandika mistari yangu, mimi ni mwanafunzi wa sinema. Nina aibu kusema ni muda gani ninatumia kusoma Sinema ya Karne ya 20 (20th Century Cinema), lakini ndivyo nilivyo.
Jina la Kambona lilikujaje, lina maana gani na linakutambulishaje kama msanii?
Kambona lilikuwa jina la utani la marehemu baba yangu. Nilipoamua kuanza kuchana nilichukua jina ili kuweka uhusiano huo kati yetu, nadhani. Yeye na mimi tulikuwa karibu.
Kambona safari yako ya muziki ilianza vipi? Turudishe nyuma hadi mwanzo... Kwa nini uliamua kwenda na uchanaji, kwa nini Utamaduni wa Hip Hop?
Safari yangu ya muziki ilianza wakati wa janga la Uviko 19…
Nilikuwa ma mia ya maili kutoka nyumbani katika mji wa mbali huko Mombasa. Nilikuwa pale ki kazi na sikumjua mtu yeyote. Kwa hiyo ningetumia wakati wangu mwingi kusikiliza muziki wa Hip Hop na kuandika mashairi hadi siku moja nili chana moja ya mashairi yangu juu ya mdundo wa mtayarishaji ya 9th Wonder na niligundua kuwa naweza kuchana ikiwa ningejifunza jinsi ya kuzoeza sikio langu kuskia vitu kwa makini. Ilipita miaka mingine miwili na nusu kabla hata sijaingia studio lakini nakumbuka nikifikiria…
‘Inapokuja kwenye swala hili la kuchana, nadhani naweza kulifanya!’
Ni wasanii gani waliokuvutia nchini Kenya na kimataifa wakati ukianza kuchana?
Nimevutiwa na wasanii kibao hivyo jibu kwa swali hili hubadilika kila mwezi. Ninapenda kujifunza kutoka kwa wachanaji kibao iwezekanavyo bora masikio yangu yana wakati.
Hata hivyo, Abbas ni mtu ninaye mkubali sana inapokuja kwenye maswala ya uchanaji juu ya midundo ya Boom Bap. Kila kitu kinachotoka kinywani mwake ni kama upasuaji umefanyika, huwa hapotezi noti. Uwasilishaji wake ni jambo lingine ninalopenda. Yeye haipi maikrofoni nafasi yoyote ya kupumua wakati ana chana, kwa hiyo sauti yake ina ujazo mzuri sana kwenye wimbo.
Kimataifa, nilivutiwa sana na JID na Denzel Curry. JID ni mmoja wa ma rapa bora wa kizazi chake kwa sababu anaweza kuchana kuhusu chochote. Hata mpira! Kwa nishati ya uchanaji aliyonayo Denzel hakuna anayeweza kufanana naye. Alinifanya nitamani kuwa mchanaji pengine kuliko mtu mwingine yeyote. Ninakubali sana vile anavyoliamsha akiwa anachana.
Vipi kuhusu mara ya kwanza ulipoingia studio, kuliendaje? Ulirekodi wimbo gani na mashabiki zako waliupokeaje?
Nilikuwa na mchecheto kinoma!
Mdundo ulikuwa unajirudia rudia kwa takriban dakika 20 lakini bado sikuwa nimepata mwanya wa kuingia na kuanza kuchana. Kisha mtayarishaji akaanza kunitupia maneno ili nilianzishe. Hatimaye alitupia neno ‘Sesame Open’ na ubeti wa kwanza wa ‘Sesame Open’ ukaanza kutoka kwenye viganja vya vidole vyangu.
Msichana wa kwanza niliyewahi kumchezea ngoma hii alisema kuwa lugha ya Luo ni nzuri sana. Baada ya hapo niliendelea kwenda na lugha hii pia kwenye maswala ya uwasiliashaji wa mashairi yangu.
Kuwa katika taaluma yako ya muziki, unaamini ni nini kimekufanya uwe tofauti na kukutofautisha na wenzako?
Nadhani kila mtu, kutokana na karama aliyopewa, ni tofauti.
Kinachonitofautisha zaidi labda ni utengenezaji wangu wa filamu. Natumai kuwa msanii anayetumia filamu kama njia ya kujihusisha na mashabiki wake. Hiyo inamaanisha filamu fupi, insha za video na maandishi. Inachukua muda na rasilimali kufanya hivyo lakini kwa timu sahihi, inawezekana.
Ni nini kinachochochea mtindo wako wa uandishi na maudhui yako kwenye rap?
Maisha yangu ndio msukumo mkuu wa kile ninachoandika.
Tunaishi katika enzi nyeti sana ambapo wazo zima la uhuru wa kusema linapingwa mara kwa mara kwa hivyo ninajaribu kuwa mwangalifu kuhusu kuwa na sauti kubwa na maoni yangu ya kijamii. Ninaamini katika kujiangalia kiundani kabla ya kuelekeza kidole changu kwa jamii. Kwa hivyo ninahamasishwa na ukweli kwanza kabisa.
Mbali na kurap ninafahamu kuwa wewe ni mtayarishaji wa filamu. Je, hili kwa vyovyote vile linaathiri ubunifu wa muziki wako?
Bila shaka.
Hata ninapochana, naona mawazo yangu ki taswira. Hili limekuwa hivi kutokana na maelfu ya masaa ambayo nimetumia kutazama sinema. Ni kama jicho langu la tatu limekuza mtindo wa kuelekeza filamu.
Mchakato wako wa ubunifu ukoje unapoandaa muziki wako?
Unabadilika kutoka wimbo hadi wimbo.
Nyimbo zingine nitaandika hapo hapo studio kwa sababu nina mengi nataka kusema. Nyimbo nyingine nitaandika chorus kisha kukaa muda mrefu kabla ya kuamua ni mwelekeo gani wa kuchukua kwenye beti zangu. Na nyimbo nyingine naandika kama mashairi.
MARiACHi, tuambie kuhusu kanda mseto hii. Je, ni watayarishaji na wasanii gani ambao ulifanya nao kazi kwenye mradi huu? Kwa nini mradi unaitwa MARIACHi, jina linahusu nini na linamaanisha nini?
MARIACHi ni kandamseto nilipata wazo na ushawishi kutoka kwa Filamu ya zamani ya Robert Rodriguez iitwayo ‘El Mariachi’.
Filamu inaadhimishwa kwa hadithi za Indie kama toleo la kawaida la bajeti ya chini. Ninahisi kama nilirekodi mixtape kwa nguvu sawia na Robert Rodriguez alivyounda filamu ile. Nilikuwa nikijaribu kufanya kazi na watayarishaji kadhaa, walitengeneza midundo lakini baadae nikagundua kwamba hawakuwa wafuasi wa Hip Hop wala kuelewa vile midundo ile ilitakiwa iwe. Kwa hivyo kile walichotengeneza kiliishia kusikika kidogo na sikupenda kabisa kwani haikuwa na ladha yangu midundo ni ipendayo. Kwa hiyo nilikuwa napenda ladha nzuri ya midundo yenye gharama kubwa ila mfukoni nilikuwa bila bila.
Ndipo wazo la kurekodi mixtape kwa kutumia midundo mikali na michache iliyotumika likanijia. Ilikuwa ni lazima niweze kurap kwenye midundo niliyofurahia kuchana juu yake huku nikitafuta watayarishaji wa Hip Hop wanaopenda sana Utamaduni wa Hip Hop.
Kutoka kwenye kandamseto hii ni ngoma gani unayoipenda sana?
Mariachi.
Nilikua na hasira sana wakati nilipokuwa naandika ngoma hii. Nilikasirishwa na jinsi ilivyokuwa ngumu kupata watayarishaji wanaopenda Hip Hop, hasira kwa kupuuzwa, nilikuwa na hasira na mimi mwenyewe pia.
Na hasira yote hii nilijikuta nimeitoa kupitia hii ngoma. Hii hali ilikuwa mara ya kwanza kitu kama hicho kuwahi kunitokea wakati naandika na kurekodi wimbo.
Ni nini kilikuhimiza kuachia kandamseto badala ya labda EP au hata albamu? Je, ulipania kufikia malengo yepi kupitia kanda mseto hii?
'Kanda Mseto' ni msingi wa Hip Hop.
Wasanii wengi ninaowapenda walianza kwa kuachia kanda mseto kwa sababu wakati hakuna anayekujua wewe ni nani, kanda mseto inakupa nafasi ya kuonesha mapenzi uliyonayo dhidi ya Hip Hop. Ni upendo huo ambao mashabiki wako huungana nao kwanza. Mimi ni shabiki wa Hip Hop ninayetengeneza muziki wa Hip Hop kwa ajili ya mashabiki wengine kama mimi.
Lengo la kandamseto hiyo ni kutengeneza mradi ambao unaheshimika na mashabiki wa Hip Hop.
Je, ungependa wasikilizaji wako wachukue ujumbe gani kutoka kwa mradi huu?
Unaweza kuamua kubadili maisha yako ikiwa una nia ya kufanya hivyo.
Jambo moja nililoliona kutokana na kusikiliza mradi wako MARiACHi ni kuwa unachana freshi kwa lugha tatu. Je, hili linakuwezesha vipi kuonesha ubora wako inapokuja kwenye uchanaji na kuweza kueleza mawazo yako bila tatizo?
Hapa nahisi kama kuwa na uwezo huu ni kama nimeiba mtihani.
Unapoweza kughani kwa lugha 3 tofauti, unakuwa na misamiati mingi zaidi. Kwanza, hufanya mchakato wangu wa uandishi kuwa mwepesi zaidi na kisha, ndio, hufanya mtiririko wangu kuwa wa nguvu kwa sababu kila moja ya lugha hizo ina toni na muundo wa jinsi inavyosikika. Hasa kiLuo.
Ni nini tukitarajie kutoka kwako mwaka huu baada ya kudondosha kanda mseto yako ya kwanza?
Nimeanza kuandaa mradi wa ‘MARiACHi II’. Bado nina kazi ambayo haijakamilika katika ulimwengu wa kandamseto.
‘Martian Flow’ ndiyo video yako ya kwanza ya muziki. Wewe pia ndiye uliyesimamia uandaaji wake. Je, inakuaje kuongoza na kuandaa video yako mwenyewe?
Inachosha.
Kwa kawaida wakati wa kuelekeza napata kuangalia kila kitu kupitia mtazamo wa ndege, kwa juu. Lakini wakati wa kurekodi ‘Martian Flow’ nilikuwa naona mapungufu ya uigizaji wangu mwenyewe. Kwa hivyo niliji tafakari sana. Hakika nimejifunza mengi kutoka kwa kichupa hichi.
Ni wachanaji gani wa Afrika Mashariki ungependa kufanya nao kazi?
Wapo marapa kadhaa. FID Q! Kaka mbaya huyu!
Nilikutana naye mara moja miaka michache iliyopita na alikuwa kila kitu nilichotarajia angekuwa nacho!
Legend!
Ni mtayarishaji gani wa Afrika Mashariki ungependa kufanya naye kazi?
Provoke. Hip Hop inapita kwenye damu yake. Anajua yule!
Ni nini ungependa kushiriki nasi kukuhusu ambacho huenda sikukuuliza?
Ningependa tu kumshukuru kila mtu ambaye amepata mda wa kuskiliza muziki wangu hadi sasa. Wakati mimi na meneja wangu tulianza safari hii tulikuwa na lengo la kuwafikishia mashabiki muziki wa Kambona. Nina furaha kuliona hili linatimia wakati nikiishi.
Silichukulii poa hili!
Tafadhali tupatie mitandao yako ya kijamii na viunga vya dsps ambapo wasomaji wetu wanaweza kuwasiliana nawe na kuweza kuskia muziki wako...
X: https://twitter.com/KambonaOfficial
YouTube: https://www.youtube.com/@KambonaOfficial
Website: https://www.kambonamusic.online/
Asante kwa muda wako kaka Kambona, endelea kushinda.
'Kaka Kambona’ linanikalia poa mbona. Napenda sana hili!
Asante kwa kunialika.