Uchambuzi Wa Album: Kaka Kuona Mengi
Emcee: Kamusi
Tarehe iliyotoka: 22.07.2021
Nyimbo: 14
Watayarishaji: Abby MP, Ringle Beats, Kise P
Mixing & Mastering: Abby MP
Studio: Digg Down Records

Nyimbo Nilizozipenda: F.B.O(Full Battle Order), Conversation, Njozi, Who Are You, Mama Fausta, Kitendawili, Alama, Home Africa, Deep, Ghorofa La Mawimbi (Kwa Ufupi Ngoma Zote!)

Kamusi - Scavenger - Ndege Tai

Kamusi aka Ndege Tai/Scavenger ni emcee hatari sana. Binafsi mimi sikumjua kabla ya kununua na kuskia mradi wake Kaka Kuona Mengi. Kakakuona ni mnyama anayeitwa Pangolin kwa kiingereza aliepambika na magamba na mwenye mkia mrefu. Mnyama huyu akitaka kujikinga dhidi ya hatari hujikunja.

Mradi huu ambao ulisimamiwa kwa asilimia kubwa na Abby MP wa Digg Down Records ki midundo pamoja na kushirikishwa kwa mtayarishaji Ringle Beats umeundwa kiustadi sana. Cha kwanza nilichokipenda kwenye mradi huu ni ubora wa sauti, uchaguzi wa midundo, uwasilishaji, mashairi ya hali ya juu, uwasilishaji na mada zilizogusiwa kwenye mradi huu.

F.B.O(Full Battle Order) ndio ngoma inayotufungulia mradi huu na ndio single ya kwanza rasmi iliyoachiwa toka mradi huu. Ngoma hii inamkuta Kamusi akisimama kama mmoja wa wanajeshi wetu akichana kuhusu vile ameapa kujitoa mhanga kulinda nchi yake Tanzania pamoja na watu wake. Anachana kwenye mdundo wa kinanda kizuri sana akitema hisia kuhusu vile yupo tayari kwa lolote kutetea nchi yake.

Download | Kamusi Ft. Stive R&B – F.B.O [Mp3 Audio]

Baada ya hapa tunaenda kwa wimbo moto sana Conversation ulioundwa na Ringle Beats ambao ameshirikishwa Dizasta Vina. Kwenye wimbo huu wawili hawa wanachana kama wana waliopoteana mda mrefu baada ya mmoja wao kutoweka kijijini. Wanapiga gumzo wakikumbuka kuhusu maisha yao ya nyuma, ya sasa na changamoto za kimaisha za mjini na kijijini. Ngoma mzuka sana maana kila emcee yupo kwenye ubora wake hapa.

Ngoma nyingine nilizozipenda ni kama Njozi akiwa na Ano Sang, Ghorofa la Mawimbi akiwa na Bin Simba, pamoja na Who Are You akiwashirikisha Nikki Mbishi na Ibra Mpanduji kwenye mdundo safi sana toka kwa Abby MP.

Ngoma nyingine ambazo zimesimama ni kama Mama Fausta ambapo Ndege Tai anajikuta anamuamsha shemeji yetu Mama Fausta baada ya kushtuka toka kwenye njozi mbaya sana. Wimbo unaisha vizuri sana kwa sala toka kwa Kamusi hadi anapohitimisha maombi na Amen. Hadi utahisi mvuto wa hisia za woga kwenye wimbo huu.

Wimbo wa Kitendawili ni wimbo mzuka sana pia ambapo Abby MP anambariki Kamusi na mdundo mzuri sana. Kwenye kiitikio Malia Gan anatia wimbo nakshi kwa sauti inayovutia Mashallah. Huu ndio moja wa wimbo wangu bora kwenye mradi huu. Kamusi anachana akisema,

“Ayo Mungu angetuambia siku zetu ngapi zimebaki hapa duniani/
Kuna mtu mjunki ambae angefia kwenye drugs? /
Wezi wanga wasingechomwa kwenye umati/ wangeenda mbele ya madhabahu wangemlilia aliye na haki/
Nguzo tano za ki Islam hakuna ambaye angepuuza kuzifuata tunge tunza kwa nidham/
Hata dhambi na majini yasingekuepo/
Tungefuata dini tungekua na idhini ya kuiona pepo/”

Rapper aliyebobea ki mainstream Darasa ameshirikishwa kwenye Leo, kabla ya Kamusi kwenda solo tena kwenye Home Afrika akisifia bara letu. Deep akiwa na Bin Simba, Mabaki Ya Maiti akiwa na Mantiki Barz pamoja na Alama akiwa na Mizzo Vocal zote moto!

Mradi huu kusema kweli ndio umemtambulisha na kuonesha wazi kuwa  Kamusi, Scavenger, Ndege Tai ni Kaka Kuona Mengi.

Mfuate Kamusi kwenye mitandao ya kijamii;

Kununua mradi huu kwa Tshs 10000/= wasiliana na

WhatsApp: Abby MP +255659418801
Instagram: Kamusi
Twitter: scavenger036