Kamusi - Scavenger - Ndege Tai

Binafsi sikuwahi kumfahamu emcee Kamusi kabla ya kujinyakulia kanda yake Kaka Kuona Mengi. Ila nilichokiona kwa haraka haraka baada ya kunasa kanda hii ni kuwa jamaa ni mwandishi mzuri sana kando na kua na sauti na uwasilishaji mzuri wa mashairi yake.

Mradi huu ulikuwa wa viwango vya juu hata baada ya kumshirikisha Darassa ambaye ni rapper wa mainstream kwani hata kwenye ngoma aliyoshirikishwa Leo vigezo na masharti vilizingatiwa.

Nilimsaka jamaa huyu na nikapata fursa ya kupiga naye gumzo. Karibuni.

Karibu sana kaka Kamusi. Kwanza kabisa tuanze kwa kukufahamu, unaitwaje, unatokea wapi na unajihusisha na nini ? Kielimu umesomea wapi na kufikia hadi kiwango gani ?

Majina yangu kiserikali ni James Bruno Mpangala ni mwajiriwa serikalini mwenye elimu ya sekondari nliyohitimu Meta High School (Mbeya) na Makongo (Dsm).

Tueleze kidogo kuhusu haya majina yako unayoyatumia kwa shughuli zako za mziki, Kamusi, Scavenger na Ndege Tai. Yalikujaje na yanamaanisha nini ? Hivi mbona unapenda kutumia majina ya wanyama maana hata album yako umeiita jina la mnyama?

Well, majina kama Kamusi limetokana na vile utunzi wangu umejikita zaidi katika kutafsiri changamoto tofauti tofauti katika jamii, wakati Scavenger na Ndegetai zikiwa na maana karibu sawa kumaanisha mi ni aina ya ndege mla nyama na mizoga kwa namna vocals zangu vile nzito niki rhyme na jina la album kuitwa Kaka Kuona Mengi linatafsirika kwa maana zaidi ya moja ni wewe tu kutuliza vyema upeo wako.

Tueleze kuhusu historia ya nyuma ya mziki, ulianzaje hadi hapa ulipofika? Hadi sasa una miradi mingapi, inaitwaje na imetoka lini ?

Mwaka 2009 nilifanikiwa kurekodi kibao changu cha kwanza studio za Tattoo records na mtayarishaji mahiri Abby MP kwa Inspiration ya watu kama Fredy Saganda ,Sugu, Mabovu, Maujanja Saplayaz na wengineo. hadi sasa nina mradi mmoja tu uitwao Kaka Kuona Mengi iliyotoka mwishoni mwa mwaka 2021.

Kamusi tueleze kuhusu album yako Kaka Kuona Mengi. Mradi huu una maana gani kwako?  Wazo la mradi huu lilikujaje na maudhui yake ni yepi?

Wazo kuu la mradi wangu kuuita Kaka Kuona Mengi limebeba dhima ya maisha halisi niliyopitia katika kukua kimwili, afya ya akili na muziki wenyewe huku maudhui yake yakichagizwa vyema kwenye kila wimbo uliopo ndani ya mradi huo.

Mradi huu kwa asilimia kubwa umesimamiwa na Abby MP wa Digg Down Records. Ilikuaje mkafanya huu mradi pamoja maana nilihisi kulikua na chemistry nzuri kati yenu iliyo fanikisha mradi huu?

Kama nlivyotangulia kusema hapo awali Abby MP na mimi ukihesabu miaka tangu kufahamiana kwetu kikazi mpaka sasa(takribani 12 yrs)inatosha kukuaminisha kwa nini nilimpatia karibu 95% ya kufanikisha mradi wangu.

Kamusi kando na muziki unafanya shughuli gani nyingine?

Kwa bahati mbaya sipendi kuhusianisha maisha binafsi na muziki, tuache muda uongee.

Umekuwa huonekani kwenye mitandao ya kijamii kwa mda sasa, hata kwa upande wa promo ya mradi wako Kaka Kuona Mengi hukuhusika kabisa. Hii ilisababishwa na nini na hali hii itaendelea hadi lini?

Yamkini sio chaguo langu bora maishani mwangu ama pengine ni kutokana na aina ya shughuli zangu za utafutaji mkate wa kila siku hazinipi muda mzuri ku push mitandaoni.

Muziki kwa sasa umekuwa ukisogezwa karibu na shabiki kwa kuwekwa kwa Digital platforms, wewe kazi zako zipo kule au zinapatikana wapi? Je unazungumziaje hizi digital platforms, unaona kama zina manufaa kwa wasanii?

Digital platforms si kitu kibaya kwa msanii wa dunia ya leo inayozunguka upande huo na mi pia napatikana huko japo kwa uchache sana but ntajitahidi kutanua wigo zaidi Inshaallah !

Kamusi kuna chochote unachotuandalia sisi mashabiki zako na tukitarajie tutakipokea lini?

Nanukuu mstari wa Fid Q usemao "Mlango sio mlango hadi ufungwe au uachwe wazi” so, time will tell.

Ni changamoto gani unazozipitia wewe binafsi kama mwana Hip Hop aliyejichimbia handakini ? Je unakabiliana nazo vipi? Ungependa kushauri nini ma emcee chipukizi?

Binafsi sina changamoto kubwa kihivyo, zaidi ni ule wimbo wetu pendwa wa kila siku wa kupaza sauti kwa wana Hip Hop tulio wengi kutopata mialiko ya matamasha mengi makubwa ya muziki nje na ndani na urasimu kwenye mifumo ya kiuendeshaji sanaa ya muziki hapa nchini, so emceez wanaochipukia wanayo nafasi ya kurekebisha dosari kwa kuwaiga waliofanikiwa.

Kipi cha mwisho ungependa kutuambia ambacho sijakuuliza ?

Labda kingine usichokijua kuhusu mimi na Nikki Mbishi ni school mates elimu ya msingi tuliokuja kutambuana ukubwani na akiwa ni moja ya mentors wangu kwa Rap game niliyevutiwa na uwezo wake kabla hata ya kuonana kwetu.

Shukran sana kaka Kamusi kwa mda wako.

Karibu, imekuwa heshima kubwa na fahari kushiriki na wewe katika mahojiano haya na nikupongeze kwa kuthubutu na kuwa chachu ya mabadiliko na mapinduzi ya Hiphop Tz, keep going bro !